Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 006 kati ya 103
Al-Hayy — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Hayyu: Aliye Hai daima; Mwenye uhai kamili usiotanguliwa na kutokuwepo, wala usiofikwa na kutoweka.

Al-Hayyu ni kinyume cha maiti. Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mwenye uhai mkamilifu katika Dhati Yake na mkamilifu katika muda wake; hakuna katika viumbe mwenye uhai kwa dhati yake isipokuwa Allaah (عزّ وجلّ) Peke Yake, na kila mwenye uhai amepewa uhai huo na Yeye. Uhai Wake haukutanguliwa na kutokuwepo, wala haumfikii kutoweka wala kuondoka. Kila kitu kitaangamia isipokuwa Yeye kama Anavyosema:

وَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۘ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٨٨﴾

Na wala usiombe pamoja na Allaah mwabudiwa mwingine. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Kila kitu ni chenye kuhiliki isipokuwa Wajihi Wake. Hukumu ni Yake Pekee na Kwake Pekee mtarejeshwa. [Al-Qaswasw (28:88)]

Na Anasema pia:

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٢٧﴾

Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka. Na utabakia Wajihi wa Rabb wako Mwenye Ujalali na Ukarimu. [Ar-Rahmaan (55:26-27)]

Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amesema:

أي: كل من على الأرض، من إنس وجن ودواب وسائر المخلوقات، يفنى ويموت ويبيد، ويبقى الحي الذي لا يموت

“Yaani, kila kilichopo juu ya ardhi miongoni mwa binaadam, majini, wanyama na viumbe vyote vinginevyo, vitatoweka, vitakufa na vitaangamia, na Atabakia Aliye Hai Ambaye Hafi.” [Tafsiyr As-Sa’diy]

Na katika ukamilifu wa uhai Wake, Hachukuliwi na usingizi wala kusinzia, wala Hapatwi na upungufu, udhaifu wala usahaulifu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ ﴿٢٥٥﴾

Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Al-Hayyu (Aliye Hai daima) Al-Qayyuwm (Msimamia kila kitu). Haumchukui usingizi wala kulala. Ni Vyake Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya Idhini Yake? Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawawezi kufikia kuelewa chochote kuhusu Ujuzi Wake isipokuwa kwa Alitakalo. Imeenea Kursiyy Yake mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Naye ni Mwenye ‘Uluwa, Mwenye Taadhima. [Al-Baqarah (2:255)]

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara tano (5). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ وَسَبِّحْ بِحَمْدِهِ ۚ وَكَفَىٰ بِهِ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا ﴿٥٨﴾

Na tawakali kwa Aliye Hai Ambaye Hafi, na sabihi ukimhimidi. Na Inamtosheleza kuwa Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kuhusu dhambi za Waja Wake. [Al-Furqaan (25:58)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ الْحَيُّ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ ۗ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴿٦٥﴾

Yeye Ndiye Aliye Hai daima, hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi muombeni Yeye kwa kumtakasia Dini. AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Rabb wa walimwengu. [Ghaafir (40:65)]

Na limetajwa pamoja na Jina Lake Al-Qayyuwm (Msimamizi wa kila kitu) mara tatu: katika Aayatul-Kursiy; Al-Baqarah (2:255) (Rejea juu), na katika Aayah zifuatazo:

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ﴿٢﴾

Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Al-Hayyu (Aliye Hai daima) Al-Qayyuwm (Msimamia kila kitu). [Aal-‘Imraan (3:2)]

وَعَنَتِ الْوُجُوهُ لِلْحَيِّ الْقَيُّومِ ۖ وَقَدْ خَابَ مَنْ حَمَلَ ظُلْمًا ﴿١١١﴾

Nyuso zitanyenyekea kwa Al-Hayyu (Aliye Hai daima), Al-Qayyuwm (Msimamizi wa kila kitu). Na kwa yakini ameharibikiwa abebaye dhulma. [Twaahaa (20:111)]

Al-Hayyu Al-Qayyuwm Na Jina Tukufu Kabisa La Allaah:

Majina haya mawili ni miongoni mwa yale ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametaja kuwa Jina Tukufu kabisa la Allaah (الاسم الأعظم) limo ndani yake; Jina ambalo Akiombwa kwalo Huitikia.1 Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي أُمَامَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((اسْمُ اللَّهِ الأَعْظَمُ الَّذِي إِذَا دُعِيَ بِهِ أَجَابَ فِي سُوَرٍ ثَلاَثٍ: الْبَقَرَةِ وَآلِ عِمْرَانَ وَطه))

Amesimulia Abuu Umaamah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Jina Tukufu kabisa la Allaah Ambalo Akiombwa kwalo Huitikia, limo katika Suwrah tatu: Al-Baqarah, Aal-‘Imraan na Twaahaa.” [Ibn Maajah (3856), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Al-Jaami’ (979)]

Na pia:

عَنْ أَسْمَاءَ بِنْتِ يَزِيدَ (رضي الله عنها) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((اسْمُ اللَّهِ الأَعْظَمُ فِي هَاتَيْنِ الآيَتَيْنِ: وَإِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الرَّحْمَنُ الرَّحِيمُ، وَفَاتِحَةِ آلِ عِمْرَانَ: الم اللَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ))

Amesimulia Asmaa bint Yaziyd (رضي الله عنها) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Jina Tukufu kabisa la Allaah limo katika Aayah mbili hizi: ‘Na Ilaah wenu ni Ilaah Mmoja, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Ar-Rahmaan, Ar-Rahiym’, na mwanzo wa Aal-‘Imraan: ‘Alif Laam Miym. Allaah, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Al-Hayyu Al-Qayyuwm’.” [Abuu Daawuwd (1496), At-Tirmidhiy (3478), Ibn Maajah (3855), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Al-Jaami’ (980)]

Aayah ya kwanza ni Al-Baqarah (2:163), na ya pili ni Aal-‘Imraan (3:2). Rejea juu.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Hayyu:

1-Uhai Kamili Ni Wa Allaah Pekee, Na Uhai Wa Viumbe Ni Kupewa Na Utaisha:

Tambua kwamba uhai wako ni amana na zawadi kutoka kwa Al-Hayyu; Yeye Ndiye Anayehuisha na Kufisha. Basi utumie uhai wako katika kumtii Aliyekupa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ فَإِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ﴿٦٨﴾

Yeye Ni Yule Anayehuisha na Anayefisha. Na Anapolikidhia jambo lolote basi Huliambia: Kun! (Kuwa), nalo linakuwa. [Ghaafir (40:68)]

2-Asiyekuwa Na Uhai Wa Dhati Hastahiki Kuabudiwa:

Tambua, ee Mja wa Al-Hayy: Kila kinachoabudiwa badala ya Allaah kinakufa au hakina uhai kabisa, basi vipi kiombwe au kitegemewe? Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَاتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً لَّا يَخْلُقُونَ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ وَلَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا وَلَا يَمْلِكُونَ مَوْتًا وَلَا حَيَاةً وَلَا نُشُورًا ﴿٣﴾

Na wakachukua badala Yake (Allaah) waabudiwa wasioumba chochote na hali wao wanaumbwa, wala hawamiliki kwa ajili ya nafsi zao dhara wala manufaa, wala hawamiliki mauti wala uhai wala ufufuo. [Al-Furqaan (25:3)]

3-Al-Hayyu Anahuisha Ardhi Iliyokufa, Na Hiyo Ni Dalili Ya Kufufuliwa:

Tambua, ee Mja wa Al-Hayy: Aliye Hai daima Ndiye Mwenye kutoa uhai. Kama Anavyoihuisha ardhi kwa mvua baada ya kufa kwake, ndivyo Atakavyowafufua wafu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَانظُرْ إِلَىٰ آثَارِ رَحْمَتِ اللَّـهِ كَيْفَ يُحْيِي الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٥٠﴾

Basi tazama athari za Rehma ya Allaah! Vipi Anaihuisha ardhi baada ya kufa kwake! Hakika (Afanyayo) hayo, Ndiye bila shaka Mwenye Kuhuisha wafu, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza. [Ar-Ruwm (30:50)]

4-Tawakali Kwa Al-Hayyu Asiyekufa:

Tambua, ee Mja wa Al-Hayy: Anayemtegemea kiumbe, anamtegemea anayekufa; na anayemtegemea Allaah, anamtegemea Aliye Hai Asiyekufa. Rejea Al-Furqaan (25:58) juu. Na katika du’aa za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُولُ: ((اللَّهُمَّ لَكَ أَسْلَمْتُ، وَبِكَ آمَنْتُ، وَعَلَيْكَ تَوَكَّلْتُ، وَإِلَيْكَ أَنَبْتُ، وَبِكَ خَاصَمْتُ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِعِزَّتِكَ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ أَنْ تُضِلَّنِي، أَنْتَ الْحَيُّ الَّذِي لاَ يَمُوتُ، وَالْجِنُّ وَالإِنْسُ يَمُوتُونَ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema:

اللَّهُمَّ لَكَ أَسْلَمْتُ، وَبِكَ آمَنْتُ، وَعَلَيْكَ تَوَكَّلْتُ، وَإِلَيْكَ أَنَبْتُ، وَبِكَ خَاصَمْتُ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِعِزَّتِكَ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ أَنْ تُضِلَّنِي، أَنْتَ الْحَيُّ الَّذِي لاَ يَمُوتُ، وَالْجِنُّ وَالإِنْسُ يَمُوتُونَ

“Yaa Allaah! Kwako nimejisalimisha, na Kwako nimeamini, na Kwako nimetawakali, na Kwako nimerejea kutubia, na kwa (hoja Zako) nimeshindana (na maadui). Yaa Allaah! Hakika mimi najikinga kwa Utukufu wa Enzi Yako, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Usinipoteze. Wewe Ndiye Uliye Hai Usiyekufa, na majini na wanaadam wanakufa.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Mwombe Al-Hayyu Peke Yake Kwa Ikhlaasw:

Allaah Ameamrisha kuombwa Yeye Pekee kwa kumtakasia Dini baada ya kujitaja kwa Jina Lake Al-Hayyu; rejea Ghaafir (40:65) juu. Na Ameahidi kuwaitikia wanaomwomba:

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ ﴿٦٠﴾

Na Rabb wenu Amesema: Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu wataingia Jahannam wadhalilike. [Ghaafir (40:60)]

6-Itikia Wito Wa Allaah Na Rasuli Wake Upate Uhai Wa Kweli:

Tambua kwamba uhai wa kweli wa moyo ni kuitikia wito wa Al-Hayy na Rasuli Wake; asiyeitikia, moyo wake ni kama maiti hata kama mwili wake uko hai. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ۖ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ﴿٢٤﴾

Enyi walioamini! Muitikieni Allaah na Rasuli Anapokuiteni kwenye yale yenye kukupeni uhai mwema (wa dunia na Aakhirah). Na jueni kwamba Allaah Anaingilia kati baina ya mtu na moyo wake, na kwamba Kwake mtakusanywa. [Al-Anfaal (8:24)]

7-Uhai Wa Moyo Ni Kwa Nuru Ya Imaan Na Qur-aan:

Tambua kwamba Al-Hayy Ameufananisha moyo usio na imaan na maiti, na Uongofu na nuru kuwa ndio uhai wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَوَمَن كَانَ مَيْتًا فَأَحْيَيْنَاهُ وَجَعَلْنَا لَهُ نُورًا يَمْشِي بِهِ فِي النَّاسِ كَمَن مَّثَلُهُ فِي الظُّلُمَاتِ لَيْسَ بِخَارِجٍ مِّنْهَا ۚ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْكَافِرِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٢٢﴾

Je, aliyekuwa maiti kisha Tukamhuisha na Tukamjaalia nuru anatembea nayo kati ya watu, ni sawa na yule ambaye yumo katika viza hawezi kutoka humo? Hivyo ndivyo walivyopambiwa makafiri yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-An’aam (6:122)]

8-Mdhukuru Al-Hayyu Upate Uhai Wa Moyo:

Tambua kwamba kumdhukuru Al-Hayy ndiko kunakoupa moyo uhai. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي مُوسَى (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((مَثَلُ الَّذِي يَذْكُرُ رَبَّهُ وَالَّذِي لاَ يَذْكُرُ رَبَّهُ مَثَلُ الْحَيِّ وَالْمَيِّتِ))

Amesimulia Abuu Muwsaa (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mfano wa anayemdhukuru Rabb wake na asiyemdhukuru Rabb wake ni kama mfano wa aliye hai na maiti.” [Al-Bukhaariy]

9-Tenda Mema Upate Uhai Mzuri Duniani Na Malipo Aakhirah:

Al-Hayyu Ameahidi uhai mzuri kwa Muumini anayetenda mema; uhai wa utulivu, kuridhika na rizqi ya halali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٧﴾

Mwenye kutenda mema miongoni mwa wanamume au wanawake naye ni Muumin, hakika Tutamhuisha uhai mzuri, na bila shaka Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda. [An-Nahl (16:97)]

10-Tambua Kwamba Uhai Halisi Ni Uhai Wa Aakhirah:

Tambua, ee Mja wa Al-Hayy: Uhai wa dunia ni mchezo na pumbao, na uhai wa kweli usiokwisha ni ule wa Aakhirah; basi jiandae kwa ajili yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ ۚ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٦٤﴾

Na huu uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni pumbao na mchezo. Na hakika Nyumba ya Aakhirah bila shaka ndiyo yenye uhai wa kweli hasa (wa milele), lau wangelikuwa wanajua! [Al-‘Ankabuwt (29:64)]

11-Mdhukuru Al-Hayyu Hata Katika Masoko Na Sehemu Za Mighafala:

Tambua kwamba katika masoko watu hughafilika kwa mambo ya dunia; basi mwenye kumdhukuru Al-Hayy humo hupata malipo makubwa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ دَخَلَ السُّوقَ فَقَالَ: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، يُحْيِي وَيُمِيتُ، وَهُوَ حَيٌّ لاَ يَمُوتُ، بِيَدِهِ الْخَيْرُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، كَتَبَ اللَّهُ لَهُ أَلْفَ أَلْفِ حَسَنَةٍ، وَمَحَا عَنْهُ أَلْفَ أَلْفِ سَيِّئَةٍ، وَرَفَعَ لَهُ أَلْفَ أَلْفِ دَرَجَةٍ))

Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayeingia sokoni akasema:

لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، يُحْيِي وَيُمِيتُ، وَهُوَ حَيٌّ لاَ يَمُوتُ، بِيَدِهِ الْخَيْرُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Peke Yake, Hana mshirika, ni Wake Ufalme na ni Zake Himdi, Anahuisha na Anafisha, Naye Ni Hai Hafi, kheri imo Mkononi Mwake, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza; Allaah Atamwandikia mema milioni moja, na Atamfutia maovu milioni moja, na Atamnyanyua daraja milioni moja.” [At-Tirmidhiy (3428), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

12-Omba Uokozi Kwa Al-Hayyu Al-Qayyuwm Katika Shida:

Omba, ee Mja wa Al-Hayy, du’aa hii unapofikwa na jambo zito, kama alivyokuwa akifanya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiomba kwa Majina haya mawili anapofikwa na dhiki:

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم) إِذَا كَرَبَهُ أَمْرٌ قَالَ: ((يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ بِرَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ))

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapofikwa na jambo zito husema:

يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ بِرَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ

“Yaa Uliye Hai daima, yaa Msimamizi wa kila kitu, kwa Rehma Yako naomba uokozi.” [At-Tirmidhiy (3524), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

13-Dumisha Du’aa Ya Asubuhi Na Jioni Kwa Al-Hayyu Al-Qayyuwm:

Omba du’aa hii kila asubuhi na jioni, ukimwomba Al-Hayyu Al-Qayyuwm Akutengenezee mambo yako yote.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuusia binti yake Faatwimah (رضي الله عنها) du’aa hii:

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) لِفَاطِمَةَ (رضي الله عنها): ((مَا يَمْنَعُكِ أَنْ تَسْمَعِي مَا أُوصِيكِ بِهِ؟ أَنْ تَقُولِي إِذَا أَصْبَحْتِ وَإِذَا أَمْسَيْتِ: يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ بِرَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ، أَصْلِحْ لِي شَأْنِي كُلَّهُ، وَلاَ تَكِلْنِي إِلَى نَفْسِي طَرْفَةَ عَيْنٍ))

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Faatwimah (رضي الله عنها): “Nini kinakuzuia kusikiliza ninayokuusia? Useme unapoamka asubuhi na unapoingia jioni:

يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ بِرَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ، أَصْلِحْ لِي شَأْنِي كُلَّهُ، وَلاَ تَكِلْنِي إِلَى نَفْسِي طَرْفَةَ عَيْنٍ

Yaa Uliye Hai daima, yaa Msimamizi wa kila kitu, kwa Rehma Yako naomba uokozi; nitengenezee mambo yangu yote, wala Usiniachie nafsi yangu hata kwa muda wa kupepesa jicho.” [An-Nasaaiy katika As-Sunan Al-Kubraa (10405), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Al-Jaami’ (5820)]

14-Omba Maghfirah Kwa Al-Hayyu Al-Qayyuwm:

Omba maghfirah kwa maneno haya, ukimtaja Allaah kwa Majina Yake Al-Hayyu Al-Qayyuwm.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ زَيْدٍ مَوْلَى النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ سَمِعَ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((مَنْ قَالَ: أَسْتَغْفِرُ اللَّهَ الَّذِي لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيَّ الْقَيُّومَ وَأَتُوبُ إِلَيْهِ، غُفِرَ لَهُ وَإِنْ كَانَ فَرَّ مِنَ الزَّحْفِ))

Amesimulia Zayd, Mawlaa wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), kwamba alimsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Atakayesema:

أَسْتَغْفِرُ اللَّهَ الَّذِي لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيَّ الْقَيُّومَ وَأَتُوبُ إِلَيْهِ

Namuomba maghfirah Allaah Ambaye hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Aliye Hai daima, Msimamizi wa kila kitu, na natubia Kwake; ataghufuriwa hata kama amekimbia katika safu ya vita.” [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (2727)]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema: فَإِنَّ صِفَةَ الْحَيَاةِ مُتَضَمِّنَةٌ لِجَمِيعِ صِفَاتِ الْكَمَالِ، مُسْتَلْزِمَةٌ لَهَا، وَصِفَةُ الْقَيُّومِيَّةِ مُتَضَمِّنَةٌ لِجَمِيعِ صِفَاتِ الْأَفْعَالِ، وَلِهَذَا كَانَ اسْمُ اللَّهِ الْأَعْظَمُ الَّذِي إِذَا دُعِيَ بِهِ أَجَابَ، وَإِذَا سُئِلَ بِهِ أَعْطَى: هُوَ اسْمُ الْحَيِّ الْقَيُّومِ — “Hakika Sifa ya uhai inajumuisha Sifa zote za ukamilifu na inazilazimisha, na Sifa ya usimamizi (Al-Qayyuwmiyyah) inajumuisha Sifa zote za vitendo. Na kwa ajili hiyo Jina Tukufu kabisa la Allaah, Ambalo Akiombwa kwalo Huitikia na Akitakwa kwalo Hutoa, ni Jina Al-Hayyu Al-Qayyuwm.” [Zaad Al-Ma’aad, mlango wa matibabu ya dhiki na huzuni; imenukuliwa pia na Islamweb (Fatwa 425611)]