Asw-Swamad: Bwana Aliyekamilika katika ubwana na Utukufu Wake, Anayekusudiwa na viumbe wote kwa haja zao zote, Naye Hamhitajii yeyote.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1) tu, katika Suwrah Al-Ikhlaasw. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ ﴿١﴾ اللَّـهُ الصَّمَدُ ﴿٢﴾ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ﴿٣﴾ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ﴿٤﴾
Sema: Yeye Allaah Ni Mmoja Pekee. Allaah Aliyekamilika Sifa za Utukufu Wake, Mkusudiwa haja zote. Hakuzaa wala Hakuzaliwa. Na wala haiwi Awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye. [Al-Ikhlaasw (112:1-4)]
Maana Ya Asw-Swamad:
1-Asw-Swamad ni As-Sayyid (Bwana) Aliyekamilika katika ubwana Wake, na Aliyekamilika katika aina zote za ubwana na utukufu mbinguni na ardhini.1 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَلِلَّـهِ الْحَمْدُ رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَرَبِّ الْأَرْضِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٣٦﴾ وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٣٧﴾
Basi AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi, Rabb wa walimwengu. Na Ukubwa, Uadhama, Ujalali ni Wake Pekee mbinguni na ardhini. Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Jaathiyah (45:36-37)]
2-Ni Sifa ambayo haimstahiki yeyote isipokuwa Allaah (عزّ وجلّ). Yeye Ndiye Anayekusudiwa na viumbe Vyake vyote; wanaadam na majini, ulimwengu wa juu na wa chini; wote wanamwelekea Yeye Pekee kwa haja zao.
3-Hakuzaa wala Hakuzaliwa; Hafi wala Harithiwi, kwa sababu kila anayezaliwa atakufa, na kila anayekufa hurithiwa. Na katika Hadiyth Al-Qudsiy Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((قَالَ اللَّهُ: كَذَّبَنِي ابْنُ آدَمَ وَلَمْ يَكُنْ لَهُ ذَلِكَ، وَشَتَمَنِي وَلَمْ يَكُنْ لَهُ ذَلِكَ، فَأَمَّا تَكْذِيبُهُ إِيَّايَ فَقَوْلُهُ: لَنْ يُعِيدَنِي كَمَا بَدَأَنِي، وَلَيْسَ أَوَّلُ الْخَلْقِ بِأَهْوَنَ عَلَيَّ مِنْ إِعَادَتِهِ، وَأَمَّا شَتْمُهُ إِيَّايَ فَقَوْلُهُ: اتَّخَذَ اللَّهُ وَلَدًا، وَأَنَا الأَحَدُ الصَّمَدُ، لَمْ أَلِدْ وَلَمْ أُولَدْ، وَلَمْ يَكُنْ لِي كُفْئًا أَحَدٌ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Amesema: Mwanaadam amenikadhibisha na hakuwa na haki ya kufanya hivyo, na amenitukana na hakuwa na haki ya kufanya hivyo. Ama kunikadhibisha kwake ni kusema: Hatonirudisha (kunifufua) kama Alivyonianzisha. Na uumbaji wa mwanzo si mwepesi zaidi Kwangu kuliko kuurejesha. Ama kunitukana kwake ni kusema: Allaah Amejifanyia mwana. Na hali Mimi Ni Mmoja Pekee, Asw-Swamad, Sikuzaa wala Sikuzaliwa, wala hakuna yeyote anayelingana Nami.” [Al-Bukhaariy]
4-Asw-Swamad ni Yule Ambaye Halishwi wala Hahitaji chakula, bali Yeye Ndiye Anayewalisha viumbe Vyake vyote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلْ أَغَيْرَ اللَّـهِ أَتَّخِذُ وَلِيًّا فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ يُطْعِمُ وَلَا يُطْعَمُ ۗ قُلْ إِنِّي أُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ أَوَّلَ مَنْ أَسْلَمَ ۖ وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٤﴾
Sema: Je, nimfanye rafiki mlinzi asiyekuwa Allaah Mwanzilishi wa mbingu na ardhi, Naye Ndiye Anayelisha na wala Halishwi? Sema: Hakika mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza katika wenye kusilimu. Na wala usijekuwa kabisa miongoni mwa washirikina. [Al-An’aam (6:14)]
5-Ni Yule Ambaye mambo yote yanaishia Kwake, wala halikidhiwi jambo lolote bila ya Yeye; Amri Zake zinatekelezwa mbinguni na ardhini, Naye Atabakia daima baada ya kutoweka kwa viumbe Vyake vyote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلِلَّـهِ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَإِلَيْهِ يُرْجَعُ الْأَمْرُ كُلُّهُ فَاعْبُدْهُ وَتَوَكَّلْ عَلَيْهِ ۚ وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ﴿١٢٣﴾
Na ni ya Allaah (Pekee) ghaibu ya mbingu na ardhi, na Kwake hurudishwa mambo yote, basi mwabudu Yeye na tawakali Kwake. Na Rabb wako Si Mwenye Kughafilika na yale myatendayo. [Huwd (11:123)]
Na Anasema pia:
ثُمَّ أَنزَلَ عَلَيْكُم مِّن بَعْدِ الْغَمِّ أَمَنَةً نُّعَاسًا يَغْشَىٰ طَائِفَةً مِّنكُمْ ۖ وَطَائِفَةٌ قَدْ أَهَمَّتْهُمْ أَنفُسُهُمْ يَظُنُّونَ بِاللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ ظَنَّ الْجَاهِلِيَّةِ ۖ يَقُولُونَ هَل لَّنَا مِنَ الْأَمْرِ مِن شَيْءٍ ۗ قُلْ إِنَّ الْأَمْرَ كُلَّهُ لِلَّـهِ ۗ يُخْفُونَ فِي أَنفُسِهِم مَّا لَا يُبْدُونَ لَكَ ۖ يَقُولُونَ لَوْ كَانَ لَنَا مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ مَّا قُتِلْنَا هَاهُنَا ۗ قُل لَّوْ كُنتُمْ فِي بُيُوتِكُمْ لَبَرَزَ الَّذِينَ كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقَتْلُ إِلَىٰ مَضَاجِعِهِمْ ۖ وَلِيَبْتَلِيَ اللَّـهُ مَا فِي صُدُورِكُمْ وَلِيُمَحِّصَ مَا فِي قُلُوبِكُمْ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿١٥٤﴾
Kisha Akakuteremshieni amani baada ya dhiki; usingizi unaofunika kundi miongoni mwenu na kundi likawashughulisha nafsi zao wakamdhania Allaah pasi na haki dhana ya kijahili, wanasema: Je, tuna amri yoyote sisi katika jambo hili? Sema: Hakika amri yote ni ya Allaah. Wanaficha katika nafsi zao yale wasiyokubainishia. Wanasema: Lau tungelikuwa tuna amri yoyote katika jambo basi tusingeliuliwa hapa. Sema: Lau mngelikuwa majumbani mwenu, bila shaka wangejitokeza wale walioandikiwa kuuawa kwenye mahali pa kuangukia wafe. Ili Allaah Ayajaribu yale yaliyomo katika vifua vyenu na Atakase yale yaliyomo katika nyoyo zenu. Na Allaah Anayajua vyema yaliyomo vifuani. [Aal-‘Imraan (3:154)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Asw-Swamad:
1-Mkusudie Asw-Swamad Peke Yake Kwa Haja Zako Zote:
Tambua, ee Mja wa Asw-Swamad: Kwa kuwa viumbe vyote ni wahitaji Kwake, basi usiielekeze haja yako kwa kiumbe kama unavyomwelekea Muumba; mwombe Yeye Pekee kwanza na mwisho, na moyo wako umwelekee Yeye kwa matumaini na khofu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿١٥﴾
Enyi watu! Nyinyi ni mafakiri kwa Allaah! Na Allaah Ndiye Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Faatwir (35:15)]
2-Tambua Tofauti Ya Muumba Na Kiumbe: Asw-Swamad Hahitaji Chakula Wala Chochote:
Baadhi ya Salaf wamelifasiri Jina Asw-Swamad kwamba ni Yule Ambaye Hana tumbo, Hali wala Hanywi. Kila kiumbe kinahitaji chakula na kinywaji ili kiishi, na hiyo ni dalili ya upungufu wake na kwamba hakistahiki kuabudiwa. Ndio maana Allaah Ametaja kula chakula kwa Nabiy ‘Iysaa na mama yake (عليهما السلام) kuwa ni dalili kwamba si waabudiwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَّا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ ۖ كَانَا يَأْكُلَانِ الطَّعَامَ ۗ انظُرْ كَيْفَ نُبَيِّنُ لَهُمُ الْآيَاتِ ثُمَّ انظُرْ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٧٥﴾
Al-Masiyh mwana wa Maryam si chochote ila ni Rasuli tu, wamekwishapita kabla yake Rusuli (wengine). Na mama yake ni Muumini mkweli wa dhati. Wote wawili walikuwa wanakula chakula. Tazama jinsi Tunavyowabainishia Aayaat (Ishara, Hoja, Dalili) kisha tazama vipi wanavyoghilibiwa. [Al-Maaidah (5:75)]
3-Mtakase Asw-Swamad Na Kila Upungufu, Na Kuwa Na Mke Au Mwana:
Tambua kwamba anayemnasibishia Asw-Swamad mwana au mke amemtukana, kama ilivyotangulia katika Hadiyth Al-Qudsiy juu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ أَنَّىٰ يَكُونُ لَهُ وَلَدٌ وَلَمْ تَكُن لَّهُ صَاحِبَةٌ ۖ وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١٠١﴾
Mbunifu wa mbingu na ardhi (bila ya mfano uliotangulia). Inamkinikaje kuwa Yeye Ana mwana ilhali Hana mke? Naye Ameumba kila kitu, Naye Ni Mjuzi wa kila kitu. [Al-An’aam (6:101)]
4-Suwrah Al-Ikhlaasw Imekusanya Sifa Zote Za Ukamilifu:
Suwrah Al-Ikhlaasw imekusanya Majina mawili ya Allaah; Al-Ahad na Asw-Swamad, ambayo hayakutajwa katika Suwrah nyingine yoyote, na yamekusanya Sifa zote za ukamilifu, na kumtakasa Allaah na kila upungufu. Kwa hiyo inampasa mja ajue kwamba Allaah Ndiye Al-Ahad Asw-Swamad Peke Yake, Hana mshirika; basi asimkusudie mwingine katika ‘ibaadah yake, wala asikimbilie kwa mwingine katika haja zake.2
5-Tosheka Na Asw-Swamad Kwani Yeye Anamtosheleza Mja Wake:
Anayemkusudia Asw-Swamad kwa ukweli hatahitaji kumnyenyekea kiumbe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ ۖ وَيُخَوِّفُونَكَ بِالَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ﴿٣٦﴾
Je, kwani Allaah Si Mwenye Kumtosheleza Mja Wake? Na eti wanakutisha na wale wasiokuwa Yeye. Na ambaye Allaah Amempotoa basi hana wa kumhidi. [Az-Zumar (39:36)]
6-Jiheshimu Na Usijidhalilishe Kwa Kuwaomba Viumbe:
Mwenye kumjua Asw-Swamad huhifadhi heshima yake, kwani anajua kwamba viumbe nao ni wahitaji kama yeye. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuusia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما):
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: كُنْتُ خَلْفَ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَوْمًا فَقَالَ: ((يَا غُلاَمُ، إِنِّي أُعَلِّمُكَ كَلِمَاتٍ: احْفَظِ اللَّهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظِ اللَّهَ تَجِدْهُ تُجَاهَكَ، إِذَا سَأَلْتَ فَاسْأَلِ اللَّهَ، وَإِذَا اسْتَعَنْتَ فَاسْتَعِنْ بِاللَّهِ، وَاعْلَمْ أَنَّ الأُمَّةَ لَوِ اجْتَمَعَتْ عَلَى أَنْ يَنْفَعُوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ لَكَ، وَلَوِ اجْتَمَعُوا عَلَى أَنْ يَضُرُّوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَضُرُّوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ عَلَيْكَ، رُفِعَتِ الأَقْلاَمُ وَجَفَّتِ الصُّحُفُ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nilikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) siku moja, akasema: “Yaa kijana! Hakika mimi nitakufundisha maneno: Mhifadhi Allaah (kwa kutekeleza Amri Zake) Atakuhifadhi. Mhifadhi Allaah utamkuta mbele yako. Ukiomba, muombe Allaah, na ukitaka msaada, taka msaada kwa Allaah. Na jua kwamba lau ummah wote ungekusanyika ili ukunufaishe kwa kitu, usingekunufaisha isipokuwa kwa kitu ambacho Allaah Amekwisha kukuandikia. Na lau wangekusanyika ili wakudhuru kwa kitu, wasingekudhuru isipokuwa kwa kitu ambacho Allaah Amekwisha kukuandikia. Kalamu zimeshainuliwa na sahifa zimekauka.” [At-Tirmidhiy (2516), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
7-Mkimbilie Asw-Swamad Katika Dhiki Na Shida:
Asw-Swamad Ndiye Anayekusudiwa pale haja zinapozidi na njia zinapofungika; Yeye Pekee Ndiye Mwenye kuitikia na kuondoa dhiki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٦٢﴾
Au nani Anayemuitika mwenye dhiki mno anapomwomba, na Akamuondoshea uovu na Akakufanyeni warithi wa ardhi? Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Ni machache mno mnayokumbuka. [An-Naml (27:62)]
8-Kithirisha Kusoma Suwrah Al-Ikhlaasw Ambayo Ni Sawa Na Thuluthi Ya Qur-aan:
Suwrah hii iliyobeba Jina la Asw-Swamad ina fadhila kubwa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم) لأَصْحَابِهِ: ((أَيَعْجِزُ أَحَدُكُمْ أَنْ يَقْرَأَ ثُلُثَ الْقُرْآنِ فِي لَيْلَةٍ؟)) فَشَقَّ ذَلِكَ عَلَيْهِمْ وَقَالُوا: أَيُّنَا يُطِيقُ ذَلِكَ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ فَقَالَ: ((اللَّهُ الْوَاحِدُ الصَّمَدُ ثُلُثُ الْقُرْآنِ))
Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwaambia Swahaba zake: “Je, mmoja wenu anashindwa kusoma thuluthi ya Qur-aan katika usiku mmoja?” Likawa zito kwao, wakasema: Nani kati yetu anaweza hilo yaa Rasula-Allaah? Akasema: “Allaah Al-Waahid Asw-Swamad (Suwrah Al-Ikhlaasw) ni thuluthi ya Qur-aan.” [Al-Bukhaariy]
Na pia:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَجُلاً سَمِعَ رَجُلاً يَقْرَأُ: قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ يُرَدِّدُهَا، فَلَمَّا أَصْبَحَ جَاءَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) فَذَكَرَ ذَلِكَ لَهُ، وَكَأَنَّ الرَّجُلَ يَتَقَالُّهَا، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ إِنَّهَا لَتَعْدِلُ ثُلُثَ الْقُرْآنِ))
Amesimulia Abuu Sa’iyd (رضي الله عنه) kwamba mtu mmoja alimsikia mtu mwingine akisoma ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾ akiikariri. Asubuhi yake akaenda kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamtajia hilo, na ni kana kwamba aliiona ni kisomo kidogo. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mkononi Mwake, hakika hiyo ni sawa na thuluthi ya Qur-aan.” [Al-Bukhaariy]
9-Ipende Suwrah Al-Ikhlaasw Kwa Kuwa Ni Sifa Ya Ar-Rahmaan, Nawe Allaah Atakupenda:
Tambua kwamba mwenye kuipenda Suwrah hii kwa sababu ya Sifa za Asw-Swamad zilizomo ndani yake, hupata Mapenzi ya Allaah:
عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) بَعَثَ رَجُلاً عَلَى سَرِيَّةٍ، وَكَانَ يَقْرَأُ لأَصْحَابِهِ فِي صَلاَتِهِمْ فَيَخْتِمُ بِـ ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾، فَلَمَّا رَجَعُوا ذَكَرُوا ذَلِكَ لِلنَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فَقَالَ: ((سَلُوهُ لأَيِّ شَيْءٍ يَصْنَعُ ذَلِكَ؟)) فَسَأَلُوهُ فَقَالَ: لأَنَّهَا صِفَةُ الرَّحْمَنِ، وَأَنَا أُحِبُّ أَنْ أَقْرَأَ بِهَا. فَقَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((أَخْبِرُوهُ أَنَّ اللَّهَ يُحِبُّهُ))
Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimtuma mtu mmoja kuongoza kikosi, naye alikuwa akiwaswalisha wenzake na kumalizia (kisomo chake) kwa ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾. Waliporudi walimtajia hilo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), akasema: “Muulizeni kwa nini anafanya hivyo?” Wakamuuliza, akasema: Kwa sababu hiyo ni Sifa ya Ar-Rahmaan, nami napenda kuisoma. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Mjulisheni kwamba Allaah Anampenda.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
10-Isome Suwrah Al-Ikhlaasw Pamoja Na Al-Mu’awwidhatayn Asubuhi Na Jioni:
Kinga kamili ya mja iko kwa Asw-Swamad, Ambaye Anamtosheleza aliyemkusudia. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ خُبَيْبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: خَرَجْنَا فِي لَيْلَةِ مَطَرٍ وَظُلْمَةٍ شَدِيدَةٍ نَطْلُبُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) لِيُصَلِّيَ لَنَا فَأَدْرَكْنَاهُ فَقَالَ: ((قُلْ)). فَلَمْ أَقُلْ شَيْئًا، ثُمَّ قَالَ: ((قُلْ)). فَلَمْ أَقُلْ شَيْئًا، ثُمَّ قَالَ: ((قُلْ)). فَقُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ مَا أَقُولُ؟ قَالَ: ((قُلْ: ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾ وَالْمُعَوِّذَتَيْنِ حِينَ تُمْسِي وَحِينَ تُصْبِحُ ثَلاَثَ مَرَّاتٍ، تَكْفِيكَ مِنْ كُلِّ شَيْءٍ))
Amesimulia ‘Abdullaah bin Khubayb (رضي الله عنه): Tulitoka usiku wa mvua na giza kali kumtafuta Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ili atuswalishe, tukamkuta. Akasema: “Sema.” Sikusema kitu. Kisha akasema: “Sema.” Sikusema kitu. Kisha akasema: “Sema.” Nikasema: Yaa Rasula-Allaah, niseme nini? Akasema: “Soma ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾ na Al-Mu’awwidhatayn (Al-Falaq na An-Naas) unapoingia jioni na unapoamka asubuhi mara tatu, zitakutosheleza kutokana na kila kitu.” [Abuu Daawuwd (5082), At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
11-Mwombe Allaah Kwa Jina Lake Tukufu Kabisa Kupitia Al-Ahad Asw-Swamad:
Omba du’aa kwa Jina Tukufu kabisa la Allaah, ukimtaja kwa Majina Yake Al-Ahad Asw-Swamad.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimsikia mtu akiomba kwa du’aa ifuatayo, akathibitisha kuwa ameomba kwa Jina Tukufu kabisa la Allaah:
عَنْ بُرَيْدَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) سَمِعَ رَجُلاً يَقُولُ: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ بِأَنِّي أَشْهَدُ أَنَّكَ أَنْتَ اللَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ الأَحَدُ الصَّمَدُ الَّذِي لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ. فَقَالَ: ((وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَقَدْ سَأَلَ اللَّهَ بِاسْمِهِ الأَعْظَمِ الَّذِي إِذَا دُعِيَ بِهِ أَجَابَ، وَإِذَا سُئِلَ بِهِ أَعْطَى))
Amesimulia Buraydah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimsikia mtu mmoja akisema:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ بِأَنِّي أَشْهَدُ أَنَّكَ أَنْتَ اللَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ الأَحَدُ الصَّمَدُ الَّذِي لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ
Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba kwa kuwa ninashuhudia kwamba Wewe Ndiye Allaah, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Mmoja Pekee, Asw-Swamad, Ambaye Hakuzaa wala Hakuzaliwa, wala hakuna yeyote anayelingana Naye. Akasema (Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم): “Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mkononi Mwake, kwa yakini amemuomba Allaah kwa Jina Lake Tukufu kabisa Ambalo Akiombwa kwalo Huitikia, na Akitakwa kwalo Hutoa.” [Abuu Daawuwd (1493), At-Tirmidhiy (3475), Ibn Maajah (3857); At-Tirmidhiy amesema: Hasan Ghariyb]
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: هُوَ السَّيِّدُ الَّذِي قَدْ كَمُلَ فِي سُؤْدَدِهِ، وَالشَّرِيفُ الَّذِي قَدْ كَمُلَ فِي شَرَفِهِ، وَالْعَظِيمُ الَّذِي قَدْ كَمُلَ فِي عَظَمَتِهِ، وَالْحَلِيمُ الَّذِي قَدْ كَمُلَ فِي حِلْمِهِ، وَالْعَلِيمُ الَّذِي قَدْ كَمُلَ فِي عِلْمِهِ، وَالْحَكِيمُ الَّذِي قَدْ كَمُلَ فِي حِكْمَتِهِ، وَهُوَ الَّذِي قَدْ كَمُلَ فِي أَنْوَاعِ الشَّرَفِ وَالسُّؤْدَدِ، وَهُوَ اللَّهُ سُبْحَانَهُ، هَذِهِ صِفَتُهُ لَا تَنْبَغِي إِلَّا لَهُ — “Yeye (Asw-Swamad) ni Bwana Aliyekamilika katika ubwana Wake, Mtukufu Aliyekamilika katika utukufu Wake, Adhimu Aliyekamilika katika uadhimu Wake, Mpole Aliyekamilika katika upole Wake, Mjuzi Aliyekamilika katika ujuzi Wake, Mwenye Hikmah Aliyekamilika katika hikmah Yake; Naye Ndiye Aliyekamilika katika aina zote za utukufu na ubwana, Naye Ni Allaah (سبحانه وتعالى). Hii ni Sifa Yake isiyomstahiki yeyote isipokuwa Yeye.” [Tafsiyr Atw-Twabariy na Tafsiyr Ibn Kathiyr, Suwrah Al-Ikhlaasw (112:2)]
- 2Kalemtayeb, maelezo ya Jina Asw-Swamad: Suwrah Al-Ikhlaasw imekusanya Majina mawili Al-Ahad na Asw-Swamad yanayobeba Sifa za ukamilifu na kumtakasa Allaah na kila upungufu.