Al-Awwal: Wa Awali Ambaye hakuna kitu chochote kabla Yake; Aliyekuwepo bila ya mwanzo.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1), likiwa pamoja na Majina Yake mengine matatu: Al-Aakhir, Adhw-Dhwaahir na Al-Baatwin. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣﴾
Yeye Ndiye wa Awali hakuna kitu kabla Yake, na wa Mwisho hakuna kitu baada Yake, na Aliye juu hakuna kitu juu Yake, na Aliye karibu, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Yeye, Naye kwa kila kitu Ni Mjuzi. [Al-Hadiyd (57:3)]
Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameyafasiri Majina haya manne katika du’aa aliyowafundisha Swahaba zake:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَأْمُرُنَا إِذَا أَخَذْنَا مَضْجَعَنَا أَنْ نَقُولَ: ((اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ وَرَبَّ الأَرْضِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ، فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى، وَمُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ وَالْفُرْقَانِ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَيْءٍ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ، اللَّهُمَّ أَنْتَ الأَوَّلُ فَلَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الآخِرُ فَلَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الْبَاطِنُ فَلَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ، اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ، وَأَغْنِنَا مِنَ الْفَقْرِ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akituamrisha tunapolala tuseme:
اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ وَرَبَّ الأَرْضِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ، فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى، وَمُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ وَالْفُرْقَانِ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَيْءٍ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ، اللَّهُمَّ أَنْتَ الأَوَّلُ فَلَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الآخِرُ فَلَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الْبَاطِنُ فَلَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ، اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ، وَأَغْنِنَا مِنَ الْفَقْرِ
“Yaa Allaah! Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi na Rabb wa ‘Arsh adhimu, Rabb wetu na Rabb wa kila kitu, Mpasuaji wa mbegu na kokwa, Mteremshaji wa Tawraat na Injiyl na Al-Furqaan (Qur-aan); najikinga Kwako kutokana na shari ya kila kitu ambacho Wewe Umeshika utosi wake. Yaa Allaah! Wewe Ndiye wa Awali, hakuna kitu kabla Yako; na Wewe Ndiye wa Mwisho, hakuna kitu baada Yako; na Wewe Ndiye Uliye juu, hakuna kitu juu Yako; na Wewe Ndiye Uliye karibu, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Wewe. Tulipie deni, na Utukwase tuondokane na ufakiri.” [Muslim]
Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye wa Awali, na hakukuwepo kitu chochote kabla Yake, hata kabla ya kuumba kitu chochote. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عِمْرَانَ بْنِ حُصَيْنٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((كَانَ اللَّهُ وَلَمْ يَكُنْ شَيْءٌ قَبْلَهُ، وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ، ثُمَّ خَلَقَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضَ، وَكَتَبَ فِي الذِّكْرِ كُلَّ شَيْءٍ))
Amesimulia ‘Imraan bin Huswayn (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Alikuwepo na hakukuwa na kitu chochote kabla Yake, na ‘Arsh Yake ilikuwa juu ya maji, kisha Akaumba mbingu na ardhi, na Akaandika kila kitu katika Adh-Dhikr (Al-Lawh Al-Mahfuwdhw; Ubao Uliohifadhiwa).” [Al-Bukhaariy]
Maana Ya Al-Awwal:
Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Aliyetangulia kila kitu katika kuwepo Kwake na katika Sifa Zake; kuwepo Kwake hakuna mwanzo. Kila kiumbe kina mwanzo wake na mwisho wake isipokuwa Yeye (عزّ وجلّ). Kila kitu kimetoka Kwake kwa kuumbwa, kinaendelea kuwepo kwa Uwezo Wake, na kitarejea Kwake. Ndio maana Muumini anapofikwa na msiba husema maneno ya Istirjaa’ (kutamka kurejea kwa Allaah) Aliyoyafundisha Allaah katika Kitabu Chake:
الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾
Wale ambao unapowafika msiba husema: Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea. [Al-Baqarah (2:156)]
Wa Awali Ambaye kila kitu kimeanzia Kwake, basi Anastahiki kuwa Ndiye wa kwanza katika moyo wa mja; kupendwa kwanza, kutegemewa kwanza, na kukimbiliwa kwanza kabla ya sababu zote.1
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Awwal:
1-Imaan Kwamba Kila Kilichopo Kimeumbwa Baada Ya Kutokuwepo, Na Allaah Pekee Ndiye Asiye Na Mwanzo:
Tambua, ee Mja wa Al-Awwal: Kwa kuwa Allaah Ndiye wa Awali Ambaye hakuna kitu kabla Yake, basi kila kisichokuwa Yeye; mbingu, ardhi, ‘Arsh, Malaika, wanaadam na kila kiumbe, ni kipya kilichopatikana baada ya kutokuwepo. Hivyo hakuna kiumbe kinachostahiki kuabudiwa, kwani kimeumbwa na Aliye wa Awali. Na katika riwaayah nyingine ya Hadiyth ya ‘Imraan bin Huswayn (رضي الله عنهما) iliyotangulia: “Allaah Alikuwepo na hakukuwa na kitu chochote ghairi Yake.” [Al-Bukhaariy]
2-Tambua Ukwasi Kamili Wa Allaah, Kwani Aliye Kabla Ya Kila Kitu Hakihitajii Chochote:
Tambua kwamba kujua kwamba Al-Awwal Ndiye wa Awali na wa Mwisho kunathibitisha kwamba Yeye Ni Mkwasi kikamilifu; Hakuwaumba waja kwa sababu ya kuwahitajia, bali ili wamwabudu, na wao ndio wenye kumhitajia Yeye daima. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿١٥﴾
Enyi watu! Nyinyi ni mafakiri kwa Allaah! Na Allaah Ndiye Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Faatwir (35:15)]
3-Mtukuze Allaah Kwa Kutambua Kuzunguka Kwake Kwa Kila Kitu:
Majina manne; Al-Awwal, Al-Aakhir, Adhw-Dhwaahir na Al-Baatwin, yanaonyesha Allaah kukizunguka kila kitu: Al-Awwal na Al-Aakhir yanaonyesha kuzunguka Kwake kwa zama, na Adhw-Dhwaahir na Al-Baatwin yanaonyesha kuzunguka Kwake kwa mahali. Hakuna aliyetangulia isipokuwa Allaah Yuko kabla yake, wala hakuna wa mwisho isipokuwa Allaah Yuko baada yake. Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema:
هَذِهِ الْأَسْمَاءُ الْأَرْبَعَةُ: الْأَوَّلُ، وَالْآخِرُ، وَالظَّاهِرُ، وَالْبَاطِنُ، هِيَ أَرْكَانُ الْعِلْمِ وَالْمَعْرِفَةِ، فَحَقِيقٌ بِالْعَبْدِ أَنْ يَبْلُغَ فِي مَعْرِفَتِهَا إِلَى حَيْثُ يَنْتَهِي بِهِ قُوَاهُ وَفَهْمُهُ
“Majina haya manne: Al-Awwal, Al-Aakhir, Adhw-Dhwaahir na Al-Baatwin, ndio nguzo za ilimu na maarifa. Basi inampasa mja afikie katika kuyajua mpaka mwisho wa nguvu zake na ufahamu wake.”2
4-Jina Al-Awwal Linabatilisha Kauli Kwamba Allaah Yuko Kila Mahali:
Tambua kwamba Imaam Ahmad (رحمه الله) amewajibu wanaodai kwamba Al-Awwal Yuko kila mahali kwa hoja ya Jina hili: Je, si Allaah Alikuwepo na hakukuwa na kitu chochote? Watasema: Naam. Basi Alipokiumba kitu, Alikiumba ndani ya Nafsi Yake au nje ya Nafsi Yake? Akisema ndani ya Nafsi Yake, amekufuru. Akisema Alikiumba nje ya Nafsi Yake kisha Akaingia ndani yake, amekufuru pia. Na akisema Alikiumba nje ya Nafsi Yake na Hakuingia ndani yake, basi amerejea katika kauli ya Ahlus-Sunnah: Allaah Yuko juu ya ‘Arsh Yake, Ametengana na viumbe Vyake.3
Ama Kauli Zake Allaah zinazotaja kwamba Yeye Yu pamoja na Waja Wake popote walipo, maana yake ni kuwa Yu pamoja nao kwa Ujuzi Wake, Kusikia Kwake, Kuona Kwake na Uwezo Wake, na si kwa Dhati Yake. Dhati Yake (سبحانه وتعالى) Iko juu ya mbingu, juu ya ‘Arsh, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu. Na hivi ndivyo Aayah zenyewe zinavyobainisha, kwani zinaanza na kumalizika kwa kutaja Ujuzi Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٤﴾
Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arsh. Anajua yale yanayoingia ardhini, na yale yatokayo humo, na yale yanayoteremka kutoka mbinguni, na yale yanayopanda humo. Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah Ni Mwenye Kuona yote myatendayo. [Al-Hadiyd (57:4)]
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ۖ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿٧﴾
Je, huoni kwamba Allaah Anajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye Ni wa Nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye Ni wa Sita wao, na wala chini kuliko ya hivyo, na wala wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao (kwa Ujuzi Wake) popote watakapokuwa. Kisha Siku ya Qiyaamah Atawajulisha yale waliyoyatenda. Hakika Allaah kwa kila kitu Ni Mjuzi. [Al-Mujaadalah (58:7)]
Na hii ndiyo maana ya Jina Lake Al-Muhiytw (Mwenye Kukizunguka kila kitu); Amekizunguka kila kitu kwa Ujuzi Wake na Uwezo Wake, si kwa Dhati Yake kuwa ndani ya viumbe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ وَمِنَ الْأَرْضِ مِثْلَهُنَّ يَتَنَزَّلُ الْأَمْرُ بَيْنَهُنَّ لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا﴿١٢﴾
Allaah Ni Yule Aliyeumba mbingu saba na katika ardhi mfano wa hizo, inateremka amri baina yao ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu Ni Muweza, na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa Ujuzi (Wake). [Atw-Twalaaq (65:12)]
Imaam Maalik (رحمه الله) amesema:
اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ فِي السَّمَاءِ، وَعِلْمُهُ فِي كُلِّ مَكَانٍ، لَا يَخْلُو مِنْهُ شَيْءٌ
“Allaah (عزّ وجلّ) Yuko juu ya mbingu, na Ujuzi Wake uko kila mahali; hakuna kitu kinachokosa Ujuzi Wake.” Kisha akasoma Aayah: “Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye Ni wa Nne wao…”
Na Imaam Ahmad (رحمه الله) aliulizwa: Rabb wetu (تبارك وتعالى) Yuko juu ya mbingu ya saba juu ya ‘Arsh Yake, Ametengana na viumbe Vyake, na Uwezo Wake na Ujuzi Wake uko kila mahali? Akasema:
نَعَمْ، لَا يَخْلُو شَيْءٌ مِنْ عِلْمِهِ
“Naam, hakuna kitu kinachokosa Ujuzi Wake.”
Na akaifasiri Aayah ya Al-Mujaadalah (58:7) kwa kusema:
يَعْنِي: إِلَّا اللَّهُ - بِعِلْمِهِ - رَابِعُهُمْ، ﴿وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ﴾ بِعِلْمِهِ ﴿سَادِسُهُمْ﴾
“Yaani: Isipokuwa Allaah, kwa Ujuzi Wake, Ni wa Nne wao. ‘Na wala watano isipokuwa Yeye’ kwa Ujuzi Wake ‘Ni wa Sita wao’.” Na akasema kwamba Allaah Ameifungua Aayah hii kwa kutaja Ujuzi na Akaifunga kwa kutaja Ujuzi. Kisha akatoa mfano (na Allaah Ana mfano wa juu kabisa):
لَوْ أَنَّ رَجُلًا كَانَ فِي يَدَيْهِ قَدَحٌ مِنْ قَوَارِيرَ صَافٍ، وَفِيهِ شَيْءٌ صَافٍ، لَكَانَ بَصَرُ ابْنِ آدَمَ قَدْ أَحَاطَ بِالْقَدَحِ مِنْ غَيْرِ أَنْ يَكُونَ ابْنُ آدَمَ فِي الْقَدَحِ، وَاللَّهُ - وَلَهُ الْمَثَلُ الْأَعْلَى - قَدْ أَحَاطَ بِجَمِيعِ خَلْقِهِ مِنْ غَيْرِ أَنْ يَكُونَ فِي شَيْءٍ مِنْ خَلْقِهِ. وَخَصْلَةٌ أُخْرَى: لَوْ أَنَّ رَجُلًا بَنَى دَارًا بِجَمِيعِ مَرَافِقِهَا ثُمَّ أَغْلَقَ بَابَهَا وَخَرَجَ مِنْهَا، كَانَ ابْنُ آدَمَ لَا يَخْفَى عَلَيْهِ كَمْ بَيْتٍ فِي دَارِهِ، وَكَمْ سَعَةُ كُلِّ بَيْتٍ، مِنْ غَيْرِ أَنْ يَكُونَ صَاحِبُ الدَّارِ فِي جَوْفِ الدَّارِ. فَاللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ - وَلَهُ الْمَثَلُ الْأَعْلَى - قَدْ أَحَاطَ بِجَمِيعِ مَا خَلَقَ، وَعَلِمَ كَيْفَ هُوَ وَمَا هُوَ، مِنْ غَيْرِ أَنْ يَكُونَ فِي شَيْءٍ مِمَّا خَلَقَ
“Lau mtu angeshika mikononi mwake bilauri safi ya kioo na ndani yake kuna kitu safi, basi macho ya mwanaadam yangeizunguka bilauri bila yeye kuwa ndani ya bilauri. Na Allaah (na Ana mfano wa juu kabisa) Amevizunguka viumbe Vyake vyote bila Yeye kuwa ndani ya chochote katika viumbe Vyake. Na mfano mwingine: Lau mtu angejenga nyumba pamoja na vifaa vyake vyote, kisha akafunga mlango wake na kutoka, mwanaadam huyo hafichikiwi na idadi ya vyumba vilivyomo katika nyumba yake, wala ukubwa wa kila chumba, bila mwenye nyumba kuwa ndani ya nyumba. Basi Allaah (عزّ وجلّ), na Ana mfano wa juu kabisa, Amevizunguka vyote Alivyoviumba, na Anajua vilivyo na hali zake, bila Yeye kuwa ndani ya chochote katika Alivyoviumba.”4
5-Tambua Mwanzo Wako Na Mwisho Wako:
Tambua, ee Mja wa Al-Awwal: Mwanaadam atambue kwamba asili ya kuumbwa kwake ni udongo, na kwamba yeye ana mwanzo, ana uhai kwa muda maalumu, kisha ana mwisho wa kurejea kwa Rabb wa walimwengu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
كَيْفَ تَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَكُنتُمْ أَمْوَاتًا فَأَحْيَاكُمْ ۖ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢٨﴾
Vipi mnamkufuru Allaah na hali mlikuwa wafu Akakuhuisheni, kisha Atakufisheni, kisha Atakuhuisheni, kisha Kwake mtarejeshwa? [Al-Baqarah (2:28)]
Na Anasema pia:
هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٥٦﴾
Yeye Ndiye Anayehuisha na Anayefisha, na Kwake mtarejeshwa. [Yuwnus (10:56)]
6-Tambua Kwamba Kila Kilichoumbwa Kina Mwanzo, Na Allaah Ndiye Aliyekianzisha Na Atakirudisha:
Tambua kwamba kila kilichopo kina mwanzo wake, na Al-Awwal Ndiye Aliyekianzisha, Naye Atakirudisha.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِلَيْهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا ۖ وَعْدَ اللَّـهِ حَقًّا ۚ إِنَّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ بِالْقِسْطِ ۚ وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ﴿٤﴾
Kwake ni marejeo yenu nyote. Ni Ahadi ya Allaah ya kweli. Hakika Yeye Anaanzisha uumbaji, kisha Anaurejesha ili Awalipe kwa uadilifu wale walioamini na wakatenda mema. Na wale waliokufuru watapata kinywaji cha maji ya kuchemka mno, na adhabu iumizayo kwa sababu ya kukufuru kwao. [Yuwnus (10:4)]
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَوْمَ نَطْوِي السَّمَاءَ كَطَيِّ السِّجِلِّ لِلْكُتُبِ ۚ كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ ﴿١٠٤﴾
Siku Tutakapozikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi zilizoandikwa. Kama Tulivyoanza umbo la awali Tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu Yetu. Hakika Sisi Ni Wenye Kufanya. [Al-Anbiyaa (21:104)]
7-Kumbuka Kwamba Fadhila Za Allaah Zimetangulia Kila Neema Uliyonayo, Basi Mshukuru:
Tambua, ee Mja wa Al-Awwal: Kila neema; ya Dini au ya dunia, imeanzia Kwake Yeye Aliye wa Awali. Fadhila Zake zimekutangulia kabla hujaomba, na kabla hujafanya amali yoyote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَمَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَمَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٦٤﴾
Au nani Anayeanzisha uumbaji, kisha Anaurejesha? Na nani Anayekuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Sema: Leteni ushahidi wenu wa wazi mkiwa ni wakweli. [An-Naml (27:64)]
Na Anasema pia:
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَكُمْ ثُمَّ رَزَقَكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ۖ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَفْعَلُ مِن ذَٰلِكُم مِّن شَيْءٍ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٤٠﴾
Allaah, Ndiye Amekuumbeni, kisha Akakuruzukuni, kisha Anakufisheni, kisha Atakuhuisheni. Je, kati ya washirika wenu yuko yeyote yule awezaye kufanya lolote katika hayo? Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa kutokana na yale wanayomshirikisha. [Ar-Ruwm (30:40)]
8-Mwabudu Allaah Kwa Jina Lake Al-Awwal: Usizitegemee Sababu Wala Viumbe:
Tambua kwamba kumwabudu Al-Awwal kwa Jina hili ni kutambua kwamba Fadhila Yake na Ihsaan Yake zimetangulia sababu zote, hivyo moyo usielekee kwa kiumbe, wala usitulie kwa asiyekuwa Yeye, wala usimtegemee asiyekuwa Yeye. Mtangulize Allaah katika mapenzi, katika khofu, katika kutegemea na katika kuomba, na anza mambo yako kwa kumwomba msaada. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾
Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatazamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza Kusudio Lake. Allaah Amejaalia makadirio kwa kila kitu. [Atw-Twalaaq (65:3)]
9-Ridhika Na Qadar Ya Allaah, Na Usiweke Chuki Moyoni Kwa Kiumbe:
Tambua kwamba anayetambua kwamba mwanzo wa kila jambo ni kwa Al-Awwal, na kwamba hakuna kinachotokea isipokuwa kimeandikwa kabla, hupokea misiba kwa subira na ridhaa, na huondokewa na chuki dhidi ya viumbe, kwani viumbe ni sababu tu, na Mwanzilishi wa kila kitu ni Allaah (عزّ وجلّ). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿٢٢﴾
Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla Hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi. [Al-Hadiyd (57:22)]
10-Dumisha Du’aa Ya Kulala Aliyoifundisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
Tambua, ee Mja wa Al-Awwal: Du’aa iliyotajwa juu, inayofasiri Majina manne ya Allaah, isomwe kila unapokwenda kulala, kama alivyoamrisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Swahaba zake. Ndani yake kuna kumtukuza Allaah, kujikinga Kwake na shari ya kila kitu, na kumwomba Akulipie deni na Akukwase uondokane na ufakiri. Rejea Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) juu.
11-Sema Istirjaa’ Na Du’aa Yake Unapofikwa Na Msiba:
Tambua kwamba mwenye kujua kwamba yeye ametoka kwa Al-Awwal na atarejea Kwake, hupokea misiba kwa subira. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ تُصِيبُهُ مُصِيبَةٌ فَيَقُولُ مَا أَمَرَهُ اللَّهُ: إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ، اللَّهُمَّ أْجُرْنِي فِي مُصِيبَتِي وَأَخْلِفْ لِي خَيْرًا مِنْهَا، إِلاَّ أَخْلَفَ اللَّهُ لَهُ خَيْرًا مِنْهَا))
Amesimulia Umm Salamah (رضي الله عنها): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Hakuna Muislamu yeyote anayefikwa na msiba akasema yale Aliyomuamrisha Allaah:
إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ، اللَّهُمَّ أْجُرْنِي فِي مُصِيبَتِي وَأَخْلِفْ لِي خَيْرًا مِنْهَا
Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea. Yaa Allaah! Nilipe ujira katika msiba wangu, na Unipe badala yake kilicho bora kuliko hicho; isipokuwa Allaah Humpa badala yake kilicho bora kuliko hicho.” [Muslim]
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله), Twariyq Al-Hijratayn: فَيُعَامِلُ سَبْقَهُ تَعَالَى بِأَوَّلِيَّتِهِ لِكُلِّ شَيْءٍ، وَسَبْقَهُ بِفَضْلِهِ وَإِحْسَانِهِ الْأَسْبَابَ كُلَّهَا، وَعَدَمِ الِالْتِفَاتِ إِلَى غَيْرِهِ، وَعَدَمِ الْوُثُوقِ بِسِوَاهُ وَالتَّوَكُّلِ عَلَى غَيْرِهِ — “Aamiliane na kutangulia Kwake (Allaah) kwa Uawali Wake kwa kila kitu, na kutangulia kwa Fadhila Yake na Ihsaan Yake kabla ya sababu zote, kwa kutoelekea kwa mwingine, wala kutomwamini asiyekuwa Yeye, wala kutomtegemea mwingine.”
- 2Twariyq Al-Hijratayn (uk. 46). Na Imaam Ibn Abil-‘Izz Al-Hanafiy (رحمه الله) amesema: فَهَذِهِ الْأَسْمَاءُ الْأَرْبَعَةُ مُتَقَابِلَةٌ: اسْمَانِ مِنْهَا لِأَزَلِيَّةِ الرَّبِّ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى وَأَبَدِيَّتِهِ، وَاسْمَانِ لِعُلُوِّهِ وَقُرْبِهِ — “Majina haya manne yanakabiliana: Majina mawili ni ya kuwepo kwa Rabb (سبحانه وتعالى) bila mwanzo na bila mwisho, na mawili ni ya ‘Uluwa Wake na ukaribu Wake.” [Sharh Al-‘Aqiydah Atw-Twahaawiyyah]
- 3Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) ameinukuu hoja hii ya Imaam Ahmad katika Ijtimaa’ Al-Juyuwsh Al-Islaamiyyah.
- 4Kauli ya Imaam Maalik: ‘Abdullaah bin Imaam Ahmad, As-Sunnah (1/106-107); Abuu Daawuwd, Masaail Al-Imaam Ahmad; na Al-Aajurriy, Ash-Sharii’ah. Swali aliloulizwa Imaam Ahmad: Al-Khallaal katika As-Sunnah, na Imaam Ibn Al-Qayyim ameinukuu katika Ijtimaa’ Al-Juyuwsh Al-Islaamiyyah (1/200). Tafsiyr yake ya (58:7) na mifano ya bilauri na nyumba: Imaam Ahmad, Ar-Radd ‘Alaa Al-Jahmiyyah Waz-Zanaadiqah, mlango wa “Maelezo ya yale waliyoyataawili Jahmiyyah katika Kauli ya Allaah: Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye Ni wa Nne wao”. Na tarjama ya Alhidaaya ya Al-Mujaadalah (58:7) imebainisha hilo kwa maneno “(kwa Ujuzi Wake)”.