Mbingu Saba Na Ardhi Saba Na Kutandazwa Dunia?

 

SWALI:

Pili ni naswali lingine ambalo nahitaji pia msaada wenu ili niweze kuelewa.

Allah anasema "“Allah is He Who created seven Firmaments and of the earth a similar number…” [Quran 65.12]

je aridhi saba na mbingu saba ni zipi?naomba nitajie. 

Tatu allah anasema "  Earth spread out (like a carpet), mountains firm…Quran 15:19

God made earth like a carpet spread out…20:53 aya hizi nimezinakili kwa kifupi. sasa swali langu ni hili "Ikiwa aridhi imeumbwa tambarare Je dunia ni aridhi ikiwa dunia ni aridhi je vipi kuhusu ukweli wa dunia kua ni duara?

 

 

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

MBINGU SABA NA ARDHI SABA

Kwa mujibu wa wafasiri mbalimbali, ardhi ziko saba kama vile mbingu zilivyo saba. Na maelezo ya Maswahaba kama Ibn Mas'uud yanathibitisha kuwa masafa ya mbingu moja hadi nyingine ni masafa ya miaka mia tano, na baina ya mbingu ya saba na KURSIY hali kadhalika na juu ya KURSIY kuna 'ARSH ambayo iko juu ya maji. (Maelezo hayo ya KURSIY na 'ARSH na MAJI ni kwa faida ya nyongeza ingawa hayapo kwenye swali kwa sababu wengi wanashindwa kutofautisha baina ya KURSIY na 'ARSH).

Na pia si wengi wetu wanaofahamu kuwa 'ARSH ipo juu ya maji na maji hayo yapo juu ya mbingu saba. Na kwa faida zaidi, tuelewe kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Yuko juu ya 'ARSH ambayo ipo juu ya MAJI na juu ya KURSIY na vilevile juu ya mbingu saba na juu ya viumbe vyote. Hakuna kitu juu Yake, Na Hakifichiki chochote katika matendo yetu  Kwake. Ametukuka na hafanani na chochote. (Maelezo haya yote yanaungwa mkono na kutiliwa nguvu na Qur-aan).

Na kwa faida nyingine kwa mujibu wa wafasiri ni kuwa baina ya hizo ardhi saba kuna viumbe ndani yake kama ilivyo kwenye Aayah hii:

((تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ))

((Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake)) [Israa: 44]

Kuhusu Aayah:

 ((اللَّهُ الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ وَمِنَ الْأَرْضِ مِثْلَهُنَّ))  

 ((Allah ni Yule Ambaye ameziumba mbingu saba, na ardhi kwa mfano wa hizo)) [At-Twalaaq 65:12] 

Ni kwamba idadi hiyo ya ardhi saba kama ilivyotajwa kuwa sawa na idadi ya mbingu. Amesema Ibnu Kathiyr katika 'Al-Bidaayah wa An-Nihaayah' kwamba kama vile Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwa: 

((إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ))

((Hakika idadi ya miezi kwa Allah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Allah tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitakatifu)) [At-Tawbah:36]

Kwa hiyo idadi hiyo ni sawa kabisa kuwa ziko ardhi saba. Vile vile kama kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((أَلَمْ تَرَوْا كَيْف خَلَقَ اللَّهُ سَبْع سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا))   

((Kwani hamuoni jinsi Allah Alivyoziumba mbingu saba kwa matabaka? )) [Nuuh: 15]

Vile vile:

(( تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْع وَالْأَرْض وَمَنْ فِيهِنَّ))  

((Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake)) [Israa: 44]

Na kauli yake hiyo 

((وَمِنْ الْأَرْض مِثْلهنَّ))

((na ardhi kwa mfano wa hizo)) [At-Twalaaq:12] 

Vile vile ina maana ni ardhi saba kama ilivyothibitika katika Swahiyhayn

((مَنْ ظَلَمَ قِيدَ شِبْر مِنْ الْأَرْض طَوَّقَهُ مِنْ سَبْع أَرَضِينَ))

((Atakayechukua ardhi ya mwenzake kwa dhulma, hata kama ni shibri moja, shingo yake itazungushwa (itafungwa) kwenye ardhi saba)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Na katika Al-Bukhaariy imesema:

((خَسَفَ بِهِ إِلَى سَبْع أَرَضِينَ))

((Atazamishwa chini katika ardhi saba))

 

KUTANDAZWA KWA ARDHI

Kuhusu Aayah: 

((وَالأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْزُونٍ)) 

((Na ardhi Tumeitandaza na humo Tumeweka milima, na Tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake)) [Al-Hijr: 19]

Na Aayah:

((الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ مَهْدًا))

((Ambaye Amekufanyieni ardhi kuwa tandiko)) [Twaaha: 53]

Ni sawa pia na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Surat Ghaafir:

((وَالْأَرْضَ فَرَشْنَاهَا فَنِعْمَ الْمَاهِدُونَ))  

((Na ardhi Tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna gani Sisi!)) [Adh-Dhaariyaat: 48]

Maana ya Farsh ni tandiko kama vile matandiko ya katika nyumba na kauli nyingi zimekuja katika neno hilo mfano:

((الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الأَرْضَ فِرَاشاً))

(Allah) Ambaye Amekufanyieni hii ardhi kuwa kama tandiko)) [al-Baqarah: 22] 

au vile vile: 

((مُتَّكِئِينَ عَلَى فُرُشٍ بَطَائِنُهَا مِنْ إِسْتَبْرَقٍ))

((Wawe wameegemea matandiko yenye bitwana ya hariri nzito)) [Ar-Rahmaan:54]

Vile vile  neno la 'Mahd' lina maana ya 'utandazaji' kama vile kusema 'kutandaza tandiko' au kutandaza vizuri, kama katika Aayah:

((وَمَهَّدتُّ لَهُ تَمْهِيدًا))   

((Na Nikamtengenezea mambo vizuri kabisa)) [al-Muddath-thir:14]

Na katika Qur-aan imetajwa kutandikwa kwa ardhi katika Aayah mbali mbali zikiwemo hizo tulizozitaja juu. 

Ibn Kathiyr amesema kuhusu kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((وَالْأَرْضَ فَرَشْنَاهَا فَنِعْمَ الْمَاهِدُونَ))  

(( Na ardhi Tumeitandaza; basi Watandazaji wazuri namna gani Sisi!)) [Adh-Dhaariyaat: 48]

ina maana :Tumeitandaza kwa wakaazi, yaani kwa ajili ya viumbe vyote vinavyoishi ardhini ili iwe wepesi kwao kuishi.

(Na waishi kwa raha kama vile yanavyoleta raha matandiko ya nyumbani, na ndio tukawekewa ardhi kavu na bahari, mito, majabali, miti, mabustani, wanyama n.k ili tuweze kuendesha maisha yetu kwa kupata mahitajio yetu yote na kuishi kwa raha).

 

KUHUSU ARDHI NI DUNIA NA MZUNGUKO WA ARDHI   

Neno la ardhi inavyoelekea kutokana  na kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Qur-aan na Sunnah ni kwamba hukusudiwa ardhi nzima kwa maana dunia nzima au kama ni nchi, au kipande tu cha ardhi kwa masafa fulani. Baadhi ya dalili katika Qur-aan kama zifuatavyo:

Ardhi nzima yaani kama dunia nzima: 

Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) 

1)  

((لَّقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَآلُواْ إِنَّ اللّهَ هُوَ الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ قُلْ فَمَن يَمْلِكُ مِنَ اللّهِ شَيْئًا إِنْ أَرَادَ أَن يُهْلِكَ الْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ وَمَن فِي الأَرْضِ جَمِيعًا وَلِلّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا يَخْلُقُ مَا يَشَاء وَاللّهُ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ))

((Hakika wamekufuru walio sema: Allahni Masihi mwana wa Maryamu. Sema: Ni nani mwenye kumiliki chochote mbele ya Allaah ikiwa Yeye Angetaka kumuangamiza Masihi mwana wa Maryamu, na mama yake, na wote waliomo katika ardhi?)) [Al-Maaidah:17] 

2) 

((وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلاَئِكَةِ إِنِّي جَاعِلٌ فِي الأَرْضِ خَلِيفَةً قَالُواْ أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاء))  

((Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi Nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakayefanya uharibifu humo na kumwaga damu)) [Al-Baqarah:30]

Kwa maana Ataumba binaadamu na kuwaweka katika hii dunia.

Ardhi kama ni nchi

Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)

1)

((وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ))

((Na tukamwokoa yeye na Luutw Tukawapeleka kwenye nchi tulioibariki kwa ajili ya walimwengu wote)) [Al-Anbiyaa:71]

(ardhi ya Shaam)

2)

((يَا قَوْمِ ادْخُلُوا الأَرْضَ المُقَدَّسَةَ الَّتِي كَتَبَ اللّهُ لَكُمْ وَلاَ تَرْتَدُّوا عَلَى أَدْبَارِكُمْ فَتَنقَلِبُوا خَاسِرِينَ)) 

((Enyi watu wangu! Ingieni katika nchi takatifu ambayo Allah Amekuandikieni. Wala msirudi nyuma, msije mkawa wenye kukhasirika)) [Al-Maaidah:21]

(Quds)

Ardhi kama ni kipande tu cha masafa fulani:

Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)

1)

فَبَعَثَ اللّهُ غُرَابًا يَبْحَثُ فِي الأَرْضِ لِيُرِيَهُ كَيْفَ يُوَارِي سَوْءةَ أَخِيهِ  

Hapo Allaah Akamleta kunguru anayefukua katika ardhi ili amwonyeshe vipi kumsitiri nduguye)) [Al-Maaidah:31]

2)

 ((وَلاَ تَمْشِ فِي الأَرْضِ مَرَحًا إِنَّكَ لَن تَخْرِقَ الأَرْضَ وَلَن تَبْلُغَ الْجِبَالَ طُولا))

((Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima)) [Al-Israa:37]

MZUNGUKO WA DUNIA:

Amesema Dkt. Zaghluul, kwamba masafa ya ardhi ni ni taqriban Milioni 510 Kilomita za mraba ikiwa ni Milioni 149 mita mraba ardhi kavu.  

Hivyo kutandikwa kwa ardhi huko tunaona kuwa ni sehemu kubwa au masafa marefu sana, kwa hiyo juu ya kwamba ardhi inazunguka kama tunavyojua, kutandikwa hukuhusiani au hakuambatani na mzunguko wa dunia kwa vile masafa kutoka Kazkazini hadi Kusini na kutoka Mashariki hadi Magharibi ni makubwa sana. Na Aayah ifuatayo inathibitisha pia usemi huu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amejaalia ardhi kuwa ya kutua:

((أَمَّن جَعَلَ الْأَرْضَ قَرَارًا وَجَعَلَ خِلَالَهَا أَنْهَارًا وَجَعَلَ لَهَا رَوَاسِيَ))

((Au nani yule aliyeifanya ardhi mahali pa kutua, na akajaalia ndani yake mito, na akaweka milima?)) [An-Naml 61] 

Na kuhusu ardhi kutandazwa au kufanywa kuwa kama tandiko, haina maana kuwa ni flat tambarare au bapa na si umbo la 'yai',  bali  ardhi au DUNIA kwa maana maarufu, umbo lake ni umbo kama tufe au mfano wa yai.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share