Masharifu Wasioswali Wana Maovu Na Maasi Watukuzwe? Je, Wao Bora Kuliko Mja Anayefuata Shari'ah?

 

Masharifu Wasioswali  Wana Maovu Na MaasiWatukuzwe?

Je, Wao Bora Kuliko Mja Anayefuata Shari'ah?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Salamun alykum jamia, rehma na amani zitufikie wote kwa ujumla, na mwenyezi mungu atuzidishie imani kwa sote.

Swali langu lilikuwa kutaka kujuwa kama masharifu tuna haki ya kuwahishimu na kuwapa heshima hata kama wao hawasali na wanafanya mambo kinyume na shariya ya kiislamu, kwa mfano wanalewa, hawafungi ramadhani wanasema uwongo wanatenda vitendo vingine hata kuvitaja siwezi.... swali ni hivi je wao bora zaidi kuliko sisi hata kama sisi tunafata sharia ya kiislamu, na woa hawafati basi wao ni bora kwa sababu ni masharifu tukiwaona wajibu wetu kuwa busu mikono yao na kuwapa heshima kubwa  hatuna haki ya kuwahukumu kwa lolote kutokana  darja lao  kubwa kwa Allaah kuliko sisi tunayefanya ibada, ibada yao 1 sawa na sisi 10 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu utukufu wa binadamu. Tufahamu kuwa Uislamu umekuja kuwaweka sawa wanaAadamu wote, ubora unakuja tu kwa uchaji wa Allaah sio kwa ukoo au kabila. Kama ingekuwa Masharifu ni bora, hivyo basi wale ambao tungetakiwa tuwaheshimu zaidi miongoni mwao ni Abu Twaalib na Abu Lahab kwani wote walikuwa ami zake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini Qur-aan imetufahamisha wazi kabisa kuwa Abu Lahab ataingia Motoni.

 

Qur-aan na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimetuwekea msingi ya uadilifu na usawa. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ﴿١٣﴾

Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana namwanamme na mwanamke, na Tukakujaalieni  mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye na hadhi zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni mwenye taqwa zaidi kati yenu. Hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Al-Hujuraat: 13]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye ametuambia katika Hijjah yake ya mwisho:

 

"Hakuna ubora kwa mweupe juu ya mweusi, wala Mwarabu juu ya asiyekuwa Mwarabu, ila kwa kumcha Allaah".

 

Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Enyi Maquraysh! Jinunueni nafsi zenu kutoka kwa Allaah, kwani mimi sitowafaa kitu kwa Allaah. Enyi Bani 'Abdi Manaaf, sitowafaa kitu kwa Allaah. Ee Swafiyyah (shangazi yake), sitokufaa kitu kwa Allaah. Ee Faatwimah (binti Muhammad) niombe utakalo, lakini sitokufaa kitu kwa Allaah" [Ahmad].

 

Na katika Hadiyth yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia kuwa yeyote atakayecheleweshwa kwenda Peponi kwa sababu ya amali zake kuwa ni nzuri hatatangulizwa mbele katika kuingia katika Pepo na nasaba yake. Hii ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"… Na mwenye kucheleweshwa kwa amali yake haitamtanguliza nasaba yake" [Ahmad na Muslim].

 

Kwa hiyo, awe mtu ni Mquraysh au Sharifu kama anavyodai lakini hafuati kanuni zilizowekwa na Allaah Aliyetukuka na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na haswa kwa kufanya madhambi makubwa basi hafai mtu kama huyo kuheshimiwa bali anatakiwa asusiwe kwa anayofanya. Huenda kufanywa hivyo akahisi makosa aliyonayo na kurudi katika Dini kwa kufuata maagizo ya Aliyetukuka.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share