Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah013 - Al-Waahid

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 013 kati ya 103
Al-Waahid — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Waahid: Mmoja Pekee Asiye Na Kifano

Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mmoja Pekee Asiye na kifano. Ni Mmoja Pekee kwa dhati Yake na Sifa Zake.

Allaah (سبحانه وتعالى) ni Mmoja Pekee katika Sifa Zake za Rubuwbiyyah (Uumbaji, Ufalme, Uola, Kuruzuku, Kuendesha mambo ya Waja Wake), na katika Uluwhiyyah (kuabudiwa Kwake) na katika Asmaa na Swifaat (Majina na Sifa).

Allaah (سبحانه وتعالى) Alikuwa ni Mmoja Pekee hapo awali hapakuwa na kitu kabla Yake na Yungali Mmoja Pekee, na Atakuwa Mmoja Pekee Milele, hakuna kitu baada Yake.

Allaah (سبحانه وتعالى) Ambaye ni Al-Waahid hakuna chochote au yeyote mwenye mfano Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾

Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:11)]

Na Ibn Jariyr akasema kuhusu maana ya ‘Kumpwekesha Allaah’ katika kuifasiri Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴿١٦٣﴾

Na Ilaah wenu (Allaah) ni Ilaah Mmoja, hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye, Mwingi wa rahmah, Mwenye kurehemu. [Al-Baqarah (2:163)]

Na Ambaye Anastahiki kutiiwa nanyi enyi watu! Na imekuwajibikieni kufanya ‘ibaadah kwa Mwenye kustahiki kuabudiwa Mmoja Pekee na Rabb Mmoja Pekee, basi msimwabudu mwengine wala msimshirikishe na yeyote, kwani mkimshirikisha na mwengine katika ‘ibaadah zenu, basi huyo mnayemshirikisha ni kiumbe kama nyinyi katika viumbe vya Ilaah wenu (Mwabudiwa wa haki). Na Ilaah wenu ni Ilaah Mmoja Pekee Hana mfano Wake wala aliye sawa Naye.1

Jina la Allaah (سبحانه وتعالى) ‘Al-Waahid’ limetajwa katika Qur-aan zaidi ya mara ishirini; baadhi ya Aayah ni:

وَقَالَ اللَّـهُ لَا تَتَّخِذُوا إِلَـٰهَيْنِ اثْنَيْنِ ۖ إِنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ﴿٥١﴾

Na Allaah Anasema: “Msijichukulie waungu wawili; hakika Yeye Ndiye Muabudiwa wa haki Mmoja (Pekee) basi Niogopeni Mimi tu.” [An-Nahl (16:51)]

فَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَلَهُ أَسْلِمُوا ۗ وَبَشِّرِ الْمُخْبِتِينَ ﴿٣٤﴾

Kwa hiyo Muabudiwa wenu wa haki ni Ilaah Mmoja, basi kwake Pekee jisalimisheni. Na wabashirie wanyenyekevu. [Al-Hajj (22:34)]

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi ni mtu kama nyinyi, nafunuliwa Wahy kwamba: Hakika Muabudiwa wa haki wenu ni Ilaah (Allaah) Mmoja. Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende ‘amali njema na wala asishirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Rabb wake.” [Al-Kahf (18:110)]

لَّقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ ثَالِثُ ثَلَاثَةٍ ۘ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۚ وَإِن لَّمْ يَنتَهُوا عَمَّا يَقُولُونَ لَيَمَسَّنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٧٣﴾

Kwa yakini wamekufuru wale waliosema: “Hakika Allaah ni watatu wa utatu.” Na hali hapana Muabudiwa wa haki isipokuwa Ilaah Mmoja (Allaah). Na wasipoacha yale wanayoyasema, bila ya shaka itawagusa wale waliokufuru miongoni mwao adhabu iumizayo. [Al-Maaidah (5:73)]

Na pia Jina hili la ‘Al-Waahid’ limeungana mara sita katika Qur-aan pamoja na ‘Al-Qahhaar’ (Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika):

لَّوْ أَرَادَ اللَّـهُ أَن يَتَّخِذَ وَلَدًا لَّاصْطَفَىٰ مِمَّا يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ سُبْحَانَهُ ۖ هُوَ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٤﴾

Lau Angelitaka Allaah kujichukulia mwana, Angelikhitari Amtakaye miongoni mwa Aliowaumba. Subhaanah! (Utakasifu ni Wake), Yeye Ndiye Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika. [Az-Zumar (39:4)]

قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ ۚ قُلْ أَفَاتَّخَذْتُم مِّن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ لَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ نَفْعًا وَلَا ضَرًّا ۚ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِي الظُّلُمَاتُ وَالنُّورُ ۗ أَمْ جَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ ۚ قُلِ اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿١٦﴾

Sema: Ni nani Rabb wa mbingu na ardhi? Sema: Ni Allaah. Sema: Je, mnawafanya wengineo badala Yake kuwa rafiki walinzi na hali hawamiliki manufaa wala dhara kwa nafsi zao? Sema: Je, kipofu analingana sawa na mwenye kuona, au je, viza vinalingana sawa na nuru? Au wamemfanyia Allaah washirika walioumba kama uumbaji Wake, kisha ukafanana uumbaji kwao (wakakanganyikiwa)? Sema: Allaah Ni Muumbaji wa kila kitu, Naye Ni Mmoja Pekee, Asiyepingika. [Ar-Ra’d (13:16)]

يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ﴿١٦﴾

Siku watakayotokeza wao, hakitofichika kitu chochote chao kwa Allaah. Ufalme ni wa nani leo? (Allaah Mwenyewe Atajijibu): Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Asiyepingika. [Ghaafir (40:16)]

يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَأَرْبَابٌ مُّتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ﴿٣٩﴾

Enyi masahibu wangu wawili wa jela. Je, marabi wengi wanaofarakana ni bora (kuabudiwa) au Allaah Mmoja Pekee, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika. [Yuwsuf (12:39)]

قُلْ إِنَّمَا أَنَا مُنذِرٌ ۖ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٦٥﴾

Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu. Na hakuna Muabudiwa wa haki yeyote isipokuwa Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika. [Swaad (38:65)]

يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ ۖ وَبَرَزُوا لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ﴿٤٨﴾

Siku ardhi itakapobadilishwa kuwa ardhi nyingine na mbingu pia, na (viumbe wote) watahudhuria kwa Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika. [Ibraahiym (14:48)]

Kutajwa Majina mawili haya mazuri pamoja, inamaanisha kuwa ni Yeye Allaah Pekee Mwenye mamlaka na uwezo wa kufanya lolote Alitakalo, hakuna wa kumpinga na hivyo kila kilichokuwa mbinguni na ardhini kinajisalimisha Kwake Yeye Pekee Al-Waahid.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Waahid:

1-Al-Waahid Ndiye Al-Qahhaar, Aliyeshinda Kila Kitu:

Jina Al-Waahid limekuja mara nyingi pamoja na Al-Qahhaar, kwani Mmoja Pekee Asiye na mshirika Ndiye Aliyedhibiti kila kitu chini ya Mamlaka Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَّوْ أَرَادَ اللَّـهُ أَن يَتَّخِذَ وَلَدًا لَّاصْطَفَىٰ مِمَّا يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ سُبْحَانَهُ ۖ هُوَ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٤﴾

Lau Angelitaka Allaah kujichukulia mwana, Angelikhitari Amtakaye miongoni mwa Aliowaumba. Subhaanah! (Utakasifu ni Wake), Yeye Ndiye Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika. [Az-Zumar (39:4)]

2-Mpwekeshe Al-Waahid Wala Usimshirikishe Na Chochote:

Tambua, ee Mja wa Al-Waahid: Mpwekeshe Muumba wako (سبحانه وتعالى) kwa kutokumshirikisha na chochote kwa sababu kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) ni dhulma kubwa mno.

3-Mwabudiwa Mmoja Ni Bora Kuliko Waabudiwa Wengi Waliotawanyika:

Tambua, ee Mja wa Al-Waahid: Nabiy Yuwsuf (عليه السلام) aliwalingania wafungwa wenzake gerezani kwa hoja hii:

يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَأَرْبَابٌ مُّتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ﴿٣٩﴾

Enyi masahibu wangu wawili wa jela! Je, miola wengi wanaofarakana ni bora au Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika? [Yuwsuf (12:39)]

4-Haki Ya Al-Waahid Juu Ya Waja Wake Ni Wamwabudu Wala Wasimshirikishe:

Tambua, ee Mja wa Al-Waahid, kwamba haki ya kwanza ya Allaah juu yako ni kumwabudu Yeye Pekee bila kumshirikisha na chochote.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كُنْتُ رِدْفَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) عَلَى حِمَارٍ فَقَالَ: ((يَا مُعَاذُ، هَلْ تَدْرِي حَقَّ اللَّهِ عَلَى عِبَادِهِ، وَمَا حَقُّ الْعِبَادِ عَلَى اللَّهِ؟)) قُلْتُ: اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ. قَالَ: ((فَإِنَّ حَقَّ اللَّهِ عَلَى الْعِبَادِ أَنْ يَعْبُدُوهُ وَلاَ يُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا، وَحَقَّ الْعِبَادِ عَلَى اللَّهِ أَنْ لاَ يُعَذِّبَ مَنْ لاَ يُشْرِكُ بِهِ شَيْئًا))

Amesimulia Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه): Nilikuwa nimepanda nyuma ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya punda, akasema: “Yaa Mu’aadh! Je, unajua ni ipi haki ya Allaah juu ya Waja Wake, na ni ipi haki ya waja kwa Allaah?” Nikasema: Allaah na Rasuli Wake Wanajua zaidi. Akasema: “Hakika haki ya Allaah juu ya waja ni wamwabudu na wasimshirikishe na chochote; na haki ya waja kwa Allaah ni kwamba Asimuadhibu asiyemshirikisha na chochote.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Tafakari Dalili Za Upweke Wa Al-Waahid Katika Uumbaji Wake:

Tafakari na zingatia dalili za Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Uumbaji Wake (Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah) kwa kuangaza kila aina ya Uumbaji Wake unaokuzunguka mahali popote ulipo, ujue kuwa hakuna yeyote awezaye kuumba kama Uumbaji wa Al-Waahid.

6-Tawhiyd Ndiyo Msingi Wa Umoja Wa Ummah:

Kumwabudu Al-Waahid Pekee ndiko kunakowaunganisha Waislamu, na kushikamana na Kamba Yake ndiko kunakowaepusha na mfarakano. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا وَكُنتُمْ عَلَىٰ شَفَا حُفْرَةٍ مِّنَ النَّارِ فَأَنقَذَكُم مِّنْهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴿١٠٣﴾

Na shikamaneni kwa Kamba ya Allaah nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni Neema ya Allaah juu yenu, pale mlipokuwa maadui (kati yenu), kisha Akaunganisha nyoyo zenu, mkawa ndugu kwa Neema Yake, na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto Akakuokoeni humo. Hivyo ndivyo Allaah Anavyokubainishieni Aayaat (na Ishara) Zake mpate kuhidika. [Aal-‘Imraan (3:103)]

7-Fanya Amali Njema Bila Kumshirikisha Mmoja Na Yeyote, Ili Upate Kukutana Naye:

Mwenye kutaraji kukutana na Rabb wake, basi amali yake iwe njema na iwe kwa ajili ya Al-Waahid Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾

Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi, nafunuliwa Wahy kwamba: Hakika Mwabudiwa wa haki wenu ni Ilaah Mmoja Pekee. Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende amali njema na wala asimshirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Rabb wake. [Al-Kahf (18:110)]

8-Tawakali Kwa Al-Waahid Pekee:

Tawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee katika mambo yako yote. Usikhofu chochote kitakachokupeleka katika shirki bali tawakali kwa Al-Waahid Al-Ahad. Kumbuka kisa cha Bilaal (رضي الله عنه) ambaye alikuwa ni mtumwa wa Umayyah bin Khalaf pale alipoghadhibika naye alipotambua kuwa ameacha dini yao ya kuabudu masanamu akaingia Uislamu. Akawa anamtesa Bilaal (رضي الله عنه) kwa kumweka katika jua kali bila ya chakula wala maji huku akimwekea jiwe kubwa kifuani mwake lililokaribia kumzuia pumzi. Aliendelea kumtesa kwa kuwa alimtaka amkanushe Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ili arudi katika ukafiri akimtishia kuwa atamuua pindi akikataa kumtii amri. Lakini juu ya mateso hayo, Bilaal (رضي الله عنه) alitamka maneno mazito ya kusisimua yenye kumbukumbu katika Siyrah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) nayo ni: «أَحَدٌ أَحَدٌ» (Mmoja, Mmoja Pekee). Baada ya masiku kupita Abuu Bakr (رضي الله عنه) akamnunua na kumwacha huru, na ndipo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akampa kazi tukufu kabisa ya kuadhini ambayo inashuhudia Tawhiyd ya Allaah na akawa maarufu kwa hili mpaka kwa watoto wadogo wa Kiislamu.

9-Atakayekufa Bila Kumshirikisha Al-Waahid Ataingia Jannah:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Waahid, kwamba Tawhiyd ndiyo ufunguo wa Jannah, na shirk ndiyo sababu ya kuingia motoni.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ جَابِرٍ (رضي الله عنه) قَالَ: أَتَى النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) رَجُلٌ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، مَا الْمُوجِبَتَانِ؟ فَقَالَ: ((مَنْ مَاتَ لاَ يُشْرِكُ بِاللَّهِ شَيْئًا دَخَلَ الْجَنَّةَ، وَمَنْ مَاتَ يُشْرِكُ بِاللَّهِ شَيْئًا دَخَلَ النَّارَ))

Amesimulia Jaabir (رضي الله عنه): Mtu mmoja alimjia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: Yaa Rasula-Allaah! Ni yapi mambo mawili yanayowajibisha (Jannah au moto)? Akasema: “Atakayekufa hali hamshirikishi Allaah na chochote ataingia Jannah; na atakayekufa hali anamshirikisha Allaah na chochote ataingia motoni.” [Muslim]

10-Kithirisha Dhikr Ya Kumpwekesha Al-Waahid:

Kithirisha, ee Mja wa Al-Waahid, dhikr hii ya kumpwekesha Allaah, kwani fadhila yake ni kubwa mno.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ قَالَ: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، فِي يَوْمٍ مِائَةَ مَرَّةٍ، كَانَتْ لَهُ عَدْلَ عَشْرِ رِقَابٍ، وَكُتِبَتْ لَهُ مِائَةُ حَسَنَةٍ، وَمُحِيَتْ عَنْهُ مِائَةُ سَيِّئَةٍ، وَكَانَتْ لَهُ حِرْزًا مِنَ الشَّيْطَانِ يَوْمَهُ ذَلِكَ حَتَّى يُمْسِيَ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesema:

لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Peke Yake, Hana mshirika, ni Wake ufalme na ni Zake Himdi, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza; mara mia moja kwa siku, itakuwa kwake ni sawa na kuacha huru watumwa kumi, ataandikiwa mema mia, atafutiwa maovu mia, na itakuwa kinga kwake kutokana na shaytwaan siku hiyo mpaka jioni.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Tafsiyr Atw-Twabariy, Ibn Jariyr.