Al-Malik: Mfalme na mwenye mamlaka
Majina haya: Al-Malik, Al-Maalik na Al-Maliyk yote yanatokana na Sifa ya Mulk (ufalme na umiliki). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢﴾
Ni Wake Pekee ufalme wa mbingu na ardhi, Anahuisha na Anafisha, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza. [Al-Hadiyd (57:2)]
Al-Malik imetajwa mara tano katika Qur-aan:
فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۗ وَلَا تَعْجَلْ بِالْقُرْآنِ مِن قَبْلِ أَن يُقْضَىٰ إِلَيْكَ وَحْيُهُ ۖ وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا ﴿١١٤﴾
Basi Ametukuka Allaah kwa ‘Uluwa, Mfalme wa haki. Na wala usiiharakize Qur-aan (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kabla haikumalizwa kufunuliwa Wahy kwako. Na sema: “Rabb wangu! Nizidishie elimu.” [Twaahaa (20:114)]
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾
Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye Kusadikisha ahadi na Kuaminisha, Mwenye Kudhibiti Kushuhudia Kuchunga na Kuhifadhi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Jabari Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye Ukubwa na Uadhama, Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha. [Al-Hashr (59:23)]
قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ﴿١﴾ مَلِكِ النَّاسِ ﴿٢﴾
Sema: Najikinga na Rabb wa watu. Mfalme wa watu. [An-Naas (114:1-2)]
فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ ﴿١١٦﴾
Basi Ametukuka Allaah kwa ‘Uluwa, Mfalme wa haki. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Rabb wa ‘Arsh Kariym. [Al-Muuminuwn (23:116)]
يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ﴿١﴾
Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi, Mfalme, Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Jumu’ah (62:1)]
Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Malik; Mwenye ufalme kamili, Anatawala Atakavyo katika Ufalme Wake, Hana mshirika wala mpingaji. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾
Hakika Amri Yake Anapotaka chochote Hukiambia: Kun! (Kuwa), nacho huwa. [Yaasiyn (36:82)]
فَسُبْحَانَ الَّذِي بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٨٣﴾
Basi Utakasifu Ni wa Ambaye Mkononi Mwake kuna ufalme wa kila kitu, na Kwake mtarejeshwa. [Yaasiyn (36:83)]
Ibn Jariyr amesema: “Ni Mfalme Ambaye hakuna ufalme juu Yake wala chochote isipokuwa kiko kwenye mamlaka Yake”.1
Na Ibn Al-Qayyim amesema: “Mfalme wa haki. Yeye Ambaye Anaamrisha na kukataza na Anafanya/Anapanga na kugeuza Atakavyo kwa viumbe Vyake kwa kauli na Amri Zake, na hii ndio tofauti baina ya Al-Malik na Al-Maalik. Hivyo basi Al-Maalik ni Mwenye kufanya Atakavyo kwa vitendo Vyake. Na Al-Malik ni Mwenye kutenda Atakavyo kwa vitendo Vyake na Amri Zake. Na Rabb (Ta’aalaa) ni Maalik-Al-Mulk (Mmiliki wa ufalme wote) basi Hufanya Atakavyo kwa vitendo Vyake na Amri Zake.”2
Na Ibn Kathiyr amesema kuhusu Kauli Yake (سبحانه وتعالى) katika Al-Hashr (59:23), Rejea juu: Kwa maana: Ni Mfalme wa kila kitu Anayefanya Atakavyo bila ya mwenye kumkataza au kumpinga.3
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Malik:
1-Al-Malik Ni Mfalme Wa Haki, Na Ufalme Wa Wengine Ni Wa Muda:
Tambua, ee Mja wa Al-Malik: Ufalme wa Allaah ni wa kweli usiokwisha, Naye Ametukuka juu ya kila mfalme. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ ﴿١١٦﴾
Basi Ametukuka Allaah kwa ‘Uluwa, Mfalme wa haki. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Rabb wa ‘Arsh Kariym. [Al-Muuminuwn (23:116)]
2-Kila Kilichomo Mbinguni Na Ardhini Kinamsabbih Al-Malik:
Tambua, ee Mja wa Al-Malik: Viumbe vyote vinamtakasa Mfalme wa haki kwa lugha zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ﴿١﴾
Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi, Mfalme, Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Jumu’ah (62:1)]
3-Nyenyekea Mbele Ya Mfalme Wa Wafalme:
Ikiwa Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mfalme wa wafalme, na hakuna anayeweza kushindana Naye kwa lolote, wala hakuna mshirika, na Ndiye rejea yetu na matarajio yetu, hatuwezi kutoshelezwa na asiyekuwa Yeye. Hivyo hakuna haja ya kuogopa, wala kutarajia asiyekuwa Yeye, wala kumpenda asiyekuwa Yeye, wala kumtegemea asiyekuwa Yeye, kwani mwenye kumtegemea na kumuogopa Yeye Al-Malik, Al-Maalik, Al-Maliyk, basi atakuwa chini ya uangalizi Wake.
4-Usijiite Kwa Majina Yanayomhusu Allaah Pekee:
Haipasi kujiita Majina ya Allaah (سبحانه وتعالى) yanayomhusu Yeye Pekee kama haya yenye kuanzia na ‘AL’ (Al-Malik) au ‘Malik Al-Amlaak’ (mfalme wa wafalme) kwani Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametahadharisha:
أَغْيَظُ رَجُلٍ عَلَى اللَّهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَأَخْبَثُهُ وَأَغْيَظُهُ عَلَيْهِ رَجُلٌ كَانَ يُسَمَّى مَلِكَ الأَمْلاَكِ لاَ مَلِكَ إِلاَّ اللَّهُ
Mtu anayechukiza kabisa mbele ya Allaah Siku ya Qiyaamah ni muovu kabisa na anayechukiza mno kuliko wote Kwake ni mtu aliyekuwa akijiita: “Malik Al-Amlaak” (Mfalme wa wafalme). Kwani hakuna mfalme isipokuwa Allaah. [Al-Bukhaariy] [Muslim]
5-Tambua Udogo Wa Ufalme Wa Duniani:
Wafalme wa duniani wana mamlaka ya watu wao duniani tu na ni mamlaka ya muda mfupi tu. Ama Allaah (سبحانه وتعالى) ni Al-Malik, Al-Maalik, Al-Maliyk, Mfalme wa wafalme wote, na Mwenye ufalme wa kudumu. Ni Mfalme wa duniani na Aakhirah. Siku watakapofishwa viumbe wote Atabakia Maalikul-Mulk (Mfalme wa wafalme). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ﴿١٦﴾
Siku watakayotokeza wao, hakitofichika kitu chochote chao kwa Allaah. “Ufalme ni wa nani leo?” (Allaah Mwenyewe Atajijibu): “Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika.” [Ghaafir (40:16)]
Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):
وَيَوْمَ تَشَقَّقُ السَّمَاءُ بِالْغَمَامِ وَنُزِّلَ الْمَلَائِكَةُ تَنزِيلًا ﴿٢٥﴾ الْمُلْكُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ لِلرَّحْمَـٰنِ ۚ وَكَانَ يَوْمًا عَلَى الْكَافِرِينَ عَسِيرًا ﴿٢٦﴾
Na Siku itakayoraruka mbingu kwa mawingu; na Malaika watateremshwa mteremsho mkubwa wa mfuatano. Ufalme wa haki Siku hiyo utakuwa ni wa Ar-Rahmaan; Mwingi wa Rahmah. Na itakuwa ni siku ngumu kwa makafiri. [Al-Furqaan (25:25-26)]
Na katika Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):
يَقْبِضُ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى الأَرْضَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَطْوِي السَّمَاءَ بِيَمِينِهِ ثُمَّ يَقُولُ أَنَا الْمَلِكُ أَيْنَ مُلُوكُ الأَرْضِ
Allaah (تبارك وتعالى) Ataikamata ardhi Mkononi na Atazikunja mbingu kwa Mkono Wake wa kulia kisha Atasema: Mimi Ndiye Mfalme! Wako wapi wafalme wa duniani? [Al-Bukhaariy] [Muslim]
6-Ukipewa Madaraka, Kumbuka Kwamba Ufalme Wote Ni Wa Allaah:
Kwa mwenye madaraka, au mamlaka au cheo chochote kile duniani, au umiliki wa chochote kile, awe mnyenyekevu kwa walio chini yake kwa kuzingatia kuwa Yuko Al-Malik na Al-Maliyk Ambaye Ana mamlaka juu yake. Hivyo basi unapohukumu, uhukumu kwa haki bila ya uonevu. Unapotoa, toa bila ya kupendelea, na wala usitakabari bali ukhofie kauli ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):
يَطوي اللهُ عزَّ وجلَّ السَّماواتِ يومَ القيامةِ. ثمَّ يأخذُهنَّ بيدِه اليُمنَى. ثمَّ يقولُ: أنا الملِكُ. أين الجبَّارون؟ أين المُتكبِّرون؟ ثمَّ يَطوي الأرضين بشمالِه. ثمَّ يقولُ: أنا الملِكُ. أين الجبَّارون؟ أين المُتكبِّرون؟
Allaah (عزّ وجلّ) Atakunja mbingu zote Siku ya Qiyaamah kisha Atazikamata Mkononi Mwake wa kuume Atasema: Mimi Ndiye Mfalme. Wako wapi waliojifanya majabari? Wako wapi waliotakabari? Kisha Atakunja ardhi zote kwa Mkono Wake wa kushoto Atasema: Mimi Ndiye Mfalme, wako wapi waliojifanya majabari? Wako wapi waliotakabari? [Muslim]
7-Omba Kinga Kwa Mfalme Wa Watu:
Tambua, ee Mja wa Al-Malik: Katika Suwrah An-Naas, Allaah Amejitaja kuwa ni Mfalme wa watu, na Akatufundisha kujikinga Kwake kutokana na shari ya wasiwasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ﴿١﴾ مَلِكِ النَّاسِ ﴿٢﴾ إِلَـٰهِ النَّاسِ ﴿٣﴾
Sema: Najikinga na Rabb wa watu. Mfalme wa watu. Muabudiwa wa Haki wa watu. [An-Naas (114:1-3)]
8-Tumia Theluthi Ya Mwisho Ya Usiku, Wakati Al-Malik Anapowaita Waja Wake:
Tumia, ee Mja wa Al-Malik, theluthi ya mwisho ya usiku kwa du’aa na istighfaar, kwani ni wakati wa kuitikiwa.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((يَنْزِلُ اللَّهُ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا كُلَّ لَيْلَةٍ حِينَ يَمْضِي ثُلُثُ اللَّيْلِ الأَوَّلُ، فَيَقُولُ: أَنَا الْمَلِكُ، أَنَا الْمَلِكُ، مَنْ ذَا الَّذِي يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ ذَا الَّذِي يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ ذَا الَّذِي يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ، فَلاَ يَزَالُ كَذَلِكَ حَتَّى يُضِيءَ الْفَجْرُ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Huteremka kwenye mbingu ya dunia kila usiku inapopita theluthi ya kwanza ya usiku, Anasema: Mimi Ndiye Mfalme! Mimi Ndiye Mfalme! Nani ananiomba Nimwitikie? Nani ananitaka kitu Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie? Na huendelea hivyo mpaka Alfajiri inapong’aa.” [Muslim]
9-Soma Adhkaar Zenye Kumtaja Allaah Kwa Jina Hili:
Tambua, ee Mja wa Al-Malik: Kusoma adhkaar zilizothibiti zenye kutajwa Majina haya ya Allaah au Sifa Zake mfano:
اللّهُـمَّ أَنْتَ المَلِكُ لا إِلهَ إِلاّ أَنْت، أَنْتَ رَبِّـي وَأَنـا عَبْـدُك، ظَلَمْـتُ نَفْسـي وَاعْـتَرَفْتُ بِذَنْبـي فَاغْفِرْ لي ذُنوبي جَميعاً إِنَّـه لا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إلاّ أَنْت،
Yaa Allaah, Wewe Ndiye Mfalme, hapana Muabudiwa wa haki ila Wewe, Wewe Ndiye Rabb wangu na mimi ni Mja Wako. Nimedhulumu nafsi yangu, na nimekiri madhambi yangu kwa hivyo Nighufurie madhambi yangu yote, hakika haghufurii madhambi, ila Wewe.
Na pia:
لا إلهَ إلاّ اللّهُ وحْـدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ المُلكُ ولهُ الحَمْد، يُحيـي وَيُمـيتُ وهُوَ على كُلّ شيءٍ قدير.
Hapana Muabudiwa wa haki ila Allaah, ni Mmoja Pekee, Hana mshirika. Ni Wake Ufalme, na kuhimidiwa ni Kwake, Anahuisha, Anafisha, na Yeye Ni Muweza wa kila kitu.
Fadhila zake mbalimbali zimetajwa katika Hiswn Al-Muslim.
10-Mtakase Al-Malik Baada Ya Swalaah Ya Witri:
Mtakase Al-Malik Al-Qudduws baada ya Swalaah ya Witri kama alivyokuwa akifanya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapomaliza Witri husema mara tatu:
عَنْ أُبَيِّ بْنِ كَعْبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يُوتِرُ ... فَإِذَا فَرَغَ قَالَ عِنْدَ فَرَاغِهِ: ((سُبْحَانَ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ)) ثَلاَثَ مَرَّاتٍ، يُطِيلُ فِي آخِرِهِنَّ
Amesimulia Ubayy bin Ka’b (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiswali Witri … na anapomaliza husema:
سُبْحَانَ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ
Utakasifu ni wa Mfalme, Mtakatifu; mara tatu, akirefusha (sauti) katika ya mwisho. [An-Nasaaiy (1698), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh An-Nasaaiy]
Na Allaah Mjuzi zaidi