Ar-Rahiym: Mwenye Kurehemu; Mwenye kuwafikishia Waja Wake Rehma Yake, na khaswa Rehma makhsusi kwa Waumini duniani na Aakhirah.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara mia moja na kumi na nne (114). Majina mawili Ar-Rahmaan na Ar-Rahiym yanatokana na asili moja ya herufi (ر ح م), na yote mawili yanabeba Sifa ya Rahmah. Lakini kama ilivyobainishwa katika Jina la Ar-Rahmaan, Jina hilo ni pana zaidi na linaenea viumbe wote; Waumini na makafiri, wema na waovu. Ama Ar-Rahiym linaonyesha kufikia kwa Rehma hiyo kwa wanaorehemewa, na khaswa Waumini.1 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ الَّذِي يُصَلِّي عَلَيْكُمْ وَمَلَائِكَتُهُ لِيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا ﴿٤٣﴾
Yeye (Allaah) Ndiye Anakurehemuni, na Malaika Wake (wanakuombeeni maghfirah na rehma) ili Akutoeni kutoka katika viza kuingia katika Nuru. Naye daima Ni Mwenye Kurehemu Waumini. [Al-Ahzaab (33:43)]
Na Anasema kuhusu Waja Wake:
نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٤٩﴾
Wajulishe Waja Wangu, kwamba: Hakika Mimi Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Al-Hijr (15:49)]
Na Anasema kuhusu Swahaba waliomfuata Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika saa ya dhiki (Vita vya Tabuwk):
لَّقَد تَّابَ اللَّـهُ عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّهُ بِهِمْ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١١٧﴾
Kwa yakini Allaah Amepokea tawbah ya Nabiy na Muhaajiruwn na Answaar ambao wamemfuata (Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم) katika saa ya dhiki baada ya nyoyo za kundi miongoni mwao kukurubia kuelemea mbali na haki, kisha Akapokea tawbah yao. Hakika Yeye kwao Ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu. [At-Tawbah (9:117)]
Na Waumini watakapoingia Jannah, watapokelewa kwa maamkizi kutoka kwa Rabb Mwenye Kurehemu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ ﴿٥٥﴾ هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ ﴿٥٦﴾ لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُم مَّا يَدَّعُونَ ﴿٥٧﴾ سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾
Hakika watu wa Jannah leo wamo katika kushughulika wakifurahi. Wao na wake zao, wakiwa katika vivuli, juu ya makochi ya fakhari wakiegemea. Watapata humo kila aina ya matunda, na watapata wanavyoomba. Salaamun! Kauli kutoka kwa Rabb Mwenye Kurehemu. [Yaasiyn (36:55-58)]
Na pia katika hali ya Waumini wanapofishwa na kubashiriwa Jannah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾ نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ﴿٣١﴾ نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ﴿٣٢﴾
Hakika wale waliosema: Rabb wetu ni Allaah, kisha wakathibiti imara, Malaika huwateremkia (kuwaambia): Msikhofu, wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa. Sisi ni rafiki zenu walinzi katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoyahitajia. Ni mapokezi ya takrima kutoka kwa Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Fusw-Swilat (41:30-32)]
Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amemsifu pia Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa sifa ya huruma na rehma kwa Waumini, kwa kiwango kinacholaikiana na kiumbe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٢٨﴾
Kwa yakini amekujieni Rasuli anayetokana na nyinyi wenyewe, yanamtia mashaka (na huzuni) yanayokutaabisheni, anakujalini, kwa Waumini ni mwenye huruma mno, mwenye rehma. [At-Tawbah (9:128)]
Hivyo Waumini ni wenye bahati kubwa kwa Majina haya mawili Ar-Rahmaan na Ar-Rahiym, kwani Rehma mia za Allaah zitakamilishwa kwao Siku ya Qiyaamah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ سَلْمَانَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ خَلَقَ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ مِائَةَ رَحْمَةٍ، كُلُّ رَحْمَةٍ طِبَاقَ مَا بَيْنَ السَّمَاءِ وَالأَرْضِ، فَجَعَلَ مِنْهَا فِي الأَرْضِ رَحْمَةً، فَبِهَا تَعْطِفُ الْوَالِدَةُ عَلَى وَلَدِهَا، وَالْوَحْشُ وَالطَّيْرُ بَعْضُهَا عَلَى بَعْضٍ، فَإِذَا كَانَ يَوْمُ الْقِيَامَةِ أَكْمَلَهَا بِهَذِهِ الرَّحْمَةِ))
Amesimulia Salmaan (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah siku Alipoumba mbingu na ardhi Aliumba Rehma mia, kila Rehma ni kiasi cha kujaza baina ya mbingu na ardhi. Akaweka ardhini Rehma moja kati yake; kwayo mama humhurumia mwanawe, na wanyama na ndege wanahurumiana wao kwa wao. Itakapokuwa Siku ya Qiyaamah, Ataikamilisha (mia) kwa Rehma hii.” [Muslim]
Kutajwa Pamoja Kwa Ar-Rahmaan Na Ar-Rahiym:
Majina haya mawili yametajwa pamoja katika Qur-aan katika Aayaat kadhaa, mfano:
وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴿١٦٣﴾
Na Ilaah wenu (Allaah) ni Ilaah Mmoja, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu. [Al-Baqarah (2:163)]
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
حم﴿١﴾ تَنزِيلٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ﴿٢﴾
Haa Miym. Ni uteremsho kutoka kwa Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma), Mwenye Kurehemu. [Fusw-Swilat (41:1-2)]
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ ۖ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ﴿٢٢﴾
Yeye Ni Allaah, Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye. Mjuzi wa ya ghaibu na ya dhahiri, Yeye Ndiye Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu. [Al-Hashr (59:22)]
Kutajwa Kwa Ar-Rahiym Pamoja Na Majina Mengine:
Ama Ar-Rahiym, limetajwa pamoja na Majina mengineyo ya Allaah (سبحانه وتعالى), khaswa Al-Ghafuwr (Mwingi wa Kughufuria), na pia Ar-Rauwf, Al-Waduwd, At-Tawwaab, Al-‘Aziyz na Al-Barr. Mifano michache: Pamoja na Al-Ghafuwr:
قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾
Sema: Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Aal-‘Imraan (3:31)]
Pamoja na Ar-Rauwf (Mwenye huruma mno):
وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّـهَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٠﴾
Na lau si Fadhila ya Allaah juu yenu na Rehma Yake, na kwamba Allaah Ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu (basi Angeliwaadhibuni bila kukawia). [An-Nuwr (24:20)]
Pamoja na Al-Waduwd (Mwenye upendo khalisi):
وَاسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي رَحِيمٌ وَدُودٌ﴿٩٠﴾
Na ombeni maghfirah kwa Rabb wenu, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu Ni Mwenye Kurehemu, Mwenye upendo khalisi. [Huwd (11:90)]
Pamoja na At-Tawwaab (Mwingi wa Kupokea Tawbah):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾
Enyi walioamini! Jiepusheni sana na dhana, kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msichunguzane, na wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je, anapenda mmoja wenu kwamba ale nyama ya nduguye aliyekufa? Basi mmelichukia hilo! Na mcheni Allaah! Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Kurehemu. [Al-Hujuraat (49:12)]
Pamoja na Al-‘Aziyz (Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika):
بِنَصْرِ اللَّـهِ ۚ يَنصُرُ مَن يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٥﴾
Kwa Nusura ya Allaah. Anamnusuru Amtakaye, Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu. [Ar-Ruwm (30:5)]
Pamoja na Al-Barr (Mwingi wa wema):
إِنَّا كُنَّا مِن قَبْلُ نَدْعُوهُ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ ﴿٢٨﴾
Hakika sisi tulikuwa kabla tunamuomba Yeye Pekee. Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa Ihsaan na Fadhila, Mwenye Kurehemu. [Atw-Twuwr (52:28)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ar-Rahiym:
1-Tambua Kwamba Rehma Makhsusi Ya Ar-Rahiym Ni Ya Waumini, Basi Kamilisha Imaan Yako:
Kumbuka, ee Mja wa Ar-Rahiym, kwamba Rehma ya jumla imewaenea viumbe wote duniani, lakini Rehma makhsusi, ya hidaaya, tawfiyq, maghfirah na Jannah, ni ya Waumini watiifu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٧١﴾
Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki wandani. Wanaamrisha mema na wanakataza munkari na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [At-Tawbah (9:71)]
2-Rehma Ya Allaah Imekienea Kila Kitu, Na Ameiandika Makhsusi Kwa Wenye Taqwa:
Kumbuka kwamba Rehma ya Ar-Rahiym imeenea kila kitu duniani, lakini Rehma makhsusi ya Aakhirah Ameiandika kwa wenye taqwa.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاكْتُبْ لَنَا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ إِنَّا هُدْنَا إِلَيْكَ ۚ قَالَ عَذَابِي أُصِيبُ بِهِ مَنْ أَشَاءُ ۖ وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ۚ فَسَأَكْتُبُهَا لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِنَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٥٦﴾
Na Tuandikie katika dunia hii mazuri na katika Aakhirah. Hakika sisi tumerudi kutubu Kwako. (Allaah) Akasema: Adhabu Yangu Nitamsibu nayo Nimtakaye. Na Rehma Yangu imeenea kila kitu. Basi Nitawaandikia wale wenye taqwa na wanaotoa Zakaah na ambao wao wanaziamini Aayaat (na Ishara, Hoja, Dalili) Zetu. [Al-A’raaf (7:156)]
3-Rehma Yake Imeshinda Ghadhabu Yake:
Rehma ya Ar-Rahiym inatangulia na kushinda Ghadhabu Yake; na hili linamjaza Muumini matumaini makubwa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لَمَّا قَضَى اللَّهُ الْخَلْقَ كَتَبَ فِي كِتَابِهِ، فَهُوَ عِنْدَهُ فَوْقَ الْعَرْشِ: إِنَّ رَحْمَتِي غَلَبَتْ غَضَبِي))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Alipomaliza kuumba viumbe, Aliandika katika Kitabu Chake, nacho kiko Kwake juu ya ‘Arsh: Hakika Rehma Yangu imeshinda Ghadhabu Yangu.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
4-Allaah Ana Rehma Zaidi Kwa Waja Wake Kuliko Mama Kwa Mwanawe:
Tambua kwamba Rehma ya Ar-Rahiym kwa Waja Wake ni kubwa kuliko rehma ya mama kwa mwanawe:
عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) قَالَ: قُدِمَ عَلَى النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) سَبْيٌ، فَإِذَا امْرَأَةٌ مِنَ السَّبْيِ قَدْ تَحْلُبُ ثَدْيَهَا تَسْقِي، إِذَا وَجَدَتْ صَبِيًّا فِي السَّبْيِ أَخَذَتْهُ فَأَلْصَقَتْهُ بِبَطْنِهَا وَأَرْضَعَتْهُ، فَقَالَ لَنَا النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((أَتُرَوْنَ هَذِهِ طَارِحَةً وَلَدَهَا فِي النَّارِ؟)) قُلْنَا: لاَ، وَهِيَ تَقْدِرُ عَلَى أَنْ لاَ تَطْرَحَهُ. فَقَالَ: ((لَلَّهُ أَرْحَمُ بِعِبَادِهِ مِنْ هَذِهِ بِوَلَدِهَا))
Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه): Waliletwa mateka kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na mwanamke mmoja kati yao alikuwa amejaa maziwa matitini, akimtafuta mwanawe. Alipomwona mtoto kati ya mateka, alimchukua, akamkumbatia tumboni mwake na kumnyonyesha. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akatuambia: “Je, mnaona mwanamke huyu atamtupa mwanawe motoni?” Tukasema: Hapana, maadamu anaweza kutomtupa. Akasema: “Allaah Ana Rehma zaidi kwa Waja Wake kuliko mwanamke huyu kwa mwanawe.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
5-Usikate Tamaa Na Rehma Ya Rabb Wako:
Tambua kwamba kukata tamaa na Rehma ya Ar-Rahiym ni sifa ya wapotofu, na Muumini daima yuko kati ya khofu na matumaini. Haya ni maneno ya Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) alipobashiriwa mwana katika uzee wake:
قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ﴿٥٦﴾
Akasema: Na nani anayekata tamaa na Rehma ya Rabb wake isipokuwa wapotofu? [Al-Hijr (15:56)]
6-Kuingia Jannah Ni Kwa Rehma Ya Allaah, Basi Usijione Kwa Amali Yako:
Mja asitegemee amali yake peke yake, bali atambue kwamba kuingia Jannah ni kwa Rehma ya Ar-Rahiym, hata kama amali ni sababu. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((لَنْ يُدْخِلَ أَحَدًا عَمَلُهُ الْجَنَّةَ)) قَالُوا: وَلاَ أَنْتَ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: ((لاَ، وَلاَ أَنَا، إِلاَّ أَنْ يَتَغَمَّدَنِي اللَّهُ بِفَضْلٍ وَرَحْمَةٍ، فَسَدِّدُوا وَقَارِبُوا))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Hakuna yeyote ambaye amali yake itamwingiza Jannah.” Wakasema: Hata wewe Yaa Rasula-Allaah? Akasema: “Hapana, hata mimi, isipokuwa Allaah Anifunike kwa Fadhila na Rehma (Yake). Basi fanyeni sawasawa na kurubianeni (na ukamilifu).” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
7-Kithirisha Tawbah Kwani Ar-Rahiym Anapokea Tawbah Ya Waja Wake:
Tambua, ee Mja wa Ar-Rahiym: Kila unapoteleza, rejea kwa Allaah kwa tawbah ya kweli, kwani Yeye Ndiye Mwenye kuipokea na kuwarehemu wenye kutubia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ﴿١٠٤﴾
Je, hawajui kwamba Allaah Ndiye Anayekubali tawbah ya Waja Wake, na Anapokea swadaqa, na kwamba Allaah Ndiye Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Kurehemu? [At-Tawbah (9:104)]
8-Mtii Allaah Na Rasuli Wake Upate Kurehemewa:
Utiifu ndio njia ya kupata Rehma ya Ar-Rahiym. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿١٣٢﴾
Na mtiini Allaah na Rasuli mpate kurehemewa. [Aal-‘Imraan (3:132)]
9-Fanya Ihsaan Kwani Rehma Ya Allaah Iko Karibu Na Wafanyao Ihsaan:
Tambua kwamba kadiri unavyofanya ihsaan, ndivyo unavyokaribia Rehma ya Ar-Rahiym.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا وَادْعُوهُ خَوْفًا وَطَمَعًا ۚ إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾
Na wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya (Allaah) kuitengeneza sawa, na muombeni kwa khofu na matumaini. Hakika Rehma ya Allaah iko karibu na wafanyao ihsaan. [Al-A’raaf (7:56)]
10-Warehemu Watu Ili Allaah Akurehemu:
Tahadhari na ususuwavu wa moyo, kwani asiyewarehemu watu hanyimwi isipokuwa Rehma ya Ar-Rahiym. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ جَرِيرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((لاَ يَرْحَمُ اللَّهُ مَنْ لاَ يَرْحَمُ النَّاسَ))
Amesimulia Jariyr bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Hamrehemu asiyewarehemu watu.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
11-Warehemu Hata Wanyama:
Tambua kwamba Rehma ya Muumini inaenea hata kwa wanyama, na kwa hiyo hupata Rehma ya Ar-Rahiym na Maghfirah Yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((بَيْنَا رَجُلٌ يَمْشِي فَاشْتَدَّ عَلَيْهِ الْعَطَشُ، فَنَزَلَ بِئْرًا فَشَرِبَ مِنْهَا، ثُمَّ خَرَجَ فَإِذَا هُوَ بِكَلْبٍ يَلْهَثُ يَأْكُلُ الثَّرَى مِنَ الْعَطَشِ، فَقَالَ: لَقَدْ بَلَغَ هَذَا مِثْلُ الَّذِي بَلَغَ بِي، فَمَلأَ خُفَّهُ ثُمَّ أَمْسَكَهُ بِفِيهِ، ثُمَّ رَقِيَ فَسَقَى الْكَلْبَ، فَشَكَرَ اللَّهُ لَهُ فَغَفَرَ لَهُ)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، وَإِنَّ لَنَا فِي الْبَهَائِمِ أَجْرًا؟ قَالَ: ((فِي كُلِّ كَبِدٍ رَطْبَةٍ أَجْرٌ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mtu mmoja alikuwa akitembea, kiu ikamzidi. Akateremka kisimani akanywa, kisha akatoka, akamkuta mbwa anahema kwa ulimi akila udongo kwa kiu. Akasema: Huyu amefikwa na (kiu) kama iliyonifika mimi. Akajaza khufu lake maji, kisha akalishika kwa mdomo wake, akapanda, akamnywesha mbwa. Allaah Akamshukuru, Akamghufuria.” Wakasema: Yaa Rasula-Allaah! Je, hata kwa wanyama tuna ujira? Akasema: “Katika kila (kiumbe) chenye ini bichi (hai) kuna ujira.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
12-Jaalia Nyumba Yako Kuwa Mahali Pa Mapenzi Na Rehma:
Katika Neema za Ar-Rahiym ni kujaalia baina ya mume na mke mapenzi na rehma; basi zihifadhi neema hizi kwa kuhurumiana na kusameheana. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٢١﴾
Na katika Aayaat (Ishara, Dalili) Zake ni kwamba Amekuumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao, na Amekujaalieni baina yenu mapenzi na rehma. Hakika katika hayo, bila shaka kuna Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa watu wanaotafakari. [Ar-Ruwm (30:21)]
13-Muombe Ar-Rahmaan Ar-Rahiym Akurehemu Duniani Na Aakhirah:
Muombe, ee Mja wa Ar-Rahiym, Allaah kwa Majina Yake haya mawili, kama alivyofundisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) du’aa hii:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ لِمُعَاذٍ: ((أَلَا أُعَلِّمُكَ دُعَاءً تَدْعُو بِهِ لَوْ كَانَ عَلَيْكَ مِثْلُ جَبَلِ أُحُدٍ دَيْنًا لَأَدَّاهُ اللَّهُ عَنْكَ؟ قُلْ يَا مُعَاذُ: اللَّهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَنْ تَشَاءُ وَتَنْزِعُ الْمُلْكَ مِمَّنْ تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَنْ تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَنْ تَشَاءُ بِيَدِكَ الْخَيْرُ إِنَّكَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، رَحْمَنَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَرَحِيمَهُمَا، تُعْطِيهِمَا مَنْ تَشَاءُ وَتَمْنَعُ مِنْهُمَا مَنْ تَشَاءُ، ارْحَمْنِي رَحْمَةً تُغْنِينِي بِهَا عَنْ رَحْمَةِ مَنْ سِوَاكَ))
Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Mu’aadh: “Je, nikufundishe du’aa utakayoiomba, hata kama ungekuwa na deni mfano wa mlima wa Uhud, Allaah Angekulipia? Sema Yaa Mu’aadh:
اللَّهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَنْ تَشَاءُ وَتَنْزِعُ الْمُلْكَ مِمَّنْ تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَنْ تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَنْ تَشَاءُ بِيَدِكَ الْخَيْرُ إِنَّكَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، رَحْمَنَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَرَحِيمَهُمَا، تُعْطِيهِمَا مَنْ تَشَاءُ وَتَمْنَعُ مِنْهُمَا مَنْ تَشَاءُ، ارْحَمْنِي رَحْمَةً تُغْنِينِي بِهَا عَنْ رَحْمَةِ مَنْ سِوَاكَ
Yaa Allaah, Mfalme Uliyemiliki ufalme wote, Unampa ufalme Umtakaye na Unamuondoshea ufalme Umtakaye, na Unamtukuza Umtakaye na Unamdhalilisha Umtakaye; kheri imo Mkononi Mwako, hakika Wewe juu ya kila kitu Ni Muweza. Mwingi wa Rehma wa dunia na Aakhirah na Mwenye Kurehemu katika zote mbili, Unampa Umtakaye (Rehma ya) zote mbili, na Unamnyima Umtakaye; nirehemu Rehma itakayonitosheleza kwayo na rehma ya asiyekuwa Wewe.” [Atw-Twabaraaniy, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh At-Targhiyb (1821)]
14-Muombe Ar-Rahiym Akughufurie Na Akurehemu:
Omba, ee Mja wa Ar-Rahiym, du’aa ya Nabiy Nuwh (عليه السلام) aliyoiomba baada ya kuonywa na Rabb wake:
قَالَ رَبِّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ أَنْ أَسْأَلَكَ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ ۖ وَإِلَّا تَغْفِرْ لِي وَتَرْحَمْنِي أَكُن مِّنَ الْخَاسِرِينَ﴿٤٧﴾
Akasema: Ee Rabb wangu! Hakika mimi najikinga Kwako kukuomba yale nisiyo na ilimu nayo. Na Usiponighufuria na Ukanirehemu, nitakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Huwd (11:47)]
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema: الرَّحْمَنُ دَالٌّ عَلَى الصِّفَةِ الْقَائِمَةِ بِهِ سُبْحَانَهُ، وَالرَّحِيمُ دَالٌّ عَلَى تَعَلُّقِهَا بِالْمَرْحُومِ، فَكَانَ الْأَوَّلُ لِلْوَصْفِ وَالثَّانِي لِلْفِعْلِ، فَالْأَوَّلُ دَالٌّ أَنَّ الرَّحْمَةَ صِفَتُهُ، وَالثَّانِي دَالٌّ عَلَى أَنَّهُ يَرْحَمُ خَلْقَهُ بِرَحْمَتِهِ، وَإِذَا أَرَدْتَ فَهْمَ هَذَا فَتَأَمَّلْ قَوْلَهُ: ﴿وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا﴾، ﴿إِنَّهُ بِهِمْ رَءُوفٌ رَحِيمٌ﴾، وَلَمْ يَجِئْ قَطُّ: رَحْمَنٌ بِهِمْ — “Ar-Rahmaan linajulisha Sifa iliyosimama Kwake (سبحانه وتعالى), na Ar-Rahiym linajulisha kufikia kwake (Rehma hiyo) kwa anayerehemewa. Kwa hiyo la kwanza ni la Sifa, na la pili ni la kitendo; la kwanza linaonyesha kwamba Rehma ni Sifa Yake, na la pili linaonyesha kwamba Anawarehemu viumbe Vyake kwa Rehma Yake. Ukitaka kulifahamu hili, tafakari Kauli Yake: ‘Na kwa Waumini daima Ni Mwenye Kurehemu’, na ‘Hakika Yeye kwao Ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu’; na haijapata kuja kamwe: ‘Rahmaan kwao’.” [Badaai’ Al-Fawaaid; imenukuliwa pia na Kalemtayeb na IslamQA (283502)]