Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 002 kati ya 103
Ilaah — Majina Mazuri ya Allaah

Ilaah: Muabudiwa wa Haki; Anayestahiki Kuabudiwa Pekee

Ilaah ni Mwenye kustahiki kuabudiwa, na Mwenye kuabudiwa kwa mapenzi, kwa kujidhalilisha Kwake, kwa kumkhofu, kwa kumtaraji na kwa kumtukuza kwa utiifu, kwa sababu Yeye Ndiye Anayeabudiwa kwa haki. Hivyo kila chenye kuabudiwa badala Yake, chini ya ‘Arsh Yake hadi ardhini, ni baatwil.

Na Sifa ya Uluwhiyyah (الأُلُوهِيَّة) imethibiti kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kutokana na Majina Yake mawili: Allaah na Al-Ilaah.

Jina hili limetajwa katika Qur-aan katika sehemu nyingi mno, khaswa katika Kalimah ya Tawhiyd: لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ. Miongoni mwa Aayaat hizo ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴿١٦٣﴾

Na Ilaah wenu (Allaah) ni Ilaah Mmoja, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu. [Al-Baqarah (2:163)]

Na Anasema (سبحانه وتعالى):

قُلْ إِنَّمَا يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٠٨﴾

Sema: Hakika nimefunuliwa Wahy kwamba: Mwabudiwa wenu wa haki ni Ilaah Mmoja. Basi je, nyinyi mumesilimu? [Al-Anbiyaa (21:108)]

Na Anasema (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَـٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَـٰهٌ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ﴿٨٤﴾

Na Yeye Ndiye Muabudiwa wa haki mbinguni na ardhini pia (Ndiye Huyo Huyo) Ilaah. Naye Ndiye Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. [Az-Zukhruf (43:84)]

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah amesema: Katika kauli: لَا إِلَٰهَ إِلَّا أَنْتَ kuna kuthibitisha Upweke Wake na Uluwhiyyah Wake, na Uluwhiyyah Wake unathibitisha wema Wake kwa Waja Wake. Na Ilaah Ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa; na kwa kuwa Anastahiki kuabudiwa, basi Yeye Ni kama Alivyojisifu kwa Sifa Zake zinazolazimu Apendwe mapenzi yote hadi kilele cha mapenzi, na Anyenyekewe hadi kilele cha unyenyekevu; kwani ‘ibaadah inakusanya kilele cha mapenzi pamoja na kilele cha unyenyekevu.1

Tofauti Baina Ya Ilaah Na Ar-Rabb:

Jina la Ilaah linatofautiana maana yake na Jina la Ar-Rabb katika mambo kadhaa, miongoni mwayo ni:

1-Ar-Rabb maana yake inarejea katika kupwekeka katika kuumba, kumiliki na kuendesha mambo. Ama Ilaah, ni Ambaye Anastahiki kuabudiwa, Ambaye nyoyo zinamtukuza na kumnyenyekea kwa mapenzi na taadhima, Mwenye kustahiki ‘ibaadah kwa aina zake zote.

2-Jina la Ilaah linakusanya lengo la mja na mwisho wake, na kile alichoumbiwa, nacho ni kumwabudu Allaah. Ama Jina la Ar-Rabb linakusanya kuumbwa kwa mja na mwanzo wake, kwamba Allaah Ndiye Anayemlea na kumtawalia mambo yake.2 Na ndio maana da’wah ya Rusuli ilianza kwa kuamrisha ‘ibaadah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿٢١﴾

Enyi watu! Mwabuduni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni, na wale wa kabla yenu, mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah (2:21)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنِ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((أُمِرْتُ أَنْ أُقَاتِلَ النَّاسَ حَتَّى يَشْهَدُوا أَنْ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ، وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ، وَيُقِيمُوا الصَّلاَةَ، وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ، فَإِذَا فَعَلُوا ذَلِكَ عَصَمُوا مِنِّي دِمَاءَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ إِلاَّ بِحَقِّ الإِسْلاَمِ، وَحِسَابُهُمْ عَلَى اللَّهِ))

Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Nimeamrishwa nipigane na watu mpaka washuhudie kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, na wasimamishe Swalaah, na watoe Zakaah. Watakapofanya hayo, watakuwa wamezihifadhi damu zao na mali zao kutoka kwangu isipokuwa kwa haki ya Uislamu, na hesabu yao iko kwa Allaah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Na hakusema: Mpaka washuhudie kwamba hapana Rabb isipokuwa Allaah; kwani Jina la Allaah (lenye maana ya Ilaah) linaonyesha zaidi lengo la ‘ibaadah ambalo kwalo viumbe wameumbwa, na kwalo wameamrishwa.3

3-Jina la Ar-Rabb linastahiki zaidi katika hali ya kuomba msaada na kuomba haja; ndio maana du’aa nyingi za Manabii (عليهم السلام) katika Qur-aan zimeanza kwa: رَبِّ au رَبَّنَا. Ama Jina la Ilaah, linastahiki zaidi katika hali ya ‘ibaadah, kujisalimisha na kurejea Kwake.

4-Viumbe kukiri Rubuwbiyyah (Uola) wa Allaah kumetangulia kukiri kwao Uluwhiyyah Yake. Hata washirikina walikiri kwamba Allaah Ndiye Muumbaji, lakini walikanusha kumpwekesha katika ‘ibaadah. Ndio maana Rusuli wote walikuja kulingania Tawhiyd ya Uluwhiyyah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ ﴿٢٥﴾

Na Hatukutuma kabla yako Rasuli yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: Hakika hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi, basi Niabuduni. [Al-Anbiyaa (21:25)]

Tofauti Baina Ya Allaah Na Ilaah:

Ilaah ni wasifu ambao washirikina walimshirikisha nao Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuwaabudu baadhi ya viumbe kama jua, mwezi na sayari; lakini hawakufanya hivyo kwa Jina la Allaah, wala hawakumwita yeyote kwalo.4 Ndio maana waliviita vitu walivyoviabudu kuwa ni ‘Aalihah’ (waabudiwa), na Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaraddi kwamba hao hawawezi kuwanusuru. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَلَوْلَا نَصَرَهُمُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ قُرْبَانًا آلِهَةً ۖ بَلْ ضَلُّوا عَنْهُمْ ۚ وَذَٰلِكَ إِفْكُهُمْ وَمَا كَانُوا يَفْتَرُونَ﴿٢٨﴾

Basi kwa nini wasiwanusuru wale waliowafanya badala ya Allaah kuwa ni waabudiwa wa kikurubisho (Kwake)? Bali wamewapotea, na huo ndio uongo wao na yale waliyokuwa wakiyatunga. [Al-Ahqaaf (46:28)]

Na lau wangelikuweko waabudiwa wengine mbinguni na ardhini badala ya Allaah, basi mbingu na ardhi zingelifisidika. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّـهُ لَفَسَدَتَا ۚ فَسُبْحَانَ اللَّـهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٢٢﴾

Lau wangelikuweko humo (mbinguni na ardhini) waabudiwa badala ya Allaah, bila shaka zingelifisidika. Basi Subhaana Allaah! Utakasifu ni wa Allaah Rabb wa ‘Arsh kutokana na ambayo wanavumisha. [Al-Anbiyaa (21:22)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ilaah:

1-Tambua Maana Ya لَا إِلَٰهَ إِلَّا اللَّهُ Kabla Ya Kuitamka:

Kumbuka, ee Mja wa Ilaah, kwamba maana ya Kalimah ya Tawhiyd ni: Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah; na kila kinachoabudiwa badala Yake ni baatwil. Basi jifunze maana yake na yale inayoyalazimu, kwani manufaa yake ni kwa mwenye kuitamka huku akiijua. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عُثْمَانَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنْ مَاتَ وَهُوَ يَعْلَمُ أَنَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ دَخَلَ الْجَنَّةَ))

Amesimulia ‘Uthmaan (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayekufa huku anajua kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, ataingia Jannah.” [Muslim]

2-Tambua Kwamba Tawhiyd Ya ‘Ibaadah Ndilo Lengo La Kuumbwa Kwako:

Allaah Hakuwaumba majini na wanaadam isipokuwa ili wamwabudu Yeye Pekee; hilo ndilo lengo la uhai wako na ndiyo maana ya kumjua Ilaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

Na Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. [Adh-Dhaariyaat (51:56)]

3-Manabii Wote Walitumwa Kwa Ujumbe Mmoja: Hapana Ilaah Isipokuwa Allaah:

Da’wah ya Manabii wote tangu wa kwanza mpaka wa mwisho ilikuwa ni kumpwekesha Ilaah katika ‘ibaadah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ ﴿٢٥﴾

Na Hatukutuma kabla yako Rasuli yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: Hakika hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi, basi Niabuduni. [Al-Anbiyaa (21:25)]

4-Mpwekeshe Ilaah Katika ‘Ibaadah Zako Zote Na Jitenge Na Kila Kinachoabudiwa Badala Yake:

Tambua kwamba Kalimah ya Tawhiyd ina nguzo mbili: kukanusha (لَا إِلَٰهَ) kila kinachoabudiwa badala ya Ilaah, na kuthibitisha (إِلَّا اللَّهُ) ‘ibaadah kwa Allaah Pekee. Na hivyo ndivyo alivyofanya Nabiy Ibraahiym (عليه السلام). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاءٌ مِّمَّا تَعْبُدُونَ﴿٢٦﴾ إِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي فَإِنَّهُ سَيَهْدِينِ﴿٢٧﴾ وَجَعَلَهَا كَلِمَةً بَاقِيَةً فِي عَقِبِهِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ﴿٢٨﴾

Na pale Ibraahiym alipomwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi nimejitoa katika dhima na yale mnayoyaabudu. Isipokuwa kwa Ambaye Ameniumba, basi hakika Yeye Ataniongoza. Na akalifanya neno (laa ilaaha illaa-Allaah) lenye kubakia katika kizazi chake ili wapate kurejea. [Az-Zukhruf (43:26-28)]

5-Jiepushe Na Shirk Kwani Ndiyo Dhambi Kubwa Kabisa Isiyoghufuriwa:

Kumfanyia Allaah mshirika katika ‘ibaadah ndio kinyume cha maana ya Ilaah, na ni dhambi ambayo Allaah Haighufurii kwa atakayekufa nayo bila kutubu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa, lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakaye. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu kabisa. [An-Nisaa (4:48)]

6-Tawhiyd Ndiyo Amani Na Uongofu Wa Kweli:

Tambua, ee Mja wa Ilaah: Tawhiyd ndiyo sababu ya amani na uongofu duniani na Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٨٢﴾

Wale walioamini na hawakuchanganya imaan zao na dhulma, hao ndio watakaopata amani nao ndio waliohidika. [Al-An’aam (6:82)]

Na Swahaba walipoteremshiwa Aayah hii waliona uzito wake, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akawabainishia kwamba dhulma inayokusudiwa ni shirk:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: لَمَّا نَزَلَتْ: ﴿الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُمْ بِظُلْمٍ﴾ قَالَ أَصْحَابُ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): أَيُّنَا لَمْ يَظْلِمْ؟ فَأَنْزَلَ اللَّهُ: ﴿إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ﴾

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Ilipoteremka Aayah: “Wale walioamini na hawakuchanganya imaan yao na dhulma”, Swahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) walisema: Nani kati yetu ambaye hajadhulumu? Allaah Akateremsha: “Hakika shirki ni dhulma kubwa mno!” [Al-Bukhaariy]

7-Wausie Watoto Wako Kumwabudu Ilaah Mmoja Pekee:

Tambua, ee Mja wa Ilaah, kwamba wasiya mkubwa kabisa unaoweza kuwaachia watoto wako ni Tawhiyd, kama walivyofanya Manabii (عليهم السلام). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَمْ كُنتُمْ شُهَدَاءَ إِذْ حَضَرَ يَعْقُوبَ الْمَوْتُ إِذْ قَالَ لِبَنِيهِ مَا تَعْبُدُونَ مِن بَعْدِي قَالُوا نَعْبُدُ إِلَـٰهَكَ وَإِلَـٰهَ آبَائِكَ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ ﴿١٣٣﴾

Je, mlikuwa mashahidi wakati mauti yalipomfikia Ya’quwb pale alipowaambia wanawe: Mtaabudu nini baada yangu? Wakasema: Tutamwabudu Ilaaha wako (Allaah) na Ilaaha wa baba zako Ibraahiym na Ismaa’iyl na Is-haaq; Ilaaha Mmoja, nasi ni Waislamu (Wenye kujisalimisha) Kwake. [Al-Baqarah (2:133)]

8-Mpende Ilaah Kuliko Kila Kitu, Kwani Kumwabudu Ni Kumpenda Na Kumnyenyekea:

Maana ya Ilaah ni Yule Anayeabudiwa kwa mapenzi makubwa kabisa pamoja na unyenyekevu na utukufu; basi mapenzi ya Waumini kwa Allaah ni makubwa kuliko mapenzi ya washirikina kwa waabudiwa wao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ ۗ وَلَوْ يَرَى الَّذِينَ ظَلَمُوا إِذْ يَرَوْنَ الْعَذَابَ أَنَّ الْقُوَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا وَأَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعَذَابِ ﴿١٦٥﴾

Na miongoni mwa watu wako wenye kuwafanya viumbe miungu badala ya Allaah, wanawapenda kama kumpenda Allaah. Na wale walioamini wana mapenzi zaidi kwa Allaah. Na lau wale waliodhulumu wangelitambua watakapoona adhabu, kwamba nguvu zote ni za Allaah, na kwamba hakika Allaah ni Mkali wa Kuadhibu, (basi wasingelimfanyia Allaah washirika). [Al-Baqarah (2:165)]

9-Usimwombe Wala Usimtegemee Asiyekuwa Allaah:

Kila kinachoabudiwa badala ya Allaah hakimiliki manufaa wala dhara, na hakisikii wala hakiitikii du’aa. Basi elekeza du’aa zako na tawakkul yako kwa Ilaah wa haki Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ﴿٥﴾

Na nani aliyepotoka zaidi kuliko yule anayeomba asiyekuwa Allaah ambaye hamuitikii mpaka Siku ya Qiyaamah? Nao wala hawatambui maombi yao! [Al-Ahqaaf (46:5)]

10-Kithirisha Kusema: لَا إِلَٰهَ إِلَّا اللَّهُ, Kwani Ndiyo Dhikr Bora Kabisa:

Tambua, ee Mja wa Ilaah: Ulainishe ulimi wako kwa Kalimah ya Tawhiyd katika kila hali, kwani ndiyo dhikr bora kabisa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنهما) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((أَفْضَلُ الذِّكْرِ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ، وَأَفْضَلُ الدُّعَاءِ الْحَمْدُ لِلَّهِ))

Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Dhikr bora kabisa ni:

لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ

Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah.

Na du’aa bora kabisa ni:

الْحَمْدُ لِلَّهِ

Himdi Anastahiki Allaah.” [At-Tirmidhiy (3383), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3383)]

11-Wakumbushe Walio Karibu Na Mauti Kalimah Ya Tawhiyd, Na Ijaalie Kuwa Maneno Yako Ya Mwisho:

Tambua, ee Mja wa Ilaah: Kalimah ya Tawhiyd iwe ndiyo maneno ya mwisho ya Muislamu, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametuamrisha kuwatamkisha walio karibu na mauti:

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((لَقِّنُوا مَوْتَاكُمْ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ))

Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Wafundisheni (wakumbusheni kutamka) walio karibu kufa: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ (Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah).” [Muslim]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنْ كَانَ آخِرُ كَلاَمِهِ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ دَخَلَ الْجَنَّةَ))

Amesimulia Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ambaye maneno yake ya mwisho yatakuwa ni: Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, ataingia Jannah.” [Abuu Daawuwd (3116), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]

12-Omba Du’aa Kwa Kutawassal Kwa Kalimah Ya Tawhiyd:

Tambua kwamba unapofikwa na shida au janga, muombe Ilaah kwa kumpwekesha katika Uluwhiyyah Wake, kama alivyoomba Nabiy Yuwnus (عليه السلام). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾

Na Dhan-Nuwn (Yuwnus), alipoondoka akiwa ameghadhibika, akadhani kwamba Hatutamdhikisha. Akaita vizani kwamba: Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu. [Al-Anbiyaa (21:87)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ سَعْدِ بْنِ أَبِي وَقَّاصٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((دَعْوَةُ ذِي النُّونِ إِذْ دَعَا وَهُوَ فِي بَطْنِ الْحُوتِ: لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنْتُ مِنَ الظَّالِمِينَ، فَإِنَّهُ لَمْ يَدْعُ بِهَا رَجُلٌ مُسْلِمٌ فِي شَيْءٍ قَطُّ إِلاَّ اسْتَجَابَ اللَّهُ لَهُ))

Amesimulia Sa’d bin Abiy Waqqaasw (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Du’aa ya Dhan-Nuwn (Nabiy Yuwnus) alipoomba akiwa ndani ya tumbo la nyangumi:

لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنْتُ مِنَ الظَّالِمِينَ

Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.

Basi hakika hakuna Muislamu aombaye kwayo kitu chochote kile isipokuwa Allaah Atamuitikia.” [At-Tirmidhiy (3505), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Daqaaiq At-Tafsiyr (2/364).
  • 2Majmuw’ Al-Fataawaa, Ibn Taymiyyah (14/13).
  • 3Majmuw’ Al-Fataawaa, Ibn Taymiyyah (2/14).
  • 4Al-Asnaa Fiy Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa, Al-Qurtwubiy (uk. 368).