Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 014 kati ya 103
Al-Ahad — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Ahad: Mmoja Pekee Asiye Na Kifano

Allaah (سبحانه وتعالى) ni Mmoja Pekee, Hana mshirika, Hakuzaa wala Hakuzaliwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ ﴿١﴾ اللَّـهُ الصَّمَدُ ﴿٢﴾ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ﴿٣﴾ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ﴿٤﴾

Sema: Yeye Allaah Ni Mmoja Pekee. Allaah Aliyekamilika Sifa za Utukufu Wake, Mkusudiwa haja zote. Hakuzaa wala Hakuzaliwa. Na wala haiwi Awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye. [Al-Ikhlaasw (112:1-4)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ ۖ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾

Na sema: “AlhamduliLLaah Kuhimidiwa ni kwa Allaah Ambaye Hakujifanyia mwana na wala Hakuwa na mshirika katika ufalme, na wala Hakuwa dhalili hata Awe (Anahitaji) mlinzi, msaidizi; basi mtukuze matukuzo makubwa kabisa (Sema Allaahu Akbar!)” [Al-Israa (17:111)]

Jina hili la Allaah Al-Ahad limetajwa katika Qur-aan mara moja tu, nalo ni katika Suwrah Al-Ikhlaasw. Rejea juu: Al-Ikhlaasw (112:1-4).

Ni Mmoja Pekee na Atabaki kuwa Pekee na Hatakuwa na mwengine pamoja Naye.1

Baadhi ya ‘Ulamaa wametofautisha baina ya Al-Waahid na Al-Ahad wakasema kwamba: ‘Waahid’ inawezekana kukatika/kugawika katika mbili na zaidi. Mfano husemwa: Waahid (moja), ithnaan (mbili), thalaathah (tatu). Ama ‘Ahad’ maana yake ya kiasili ni kuwa haiwezekani kugawika katika mbili au zaidi; hivyo husemwa: ‘Ahad’ (moja pekee) na haisemwi: ‘ahad, ithnaan, thalaathah’ n.k. Na wakasema pia: ‘Al-Waahid’ Ni Mmoja Pekee katika/kwa dhati Yake. Ama ‘Ahad’ Ni Mmoja Pekee katika dhati Yake na Sifa Zake.2

Hivyo basi Allaah (سبحانه وتعالى) ni Al-Waahid, Al-Ahad Ambaye hakuna wa pili Naye, wala Hana mshirika, wala mfano Wake. Naye (سبحانه وتعالى) Ambaye Waja Wake wote wanamtegemea Yeye, na wanamkusudia Yeye kwa kila jambo na wala hawatawakali kwa yeyote isipokuwa Kwake Yeye.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Ahad:

1-Tambua Kwamba Al-Ahad Hana Anayefanana Naye Katika Dhati Yake, Sifa Zake Wala Matendo Yake:

Al-Ahad Ni Mmoja Pekee Asiye na mfano; hakuna kitu kinachofanana Naye kwa namna yoyote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ۖ يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾

Mwanzilishi wa mbingu na ardhi. Amekujaalieni kutokana na nafsi zenu mume na mke, na katika wanyama wa mifugo dume na jike. Anakusambazeni humo. Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:11)]

2-Al-Ahad Hana Mshirika Katika Ufalme Wake:

Tambua, ee Mja wa Al-Ahad: Kama Alivyo Mmoja katika Dhati Yake, ndivyo Alivyo Mmoja katika ufalme na uendeshaji wa ulimwengu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ ۖ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾

Na sema: AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Ambaye Hakujifanyia mwana na wala Hakuwa na mshirika katika ufalme, na wala Hakuwa dhalili hata Awe (Anahitaji) mlinzi (na msaidizi), na mtukuze matukuzo makubwa kabisa. [Al-Israa (17:111)]

3-Upweke Wa Allaah Katika Uumbaji Unalazimisha Kumpwekesha Katika ‘Ibaadah:

Tambua kwamba lau kungekuwa na waabudiwa wengine pamoja na Al-Ahad, mbingu na ardhi zingeharibika; na kuwa kwake Mmoja katika kuumba na kuendesha ni dalili kwamba Yeye Pekee Ndiye Anayestahiki kuabudiwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّـهُ لَفَسَدَتَا ۚ فَسُبْحَانَ اللَّـهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٢٢﴾

Lau wangelikuweko humo (mbinguni na ardhini) waabudiwa badala ya Allaah, bila shaka zingelifisidika. Basi Subhaana Allaah! Utakasifu ni wa Allaah Rabb wa ‘Arsh kutokana na ambayo wanavumisha. [Al-Anbiyaa (21:22)]

4-Kithirisha Kutamka Neno La Tawhiyd:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Ahad, kutamka kwa wingi neno la Tawhiyd, ambalo ni maneno yanayotajwa katika Adhaan na Iqaamah za Swalaah, na ufanyie kazi maana yake; pamoja na dhikr za baada ya Swalaah za faradhi na nyinginezo. Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amebainisha fadhila kubwa ya kulitamka:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ قَالَ: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، فِي يَوْمٍ مِائَةَ مَرَّةٍ، كَانَتْ لَهُ عَدْلَ عَشْرِ رِقَابٍ، وَكُتِبَتْ لَهُ مِائَةُ حَسَنَةٍ، وَمُحِيَتْ عَنْهُ مِائَةُ سَيِّئَةٍ، وَكَانَتْ لَهُ حِرْزًا مِنَ الشَّيْطَانِ يَوْمَهُ ذَلِكَ حَتَّى يُمْسِيَ، وَلَمْ يَأْتِ أَحَدٌ بِأَفْضَلَ مِمَّا جَاءَ بِهِ إِلاَّ أَحَدٌ عَمِلَ أَكْثَرَ مِنْ ذَلِكَ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesema:

لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Peke Yake, Hana mshirika, ni Wake ufalme na ni Zake Himdi, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza; mara mia moja kwa siku, itakuwa kwake sawa na kuwaacha huru watumwa kumi, na ataandikiwa mema mia moja, na atafutiwa maovu mia moja, na itakuwa kwake kinga dhidi ya shaytwaan siku yake hiyo mpaka ifike jioni; wala hatakuja yeyote na kilicho bora kuliko alichokuja nacho, isipokuwa mtu aliyefanya zaidi ya hivyo.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Mfanye Moyo Wako Umwelekee Mmoja Pekee:

Tambua kwamba Mja anayemwabudu Al-Ahad Pekee ana moyo uliotulia, tofauti na anayegawanya moyo wake kati ya waabudiwa wengi. Allaah Amepiga mfano wa watumwa wawili:

ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا رَّجُلًا فِيهِ شُرَكَاءُ مُتَشَاكِسُونَ وَرَجُلًا سَلَمًا لِّرَجُلٍ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا ۚ الْحَمْدُ لِلَّـهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٢٩﴾

Allaah Amepiga mfano wa mtu aliye chini ya washirika wagombanao, na mtu mwengine aliye pweke na bwana mmoja tu. Je, wanalingana sawa kwa hali zao? AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah). Bali wengi wao hawajui. [Az-Zumar (39:29)]

6-Kuwa Na Ikhlaasw Katika Amali Zako Zote:

Tambua, ee Mja wa Al-Ahad: Kuwa na ikhlaasw; kumsafishia niyyah Allaah (سبحانه وتعالى) katika ‘amali zako zote kwa kuwa hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki ila Yeye, wala kuadhimishwa isipokuwa Yeye wala kutiiwa/utiifu/twaa’ah isipokuwa Yeye wala kuridhishwa isipokuwa Yeye. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٦٣﴾

Sema: “Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafaara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah (Pekee) Rabb wa walimwengu. Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza.” [Al-An’aam (6:162-163)]

7-Jiepushe Na Riyaa, Kwani Al-Ahad Hakubali Amali Iliyoshirikishwa:

Tambua, ee Mja wa Al-Ahad: Katika Hadiyth Al-Qudsiy, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَنَا أَغْنَى الشُّرَكَاءِ عَنِ الشِّرْكِ، مَنْ عَمِلَ عَمَلاً أَشْرَكَ فِيهِ مَعِي غَيْرِي تَرَكْتُهُ وَشِرْكَهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (تبارك وتعالى) Amesema: Mimi Ni Mkwasi zaidi kuliko washirika wote kutokana na kushirikishwa. Atakayefanya amali akanishirikisha ndani yake na mwingine asiyekuwa Mimi, Nitamwacha yeye na shirki yake.” [Muslim]

8-Simama Imara Katika Tawhiyd Wakati Wa Mitihani, Kama Alivyosimama Bilaal (رضي الله عنه):

Tambua, ee Mja wa Al-Ahad: Bilaal (رضي الله عنه) alipoteswa na washirikina wa Makkah ili aache Uislamu, alikuwa akikariri: “Ahad! Ahad!” (Mmoja! Mmoja!):

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ أَوَّلَ مَنْ أَظْهَرَ إِسْلاَمَهُ سَبْعَةٌ ... وَأَمَّا سَائِرُهُمْ فَأَخَذَهُمُ الْمُشْرِكُونَ، وَأَلْبَسُوهُمْ أَدْرَاعَ الْحَدِيدِ، وَصَهَرُوهُمْ فِي الشَّمْسِ، فَمَا مِنْهُمْ مِنْ أَحَدٍ إِلاَّ وَقَدْ وَاتَاهُمْ عَلَى مَا أَرَادُوا، إِلاَّ بِلاَلاً، فَإِنَّهُ هَانَتْ عَلَيْهِ نَفْسُهُ فِي اللَّهِ، وَهَانَ عَلَى قَوْمِهِ، فَأَخَذُوهُ فَأَعْطَوْهُ الْوِلْدَانَ، فَجَعَلُوا يَطُوفُونَ بِهِ فِي شِعَابِ مَكَّةَ، وَهُوَ يَقُولُ: أَحَدٌ أَحَدٌ

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Wa kwanza kudhihirisha Uislamu wao walikuwa saba… Ama wengineo, washirikina waliwakamata, wakawavisha mavazi ya chuma, na wakawaunguza juani. Hakuna yeyote kati yao isipokuwa aliwakubalia (kwa ulimi) walichotaka, isipokuwa Bilaal. Hakika nafsi yake ilikuwa nyepesi kwake katika Njia ya Allaah, na alikuwa dhalili kwa kaumu yake; wakamkamata wakawapa watoto, nao wakawa wanamzungusha katika mabonde ya Makkah, naye akisema: Ahad! Ahad! (Mmoja! Mmoja!) [Ibn Maajah (150), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Ibn Maajah (122)]

9-Tumia Kidole Kimoja Katika Tashahhud Na Du’aa Kwa Kuashiria Upweke Wa Allaah:

Kumbuka kuashiria kwa kidole kimoja katika Tashahhud na du’aa, kama alama ya upweke wa Al-Ahad.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona mtu akiashiria kwa vidole viwili katika du’aa, akamfundisha kuashiria kwa kimoja:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَجُلاً كَانَ يَدْعُو بِإِصْبَعَيْهِ، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَحِّدْ أَحِّدْ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba mtu mmoja alikuwa akiomba du’aa kwa kuashiria kwa vidole vyake viwili, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia: “Ashiria kwa kimoja! Ashiria kwa kimoja!” [At-Tirmidhiy (3557), An-Nasaaiy (1271), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan Swahiyh katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

10-Soma Suwrah Al-Kaafiruwn Na Al-Ikhlaasw Katika Rakaa Mbili Za Sunnah Ya Alfajiri:

Tambua kwamba Suwrah mbili hizi zinaitwa Suwrah za Ikhlaasw, kwani ya kwanza inajitenga na shirk, na ya pili inathibitisha upweke wa Al-Ahad:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَرَأَ فِي رَكْعَتَيِ الْفَجْرِ: ﴿قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ﴾ وَ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisoma katika Rakaa mbili (za Sunnah) za Alfajiri: ﴿قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ﴾ na ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾. [Muslim]

11-Muombe Al-Ahad Asw-Swamad Akughufurie:

Omba du’aa hii katika Tashahhud yako, ukimwomba Al-Ahad Asw-Swamad Akughufurie.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimsikia mtu akiomba kwa du’aa ifuatayo katika Tashahhud yake, akasema mara tatu kwamba ameghufuriwa:

عَنْ مِحْجَنِ بْنِ الأَدْرَعِ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) دَخَلَ الْمَسْجِدَ، فَإِذَا هُوَ بِرَجُلٍ قَدْ قَضَى صَلاَتَهُ وَهُوَ يَتَشَهَّدُ وَهُوَ يَقُولُ: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ يَا اللَّهُ بِأَنَّكَ الْوَاحِدُ الأَحَدُ الصَّمَدُ، الَّذِي لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ، وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ، أَنْ تَغْفِرَ لِي ذُنُوبِي، إِنَّكَ أَنْتَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((قَدْ غُفِرَ لَهُ، قَدْ غُفِرَ لَهُ، قَدْ غُفِرَ لَهُ))

Amesimulia Mihjan bin Al-Adra’ (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliingia Msikitini, akamkuta mtu amemaliza Swalaah yake akiwa katika Tashahhud, akisema:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ يَا اللَّهُ بِأَنَّكَ الْوَاحِدُ الأَحَدُ الصَّمَدُ، الَّذِي لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ، وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ، أَنْ تَغْفِرَ لِي ذُنُوبِي، إِنَّكَ أَنْتَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba, Yaa Allaah, kwa kuwa Wewe Ndiye Mmoja, Al-Ahad, Asw-Swamad, Ambaye Hakuzaa wala Hakuzaliwa, wala hakuna yeyote anayelingana Naye, Unighufurie madhambi yangu; hakika Wewe Ndiye Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ameghufuriwa! Ameghufuriwa! Ameghufuriwa!” [Abuu Daawuwd (985), An-Nasaaiy (1300), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1An-Nihaayah Fiy Ghariyb Al-Hadiyth (1/35).
  • 2Tafsiyr Asmaa Allaah Al-Husnaa.