Ar-Rabb: Al-Maalik (Mfalme, Mmiliki), Ar-Razzaaq (Mwenye Kuruzuku), Al-Murabbiy (Mlezi), Al-Khaaliq (Muumbaji), Al-Mudabbir (Mwendeshaji na Mpangaji wa mambo).
Yeye Ndiye Rabb wa walimwengu, Anayeuendesha ulimwengu wote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٢﴾
AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki) Allaah Rabb wa walimwengu. [Al-Faatihah (1:2)]
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan zaidi ya mara mia tisa, likiwa peke yake au likiegemezwa kwa viumbe, kama: رَبُّ الْعَالَمِينَ, رَبُّكُمْ na رَبِّي. Miongoni mwa Aayaat hizo ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٥٤﴾
Hakika Rabb wenu ni Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arsh, Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesi upesi, na (Ameumba) jua na mwezi na nyota, (vyote) vimetiishwa kwa Amri Yake. Tanabahi! Uumbaji ni Wake Pekee na kupitisha amri. Amebarikika Allaah Rabb wa walimwengu. [Al-A’raaf (7:54)]
Na Ibn Mandhwuwr amesema: Ar-Rabb katika lugha ni: Al-Maalik (Mfalme, Mmiliki), As-Sayyid (Bwana), Al-Mudabbir (Mwendeshaji na Mpangaji), Al-Murabbiy (Mlezi), Al-Qayyim (Msimamizi) na Al-Mun’im (Mwenye kuneemesha).1
Na Ibn Al-Anbaariy amesema: Ar-Rabb lina maana tatu: Al-Maalik (Mmiliki), As-Sayyid Al-Mutwaa’ (Bwana anayetiiwa) na Al-Muswlih (Mwenye kutengeneza na kurekebisha). Na Az-Zajjaajiy amesema: Ni Mwenye kukitengeneza kitu; husemwa: رَبَبْتُ الشَّيْءَ, pale unapokitengeneza na kukisimamia.
Na Ar-Rabb linajumuisha pia maana ya Mwenye kuabudiwa; kwa dalili kwamba miongoni mwa maswali ya kaburini ni: مَنْ رَبُّكَ (Nani Rabb wako?), yaani: Nani Muabudiwa wako? Rejea chini: Nukta ya (2) katika Taathira ya imaan.
Na Ar-Rabb asili yake ni kutokana na ulezi (التَّرْبِيَة); yaani Yule Anayelea na kukuza kitu kidogo kidogo hadi kikamilike. Wala haisemwi kwa yeyote: Ar-Rabb (kwa الـ) isipokuwa kwa Allaah Pekee, na huegemezwa kwa kusema: رَبُّ الْعَالَمِينَ (Rabb wa walimwengu). Ama kwa asiyekuwa Allaah, husemwa kwa kuegemezwa kwa kitu, kama kusema: رَبُّ الدَّار (bwana au mwenye nyumba), na رَبُّ الْفَرَس (bwana au mwenye farasi), au ngamia kwa anayemmiliki.2
Jina hili tukufu linakusanya Sifa nyingi za kimatendo, bali linaweza kuunganishwa na Majina mengine matukufu ya kiutendaji na Sifa Zake tukufu.3 Hivyo Ar-Rabb huingia katika maana za: Al-Qaadir, Al-Khaaliq, Al-Baariu, Al-Muswawwir, Al-Hayyu, Al-Qayyuwm, Ar-Rahmaan na mengineyo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾
Salaamun! Kauli kutoka kwa Rabb Mwenye Kurehemu. [Yaasiyn (36:58)]
Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Rabb wa viumbe wote; kila kilichoko mbinguni na ardhini ni Mja Wake na kiko katika udhibiti Wake. Yeye Ndiye Aliyelea viumbe vyote kwa Neema Zake, kisha Akakipa kila kitu umbo lake linalokilaikia, kisha Akakiongoza, kama ilivyothibiti katika Qur-aan:
قَالَ فَمَن رَّبُّكُمَا يَا مُوسَىٰ ﴿٤٩﴾ قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴿٥٠﴾
(Firawni) akasema: Basi ni nani Rabb wenu ee Muwsaa? (Muwsaa) akasema: Rabb wetu ni Yule Aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha Akakiongoza. [Twaahaa (20:49-50)]
Katika jibu hili, Nabiy Muwsaa (عليه السلام) ameikusanya maana ya Rubuwbiyyah katika nguzo mbili: kumpwekesha Allaah katika kuumba vitu na kuvianzisha kutokana na kutokuwepo; na kumpwekesha katika kuendesha mambo ya viumbe Vyake, kuwaongoza, kuwasimamia na kupanga hali zao.
Na Imaam As-Sa’diy amesema: Ar-Rabb ni Mlezi wa Waja Wake wote kwa kuwaendeshea mambo yao na kwa aina mbalimbali za neema. Na malezi mahsusi zaidi ya hayo ni malezi Yake kwa vipenzi Vyake, kwa kuzitengeneza nyoyo zao, roho zao na tabia zao; na ndio maana du’aa zao zimekithiri kwa Jina hili tukufu, kwa kuwa wanamuomba malezi haya mahsusi.4
Akawaenezea viumbe Vyake Neema kubwa kubwa ambazo lau wangezikosa wasingeweza kuishi. Akawakuza, Akawapa malisho, na Akawalea kwa malezi kamilifu. Basi hakuna neema yoyote isipokuwa ni Neema Yake. Ndipo Jina hili likawa tukufu, lenye umuhimu mkubwa na azizi katika nafsi na nyoyo za Manabii (عليهم السلام) na vipenzi vya Allaah; na ndipo du’aa nyingi za Qur-aan, za Sunnah ya Al-Musw-twafaa (صلى الله عليه وآله وسلم) na za Salaf zikawa zinaanzia kwa: رَبَّنَا au رَبِّ; kwani Jina hili linabeba maana za kuumba, kuruzuku, kuendesha mambo, kuhuisha na kufisha, na mja anapoomba maghfirah au haja husimama mbele ya Rabb wake akiwa mja dhalili, mhitaji. Rejea chini: Nukta za (13) hadi (17) katika Taathira ya imaan.
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ar-Rabb:
1-Ridhika Na Allaah Kuwa Ndiye Rabb Wako:
Tambua kwamba Ar-Rabb Ndiye Aliyekuumba, Anayekuruzuku, Anayekulea na Anayeendesha mambo yako yote; basi ridhika Naye kuwa ni Rabb wako, uridhike na Sharia Yake na Qadar Yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنِ الْعَبَّاسِ بْنِ عَبْدِ الْمُطَّلِبِ (رضي الله عنه) أَنَّهُ سَمِعَ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((ذَاقَ طَعْمَ الإِيمَانِ مَنْ رَضِيَ بِاللَّهِ رَبًّا، وَبِالإِسْلاَمِ دِينًا، وَبِمُحَمَّدٍ رَسُولاً))
Amesimulia Al-‘Abbaas bin ‘Abdil-Muttwalib (رضي الله عنه) kwamba alimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Ameonja ladha ya imaan yule aliyeridhika na Allaah kuwa ni Rabb (wake), na Uislamu kuwa ni Dini (yake), na Muhammad kuwa ni Rasuli.” [Muslim]
2-Jiandae Kwa Swali La Kaburini: مَنْ رَبُّكَ:
Kumbuka, ee Mja wa Ar-Rabb, kwamba swali la kwanza utakaloulizwa kaburini ni kuhusu Rabb wako; na hatothibitishwa katika jibu lake isipokuwa aliyeishi duniani akimjua Rabb wake na kumpwekesha. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنِ الْبَرَاءِ بْنِ عَازِبٍ (رضي الله عنهما) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((الْمُسْلِمُ إِذَا سُئِلَ فِي الْقَبْرِ يَشْهَدُ أَنْ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ، فَذَلِكَ قَوْلُهُ: يُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ))
Amesimulia Al-Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Muislamu akiulizwa kaburini atashuhudia kwamba:
لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ
Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah.
Basi hiyo ndiyo Kauli Yake: Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
3-Tambua Kwamba Kukiri Rubuwbiyyah Pekee Hakutoshi Bila Kumpwekesha Ar-Rabb Katika ‘Ibaadah:
Tambua kwamba hata washirikina walikiri kwamba Ar-Rabb Ndiye Rabb wa mbingu na ardhi, lakini hilo halikuwafaa kwa kuwa walimshirikisha katika ‘ibaadah. Basi kukiri kwako kwamba Allaah Ndiye Rabb kukupeleke kumwabudu Yeye Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ﴿٨٦﴾ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٨٧﴾
Sema: Nani Rabb wa mbingu saba, na Rabb wa ‘Arsh ‘Adhimu? Watasema: Ni ya Allaah Pekee. Sema: Je, basi hamtokuwa na taqwa? [Al-Muuminuwn (23:86-87)]
4-Jihisi Daima Kwamba Wewe Ni Mja Mwenye Rabb:
Tambua kwamba Ar-Rabb Ana ‘Uluwa, Ukubwa na Utukufu usiopingika; basi jivike vazi la uja, na jivue vazi la kujiona, na ujidhalilishe na kujihisi mhitaji mbele Yake. Na imesimuliwa kwamba mmoja wa watu wema alipita nyumbani kwa Bishr Al-Haafiy akasikia sauti za upuuzi na ala za muziki, akabisha mlango, akamuuliza mjakazi: Je, hii ni nyumba ya mtu huru au ya mja (wa Allaah)? Bishr alipoambiwa maneno hayo, yalimuingia moyoni, akamfuata mtu huyo haraka bila viatu, na Allaah Akamfungulia mlango wa tawbah. Na kumbuka ahadi uliyoichukua mbele ya Rabb wako kabla ya kuzaliwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ ﴿١٧٢﴾
Na pindi Rabb wako Alipowaleta wana wa Aadam kutoka migongoni mwao kizazi chao, Akawashuhudisha juu ya nafsi zao: Je, Mimi siye Rabb wenu? Wakasema: Sivyo hivyo bali naam tumeshuhudia! (Allaah Akawaambia): Msije kusema Siku ya Qiyaamah: Hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya. [Al-A’raaf (7:172)]
5-Usijiite Wala Usimwite Kiumbe “Rabb” Kwa Adabu Na Ar-Rabb:
Katika adabu ya kumpwekesha Ar-Rabb ni mja kutojiita wala kutomwita mtu mwingine “rabb” wake, kwa unyenyekevu mbele ya Rabb wake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لاَ يَقُولَنَّ أَحَدُكُمْ: عَبْدِي وَأَمَتِي، وَلاَ يَقُولَنَّ الْمَمْلُوكُ: رَبِّي وَرَبَّتِي، وَلْيَقُلِ الْمَالِكُ: فَتَاىَ وَفَتَاتِي، وَلْيَقُلِ الْمَمْلُوكُ: سَيِّدِي وَسَيِّدَتِي، فَإِنَّكُمُ الْمَمْلُوكُونَ، وَالرَّبُّ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Asiseme kabisa mmoja wenu: Mtumwa wangu na mjakazi wangu. Wala asiseme kabisa mwenye kumilikiwa: Rabb wangu na rabbah wangu. Bali aseme mwenye kumiliki: Kijana wangu wa kiume na kijana wangu wa kike. Na aseme mwenye kumilikiwa: Bwana wangu na bibi yangu. Kwani nyinyi nyote ni wenye kumilikiwa, na Ar-Rabb ni Allaah (عزّ وجلّ).” [Abuu Daawuwd (4975), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
6-Mtegemee Ar-Rabb Na Umkabidhi Mambo Yako Yote:
Kwa kuwa Ar-Rabb Ndiye Mwenye kuumba, kuruzuku na kuendesha mambo yote, basi mtupie Yeye mzigo wako wote, upate utulivu na amani moyoni. Ukiwa mgonjwa, jua kwamba Yeye Pekee Ndiye Anayehuisha na kufisha; na ukiwa na wasiwasi, jua kwamba Yeye Pekee Ndiye Anayeleta manufaa na kuzuia madhara. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾
Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatazamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza Kusudio Lake. Allaah Amejaalia makadirio kwa kila kitu. [Atw-Twalaaq (65:3)]
7-Kumbuka Kwamba Mitihani Ni Malezi Ya Ar-Rabb Kwako:
Ar-Rabb Anapokujaribu kwa msiba au shida, jua kwamba Anakulea; huenda ukawa na aibu ya nafsi (kama kujiona) usiyoweza kuiondoa, kisha ukafikwa na mtihani unaokuvunja na kukurudisha katika uhalisia wako, ukasema: Rabb wangu Amenilea kwa tukio hili. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ صُهَيْبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((عَجَبًا لأَمْرِ الْمُؤْمِنِ، إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ، وَلَيْسَ ذَاكَ لأَحَدٍ إِلاَّ لِلْمُؤْمِنِ، إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ، وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ))
Amesimulia Swuhayb (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ajabu ya jambo la Muumini! Hakika mambo yake yote ni kheri, na hilo halimpati yeyote isipokuwa Muumini. Akifikwa na furaha hushukuru, ikawa ni kheri kwake; na akifikwa na dhara husubiri, ikawa ni kheri kwake.” [Muslim]
8-Ilee Nafsi Yako Na Uirekebishe Kidogo Kidogo:
Kwa kuwa katika maana za Ar-Rabb ni kulea kitu hatua kwa hatua hadi ukamilifu, basi jitahidi kuitengeneza nafsi yako kwa kuiondolea aibu zake na kuipamba kwa sifa njema, ukianza kwa kumuomba Allaah msaada, kwa ukweli na ikhlaasw, na kwa kuzijua aibu zako. Na nenda hatua kwa hatua katika kutafuta ilimu na ‘ibaadah bila kujibebesha usiyoyaweza. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ هَذَا الدِّينَ مَتِينٌ، فَأَوْغِلُوا فِيهِ بِرِفْقٍ))
Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Dini hii ni imara, basi iingieni kwa upole (hatua kwa hatua).” [Ahmad (13052), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Al-Jaami’ (2246)]
9-Mshukuru Ar-Rabb Kwa Neema Zake Upate Kuzidishiwa:
Kwa kuwa hakuna neema yoyote isipokuwa inatoka kwa Ar-Rabb, basi mshukuru kwa moyo wako, ulimi wako na viungo vyako, na zitumie Neema Zake katika kumtii. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴿٧﴾
Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (Neema Zangu), na mkikufuru, basi hakika Adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym (14:7)]
10-Hisi Utukufu Wa Ar-Rabb Unaposema: رَبِّ الْعَالَمِينَ Na سُبْحَانَ رَبِّيَ الْعَظِيمِ:
Tambua, ee Mja wa Ar-Rabb: Unasoma Al-Faatihah angalau mara kumi na saba kila siku katika Swalaah za faradhi, na unasema: رَبِّ الْعَالَمِينَ. Basi hisi Ukubwa wa Rabb wako, Ambaye Ni Rabb wa wanaadam, majini, Malaika na walimwengu wote, Anayeviendesha usiku na mchana; na hilo likuzidishie mapenzi, khofu na matarajio Kwake. Na katika kila rukuu’ unasema: سُبْحَانَ رَبِّيَ الْعَظِيمِ, na katika kila sujuwd: سُبْحَانَ رَبِّيَ الْأَعْلَى. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَلاَ وَإِنِّي نُهِيتُ أَنْ أَقْرَأَ الْقُرْآنَ رَاكِعًا أَوْ سَاجِدًا، فَأَمَّا الرُّكُوعُ فَعَظِّمُوا فِيهِ الرَّبَّ عَزَّ وَجَلَّ، وَأَمَّا السُّجُودُ فَاجْتَهِدُوا فِي الدُّعَاءِ فَقَمِنٌ أَنْ يُسْتَجَابَ لَكُمْ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Tanabahini! Hakika mimi nimekatazwa kusoma Qur-aan nikiwa katika rukuu’ au sujuwd. Ama katika rukuu’, mtukuzeni humo Ar-Rabb (عزّ وجلّ); na ama katika sujuwd, jitahidini humo kuomba du’aa, kwani inastahiki kuitikiwa kwenu.” [Muslim]
11-Mkaribie Ar-Rabb Katika Sehemu Ya Mwisho Ya Usiku:
Tafuta nyakati ambazo Ar-Rabb Anakuwa karibu zaidi na mja, na khaswa sehemu ya mwisho ya usiku, uzitumie kwa dhikr, Swalaah na du’aa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَمْرِو بْنِ عَبَسَةَ (رضي الله عنه) أَنَّهُ سَمِعَ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((أَقْرَبُ مَا يَكُونُ الرَّبُّ مِنَ الْعَبْدِ فِي جَوْفِ اللَّيْلِ الآخِرِ، فَإِنِ اسْتَطَعْتَ أَنْ تَكُونَ مِمَّنْ يَذْكُرُ اللَّهَ فِي تِلْكَ السَّاعَةِ فَكُنْ))
Amesimulia ‘Amr bin ‘Abasah (رضي الله عنه) kwamba alimsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Wakati ambao Ar-Rabb Anakuwa karibu kabisa na mja ni katikati ya sehemu ya mwisho ya usiku. Basi ukiweza kuwa miongoni mwa wanaomdhukuru Allaah katika saa hiyo, basi kuwa.” [At-Tirmidhiy (3579), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
12-Kithirisha Du’aa Katika Sujuwd Kwani Ndipo Mja Anapokuwa Karibu Kabisa Na Rabb Wake:
Kusujudu ni hali ya unyenyekevu wa hali ya juu mbele ya Ar-Rabb, na ni katika sababu za kujikurubisha Kwake na kutakabaliwa du’aa. Basi kithirisha du’aa unaposujudu. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((أَقْرَبُ مَا يَكُونُ الْعَبْدُ مِنْ رَبِّهِ وَهُوَ سَاجِدٌ، فَأَكْثِرُوا الدُّعَاءَ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hali ambayo mja huwa karibu kabisa na Rabb wake ni pale anapokuwa amesujudu, basi kithirisheni du’aa.” [Muslim]
13-Muombe Ar-Rabb Maghfirah Unapokosea Kama Alivyoomba Nabiy Aadam (عليه السلام):
Tambua, ee Mja wa Ar-Rabb: Unapoteleza katika dhambi, rejea haraka kwa Rabb wako kwa kukiri kosa lako na kuomba maghfirah na Rehma Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu Nabiy Aadam na mkewe:
قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾
Wakasema: Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na Usipotughufuria na Ukaturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Al-A’raaf (7:23)]
14-Waombee Wazazi Wako Na Waumini Kama Alivyoomba Khaliylur-Rahmaan Nabiy Ibraahiym (عليه السلام):
Tambua, ee Mja wa Ar-Rabb: Usijisahau wala usiwasahau wazazi wako na Waumini wenzako katika du’aa zako. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu du’aa ya Nabiy Ibraahiym:
رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿٤١﴾
Rabb wetu! Nighufurie mimi na wazazi wangu wawili na Waumini Siku itakayosimama hesabu. [Ibraahiym (14:41)]
15-Jikinge Kwa Ar-Rabb Kutokana Na Mashaytwaan:
Omba kinga kwa Rabb wako dhidi ya udokezi wa mashaytwaan na kuhudhuria kwao, kama Alivyomfundisha Ar-Rabb Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم):
وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ﴿٩٧﴾ وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ ﴿٩٨﴾
Na sema: Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan. Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie. [Al-Muuminuwn (23:97-98)]
16-Muombe Ar-Rabb Akuthibitishe Katika Uongofu Kama Walivyoomba Wenye Ilimu:
Nyoyo ziko Mkononi mwa Ar-Rabb, basi usijiaminishe na hidaaya uliyonayo bali muombe Akuthibitishe nayo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu du’aa ya wenye ilimu thabiti:
رَبَّنَا لَا تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْوَهَّابُ ﴿٨﴾
(Husema): Rabb wetu! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kuwa Umetuhidi na Tutunukie kutoka Kwako Rehma. Hakika Wewe Ni Mwingi wa Kutunuku na Kuneemesha. [Aal-‘Imraan (3:8)]
17-Muombe Ar-Rabb Wake Na Dhuria Wema Kama Wanavyoomba ‘Ibaadur-Rahmaan:
Omba du’aa kwa ajili ya familia yako, kwani wake wema na dhuria wema ni katika neema kubwa za Ar-Rabb. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu Waja wa Ar-Rahmaan:
وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا ﴿٧٤﴾
Na wale wanaosema: Rabb wetu! Tutunukie katika wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu, na Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye taqwa. [Al-Furqaan (25:74)]
Na Allaah Mjuzi zaidi