Kupangusa Uso Baada Ya Kusoma Du’aa Inafaa?

 

SWALI:

 Assalam aleikum

ningependa munifahamishe kuhusu mtu kufuta uso wake akimaliza dua wakati anaposema Amin, je kuna hadith yoyote ama kithibitisho kuwa Mtume swalla-llahu alaihi wassalam alikuwa akifanya hivyo? Jaza yenu iko kwa Allah subhanahu' wata'ala kwa kazi munayo fanya, Shukran

 


JIBU:

 

Sifa zote njema anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kupangusa uso baada ya kuomba du’aa si kitendo cha Sunnah, na Hadiyth nyingi zilizopokelewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam) alipokuwa akiomba du’aa zake hakuwa akipangusa uso wake baada ya du’aa. Na hata katika Khutbah ya Ijumaa au Swalah ya Istisqaa haikuthibiti kwamba alipangusa mikono yake usoni. Hadiyth moja au mbili zilizosimuliwa kuhusu kitendo hiki zimechambuliwa kuwa ni Hadiyth dhaifu, na Ma'ulaamaa wamekubaliana kwamba kitendo hiki hakipo katika Shari’ah.

 

 

Na hata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akimaliza Swalah zake na kutoa salaam, hakuwa kamwe akipangusa uso wake kama ilivyo ada ya Waislamu wengi hivi leo wanavyofanya na hawajui kwanini wanafanya hivyo na hata ukimuuliza mtu anashindwa kukupa jibu, na wengine wanajibu kuwa wamejikuta wakikuwa na kuona ikifanywa hivyo na wao wanafanya. Muislamu anapaswa kufanya matendo yake yote ya ‘Ibaadah kwa dalili na si kwa kubahatisha au kuiga bila dalili.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share