Anataka Kujua Hukumu Ya Kumfanyia Mazingaombwe Mume Wake Ili Ampende

 

 

 

 

SWALI:

 

Assalamu aleykum warahmatullah wabarakatuh.

Napenda kupongeza uongozi mzima wa Al-hidaaya kwa kazi nzuri waifanyayo. Swali langu ni kutaka kujua kutia viini vya macho kwa kumrembea mume vibaya?


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hukumu ya kumfanyia mumeo mazingaombwe.

Mazingaombwe ni aina ya udanganyifu na mara nyingi huingia uchawi na sihri. Udanganyifu katika Uislamu haufai, kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kutudanganya si katika sisi” (Muslim).

 

Ama kwenda kwa mchawi au mtizamiaji au mpiga bao ni shirki na hivyo haifai kishari’ah kabisa. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na Luqmaan alipomwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Allaah. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa” (Luqmaan [31]: 13).

Mwenye kwenda kwa mtazamiaji Swalah yake haikubaliwi siku arubaini. Na tufahamu shirki ni dhambi kubwa sana linalomtoa mtu katika Uislamu.

 

Kwa hiyo, inatakiwa kwa mke amfanyie mumewe mambo mazuri ya kishari’ah ambayo yatamfanya mumewe ampende kidhati. Huko ni kama:

 

1.     Kuwa msafi daima na kujirembesha kwa ajili yake.

2.     Kumfanyia mambo mazuri na mema.

3.     Kumtii kwa lisilokuwa la haramu.

4.     Kulinda heshima yake kwa kutofanya ya haramu.

5.     Kumpikia kwa avipendavyo, vilivyo vizuri.

6.     Kumliwaza na kumpooza anaporudi nyumbani.

7.     Na mengi mengineo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share