Ufafanuzi Kuhusu Kusema Uongo Kwa Nabii Ibraahiym Katika Kisa Chake

 

SWALI:

 

Asalaam alaykum,

Naomba kuuliza kuhusu kisa cha nabii ibrahim katika kuongopa kwake vipi ufafanuzi juu ya uwongo wake? Alifaya kosa au la?

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) na kuongopa kwake. Kisa chenyewe ni kama kifuatavyo kwani kwa kukitaja tutaweza kuufahamu uwongo huo kwa njia iliyo wazi au ni kutoelewa kwetu.

 

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nabii Ibraahiym alihama pamoja na Sarah, wakafika katika kijiji alichokuwepo mfalme au dikteta. Mfalme aliambiwa kuwa Ibraahiym amefika hapo akiwa na mwanamke mzuri. Hivyo, mfalme alituma aletwe Ibraahiym na kumuuliza, ‘Ewe Ibraahiym! Huyu mwanamke ni nani?’ Ibraahiym akajibu: Ni dadangu’. Ibraahiym alirudi wkake na kumwambia, ‘Usiende kinyume nami katika kauli kwani nimemwambia kuwa wewe ni dadangu. Naapa kwa Allaah, hakuna Waumini wa kweli katika ardhi isipokuwa mimi na wewe” (al-Bukhaariy).

 

Kwa hiyo katika kisa hiki ni wazi kabisa kuwa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) hakuongopa kwa kusema Sarah ni dadake, kwani wao ndio Waumini pekee waliokuwa hapa duniani kama Hadiyth inavyoashiria. Na Hadiyth hii ni ishara ya utumiaji wa mafumbo ili kumfanya adui asiwe ni mwenyewe kuelewa hakika ya jambo au mambo.

 

Swahaba Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye alitumia njia hii alipokuwa anahama pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam). Alipokuwa anaulizwa na watu huyu unayefuatana naye ni nani, yeye alikuwa anajibu: ‘Huyu ni yule mtu aliyeniongoza njia’. Waulizaji walikuwa wanafahamu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye mwenye kuongoza msafara ilhali Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa anamaanisha Mtume Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye aliyemuongoza katika Uislamu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi. 

 

Share