Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah004 - Ar-Rahmaan

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 004 kati ya 103
Ar-Rahmaan — Majina Mazuri ya Allaah

Ar-Rahmaan: Mwingi wa Rehma; Mwenye Rehma pana iliyoenea viumbe vyote. Ni Jina mahsusi la Allaah Peke Yake, haitwi kwalo yeyote asiyekuwa Yeye.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara hamsini na saba (57), na limekuja kama Jina linalojitegemea. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الرَّحْمَـٰنُ ﴿١﴾ عَلَّمَ الْقُرْآنَ ﴿٢﴾

Ar-Rahmaan. Amefundisha Qur-aan. [Ar-Rahmaan (55:1-2)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ الرَّحْمَـٰنُ فَاسْأَلْ بِهِ خَبِيرًا ﴿٥٩﴾

Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arsh. (Yeye ni) Ar-Rahmaan, basi ulizia kuhusu Yeye, kwani Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-Furqaan (25:59)]

Jina hili ni pana zaidi na lenye kuenea zaidi kuliko Ar-Rahiym (Mwenye Kurehemu); linakusanya maana zote za Rehma na huruma. Allaah Ndiye Mwenye Rehma iliyokusanya kila kitu, iliyoenea kwa viumbe Vyake vyote duniani: wanaadam na majini, Waumini na makafiri, wanyama na mimea; hakuna yeyote wala chochote katika kuwepo huku isipokuwa Rehma Yake imemuenea.

Na Imaam Ibn Al-Qayyim amesema: Ar-Rahmaan linajulisha Sifa iliyosimama Kwake (سبحانه وتعالى), na Ar-Rahiym linajulisha kufikia kwa Sifa hiyo kwa wanaorehemewa; kwa hiyo la kwanza ni la Sifa na la pili ni la kitendo. Ndio maana utakuta: وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا na إِنَّهُ بِهِمْ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ, wala haikuja kabisa: رَحْمَنٌ بِهِمْ.1 Kwa hiyo Ar-Rahmaan ni Jina, na Ar-Rahmah ni Sifa ya Dhati Yake inayobebwa na Jina hilo.

Na Amekuwa juu ya ‘Arsh kwa Jina Lake Ar-Rahmaan, kwa sababu ‘Arsh imezunguka viumbe vyote na ina wasaa juu yao, na Rehma Yake imewazunguka Waja Wake na ina wasaa kwao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾

Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma) Yuko juu ya ‘Arsh. [Twaahaa (20:5)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu wasaa wa Rehma Yake:

وَاكْتُبْ لَنَا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ إِنَّا هُدْنَا إِلَيْكَ ۚ قَالَ عَذَابِي أُصِيبُ بِهِ مَنْ أَشَاءُ ۖ وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ۚ فَسَأَكْتُبُهَا لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِنَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٥٦﴾

Na Tuandikie katika dunia hii mazuri na katika Aakhirah. Hakika sisi tumerudi kutubu Kwako. (Allaah) Akasema: Adhabu Yangu Nitamsibu nayo Nimtakaye. Na Rehma Yangu imeenea kila kitu. Basi Nitawaandikia wale wenye taqwa na wanaotoa Zakaah na ambao wao wanaziamini Aayaat (na Ishara, Hoja, Dalili) Zetu. [Al-A’raaf (7:156)]

Hivyo Amekuwa juu ya kiumbe kilicho kipana zaidi katika Alivyoviumba, nacho ni ‘Arsh Yake, kwa Sifa iliyo pana zaidi, nayo ni Rehma Yake; na kwa ajili hiyo Rehma Yake imeenea kila kitu.

Ar-Rahmaan ni Jina Analoitwa Allaah Peke Yake, ama athari ya Jina hili ni kwa wote; wema na waovu. Na ndio maana Allaah (سبحانه وتعالى) Amelitaja zaidi Jina hili katika Suwrah zilizoteremshwa Makkah, khaswa Suwrah Maryam, ambamo limetajwa mara nyingi zaidi kuliko Suwrah nyinginezo. Kipindi cha Makkah kilikuwa kipindi cha mwanzo cha Uislamu, na Allaah (سبحانه وتعالى) Akawadhihirishia makafiri Sifa Yake hii kwamba Yeye Ni Mwingi wa Rehma juu ya kuwa wanamshirikisha.

Na makafiri wa Makkah hawakupenda Jina hili la Ar-Rahmaan, wakakataa kuliandika katika mkataba wa Hudaybiyah pale Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipomwamrisha mwandishi wa mkataba aandike: بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ. Wakasema: Andika: بِاسْمِكَ اللَّهُمَّ. Hapo Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha:2

قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ ۖ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ

Sema: Muiteni Allaah au muiteni Ar-Rahmaan, vyovyote mtakavyomwita basi Yeye Ana Majina Mazuri kabisa. [Al-Israa (17:110)]

Na ndio maana Suwrah za Qur-aan zinaanza kwa بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ inayotaja Majina Yake Mawili Ar-Rahmaan na Ar-Rahiym, na pia Allaah (سبحانه وتعالى) Ameyataja mwanzoni mwa Suwrah Al-Faatihah.

Rehma Mia Za Allaah (سبحانه وتعالى):

Na katika Sunnah zimethibiti Hadiyth kadhaa kuhusu Rehma ya Allaah (سبحانه وتعالى) ambayo kwayo viumbe wanarehemeana ardhini. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((إِنَّ اللَّهَ خَلَقَ الرَّحْمَةَ يَوْمَ خَلَقَهَا مِائَةَ رَحْمَةٍ، فَأَمْسَكَ عِنْدَهُ تِسْعًا وَتِسْعِينَ رَحْمَةً، وَأَرْسَلَ فِي خَلْقِهِ كُلِّهِمْ رَحْمَةً وَاحِدَةً، فَلَوْ يَعْلَمُ الْكَافِرُ بِكُلِّ الَّذِي عِنْدَ اللَّهِ مِنَ الرَّحْمَةِ لَمْ يَيْأَسْ مِنَ الْجَنَّةِ، وَلَوْ يَعْلَمُ الْمُؤْمِنُ بِكُلِّ الَّذِي عِنْدَ اللَّهِ مِنَ الْعَذَابِ لَمْ يَأْمَنْ مِنَ النَّارِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Hakika Allaah Aliumba Rehma siku Alipoiumba kuwa Rehma mia, Akazuia Kwake Rehma tisini na tisa, na Akapeleka kwa viumbe Vyake vyote Rehma moja. Lau kafiri angejua yote yaliyoko kwa Allaah katika Rehma, asingekata tamaa ya Jannah. Na lau Muumini angejua yote yaliyoko kwa Allaah katika adhabu, asingejiaminisha na moto.” [Al-Bukhaariy]

Na amesema pia:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّهُ سَمِعَ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((جَعَلَ اللَّهُ الرَّحْمَةَ مِائَةَ جُزْءٍ، فَأَمْسَكَ عِنْدَهُ تِسْعَةً وَتِسْعِينَ جُزْءًا، وَأَنْزَلَ فِي الأَرْضِ جُزْءًا وَاحِدًا، فَمِنْ ذَلِكَ الْجُزْءِ يَتَرَاحَمُ الْخَلْقُ حَتَّى تَرْفَعَ الْفَرَسُ حَافِرَهَا عَنْ وَلَدِهَا خَشْيَةَ أَنْ تُصِيبَهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba alimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Allaah Amejaalia Rehma kuwa sehemu mia, Akazuia Kwake sehemu tisini na tisa, na Akateremsha ardhini sehemu moja. Basi kutokana na sehemu hiyo ndipo viumbe wanarehemeana, hadi farasi huinua kwato yake kutoka kwa mtoto wake akikhofu asimkanyage.” [Al-Bukhaariy]

Na amesema pia:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ لِلَّهِ مِائَةَ رَحْمَةٍ أَنْزَلَ مِنْهَا رَحْمَةً وَاحِدَةً بَيْنَ الْجِنِّ وَالإِنْسِ وَالْبَهَائِمِ وَالْهَوَامِّ، فَبِهَا يَتَعَاطَفُونَ، وَبِهَا يَتَرَاحَمُونَ، وَبِهَا تَعْطِفُ الْوَحْشُ عَلَى وَلَدِهَا، وَأَخَّرَ اللَّهُ تِسْعًا وَتِسْعِينَ رَحْمَةً يَرْحَمُ بِهَا عِبَادَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ana Rehma mia, Ameteremsha moja kati yake baina ya majini, wanaadam, wanyama na wadudu; kwayo wanaoneana huruma, na kwayo wanarehemeana, na kwayo mnyama mwitu humhurumia mwanawe. Na Allaah Ameakhirisha Rehma tisini na tisa, Atawarehemu kwazo Waja Wake Siku ya Qiyaamah.” [Muslim]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ar-Rahmaan:

1-Thibitisha Sifa Ya Rahmah Kwa Allaah Na Tambua Kwamba Rehma Yake Inashinda Ghadhabu Yake:

Kumbuka, ee Mja wa Ar-Rahmaan, kwamba Sifa ya Rahmah ni Sifa ya ukamilifu inayolaikiana na Dhati Yake (سبحانه وتعالى), imethibiti katika Qur-aan na Sunnah; haijuzu kuikanusha wala kuipotosha maana yake, kwani hilo ni katika kupotoka katika Majina Yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لَمَّا قَضَى الْخَلْقَ كَتَبَ عِنْدَهُ فَوْقَ عَرْشِهِ: إِنَّ رَحْمَتِي سَبَقَتْ غَضَبِي))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Alipomaliza kuumba viumbe, Aliandika Kwake juu ya ‘Arsh Yake: Hakika Rehma Yangu imetangulia Ghadhabu Yangu.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

2-Usikate Tamaa Na Rehma Ya Ar-Rahmaan Hata Madhambi Yakiwa Mengi:

Tambua kwamba milango ya Rehma ya Ar-Rahmaan iko wazi kwa kila mwenye kutubia, basi usikate tamaa bali rejea Kwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi Waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na Rehma ya Allaah, hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Az-Zumar (39:53)]

3-Tambua Kwamba Allaah Ni Mwenye Kuwarehemu Waja Wake Kuliko Mama Anavyomrehemu Mwanawe:

Kumbuka kwamba Rehma ya Ar-Rahmaan kwa Waja Wake ni kubwa kuliko rehma yoyote unayoijua duniani, hivyo mdhanie dhana njema na umkimbilie Yeye. Imepokewa kwamba:

عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَدِمَ عَلَى النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) سَبْيٌ، فَإِذَا امْرَأَةٌ مِنَ السَّبْيِ تَسْعَى، إِذَا وَجَدَتْ صَبِيًّا فِي السَّبْيِ أَخَذَتْهُ فَأَلْصَقَتْهُ بِبَطْنِهَا وَأَرْضَعَتْهُ، فَقَالَ لَنَا النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((أَتُرَوْنَ هَذِهِ طَارِحَةً وَلَدَهَا فِي النَّارِ؟)) قُلْنَا: لاَ، وَهِيَ تَقْدِرُ عَلَى أَنْ لاَ تَطْرَحَهُ. فَقَالَ: ((لَلَّهُ أَرْحَمُ بِعِبَادِهِ مِنْ هَذِهِ بِوَلَدِهَا))

Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه): Walikuja kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) mateka, na mara mwanamke mmoja kati ya mateka akawa anahangaika; kila alipomkuta mtoto kati ya mateka alimchukua, akamgandamiza tumboni mwake na kumnyonyesha. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akatuambia: “Je, mnaona mwanamke huyu atamtupa mwanawe motoni?” Tukasema: Hapana, naye akiweza kutomtupa. Akasema: “Allaah Anawarehemu Waja Wake kuliko huyu anavyomrehemu mwanawe.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

4-Kumbuka Kwamba Mitihani Ni Katika Rehma Ya Ar-Rahmaan Kwa Wenye Subira:

Tambua kwamba misiba inayokufika si kinyume cha Rehma ya Ar-Rahmaan, bali ni sababu ya kupata Rehma Yake ukisubiri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴿١٥٧﴾

Na bila shaka Tutakujaribuni kwa jambo katika khofu, njaa, upungufu wa mali, nafsi na mazao. Na wabashirie wenye subira. Wale ambao unapowafika msiba husema: Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea. Hao zitakuwa juu yao Barakah kutoka kwa Rabb wao na Rehma, na hao ndio wenye kuhidika. [Al-Baqarah (2:155-157)]

5-Mtii Allaah Na Rasuli Wake Upate Rehma:

Tambua kwamba kila mja anapozidi kumtii Allaah (سبحانه وتعالى), ndipo anapostahiki zaidi Rehma Yake; na kujiepusha na yote Aliyoyaharamisha Ar-Rahmaan na Rasuli Wake, kwani baadhi yake humfikisha mtu katika laana, nayo ni kuwekwa mbali na Rehma Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿١٣٢﴾

Na mtiini Allaah na Rasuli mpate kurehemewa. [Aal-‘Imraan (3:132)]

6-Simamisha Swalaah Na Utoe Zakaah Upate Kurehemewa:

Omba Rehma ya Ar-Rahmaan kwa kudumisha ‘ibaadah Alizokufaridhishia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٥٦﴾

Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, na mtiini Rasuli ili mpate kurehemewa. [An-Nuwr (24:56)]

7-Ifuate Qur-aan Na Kuwa Na Taqwa Upate Kurehemewa:

Tambua, ee Mja wa Ar-Rahmaan: Qur-aan ni Rehma, na kuisoma, kuizingatia na kuifanyia kazi ni katika sababu kubwa za kuteremkiwa na Rehma. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَهَـٰذَا كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ مُبَارَكٌ فَاتَّبِعُوهُ وَاتَّقُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿١٥٥﴾

Na hiki ni Kitabu (Qur-aan) Tumekiteremsha kilichobarikiwa, basi kifuateni na muwe na taqwa mpate kurehemewa. [Al-An’aam (6:155)]

8-Isikilize Qur-aan Kwa Makini Inaposomwa:

Tambua, ee Mja wa Ar-Rahmaan: Unaposomewa Qur-aan, nyamaza na uisikilize kwa mazingatio, kwani huo ni mlango wa Rehma. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٢٠٤﴾

Na inaposomwa Qur-aan, basi isikilizeni kwa makini na bakieni kimya (mzingatie) ili mpate kurehemewa. [Al-A’raaf (7:204)]

9-Fanya Ihsaan Katika ‘Ibaadah Zako Kwani Rehma Ya Allaah Iko Karibu Na Wafanyao Ihsaan:

Tambua, ee Mja wa Ar-Rahmaan: Ihsaan inaanzia katika kuitekeleza vyema kila amali, hadi kufikia kumwabudu Allaah kana kwamba unamuona; basi mkhofu Allaah faraghani kama unavyomkhofu hadharani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا وَادْعُوهُ خَوْفًا وَطَمَعًا ۚ إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾

Na wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya (Allaah) kuitengeneza sawa, na muombeni kwa khofu na matumaini. Hakika Rehma ya Allaah iko karibu na wafanyao ihsaan. [Al-A’raaf (7:56)]

10-Suluhisha Baina Ya Waumini Upate Kurehemewa:

Kumbuka kwamba kusuluhisha baina ya Waumini ni miongoni mwa sababu za kupata Rehma ya Ar-Rahmaan.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ﴿١٠﴾

Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu. Na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa. [Al-Hujuraat (49:10)]

11-Omba Maghfirah Kwa Allaah Ili Urehemewe:

Tambua, ee Mja wa Ar-Rahmaan: Huu ndio wito wa Nabiy Swaalih (عليه السلام) kwa kaumu yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالَ يَا قَوْمِ لِمَ تَسْتَعْجِلُونَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ ۖ لَوْلَا تَسْتَغْفِرُونَ اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٤٦﴾

(Swaalih) akasema: Enyi kaumu yangu! Kwa nini mnahimiza uovu kabla ya mema? Kwa nini msimwombe Allaah maghfirah ili huenda mkarehemewa? [An-Naml (27:46)]

12-Hajiri Na Upigane Jihaad Katika Njia Ya Allaah Kwa Kutaraji Rehma Yake:

Tambua, ee Mja wa Ar-Rahmaan, kwamba wanaohajiri na kupigana jihaad katika Njia ya Allaah kwa ikhlaasw ndio wanaotaraji Rehma Yake kwa haki.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ يَرْجُونَ رَحْمَتَ اللَّـهِ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢١٨﴾

Hakika wale walioamini na wale waliohajiri na wakapigana Jihaad katika Njia ya Allaah, hao wanataraji Rehma ya Allaah, na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Al-Baqarah (2:218)]

13-Jipambe Kwa Sifa Za ‘Ibaadur-Rahmaan:

Allaah (سبحانه وتعالى) Amewanasibisha Waja Wake wema na Jina Lake Ar-Rahmaan, na Akataja sifa zao katika Suwrah Al-Furqaan kuanzia Aayah ya (63) hadi (76), na Akawaahidi Jannah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا ﴿٦٣﴾

Na Waja wa Ar-Rahmaan ni wale wanaotembea katika ardhi kwa unyenyekevu na upole, na majahili wanapowasemesha, wao husema: Salaamaa (amani)! [Al-Furqaan (25:63)]

14-Unga Undugu Kwani Ar-Rahim Imetokana Na Jina La Ar-Rahmaan:

Tambua kwamba Sifa hii ya Rahmah imefungamana na الرَّحِم (undugu wa damu), ambao kwao jamaa hurehemeana; na kukata undugu ni dhambi kubwa inayosababisha laana ya Ar-Rahmaan na Ghadhabu Zake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ الرَّحِمَ شِجْنَةٌ مِنَ الرَّحْمَنِ، فَقَالَ اللَّهُ: مَنْ وَصَلَكِ وَصَلْتُهُ، وَمَنْ قَطَعَكِ قَطَعْتُهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Ar-Rahim (undugu) ni tawi linalotokana na Ar-Rahmaan. Allaah Akasema: Atakayekuunga Nitamuunga, na atakayekukata Nitamkata.” [Al-Bukhaariy]

Na amesema pia:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الرَّحِمُ مُعَلَّقَةٌ بِالْعَرْشِ، تَقُولُ: مَنْ وَصَلَنِي وَصَلَهُ اللَّهُ، وَمَنْ قَطَعَنِي قَطَعَهُ اللَّهُ))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ar-Rahim (undugu) umetundikwa kwenye ‘Arsh, unasema: Anayeniunga, Allaah Atamuunga; na anayenikata, Allaah Atamkata.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

15-Warehemu Viumbe Ili Ar-Rahmaan Akurehemu:

Tambua kwamba Rehma ni katika tabia tukufu ambazo Allaah (سبحانه وتعالى) Amewahimiza Waja Wake kujipamba nazo, na mwenye kuwarehemu watu hustahiki Rehma ya Ar-Rahmaan. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الرَّاحِمُونَ يَرْحَمُهُمُ الرَّحْمَنُ، ارْحَمُوا مَنْ فِي الأَرْضِ يَرْحَمْكُمْ مَنْ فِي السَّمَاءِ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Wenye kurehemu, Ar-Rahmaan Huwarehemu. Warehemuni walioko ardhini, Atakurehemuni Aliyeko mbinguni.” [Abuu Daawuwd (4941), At-Tirmidhiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]

16-Muombe Ar-Rahmaan Rehma Yake Kwa Uthabiti Bila Kusitasita:

Kithirisha kumuomba Ar-Rahmaan Rehma Yake, na unapoomba, azimia katika du’aa yako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِذَا دَعَا أَحَدُكُمْ فَلْيَعْزِمِ الْمَسْأَلَةَ، وَلاَ يَقُولَنَّ: اللَّهُمَّ إِنْ شِئْتَ فَأَعْطِنِي، فَإِنَّهُ لاَ مُسْتَكْرِهَ لَهُ))

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mmoja wenu anapoomba du’aa basi aazimie ombi lake, wala asiseme kabisa: Yaa Allaah, Ukitaka nipe; kwani hakuna wa kumlazimisha (Allaah).” [Al-Bukhaariy]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Badaai’ Al-Fawaaid, Ibn Al-Qayyim.
  • 2Tafsiyr Ibn Kathiyr.