Al-Qayyuwm: Msimamizi wa kila kitu; Aliyesimama kwa Dhati Yake bila kumhitajia yeyote, na Anayesimamia na kuendesha mambo ya viumbe Vyake vyote.
Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Al-Qayyuwm, Msimamizi wa kila kitu. Jina hili limetajwa katika Qur-aan mara tatu (3), na kila mara limekuja pamoja na Jina Lake Al-Hayyu, kama ilivyotangulia katika 006-Al-Hayy. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ ﴿٢٥٥﴾
Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Al-Hayyu (Aliye Hai daima) Al-Qayyuwm (Msimamia kila kitu). Haumchukui usingizi wala kulala. Ni Vyake Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya Idhini Yake? Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawawezi kufikia kuelewa chochote kuhusu Ujuzi Wake isipokuwa kwa Alitakalo. Imeenea Kursiyy Yake mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Naye ni Mwenye ‘Uluwa, Mwenye Taadhima. [Al-Baqarah (2:255)]
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ﴿٢﴾
Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Al-Hayyu (Aliye Hai daima) Al-Qayyuwm (Msimamia kila kitu). [Aal-‘Imraan (3:2)]
Na Anasema pia:
وَعَنَتِ الْوُجُوهُ لِلْحَيِّ الْقَيُّومِ ۖ وَقَدْ خَابَ مَنْ حَمَلَ ظُلْمًا ﴿١١١﴾
Nyuso zitanyenyekea kwa Al-Hayyu (Aliye Hai daima), Al-Qayyuwm (Msimamizi wa kila kitu). Na kwa yakini ameharibikiwa abebaye dhulma. [Twaahaa (20:111)]
Maana Ya Al-Qayyuwm:
1-Aliyesimama kwa Dhati Yake daima; Hamhitajii yeyote kwa namna yoyote ile, kwa sababu ya ukamilifu Wake, kujitosheleza Kwake na Uwezo Wake.
2-Anayewasimamia viumbe Vyake vyote vilivyomo ardhini na mbinguni; vyote ni mafakiri Kwake, Naye Ndiye Mkwasi Asiyehitaji chochote. Hata ‘Arsh imesimama kwa Uwezo Wake, na hali kadhaalika Malaika wanaoibeba. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿١٥﴾
Enyi watu! Nyinyi ni mafakiri kwa Allaah! Na Allaah Ndiye Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Faatwir (35:15)]
3-Anayesimamia ulimwengu wote; wa juu na wa chini, na viumbe vyote vilivyomo katika hali zao zote: kwa kuwaruzuku, kuwahifadhi, kuwaongoza, na kuwapa kila wanachokihitaji ili waendelee kuwepo na kustawi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قَالَ فَمَن رَّبُّكُمَا يَا مُوسَىٰ ﴿٤٩﴾ قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴿٥٠﴾
(Firawni) akasema: Basi ni nani Rabb wenu ee Muwsaa? (Muwsaa) akasema: Rabb wetu ni Yule Aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha Akakiongoza. [Twaahaa (20:49-50)]
Na Anasema:
وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا ۚ كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ﴿٦﴾
Na hakuna kiumbe chochote kitembeacho katika ardhi isipokuwa rizki yake iko kwa Allaah, na (Allaah) Anajua mahali pake pa kustakiri na pa kuhifadhiwa kwake. Yote yamo katika Kitabu kinachobainisha. [Huwd (11:6)]
4-Anayedumu kusimamia kila kitu daima, hata baada ya Qiyaamah pale Atakapowaingiza Waumini Jannah na makafiri motoni; Hatoweki wala Habadiliki, Amesifika kwa ukamilifu daima.
5-Anayeisimamia kila nafsi kwa kuichunga na kuihesabu, na kuilipa kwa kila dogo na kubwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَفَمَنْ هُوَ قَائِمٌ عَلَىٰ كُلِّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۗ وَجَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ قُلْ سَمُّوهُمْ ۚ أَمْ تُنَبِّئُونَهُ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي الْأَرْضِ أَم بِظَاهِرٍ مِّنَ الْقَوْلِ ۗ بَلْ زُيِّنَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا مَكْرُهُمْ وَصُدُّوا عَنِ السَّبِيلِ ۗ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ ﴿٣٣﴾
Je, basi Anayeisimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, (ni sawa na waabudiwa wa uongo?). Hata hivyo wanamfanyia Allaah washirika. Sema: Watajeni! Au, mnampa khabari kwa yale Asiyoyajua katika ardhi, au ni kudhihirisha maneno ya uongo tu? Bali waliokufuru wamepambiwa njama zao na wamezuiliwa na njia (ya haki). Na ambaye Allaah Amempotoa, basi hana wa kumhidi. [Ar-Ra’d (13:33)]
6-Usimamizi Wake umekamilika: Amezisimamisha mbingu na ardhi nazo zimetulia; mbingu zimesimama bila ya nguzo, wala hazianguki juu ya ardhi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
خَلَقَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِكُمْ وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ ۚ وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ ﴿١٠﴾
(Allaah) Ameumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona, na Akaweka katika ardhi milima iliyosimama imara ili isiyumbe nanyi, na Akaeneza humo kila viumbe vinavyotembea. Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji, Tukaotesha humo kila aina ya mimea mizuri yenye manufaa. [Luqmaan (31:10)]
Na Anasema:
إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا ۚ وَلَئِن زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِّن بَعْدِهِ ۚ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤١﴾
Hakika Allaah Anazuia mbingu na ardhi zisitoweke. Na zikitoweka, hakuna yeyote wa kuzishikilia baada Yake. Hakika Yeye daima Ni Mvumilivu, Mwingi wa Kughufuria. [Faatwir (35:41)]
Kisha Siku ya Qiyaamah Ataibadilisha ardhi kuwa ardhi nyingine, na mbingu pia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ ۖ وَبَرَزُوا لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ﴿٤٨﴾
Siku ardhi itakapobadilishwa kuwa ardhi nyingine na mbingu pia, na (viumbe wote) watahudhuria kwa Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika. [Ibraahiym (14:48)]
7-Anasimamia mambo ya viumbe Vyake na kuyapanga kwa ukamilifu, uadilifu na haki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١٨﴾
Allaah Ameshuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, na (pia) Malaika na wenye ilimu wameshuhudia hilo. Na Yeye mbali ya hilo, Anasifika kwa uadilifu. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Aal-‘Imraan (3:18)]
8-Katika ukamilifu wa usimamizi Wake ni kwamba Hashikwi na usingizi wala kusinzia; rejea Aayatul-Kursiy; Al-Baqarah (2:255) juu. Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي مُوسَى (رضي الله عنه) قَالَ: قَامَ فِينَا رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) بِخَمْسِ كَلِمَاتٍ فَقَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لاَ يَنَامُ، وَلاَ يَنْبَغِي لَهُ أَنْ يَنَامَ، يَخْفِضُ الْقِسْطَ وَيَرْفَعُهُ، يُرْفَعُ إِلَيْهِ عَمَلُ اللَّيْلِ قَبْلَ عَمَلِ النَّهَارِ، وَعَمَلُ النَّهَارِ قَبْلَ عَمَلِ اللَّيْلِ، حِجَابُهُ النُّورُ، لَوْ كَشَفَهُ لأَحْرَقَتْ سُبُحَاتُ وَجْهِهِ مَا انْتَهَى إِلَيْهِ بَصَرُهُ مِنْ خَلْقِهِ))
Amesimulia Abuu Muwsaa (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisimama kati yetu akasema mambo matano: “Hakika Allaah (عزّ وجلّ) Halali, na wala haimpasi Kulala. Anaiteremsha mizani na Kuiinua. Amali ya usiku inapandishwa Kwake kabla ya amali ya mchana, na amali ya mchana kabla ya amali ya usiku. Pazia Lake ni Nuru; lau Angeliliondoa, basi Utukufu wa Wajihi Wake ungeliunguza viumbe Vyake vyote vinavyofikiwa na Macho Yake.” [Muslim]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Qayyuwm:
1-Tambua Kwamba Wewe Ni Fakiri Kwa Al-Qayyuwm Katika Kila Pumzi:
Tambua, ee Mja wa Al-Qayyuwm: Hakuna kiumbe kinachoweza kusimama kwa nafsi yake hata kwa kupepesa jicho; kila neema uliyonayo ni kutoka Kwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ ﴿٣﴾
Enyi watu! Kumbukeni Neema za Allaah kwenu. Je, kuna muumbaji yeyote badala ya Allaah Anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi vipi mnaghilibiwa? [Faatwir (35:3)]
2-Tambua Utukufu Wa Aayatul-Kursiy Iliyobeba Jina Al-Hayyu Al-Qayyuwm:
Tambua, ee Mja wa Al-Qayyuwm: Aayah tukufu kabisa katika Kitabu cha Allaah ni ile iliyobeba Majina haya mawili pamoja na Sifa za usimamizi Wake:
عَنْ أُبَيِّ بْنِ كَعْبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((يَا أَبَا الْمُنْذِرِ، أَتَدْرِي أَيُّ آيَةٍ مِنْ كِتَابِ اللَّهِ مَعَكَ أَعْظَمُ؟)) قَالَ: قُلْتُ: اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ. قَالَ: ((يَا أَبَا الْمُنْذِرِ، أَتَدْرِي أَيُّ آيَةٍ مِنْ كِتَابِ اللَّهِ مَعَكَ أَعْظَمُ؟)) قَالَ: قُلْتُ: ﴿اللَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ﴾. قَالَ: فَضَرَبَ فِي صَدْرِي وَقَالَ: ((وَاللَّهِ لِيَهْنِكَ الْعِلْمُ أَبَا الْمُنْذِرِ))
Amesimulia Ubayy bin Ka’b (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniuliza: “Yaa Abal-Mundhir! Unajua ni Aayah ipi katika Kitabu cha Allaah uliyonayo iliyo tukufu kabisa?” Nikasema: Allaah na Rasuli Wake Wanajua zaidi. Akasema tena: “Yaa Abal-Mundhir! Unajua ni Aayah ipi katika Kitabu cha Allaah uliyonayo iliyo tukufu kabisa?” Nikasema: ﴿اللَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ﴾ (Aayatul-Kursiy). Akanipiga kifuani mwangu (kwa furaha), akasema: “Wa-Allaahi, hongera kwa ilimu yaa Abal-Mundhir!” [Muslim]
3-Mtegemee Al-Qayyuwm Peke Yake Katika Mambo Yako Yote:
Tambua, ee Mja wa Al-Qayyuwm: Anayesimamia kila kitu Ndiye Anayestahiki kutegemewa; basi mwachie mambo yako baada ya kuchukua sababu za halali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾
Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatazamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza Kusudio Lake. Allaah Amejaalia makadirio kwa kila kitu. [Atw-Twalaaq (65:3)]
4-Usijione Kuwa Unasimamia Mambo Yako Kwa Uwezo Wako:
Mja hawezi kusimamia hata jambo la kesho yake bila Mapenzi ya Al-Qayyuwm; basi aunganishe kila azimio lake na Mapenzi ya Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا ﴿٢٣﴾ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ وَاذْكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ وَقُلْ عَسَىٰ أَن يَهْدِيَنِ رَبِّي لِأَقْرَبَ مِنْ هَـٰذَا رَشَدًا ﴿٢٤﴾
Na wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile: Nitalifanya hilo kesho. Isipokuwa (useme): In Shaa Allaah. Na mdhukuru Rabb wako unaposahau. Na sema: Asaa Rabb wangu Akaniongoa njia iliyo karibu zaidi ya uongofu kuliko hii. [Al-Kahf (18:23-24)]
5-Jihesabu Kwa Kuwa Al-Qayyuwm Anaisimamia Kila Nafsi:
Tambua kwamba Al-Qayyuwm Anaisimamia kila nafsi kwa ilimu na hesabu; basi jihesabu kabla hujahesabiwa.
Rejea Ar-Ra’d (13:33) juu. Kumbuka kwamba hakuna amali, hata iwe ndogo vipi, inayofichikana Kwake:
يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ ﴿١٦﴾
Ee mwanangu! Hakika likiweko (zuri au ovu) lolote lenye uzito wa punje ya hardali, likawa katika jabali au mbinguni au ardhini, Allaah Atalileta tu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Luqmaan (31:16)]
6-Kuwa Msimamizi Madhubuti Wa Haki Na Uadilifu:
Mwenye kumjua Al-Qayyuwm Ambaye Anasimamia mambo ya viumbe kwa uadilifu, hujitahidi naye kusimama kidete kwa haki na uadilifu katika kila analolisimamia; familia yake, kazi yake na ushahidi wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّـهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ ۚ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقِيرًا فَاللَّـهُ أَوْلَىٰ بِهِمَا ۖ فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَن تَعْدِلُوا ۚ وَإِن تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿١٣٥﴾
Enyi walioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu kwa nguvu zote (na) wenye kutoa ushahidi kwa ajili ya Allaah tu japokuwa ni dhidi ya nafsi zenu, au wazazi wawili, au jamaa wa karibu. Akiwa tajiri au maskini, Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate hawaa mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkikanusha basi hakika Allaah kwa yale myatendayo Ni Mjuzi daima wa Khabari za dhahiri na siri. [An-Nisaa (4:135)]
7-Pata Utulivu Kwa Kujua Kwamba Mlinzi Wako Halali Wala Hasinzii:
Wanaadam hulala na kughafilika, lakini Al-Qayyuwm Hashikwi na usingizi wala kusinzia; basi mkabidhi Yeye hifadhi ya nafsi yako, ahli zako na mali yako. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قَالَ هَلْ آمَنُكُمْ عَلَيْهِ إِلَّا كَمَا أَمِنتُكُمْ عَلَىٰ أَخِيهِ مِن قَبْلُ ۖ فَاللَّـهُ خَيْرٌ حَافِظًا ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٦٤﴾
Akasema: Vipi nimwaminishe kwenu kama nilivyokuaminini kwa kaka yake kabla? Basi Allaah Ni Mbora wa wenye kuhifadhi. Naye Ni Mbora zaidi wa Kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu. [Yuwsuf (12:64)]
8-Tuliza Moyo Wako Kwa Kumdhukuru Al-Qayyuwm:
Tambua, ee Mja wa Al-Qayyuwm: Anayejua kwamba mambo yake yako Mikononi mwa Msimamizi wa kila kitu, hutulia moyo wake na huondokewa na wasiwasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾
Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa Dhikru-Allaah. Tanabahi! Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia! [Ar-Ra’d (13:28)]
9-Soma Aayatul-Kursiy Kabla Ya Kulala Upate Hifadhi Ya Allaah:
Tambua, ee Mja wa Al-Qayyuwm: Katika Hadiyth ndefu ya Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) alipokuwa akilinda Zakaah ya Ramadhwaan:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) فِي قِصَّةِ حِفْظِهِ زَكَاةَ رَمَضَانَ، أَنَّ الَّذِي جَاءَهُ قَالَ لَهُ: إِذَا أَوَيْتَ إِلَى فِرَاشِكَ فَاقْرَأْ آيَةَ الْكُرْسِيِّ، لَنْ يَزَالَ عَلَيْكَ مِنَ اللَّهِ حَافِظٌ، وَلاَ يَقْرَبُكَ شَيْطَانٌ حَتَّى تُصْبِحَ. فَقَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((صَدَقَكَ وَهُوَ كَذُوبٌ، ذَاكَ شَيْطَانٌ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) katika kisa chake cha kulinda Zakaah ya Ramadhwaan, kwamba yule aliyemjia alimwambia: Unapoliendea tandiko lako, soma Aayatul-Kursiy; utaendelea kuwa na mlinzi kutoka kwa Allaah, na shaytwaan hatokukaribia mpaka asubuhi. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Amekuambia kweli na hali yeye ni mwongo mkubwa; huyo ni shaytwaan.” [Al-Bukhaariy]
10-Mhimidi Al-Qayyuwm Katika Kisimamo Cha Usiku:
Mhimidi Al-Qayyuwm katika kisimamo chako cha usiku kwa maneno aliyokuwa akiyasema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akimhimidi Allaah kwa usimamizi Wake wa mbingu na ardhi katika Swalaah zake za usiku:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: كَانَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم) إِذَا قَامَ مِنَ اللَّيْلِ يَتَهَجَّدُ قَالَ: ((اللَّهُمَّ لَكَ الْحَمْدُ، أَنْتَ قَيِّمُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ وَمَنْ فِيهِنَّ، وَلَكَ الْحَمْدُ، لَكَ مُلْكُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ وَمَنْ فِيهِنَّ، وَلَكَ الْحَمْدُ، أَنْتَ نُورُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ وَمَنْ فِيهِنَّ، وَلَكَ الْحَمْدُ، أَنْتَ مَلِكُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، وَلَكَ الْحَمْدُ، أَنْتَ الْحَقُّ، وَوَعْدُكَ الْحَقُّ، وَلِقَاؤُكَ حَقٌّ، وَقَوْلُكَ حَقٌّ، وَالْجَنَّةُ حَقٌّ، وَالنَّارُ حَقٌّ، وَالنَّبِيُّونَ حَقٌّ، وَمُحَمَّدٌ (صلى الله عليه وسلم) حَقٌّ، وَالسَّاعَةُ حَقٌّ...))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anaposimama usiku kuswali tahajjud husema:
اللَّهُمَّ لَكَ الْحَمْدُ، أَنْتَ قَيِّمُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ وَمَنْ فِيهِنَّ، وَلَكَ الْحَمْدُ، لَكَ مُلْكُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ وَمَنْ فِيهِنَّ، وَلَكَ الْحَمْدُ، أَنْتَ نُورُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ وَمَنْ فِيهِنَّ، وَلَكَ الْحَمْدُ، أَنْتَ مَلِكُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، وَلَكَ الْحَمْدُ، أَنْتَ الْحَقُّ، وَوَعْدُكَ الْحَقُّ، وَلِقَاؤُكَ حَقٌّ، وَقَوْلُكَ حَقٌّ، وَالْجَنَّةُ حَقٌّ، وَالنَّارُ حَقٌّ، وَالنَّبِيُّونَ حَقٌّ، وَمُحَمَّدٌ (صلى الله عليه وسلم) حَقٌّ، وَالسَّاعَةُ حَقٌّ
“Yaa Allaah! Himdi ni Zako; Wewe Ndiye Msimamizi wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Na Himdi ni Zako; ni Wako ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Na Himdi ni Zako; Wewe Ndiye Nuru ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Na Himdi ni Zako; Wewe Ndiye Mfalme wa mbingu na ardhi. Na Himdi ni Zako; Wewe Ndiye Haki, na Ahadi Yako ni haki, na kukutana Nawe ni haki, na Kauli Yako ni haki, na Jannah ni haki, na moto ni haki, na Manabii ni haki, na Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni haki, na Saa (Qiyaamah) ni haki…” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
11-Mwombe Al-Qayyuwm Akutengenezee Mambo Yako Yote Asubuhi Na Jioni:
Omba du’aa hii asubuhi na jioni, ukimwomba Al-Qayyuwm Asimamie mambo yako yote wala Asikuachie nafsi yako.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuusia binti yake Faatwimah (رضي الله عنها) du’aa hii ya kumwomba Al-Hayyu Al-Qayyuwm Asimamie mambo yake yote:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) لِفَاطِمَةَ (رضي الله عنها): ((مَا يَمْنَعُكِ أَنْ تَسْمَعِي مَا أُوصِيكِ بِهِ؟ أَنْ تَقُولِي إِذَا أَصْبَحْتِ وَإِذَا أَمْسَيْتِ: يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ بِرَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ، أَصْلِحْ لِي شَأْنِي كُلَّهُ، وَلاَ تَكِلْنِي إِلَى نَفْسِي طَرْفَةَ عَيْنٍ))
Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Faatwimah (رضي الله عنها): “Nini kinakuzuia kusikiliza ninayokuusia? Useme unapoamka asubuhi na unapoingia jioni:
يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ بِرَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ، أَصْلِحْ لِي شَأْنِي كُلَّهُ، وَلاَ تَكِلْنِي إِلَى نَفْسِي طَرْفَةَ عَيْنٍ
Yaa Uliye Hai daima, yaa Msimamizi wa kila kitu, kwa Rehma Yako naomba uokozi; nitengenezee mambo yangu yote, wala Usiniachie nafsi yangu hata kwa muda wa kupepesa jicho.” [An-Nasaaiy katika As-Sunan Al-Kubraa (10405), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Al-Jaami’ (5820)]
12-Mwombe Allaah Kwa Jina Lake Tukufu Kabisa Al-Hayyu Al-Qayyuwm:
Omba du’aa kwa Jina Tukufu kabisa la Al-Qayyuwm, kwani Akiombwa kwalo Huitikia.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimsikia mtu akiomba kwa du’aa ifuatayo, akasema kwamba ameomba kwa Jina Tukufu kabisa la Allaah:
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) أَنَّهُ كَانَ مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) جَالِسًا وَرَجُلٌ يُصَلِّي، ثُمَّ دَعَا: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ بِأَنَّ لَكَ الْحَمْدَ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ، الْمَنَّانُ، بَدِيعُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، يَا ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرَامِ، يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ، إِنِّي أَسْأَلُكَ الْجَنَّةَ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ النَّارِ. فَقَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((لَقَدْ دَعَا اللَّهَ بِاسْمِهِ الْعَظِيمِ الَّذِي إِذَا دُعِيَ بِهِ أَجَابَ، وَإِذَا سُئِلَ بِهِ أَعْطَى))
Amesimulia Anas (رضي الله عنه) kwamba alikuwa amekaa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na mtu mmoja alikuwa akiswali, kisha akaomba:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ بِأَنَّ لَكَ الْحَمْدَ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ، الْمَنَّانُ، بَدِيعُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، يَا ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرَامِ، يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ، إِنِّي أَسْأَلُكَ الْجَنَّةَ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ النَّارِ
Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba kwa kuwa Himdi ni Zako, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Mwingi wa kuneemesha, Mbunifu wa mbingu na ardhi (bila ya mfano uliotangulia), yaa Mwenye Ujalali na Ukarimu, yaa Uliye Hai daima, yaa Msimamizi wa kila kitu, hakika mimi nakuomba Jannah, na najikinga Kwako na moto. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Kwa yakini amemuomba Allaah kwa Jina Lake Tukufu Ambalo Akiombwa kwalo Huitikia, na Akitakwa kwalo Hutoa.” [Abuu Daawuwd (1495), An-Nasaaiy (1300), Ibn Maajah (3858); Imaam Al-Albaaniy amesema isnaad yake ni nzuri (jayyid) katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (3411)]
Na Allaah Mjuzi zaidi