Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah012 - Al-Baatwin

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 012 kati ya 103
Al-Baatwin — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Baatwin: Aliye karibu kabisa, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Yeye kwa Ujuzi Wake; Anayejua undani wa kila kitu, na Aliyefichikana na macho ya viumbe duniani.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1), pamoja na Majina Al-Awwal, Al-Aakhir na Adhw-Dhwaahir. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣﴾

Yeye Ndiye wa Awali hakuna kitu kabla Yake, na wa Mwisho hakuna kitu baada Yake, na Aliye juu hakuna kitu juu Yake, na Aliye karibu, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Yeye, Naye kwa kila kitu Ni Mjuzi. [Al-Hadiyd (57:3)]

Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amelifasiri Jina hili kwa kauli yake: “Na Wewe Ndiye Uliye karibu, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Wewe”, katika du’aa ifuatayo:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَأْمُرُنَا إِذَا أَخَذْنَا مَضْجَعَنَا أَنْ نَقُولَ: ((اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ وَرَبَّ الأَرْضِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ، فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى، وَمُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ وَالْفُرْقَانِ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَيْءٍ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ، اللَّهُمَّ أَنْتَ الأَوَّلُ فَلَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الآخِرُ فَلَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الْبَاطِنُ فَلَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ، اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ، وَأَغْنِنَا مِنَ الْفَقْرِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akituamrisha tunapolala tuseme:

اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ وَرَبَّ الأَرْضِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ، فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى، وَمُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ وَالْفُرْقَانِ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَيْءٍ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ، اللَّهُمَّ أَنْتَ الأَوَّلُ فَلَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الآخِرُ فَلَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الْبَاطِنُ فَلَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ، اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ، وَأَغْنِنَا مِنَ الْفَقْرِ

“Yaa Allaah! Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi na Rabb wa ‘Arsh adhimu, Rabb wetu na Rabb wa kila kitu, Mpasuaji wa mbegu na kokwa, Mteremshaji wa Tawraat na Injiyl na Al-Furqaan (Qur-aan); najikinga Kwako kutokana na shari ya kila kitu ambacho Wewe Umeshika utosi wake. Yaa Allaah! Wewe Ndiye wa Awali, hakuna kitu kabla Yako; na Wewe Ndiye wa Mwisho, hakuna kitu baada Yako; na Wewe Ndiye Uliye juu, hakuna kitu juu Yako; na Wewe Ndiye Uliye karibu, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Wewe. Tulipie deni, na Utukwase tuondokane na ufakiri.” [Muslim]

Maana Ya Al-Baatwin:

1-Al-Baatwin ni Yule Aliye karibu kabisa na kila kitu kwa Ujuzi Wake, Kusikia Kwake, Kuona Kwake na Uwezo Wake; hakuna kitu kilicho karibu zaidi kuliko Yeye. Ukaribu huu hauna maana kwamba Dhati Yake iko ndani ya viumbe; kwani Dhati Yake (سبحانه وتعالى) Iko juu ya mbingu, juu ya ‘Arsh, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu. Imaam Ibn Jariyr Atw-Twabariy (رحمه الله) amesema:

﴿وَالْبَاطِنُ﴾ يَقُولُ: وَهُوَ الْبَاطِنُ جَمِيعَ الْأَشْيَاءِ، فَلَا شَيْءَ أَقْرَبُ إِلَى شَيْءٍ مِنْهُ، كَمَا قَالَ: ﴿وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴾

“‘Na Al-Baatwin’: Anasema: Naye Ndiye Aliye karibu na vitu vyote kwa undani wake, hakuna kitu kilicho karibu zaidi na kitu kuliko Yeye, kama Alivyosema: ‘Na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo’.” [Tafsiyr Atw-Twabariy, Suwrah Al-Hadiyd (57:3)]

Na Aayah iliyotajwa na Imaam Atw-Twabariy ni hii:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

Na kwa yakini Tumemuumba binaadam na Tunajua yale inayowaza nafsi yake na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo. [Qaaf (50:16)]

Imaam Ibn Kathiyr (رحمه الله) amebainisha kwamba neno “Sisi” katika Aayah hii linawakusudia Malaika wa Allaah walio karibu na mwanaadam kwa Idhini ya Allaah, kama Alivyosema kuhusu mtu anayekata roho: “Nasi Tuko karibu naye zaidi kuliko nyinyi, lakini hamuoni.” Na akasema kwamba aliyeifasiri kwa Ujuzi amefanya hivyo ili kuepuka dhana ya Allaah kuingia ndani ya viumbe au kuungana navyo, na mambo hayo mawili yamekanushwa kwa Ijmaa’. Amesema:

يَعْنِي مَلَائِكَتَهُ تَعَالَى أَقْرَبُ إِلَى الْإِنْسَانِ مِنْ حَبْلِ وَرِيدِهِ إِلَيْهِ، وَمَنْ تَأَوَّلَهُ عَلَى الْعِلْمِ فَإِنَّمَا فَرَّ لِئَلَّا يَلْزَمَ حُلُولٌ أَوِ اتِّحَادٌ، وَهُمَا مَنْفِيَّانِ بِالْإِجْمَاعِ، تَعَالَى اللَّهُ وَتَقَدَّسَ

“Yaani Malaika Wake (تعالى) wako karibu zaidi na mwanaadam kuliko mshipa wake wa koo; na aliyeifasiri kwa maana ya Ujuzi, amefanya hivyo tu ili kuepuka dhana ya (Allaah) kuingia ndani (ya viumbe) au kuungana (navyo), na mambo hayo mawili yamekanushwa kwa Ijmaa’. Ametukuka Allaah na Ametakasika.” [Tafsiyr Ibn Kathiyr, Suwrah Qaaf (50:16)]

وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ ﴿٨٥﴾

Nasi Tuko karibu naye zaidi kuliko nyinyi, lakini hamuoni. [Al-Waaqi’ah (56:85)]

Na kwa hali zote mbili, maana ni sahihi: Allaah Yuko karibu na mja kwa Ujuzi Wake, na Malaika Wake wako karibu naye kwa Amri Yake, na Dhati Yake (سبحانه وتعالى) Iko juu ya ‘Arsh Yake.

2-Al-Baatwin ni Aliyefichikana na macho ya viumbe duniani, hawamwoni duniani. Lakini Waumini watamwona Siku ya Qiyaamah na Jannah, kama ilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ﴿٢٢﴾ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ﴿٢٣﴾

Nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Rabb wake. [Al-Qiyaamah (75:22-23)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ جَرِيرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه) قَالَ: كُنَّا عِنْدَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فَنَظَرَ إِلَى الْقَمَرِ لَيْلَةَ الْبَدْرِ فَقَالَ: ((إِنَّكُمْ سَتَرَوْنَ رَبَّكُمْ كَمَا تَرَوْنَ هَذَا الْقَمَرَ، لاَ تُضَامُّونَ فِي رُؤْيَتِهِ))

Amesimulia Jariyr bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه): Tulikuwa pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), akautazama mwezi usiku wa mwezi mpevu, akasema: “Hakika nyinyi mtamwona Rabb wenu kama mnavyouona mwezi huu, hamtabanana (wala kudhulumiana) katika kumwona.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Na pamoja na kuonekana Kwake, macho hayamzunguki wala hayamdiriki kikamilifu kwa sababu ya Utukufu Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٠٣﴾

Macho hayamzunguki bali Yeye Anayazunguka macho yote, Naye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-An’aam (6:103)]

3-Al-Baatwin ni Mjuzi wa mambo yaliyofichikana ndani ya nafsi na vifua; hakuna siri inayofichikana Kwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ إِن تُخْفُوا مَا فِي صُدُورِكُمْ أَوْ تُبْدُوهُ يَعْلَمْهُ اللَّـهُ ۗ وَيَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢٩﴾

Sema: Mkificha yale yaliyomo katika vifua vyenu au mkiyafichua, Allaah Anayajua. Na Anajua yale yaliyomo katika mbingu na yale yaliyomo katika ardhi. Na Allaah Ni Muweza wa kila kitu. [Aal-‘Imraan (3:29)]

Na Anasema pia:

يَعْلَمُ خَائِنَةَ الْأَعْيُنِ وَمَا تُخْفِي الصُّدُورُ﴿١٩﴾

(Allaah) Anajua khiyana za macho na yale yanayoficha vifua. [Ghaafir (40:19)]

4-Na katika Neema Zake zilizoenea ni zile zilizo dhahiri na zilizofichikana ambazo waja hawazijui. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَلَمْ تَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَأَسْبَغَ عَلَيْكُمْ نِعَمَهُ ظَاهِرَةً وَبَاطِنَةً ۗ وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلَا هُدًى وَلَا كِتَابٍ مُّنِيرٍ ﴿٢٠﴾

Je, hamuoni kwamba Allaah Amekutiishieni vile vilivyomo mbinguni na vile vilivyomo ardhini, na Akakutimizieni kitimilifu Neema Zake kwa dhahiri na siri? Na miongoni mwa watu, wako wanaobishana kuhusu Allaah bila ya ilimu yoyote ile, na bila ya mwongozo wowote ule, na bila ya kitabu chochote kile chenye nuru. [Luqmaan (31:20)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Baatwin:

1-Amini Ukaribu Wa Allaah Kwa Ujuzi Wake Pamoja Na Kuwa Kwake Juu Ya ‘Arsh:

Majina mawili Adhw-Dhwaahir na Al-Baatwin yanakusanya ‘Uluwa wa Allaah na ukaribu Wake; Yeye Yuko juu ya kila kitu, na Yuko karibu na kila kitu kwa Ujuzi Wake. Ukaribu Wake hauzuii ‘Uluwa Wake, wala ‘Uluwa Wake hauzuii ukaribu Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٤﴾

Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arsh. Anajua yale yanayoingia ardhini, na yale yatokayo humo, na yale yanayoteremka kutoka mbinguni, na yale yanayopanda humo. Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah Ni Mwenye Kuona yote myatendayo. [Al-Hadiyd (57:4)]

2-Mwombe Allaah Kwa Yakini Kwamba Yuko Karibu Na Anaitikia:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Baatwin, kwamba Allaah Yuko karibu kwa Ujuzi Wake na Anaitikia; basi mwombe kwa yakini.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza Waja Wangu kuhusu Mimi, basi (waambie) hakika Mimi Niko Karibu (kwa ujuzi). Naitikia duaa ya muombaji anaponiomba. Hivyo basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah (2:186)]

3-Safisha Nia Yako Na Moyo Wako, Kwani Al-Baatwin Anajua Yaliyomo Ndani Yake:

Al-Baatwin Anajua yaliyomo ndani ya kifua chako kuliko unavyojijua mwenyewe; basi tengeneza ndani yako kama unavyotengeneza nje yako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((إِنَّمَا الأَعْمَالُ بِالنِّيَّاتِ، وَإِنَّمَا لِكُلِّ امْرِئٍ مَا نَوَى))

Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Hakika amali (zinalipwa) kwa niya, na hakika kila mtu atapata kile alichokinuia.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

4-Mche Al-Baatwin Katika Wasiwasi Wa Nafsi Na Mawazo Ya Moyo:

Al-Baatwin Anajua hata yale ambayo nafsi inayawaza; basi usiyaendekeze mawazo mabaya. Na katika Rehma Yake ni kwamba Hamchukulii mja kwa wasiwasi wa nafsi asioutamka wala kuutenda. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ تَجَاوَزَ عَنْ أُمَّتِي مَا حَدَّثَتْ بِهِ أَنْفُسَهَا، مَا لَمْ تَعْمَلْ أَوْ تَتَكَلَّمْ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ameusamehe Ummah wangu yale ambayo nafsi zao zinayawaza, maadamu hawajayatenda wala kuyazungumza.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Tamani Kumwona Rabb Wako Katika Jannah, Na Jiandae Kwa Swalaah:

Tamani, ee Mja wa Al-Baatwin, neema kubwa kabisa ya Jannah, nayo ni kumwona Rabb wako.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliunganisha kumwona Allaah Aakhirah na kuhifadhi Swalaah mbili, akasema katika Hadiyth ya Jariyr iliyotangulia: “Basi mkiweza kutoshindwa kuswali kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuzama kwake, fanyeni.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]. Basi hifadhi Swalaah ya Alfajiri na Alasiri.

6-Mshukuru Allaah Kwa Neema Zake Zilizofichikana:

Tambua, ee Mja wa Al-Baatwin: Neema nyingi za Allaah juu yako hujazijua: shari Alizokuepusha nazo, maradhi Aliyokukinga nayo, na hatari usizozijua. Basi Mshukuru kwa Neema zote, zilizo dhahiri na zilizofichikana; rejea Luqmaan (31:20) juu.

7-Jitahidi Katika Amali Za Siri Zinazojulikana Na Al-Baatwin Pekee:

Tambua kwamba amali ya siri ni dalili ya ikhlaasw, kwa sababu haikusudiwi isipokuwa Allaah. Miongoni mwa watu saba watakaofunikwa na kivuli cha Al-Baatwin ni:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((سَبْعَةٌ يُظِلُّهُمُ اللَّهُ فِي ظِلِّهِ يَوْمَ لاَ ظِلَّ إِلاَّ ظِلُّهُ ... وَرَجُلٌ تَصَدَّقَ بِصَدَقَةٍ فَأَخْفَاهَا حَتَّى لاَ تَعْلَمَ شِمَالُهُ مَا تُنْفِقُ يَمِينُهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu saba Allaah Atawafunika kwa kivuli Chake Siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa kivuli Chake: … na mtu aliyetoa swadaqah akaificha, mpaka mkono wake wa kushoto usijue kile ulichotoa mkono wake wa kulia.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

8-Usiwe Na Sura Mbili; Ndani Na Nje Yako Viwe Sawa:

Mnafiki hudhihirisha kinyume cha anachokificha, na Al-Baatwin Anajua yote. Basi Muumini huwa na ndani iliyo bora kuliko nje yake. Rejea Ghaafir (40:19) juu: “(Allaah) Anajua khiyana za macho na yale yanayoficha vifua.”

9-Usiwahukumu Watu Kwa Nia Zao, Kwani Hayo Ni Ya Al-Baatwin:

Tambua kwamba siri za nyoyo zinajulikana na Al-Baatwin Pekee; basi wahukumu watu kwa yale yaliyo dhahiri kwao, na mwachie Allaah siri zao. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimkemea Usaamah bin Zayd (رضي الله عنهما) alipomuua mtu aliyetamka Kalimah ya Tawhiyd akidhani kuwa ameisema kwa khofu, akamwambia:

عَنْ أُسَامَةَ بْنِ زَيْدٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: ... فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَقَالَ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَقَتَلْتَهُ؟)) قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّمَا قَالَهَا خَوْفًا مِنَ السِّلاَحِ. قَالَ: ((أَفَلاَ شَقَقْتَ عَنْ قَلْبِهِ حَتَّى تَعْلَمَ أَقَالَهَا أَمْ لاَ))

Amesimulia Usaamah bin Zayd (رضي الله عنهما): … Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Je, alisema: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ, nawe ukamuua?” Nikasema: Yaa Rasula-Allaah! Hakika aliisema kwa kuogopa silaha. Akasema: “Je, uliupasua moyo wake ukajua kama aliisema (kwa ukweli) au la?” [Muslim]

10-Mpende Allaah Aliye Karibu Nawe Kuliko Kila Kitu:

Kumwabudu Allaah kwa Jina Lake Al-Baatwin ni kumpenda kwa mapenzi ya kweli, kwa kutambua kwamba Yuko karibu nawe kwa Ujuzi Wake, Anasikia du’aa yako, Anaona hali yako, na Anajua haja yako kabla hujaitamka; pamoja na kuwa Yeye Yuko juu ya kila kitu.

11-Dumisha Du’aa Ya Kulala Inayomtaja Allaah Kwa Jina Lake Al-Baatwin:

Tambua, ee Mja wa Al-Baatwin: Soma du’aa iliyotajwa juu kila unapokwenda kulala. Rejea Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) juu.

Na Allaah Mjuzi zaidi