Al-Aakhir: Wa Mwisho Ambaye hakuna kitu chochote baada Yake; Mwenye kubakia daima baada ya kutoweka kwa kila kiumbe.
Kama ilivyotangulia katika 009-Al-Awwal, Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1), pamoja na Majina Yake mengine matatu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣﴾
Yeye Ndiye wa Awali hakuna kitu kabla Yake, na wa Mwisho hakuna kitu baada Yake, na Aliye juu hakuna kitu juu Yake, na Aliye karibu, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Yeye, Naye kwa kila kitu Ni Mjuzi. [Al-Hadiyd (57:3)]
Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amelifasiri Jina hili kwa kauli yake: “Na Wewe Ndiye wa Mwisho, hakuna kitu baada Yako”, katika du’aa ifuatayo:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَأْمُرُنَا إِذَا أَخَذْنَا مَضْجَعَنَا أَنْ نَقُولَ: ((اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ وَرَبَّ الأَرْضِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ، فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى، وَمُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ وَالْفُرْقَانِ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَيْءٍ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ، اللَّهُمَّ أَنْتَ الأَوَّلُ فَلَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الآخِرُ فَلَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الْبَاطِنُ فَلَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ، اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ، وَأَغْنِنَا مِنَ الْفَقْرِ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akituamrisha tunapolala tuseme:
اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ وَرَبَّ الأَرْضِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ، فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى، وَمُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ وَالْفُرْقَانِ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَيْءٍ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ، اللَّهُمَّ أَنْتَ الأَوَّلُ فَلَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الآخِرُ فَلَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الْبَاطِنُ فَلَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ، اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ، وَأَغْنِنَا مِنَ الْفَقْرِ
“Yaa Allaah! Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi na Rabb wa ‘Arsh adhimu, Rabb wetu na Rabb wa kila kitu, Mpasuaji wa mbegu na kokwa, Mteremshaji wa Tawraat na Injiyl na Al-Furqaan (Qur-aan); najikinga Kwako kutokana na shari ya kila kitu ambacho Wewe Umeshika utosi wake. Yaa Allaah! Wewe Ndiye wa Awali, hakuna kitu kabla Yako; na Wewe Ndiye wa Mwisho, hakuna kitu baada Yako; na Wewe Ndiye Uliye juu, hakuna kitu juu Yako; na Wewe Ndiye Uliye karibu, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Wewe. Tulipie deni, na Utukwase tuondokane na ufakiri.” [Muslim]
Maana Ya Al-Aakhir:
Majina mawili Al-Awwal na Al-Aakhir yanaonyesha kuenea kwa Allaah (عزّ وجلّ) katika zama zote.1 Al-Aakhir ni Yule Ambaye hana ukomo katika kuwepo Kwake wala katika Sifa Zake; Atabakia baada ya kufa na kutoweka kwa kila kitu. Kudumu Kwake ni kwa Dhati Yake, tofauti na viumbe ambavyo Allaah Amevijaalia kudumu kama Jannah, moto, ‘Arsh, Al-Kursiy na Al-Qalam; hivyo havidumu kwa dhati yake, bali vinadumu kwa Idhini ya Allaah na Mapenzi Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۘ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٨٨﴾
Na wala usiombe pamoja na Allaah mwabudiwa mwingine. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Kila kitu ni chenye kuhiliki isipokuwa Wajihi Wake. Hukumu ni Yake Pekee na Kwake Pekee mtarejeshwa. [Al-Qaswasw (28:88)]
Hakuna atakayebakia ardhini wala mbinguni, kwani kila kitu kina mwanzo na mwisho isipokuwa Yeye (عزّ وجلّ). Siku ya Qiyaamah Ataita, na hakuna atakayemjibu, kisha Atajijibu Mwenyewe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
رَفِيعُ الدَّرَجَاتِ ذُو الْعَرْشِ يُلْقِي الرُّوحَ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ لِيُنذِرَ يَوْمَ التَّلَاقِ﴿١٥﴾ يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ﴿١٦﴾
(Allaah) Mwenye ‘Uluwa juu ya vyeo na daraja. Mwenye ‘Arsh, Anapelekea Ar-Ruwh (Wahy) kwa Amri Yake kwa Amtakaye miongoni mwa Waja Wake, ili aonye Siku ya kukutana. Siku watakayotokeza wao, hakitofichika kitu chochote chao kwa Allaah. Ufalme ni wa nani leo? (Allaah Mwenyewe Atajijibu): Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Asiyepingika. [Ghaafir (40:15-16)]
Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((يَطْوِي اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ السَّمَوَاتِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، ثُمَّ يَأْخُذُهُنَّ بِيَدِهِ الْيُمْنَى، ثُمَّ يَقُولُ: أَنَا الْمَلِكُ، أَيْنَ الْجَبَّارُونَ؟ أَيْنَ الْمُتَكَبِّرُونَ؟ ثُمَّ يَطْوِي الأَرَضِينَ بِشِمَالِهِ، ثُمَّ يَقُولُ: أَنَا الْمَلِكُ، أَيْنَ الْجَبَّارُونَ؟ أَيْنَ الْمُتَكَبِّرُونَ؟))
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (عزّ وجلّ) Atazikunja mbingu Siku ya Qiyaamah, kisha Atazishika kwa Mkono Wake wa kulia, kisha Atasema: Mimi Ndiye Mfalme! Wako wapi majabari? Wako wapi wenye kutakabari? Kisha Atazikunja ardhi kwa Mkono Wake mwingine, kisha Atasema: Mimi Ndiye Mfalme! Wako wapi majabari? Wako wapi wenye kutakabari?” [Muslim]
Jina hili linathibitisha kwamba hatima ya wanaadam wote ni kwa Allaah (سبحانه وتعالى), Ambaye Hana mwisho. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۖ ثُمَّ إِلَيْنَا تُرْجَعُونَ ﴿٥٧﴾
Kila nafsi itaonja mauti, kisha Kwetu mtarejeshwa. [Al-‘Ankabuwt (29:57)]
Na Anasema:
قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ ﴿١١﴾
Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu, kisha kwa Rabb wenu mtarejeshwa. [As-Sajdah (32:11)]
Na kwamba mwisho wa mwanaadam ni kurejea kwa Muumba wake (عزّ وجلّ) na kusimamishwa mbele Yake kuhesabiwa matendo yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِلَيْهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا ۖ وَعْدَ اللَّـهِ حَقًّا ۚ إِنَّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ بِالْقِسْطِ ۚ وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ﴿٤﴾
Kwake ni marejeo yenu nyote. Ni Ahadi ya Allaah ya kweli. Hakika Yeye Anaanzisha uumbaji, kisha Anaurejesha ili Awalipe kwa uadilifu wale walioamini na wakatenda mema. Na wale waliokufuru watapata kinywaji cha maji ya kuchemka mno, na adhabu iumizayo kwa sababu ya kukufuru kwao. [Yuwnus (10:4)]
Na Anasema pia:
أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ ﴿١١٥﴾
Je, mlidhania kwamba Sisi Tulikuumbeni bila kusudio mcheze tu, na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa? [Al-Muuminuwn (23:115)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Aakhir:
1-Imaan Kwamba Allaah Pekee Ndiye Anayedumu Kwa Dhati Yake:
Tambua, ee Mja wa Al-Aakhir: Kila kinachoonekana kuwa na nguvu, utajiri au ufalme kitatoweka, na atabakia Allaah Pekee. Basi moyo usishikamane na kitu kitakachotoweka. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٢٧﴾
Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka. Na utabakia Wajihi wa Rabb wako Mwenye Ujalali na Ukarimu. [Ar-Rahmaan (55:26-27)]
2-Mfanye Allaah Kuwa Ndilo Lengo Lako La Mwisho:
Kumwabudu Allaah kwa Jina Lake Al-Aakhir ni kumfanya Yeye Pekee kuwa ndilo lengo lako la mwisho, Ambalo hakuna lengo jingine baada Yake. Kama mambo yote yanavyoishia Kwake, basi jaalia mwisho wa makusudio yako kuwa ni Yeye.2 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَنَّ إِلَىٰ رَبِّكَ الْمُنتَهَىٰ ﴿٤٢﴾
Na kwamba kwa Rabb wako ndio kikomo. [An-Najm (53:42)]
3-Tambua Kwamba Dunia Ni Starehe Ya Muda Mfupi Nayo Itaisha:
Kumbuka kwamba dunia ni starehe fupi itakayoisha, na Al-Aakhir Pekee Ndiye Atakayebakia.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اعْلَمُوا أَنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَزِينَةٌ وَتَفَاخُرٌ بَيْنَكُمْ وَتَكَاثُرٌ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ ۖ كَمَثَلِ غَيْثٍ أَعْجَبَ الْكُفَّارَ نَبَاتُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَكُونُ حُطَامًا ۖ وَفِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَغْفِرَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانٌ ۚ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿٢٠﴾
Jueni kwamba hakika uhai wa dunia ni mchezo na pumbao na mapambo, na kufakharishana baina yenu, na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Ni kama mfano wa mvua inayowafurahisha wakulima mimea yake, kisha inanyweya, basi utaiona imepiga unjano, kisha inakuwa mabua yaliyonyauka na kupondekapondeka. Na Aakhirah kuna adhabu kali, na maghfirah kutoka kwa Allaah na radhi. Na uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni starehe fupi za kughuri. [Al-Hadiyd (57:20)]
4-Kilicho Kwa Allaah Ndicho Kitakachobakia:
Tambua kwamba mali, cheo na starehe zitakwisha, lakini ujira ulio kwa Al-Aakhir hautakwisha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ بَاقٍ ۗ وَلَنَجْزِيَنَّ الَّذِينَ صَبَرُوا أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٦﴾
Mlivyo navyo nyinyi vinatoweka, na vilivyoko kwa Allaah ni vya kubakia. Na kwa yakini Tutawalipa wale waliovuta subira ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda. [An-Nahl (16:96)]
5-Tanguliza Mema Yanayobakia:
Tambua kwamba mema yanayobakia ndiyo akiba yako ya kweli mbele ya Al-Aakhir.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَالْبَاقِيَاتُ الصَّالِحَاتُ خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ أَمَلًا ﴿٤٦﴾
Mali na watoto ni pambo la uhai wa dunia. Na mema yanayobakia ni bora mbele ya Rabb wako kwa thawabu na matumaini mema zaidi. [Al-Kahf (18:46)]
6-Ipe Aakhirah Kipaumbele Kwani Ni Bora Na Ya Kudumu Zaidi:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Aakhir, kwamba Aakhirah ni bora na ya kudumu zaidi; basi usiitangulize dunia juu yake.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
بَلْ تُؤْثِرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿١٦﴾ وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٧﴾
Bali mnahiari zaidi uhai wa dunia. Na hali Aakhirah ni bora zaidi na ya kudumu zaidi. [Al-A’laa (87:16-17)]
7-Kithirisha Kukumbuka Mauti Na Ujiandae Kwa Kukutana Na Rabb Wako:
Tambua, ee Mja wa Al-Aakhir, kwamba kukumbuka mauti huuzindua moyo na humfanya mja ajiandae kwa kukutana na Rabb wake.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَكْثِرُوا ذِكْرَ هَاذِمِ اللَّذَّاتِ)) يَعْنِي الْمَوْتَ
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kithirisheni kukumbuka chenye kukata ladha (za dunia)” yaani mauti. [At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy (1823), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan Swahiyh katika Swahiyh An-Nasaaiy]
8-Jiepushe Na Kiburi Na Dhulma, Kwani Ufalme Wote Utarejea Kwa Allaah:
Tahadhari na kiburi na dhulma, kwani ufalme wote wa dunia utarejea kwa Al-Aakhir.
Rejea Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنهما) juu: “Wako wapi majabari? Wako wapi wenye kutakabari?” Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
تِلْكَ الدَّارُ الْآخِرَةُ نَجْعَلُهَا لِلَّذِينَ لَا يُرِيدُونَ عُلُوًّا فِي الْأَرْضِ وَلَا فَسَادًا ۚ وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٨٣﴾
Hiyo ni nyumba ya Aakhirah, Tunaijaalia kwa wale wasiotaka kujitukuza katika ardhi wala ufisadi. Na hatima njema ni kwa wenye taqwa. [Al-Qaswasw (28:83)]
9-Omba Mwisho Mwema Na Uchunge Amali Zako Za Mwisho:
Tambua, ee Mja wa Al-Aakhir: Kwa kuwa mambo yote yana mwisho, basi mja ahangaikie mwisho wake; kwani amali hupimwa kwa hatima yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّمَا الأَعْمَالُ بِالْخَوَاتِيمِ))
Amesimulia Sahl bin Sa’d (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika amali (hupimwa) kwa hatima zake.” [Al-Bukhaariy]
10-Mkabidhi Allaah Nafsi Yako Na Mambo Yako Kabla Ya Kulala, Na Yajaalie Kuwa Maneno Yako Ya Mwisho:
Tambua kwamba mwenye kutambua kwamba mambo yote yanaishia kwa Al-Aakhir, humkabidhi Yeye nafsi yake na mambo yake yote, kama alivyofundisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
عَنِ الْبَرَاءِ بْنِ عَازِبٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((إِذَا أَتَيْتَ مَضْجَعَكَ فَتَوَضَّأْ وُضُوءَكَ لِلصَّلاَةِ، ثُمَّ اضْطَجِعْ عَلَى شِقِّكَ الأَيْمَنِ، ثُمَّ قُلِ: اللَّهُمَّ أَسْلَمْتُ وَجْهِي إِلَيْكَ، وَفَوَّضْتُ أَمْرِي إِلَيْكَ، وَأَلْجَأْتُ ظَهْرِي إِلَيْكَ، رَغْبَةً وَرَهْبَةً إِلَيْكَ، لاَ مَلْجَأَ وَلاَ مَنْجَا مِنْكَ إِلاَّ إِلَيْكَ، اللَّهُمَّ آمَنْتُ بِكِتَابِكَ الَّذِي أَنْزَلْتَ، وَبِنَبِيِّكَ الَّذِي أَرْسَلْتَ. فَإِنْ مُتَّ مِنْ لَيْلَتِكَ فَأَنْتَ عَلَى الْفِطْرَةِ، وَاجْعَلْهُنَّ آخِرَ مَا تَتَكَلَّمُ بِهِ))
Amesimulia Al-Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Unapoiendea sehemu yako ya kulala, tawadha kama unavyotawadha kwa ajili ya Swalaah, kisha lala kwa ubavu wako wa kulia, kisha sema:
اللَّهُمَّ أَسْلَمْتُ وَجْهِي إِلَيْكَ، وَفَوَّضْتُ أَمْرِي إِلَيْكَ، وَأَلْجَأْتُ ظَهْرِي إِلَيْكَ، رَغْبَةً وَرَهْبَةً إِلَيْكَ، لاَ مَلْجَأَ وَلاَ مَنْجَا مِنْكَ إِلاَّ إِلَيْكَ، اللَّهُمَّ آمَنْتُ بِكِتَابِكَ الَّذِي أَنْزَلْتَ، وَبِنَبِيِّكَ الَّذِي أَرْسَلْتَ
Yaa Allaah! Nimeusalimisha uso wangu Kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe, na nimeutegemeza mgongo wangu Kwako, kwa matumaini na kwa khofu Kwako. Hakuna pa kukimbilia wala pa kuokoka Kwako isipokuwa Kwako. Yaa Allaah! Nimekiamini Kitabu Chako Ulichokiteremsha, na Nabiy Wako Uliyemtuma. Basi ukifa usiku huo, utakuwa juu ya Fitwrah (Uislamu), na jaalia maneno hayo kuwa ya mwisho unayoyatamka.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله), Madaarij As-Saalikiyn (1/31) na Twariyq Al-Hijratayn.
- 2Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله), Twariyq Al-Hijratayn: ثُمَّ تَعَبَّدْ لَهُ بِاسْمِهِ الْآخِرِ: بِأَنْ تَجْعَلَهُ وَحْدَهُ غَايَتَكَ الَّتِي لَا غَايَةَ لَكَ سِوَاهُ، وَلَا مَطْلُوبَ لَكَ وَرَاءَهُ، فَكَمَا انْتَهَتْ إِلَيْهِ الْأَوَاخِرُ، وَكَانَ بَعْدَ كُلِّ آخِرٍ، فَكَذَلِكَ اجْعَلْ نِهَايَتَكَ إِلَيْهِ — “Kisha mwabudu kwa Jina Lake Al-Aakhir: kwa kumfanya Yeye Pekee kuwa lengo lako ambalo huna lengo jingine ghairi Yake, wala huna matakwa baada Yake. Kama mambo ya mwisho yanavyoishia Kwake, na Yeye Yuko baada ya kila wa mwisho, basi hivyo hivyo jaalia mwisho wako kuwa ni Kwake.”