Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah011 - Adhw-Dhwaahir

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 011 kati ya 103
Adhw-Dhwaahir — Majina Mazuri ya Allaah

Adhw-Dhwaahir: Aliye juu kabisa, hakuna kitu juu Yake; Aliyeshinda kila kitu, na Aliyedhihirika kwa Dalili Zake.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1), pamoja na Majina Al-Awwal, Al-Aakhir na Al-Baatwin. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣﴾

Yeye Ndiye wa Awali hakuna kitu kabla Yake, na wa Mwisho hakuna kitu baada Yake, na Aliye juu hakuna kitu juu Yake, na Aliye karibu, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Yeye, Naye kwa kila kitu Ni Mjuzi. [Al-Hadiyd (57:3)]

Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amelifasiri Jina hili kwa kauli yake: “Na Wewe Ndiye Uliye juu, hakuna kitu juu Yako”, katika du’aa ifuatayo:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَأْمُرُنَا إِذَا أَخَذْنَا مَضْجَعَنَا أَنْ نَقُولَ: ((اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ وَرَبَّ الأَرْضِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ، فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى، وَمُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ وَالْفُرْقَانِ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَيْءٍ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ، اللَّهُمَّ أَنْتَ الأَوَّلُ فَلَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الآخِرُ فَلَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الْبَاطِنُ فَلَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ، اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ، وَأَغْنِنَا مِنَ الْفَقْرِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akituamrisha tunapolala tuseme:

اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ وَرَبَّ الأَرْضِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ، رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ، فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى، وَمُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ وَالْفُرْقَانِ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَيْءٍ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ، اللَّهُمَّ أَنْتَ الأَوَّلُ فَلَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الآخِرُ فَلَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ، وَأَنْتَ الْبَاطِنُ فَلَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ، اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ، وَأَغْنِنَا مِنَ الْفَقْرِ

“Yaa Allaah! Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi na Rabb wa ‘Arsh adhimu, Rabb wetu na Rabb wa kila kitu, Mpasuaji wa mbegu na kokwa, Mteremshaji wa Tawraat na Injiyl na Al-Furqaan (Qur-aan); najikinga Kwako kutokana na shari ya kila kitu ambacho Wewe Umeshika utosi wake. Yaa Allaah! Wewe Ndiye wa Awali, hakuna kitu kabla Yako; na Wewe Ndiye wa Mwisho, hakuna kitu baada Yako; na Wewe Ndiye Uliye juu, hakuna kitu juu Yako; na Wewe Ndiye Uliye karibu, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Wewe. Tulipie deni, na Utukwase tuondokane na ufakiri.” [Muslim]

Imaam Ibn Jariyr Atw-Twabariy (رحمه الله) amesema katika tafsiyr ya Aayah hii:

وَقَوْلُهُ: ﴿وَالظَّاهِرُ﴾ يَقُولُ: وَهُوَ الظَّاهِرُ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ دُونَهُ، وَهُوَ الْعَالِي فَوْقَ كُلِّ شَيْءٍ، فَلَا شَيْءَ أَعْلَى مِنْهُ

“Na Kauli Yake: ‘Na Adhw-Dhwaahir’, Anasema: Naye Ndiye Aliyeshinda na kuwa juu ya kila kilicho chini Yake, Naye Ndiye Aliye juu ya kila kitu; hakuna kitu kilicho juu kuliko Yeye.” [Tafsiyr Atw-Twabariy, Suwrah Al-Hadiyd (57:3)]

Maana Za Neno الظَّاهِر Katika Lugha:

Neno hili lina maana kadhaa katika lugha ya Kiarabu, na zote zimekuja katika Qur-aan. Miongoni mwake ni kuwa juu na kupanda juu ya kitu, kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu Ya-juwj na Ma-juwj:

فَمَا اسْطَاعُوا أَن يَظْهَرُوهُ وَمَا اسْتَطَاعُوا لَهُ نَقْبًا ﴿٩٧﴾

Basi (Ya-juwj na Ma-juwj) hawakuweza kukikwea na wala hawakuweza kukitoboa. [Al-Kahf (18:97)]

Na lina maana ya kushinda, kama Anavyosema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا أَنصَارَ اللَّـهِ كَمَا قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ لِلْحَوَارِيِّينَ مَنْ أَنصَارِي إِلَى اللَّـهِ ۖ قَالَ الْحَوَارِيُّونَ نَحْنُ أَنصَارُ اللَّـهِ ۖ فَآمَنَت طَّائِفَةٌ مِّن بَنِي إِسْرَائِيلَ وَكَفَرَت طَّائِفَةٌ ۖ فَأَيَّدْنَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَىٰ عَدُوِّهِمْ فَأَصْبَحُوا ظَاهِرِينَ﴿١٤﴾

Enyi walioamini! Kuweni wasaidizi wa Allaah kama alivyosema ‘Iysaa mwana wa Maryam kwa wafuasi wake watiifu: Nani watakuwa wasaidizi wangu kwa ajili ya Allaah? Wafuasi watiifu wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Allaah. Basi likaamini kundi miongoni mwa wana wa Israaiyl na likakufuru kundi jingine. Tukawatia nguvu wale walioamini dhidi ya maadui zao, wakapambaukiwa wakiwa washindi. [Asw-Swaff (61:14)]

Na lina maana ya kusaidiana, kama Anavyosema:

إِن تَتُوبَا إِلَى اللَّـهِ فَقَدْ صَغَتْ قُلُوبُكُمَا ۖ وَإِن تَظَاهَرَا عَلَيْهِ فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ مَوْلَاهُ وَجِبْرِيلُ وَصَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ بَعْدَ ذَٰلِكَ ظَهِيرٌ﴿٤﴾

Ikiwa nyinyi wawili mtatubia kwa Allaah (basi ni kheri kwenu), kwani kwa hakika nyoyo zenu zimeelemea (kwa yanayomchukiza Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم). Na mkisaidiana dhidi yake, basi hakika Allaah Ndiye Mawlaa wake na Jibriyl na Waumini wema, na zaidi ya hayo, Malaika pia watasaidia. [At-Tahriym (66:4)]

Na Anasema pia:

إِنَّمَا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ قَاتَلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَأَخْرَجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ وَظَاهَرُوا عَلَىٰ إِخْرَاجِكُمْ أَن تَوَلَّوْهُمْ ۚ وَمَن يَتَوَلَّهُمْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴿٩﴾

Hakika Allaah Anakukatazeni tu kuhusu wale waliokupigeni vita katika Dini, na wakakutoeni kutoka majumbani mwenu, na wakasaidiana juu ya kukutoeni ndio msifanye urafiki nao. Na yeyote atakayewafanya marafiki, basi hao ndio madhalimu. [Al-Mumtahinah (60:9)]

Maana Ya Adhw-Dhwaahir:

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Aliye juu ya kila kitu, na kila kitu kiko chini Yake. Ana ‘Uluwa (kuwa juu) wa aina zote: ‘Uluwa wa Dhati, ‘Uluwa wa kushinda na kudhibiti, na ‘Uluwa wa hadhi na Sifa za ukamilifu. Dhati Yake (سبحانه وتعالى) Iko juu ya mbingu, juu ya ‘Arsh, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu. Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema:

اسْمُهُ الظَّاهِرُ مِنْ لَوَازِمِهِ أَنْ لَا يَكُونَ فَوْقَهُ شَيْءٌ، كَمَا فِي الصَّحِيحِ: «وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ»، بَلْ هُوَ سُبْحَانَهُ فَوْقَ كُلِّ شَيْءٍ، فَمَنْ جَحَدَ فَوْقِيَّتَهُ سُبْحَانَهُ فَقَدْ جَحَدَ لَوَازِمَ اسْمِهِ الظَّاهِرِ

“Jina Lake Adhw-Dhwaahir linalazimisha kwamba hakuna kitu juu Yake, kama ilivyo katika (Hadiyth) Swahiyh: ‘Na Wewe Ndiye Uliye juu, hakuna kitu juu Yako’. Bali Yeye (سبحانه وتعالى) Yuko juu ya kila kitu; basi mwenye kukanusha kuwa Kwake juu, amekanusha yale yanayolazimishwa na Jina Lake Adhw-Dhwaahir.”1

2-Adhw-Dhwaahir ni Yule Aliyedhihirika kwa Dalili Zake na Aayaat Zake zilizoenea katika kila kitu. Shaykh Ibn Baaz (رحمه الله) amesema:

فَالظَّاهِرُ مَعْنَاهَا: الْعَالِي فَوْقَ جَمِيعِ الْخَلْقِ، وَلَكِنْ آيَاتُهُ وَدَلَائِلُ وُجُودِهِ وَمُلْكِهِ وَعِلْمِهِ مَوْجُودَةٌ فِي كُلِّ شَيْءٍ

“Maana ya Adhw-Dhwaahir ni: Aliye juu ya viumbe vyote; lakini Aayaat Zake na dalili za kuwepo Kwake, Ufalme Wake na Ujuzi Wake zimo katika kila kitu.”2

3-Adhw-Dhwaahir Humdhihirishia Amtakaye katika Waja Wake yale yaliyofichikana, kama Alivyomdhihirishia Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) siri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذْ أَسَرَّ النَّبِيُّ إِلَىٰ بَعْضِ أَزْوَاجِهِ حَدِيثًا فَلَمَّا نَبَّأَتْ بِهِ وَأَظْهَرَهُ اللَّـهُ عَلَيْهِ عَرَّفَ بَعْضَهُ وَأَعْرَضَ عَن بَعْضٍ ۖ فَلَمَّا نَبَّأَهَا بِهِ قَالَتْ مَنْ أَنبَأَكَ هَـٰذَا ۖ قَالَ نَبَّأَنِيَ الْعَلِيمُ الْخَبِيرُ﴿٣﴾

Na pale Nabiy alipompa mmoja wa wake zake jambo la siri, na huyo mke alipoipasha habari na Allaah Akamdhihirishia (Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم), akataarifu baadhi yake na akaacha nyingine. Basi alipomjulisha hayo, akasema: Nani aliyekujulisha haya? Akasema: Amenijulisha Mjuzi wa yote, Mwenye Ujuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [At-Tahriym (66:3)]

Wala Hamdhihirishii yeyote ghaibu Yake isipokuwa Rasuli Aliyemridhia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا﴿٢٦﴾ إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ فَإِنَّهُ يَسْلُكُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ رَصَدًا﴿٢٧﴾

Mjuzi wa ghaibu, na wala Hamdhihirishii yeyote Ghaibu Yake. Isipokuwa Rasuli ambaye Yeye Amemridhia. Basi hakika Yeye Anamwekea walinzi mbele yake na nyuma yake. [Al-Jinn (72:26-27)]

4-Adhw-Dhwaahir Ameidhihirisha Dini Yake na kuishindisha juu ya dini zote kwa hoja na nguvu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ﴿٣٣﴾

Yeye Ndiye Aliyemtuma Rasuli Wake kwa mwongozo na Dini ya haki ili Aishindishe juu ya dini zote, japo watakirihika washirikina. [At-Tawbah (9:33)]

5-Adhw-Dhwaahir Huwasaidia na kuwanusuru vipenzi Vyake, kama ilivyotangulia katika Kauli Yake: “Tukawatia nguvu wale walioamini dhidi ya maadui zao, wakapambaukiwa wakiwa washindi.” Asw-Swaff (61:14) (Rejea juu).

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Adhw-Dhwaahir:

1-Amini ‘Uluwa Wa Allaah Juu Ya Viumbe Vyake Vyote:

Tambua, ee Mja wa Adhw-Dhwaahir: Hii ndiyo ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliipima imaan ya mjakazi kwa swali hili:

عَنْ مُعَاوِيَةَ بْنِ الْحَكَمِ السُّلَمِيِّ (رضي الله عنه) ... فَأَتَيْتُهُ بِهَا، فَقَالَ لَهَا: ((أَيْنَ اللَّهُ؟)) قَالَتْ: فِي السَّمَاءِ. قَالَ: ((مَنْ أَنَا؟)) قَالَتْ: أَنْتَ رَسُولُ اللَّهِ. قَالَ: ((أَعْتِقْهَا فَإِنَّهَا مُؤْمِنَةٌ))

Amesimulia Mu’aawiyah bin Al-Hakam As-Sulamiyy (رضي الله عنه): … Nikamleta (mjakazi) kwake, akamuuliza: “Allaah Yuko wapi?” Akasema: Yuko juu mbinguni. Akamuuliza: “Mimi ni nani?” Akasema: Wewe ni Rasuli wa Allaah. Akasema: “Mwache huru, kwani hakika yeye ni Muumini.” [Muslim]

2-Tambua Kwamba Allaah Yuko Juu Ya ‘Arsh Yake:

Tambua kwamba Adhw-Dhwaahir Yuko juu ya ‘Arsh Yake kama Alivyojieleza Mwenyewe, bila kufananishwa wala kuulizwa namna.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾

Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma) Yuko juu ya ‘Arsh. [Twaahaa (20:5)]

3-Mche Aliye Juu Ya Mbingu:

Tambua, ee Mja wa Adhw-Dhwaahir: Aliye juu ya kila kitu Anaweza kuwaadhibu wanaomuasi kwa namna yoyote Atakayo; basi Mche na usijione uko katika amani ukiwa unamuasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ﴿١٦﴾

Je, mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika? [Al-Mulk (67:16)]

4-Kumbuka Kwamba Amali Njema Hupandishwa Kwa Aliye Juu:

Kumbuka, ee Mja wa Adhw-Dhwaahir, kwamba kila neno zuri na amali njema hupandishwa kwa Aliye juu; basi zipambe amali zako.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَن كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا ۚ إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ ۚ وَالَّذِينَ يَمْكُرُونَ السَّيِّئَاتِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَمَكْرُ أُولَـٰئِكَ هُوَ يَبُورُ ﴿١٠﴾

Yeyote anayetaka utukufu, basi utukufu wote uko kwa Allaah. Kwake Pekee linapanda Neno zuri na amali njema Huitukuza. Na wale wanaopanga njama za maovu watapata adhabu shadidi. Na njama za hao ni zenye kuangamia. [Faatwir (35:10)]

5-Mtukuze Aliye Juu Katika Sujuud Yako:

Mtukuze, ee Mja wa Adhw-Dhwaahir, Aliye juu kabisa katika Sujuud yako, kama alivyofanya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akimtukuza Allaah kwa ‘Uluwa Wake katika Sujuud, na mja huwa karibu zaidi na Rabb wake anapokuwa amesujudu:

عَنْ حُذَيْفَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: صَلَّيْتُ مَعَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) ... فَكَانَ يَقُولُ فِي رُكُوعِهِ: ((سُبْحَانَ رَبِّيَ الْعَظِيمِ)) وَفِي سُجُودِهِ: ((سُبْحَانَ رَبِّيَ الأَعْلَى))

Amesimulia Hudhayfah (رضي الله عنه): Niliswali pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) … akawa anasema katika Rukuu yake:

سُبْحَانَ رَبِّيَ الْعَظِيمِ

Utakasifu ni wa Rabb wangu Mtukufu. Na katika Sujuud yake:

سُبْحَانَ رَبِّيَ الأَعْلَى

Utakasifu ni wa Rabb wangu Aliye juu kabisa. [Muslim]

6-Tafakari Dalili Za Adhw-Dhwaahir Katika Ulimwengu Na Katika Nafsi Yako:

Tambua kwamba Aayaat za Adhw-Dhwaahir zimedhihirika katika kila kitu, zikishuhudia kwamba Yeye Ndiye Haki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٥٣﴾

Tutawaonyesha Aayaat (Ishara na Dalili) Zetu katika peo za mbali na katika nafsi zao, mpaka iwabainikie kwamba hii (Qur-aan) ni haki! Je, haitoshelezi Rabb wako kuwa Yeye Ni Shahidi juu ya kila kitu? [Fusw-Swilat (41:53)]

7-Kuwa Na Yakini Kwamba Dini Ya Allaah Itashinda:

Adhw-Dhwaahir Ameahidi kuidhihirisha Dini Yake juu ya dini zote (Rejea At-Tawbah (9:33) juu). Basi usikate tamaa kwa udhaifu wa Waislamu, bali shikamana na imaan na amali njema. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا ۚ وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٥٥﴾

Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba bila shaka Atawafanya warithi katika ardhi kama Alivyowafanya warithi wale waliokuwa kabla yao, na bila shaka Atawamakinishia Dini yao Aliyowaridhia, na bila shaka Atawabadilishia amani badala ya khofu yao, wawe wananiabudu Mimi wasinishirikishe na chochote. Na yeyote atakayekufuru baada ya hapo, basi hao ndio mafasiki. [An-Nuwr (24:55)]

8-Mnusuru Allaah Akunusuru Na Akushindishe:

Nusura ya Adhw-Dhwaahir inapatikana kwa kuinusuru Dini Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ﴿٧﴾

Enyi walioamini! Mkisaidia kunusuru Dini ya Allaah, (Allaah) Atakunusuruni na Ataithibitisha miguu yenu. [Muhammad (47:7)]

9-Nyenyekea, Kwani Mwenye Kunyenyekea Kwa Ajili Ya Allaah Hunyanyuliwa:

Tambua, ee Mja wa Adhw-Dhwaahir: Aliye juu kabisa ni Allaah Pekee; basi mja asijikweze. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَا نَقَصَتْ صَدَقَةٌ مِنْ مَالٍ، وَمَا زَادَ اللَّهُ عَبْدًا بِعَفْوٍ إِلاَّ عِزًّا، وَمَا تَوَاضَعَ أَحَدٌ لِلَّهِ إِلاَّ رَفَعَهُ اللَّهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Swadaqah haipunguzi mali; na Allaah Hamzidishii mja kwa kusamehe isipokuwa utukufu; na hakuna aliyenyenyekea kwa ajili ya Allaah isipokuwa Allaah Humnyanyua.” [Muslim]

10-Unganisha Moyo Wako Na Aliye Juu Katika Kila Haja:

Mja anapotambua kwamba Rabb wake Ndiye Adhw-Dhwaahir, Aliye juu ya kila kitu na Aliyeshinda kila kitu, moyo wake hukusanyika Kwake Pekee; humkusudia katika haja zake zote, na humrejea katika kila jambo, na hivyo uja wake hunyooka.

11-Dumisha Du’aa Ya Kulala Inayomtaja Allaah Kwa Jina Lake Adhw-Dhwaahir:

Tambua, ee Mja wa Adhw-Dhwaahir: Soma du’aa iliyotajwa juu kila unapokwenda kulala, kama alivyowafundisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Swahaba zake. Rejea Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) juu.

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله), kama alivyonukuliwa na Knowingallah katika maelezo ya Majina Al-Awwal, Al-Aakhir, Adhw-Dhwaahir na Al-Baatwin.
  • 2Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz (رحمه الله), Fatwa: Tafsiyr ya Kauli ya Allaah: “Yeye Ndiye wa Awali na wa Mwisho, na Aliye juu na Aliye karibu” (binbaz.org.sa, 19798).