Mwanamke Anaweza Kwenda Hijjah Bila Ya Mume Ikiwa Mumewe Haswali Na Analewa

 

SWALI:

Asalaam alaykum warahmaturullah taala wabarakatu. Mimi nina mme. mme huyo anakunywa pombe na haswali. Nimejaribu kumlingania kwa hilo bila mafanikio. Mimi maashallah naswali. Swali langu ni je! naweza kwenda hajj nikijaaliwa? Mwenyeezi mungu awajaarie kheri kwa kuunda chombo hiki na kutuelimisha. Inshallah amiin. 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali hilo kuhusu Hajj. Mwanamke hawezi kwenda Hajj pasi na maharimu wake. Maharimu wake ni yule ambaye kisheria hawezi kumuoa kama baba, ndugu yake wa kiume, ami yake, mjombake au mtoto wake wa kiume ambaye tayari amebaleghe.

Ikiwa hutapata maharimu wa kwenda naye basi Hajj haijakupasa wewe na InshaAllaah Atakufanyia sahali na wepesi upate wa kwenda naye.

Soma katika viungo vifuatavyo upate ufafanuzi kwa upana:

Mwanamke Asiye Na Mahram Hawajibiki Kufanya Hajj

Hijja Yake Imekubaliwa Ikiwa Amekwenda Bila Mahram?

Mwanamke Kumfanyia Hijja Mtu bila Mahram Haifai

Kulingana na maelezo yako ni kuwa wewe uko katika matatizo makubwa ambayo yanafaa yapatiwe ufumbuzi. Shida uliyo nayo ni ile ya unyumba na ikiwa hutachukuwa tahadhari za Kidini basi huenda na Imani yako ikafifia. Hukutueleza kama mumeo alikuwa akifanya hayo kabla ya kukuoa au vipi. Kwa hali yoyote inatakiwa uchukue hatua za haraka na dharura ili upate ufumbuzi.

Umetuelezea kuwa umejaribu kiasi cha uwezo wako bila mafanikio yoyote. Kwa ajili unatakiwa ufanye yafuatayo:

  1. Itisha kikao baina yako, mumeo, wawakilishi wa mumeo na wako kwa ajili ya kukaa pamoja ili kutafuta ufumbuzi. Ajenda iwe ni tabia za mumeo wala usifiche. Ikiwa hakutakuwa na muafaka wowote basi,

  2. Nenda kwa Qaadhi au muhusika yeyote mkubwa wa dini kama Shaykh ambaye ni muadilifu kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo. Ikiwa atajirekebisha utaendelea kukaa naye kama mumeo, na lau hatajirekebisha basi Qaadhi huyo atoe uamuzi wa kukuachisha.

Muislamu hafai kukaa na mume ambaye haswali, kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Baina ya mtu na ushirikina na ukafiri ni kuacha Swalah" (Muslim) na baya zaidi kwa mume huyo wako ni kazidisha madhambi zaidi kwa kunywa na pombe.

Tunakutakia kila la kheri na tawfiki katika mambo yako yote mawili. 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share