Al-Maalik: Mwenye Kumiliki Kila Kitu
Al-Maalik Ni Mwenye kumiliki kila kitu; ufalme wote ni Wake, Anampa Amtakaye na Anamnyang’anya Amtakaye.
Al-Maalik imetajwa mara mbili katika Kauli za Allaah (سبحانه وتعالى):
مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٤﴾
Mfalme wa Siku ya Malipo. [Al-Faatihah (1:4)]
قُلِ اللَّـهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَن تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَن تَشَاءُ ۖ بِيَدِكَ الْخَيْرُ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢٦﴾
Sema: Ee Allaah Mfalme Uliyemiliki ufalme wote, Unampa ufalme Umtakaye, na Unamuondoshea ufalme Umtakaye, na Unamtukuza Umtakaye, na Unamdhalilisha Umtakaye, kheri imo Mkononi Mwako. Hakika Wewe Ni Muweza wa kila kitu. [Aal-‘Imraan (3:26)]
Allaah (عزّ وجلّ) Anapanga Pekee mamlaka Yake. Anatoa na kuzuia, Anakirimu, Anatukuza na Anadhalilisha, Anaumba na kuruzuku, Anaamrisha na Anakataza, Anafisha na kuhuisha, Anakadiria na Anahukumu. Anaingiza usiku kwa mchana, na Anaingiza mchana kwa usiku. Anasema (سبحانه وتعالى):
تُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَتُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ ۖ وَتُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَتُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ ۖ وَتَرْزُقُ مَن تَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٢٧﴾
Unauingiza usiku katika mchana na Unauingiza mchana katika usiku, na Unatoa kilicho hai kutokana na kilicho mfu na Unatoa kilicho mfu kutokana na kilicho hai, na Unamruzuku Umtakaye bila ya hesabu. [Aal-‘Imraan (3:27)]
Anatawala Atakavyo, Anamiliki Atakayo. Ni Muweza hakuna mwenye kushindana Naye katika mamlaka Yake, wala hakuna mwenye kuweza kumpinga.
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Maalik:
1-Al-Maalik Anamiliki Kila Kitu Umiliki Kamili:
Tambua, ee Mja wa Al-Maalik: Umiliki wa Allaah ni wa kweli na kamili; Anamiliki dhati za vitu, na Anafanya ndani yake Atakavyo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا فِيهِنَّ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١٢٠﴾
Ni wa Allaah ufalme wa mbingu na ardhi na yote yaliyomo humo. Naye juu ya kila kitu Ni Muweza. [Al-Maaidah (5:120)]
2-Waabudiwa Wa Uongo Hawamiliki Hata Kitu Kidogo Kabisa:
Tambua, ee Mja wa Al-Maalik: Asiyemiliki chochote hastahiki kuombwa wala kuabudiwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ ﴿١٣﴾
Anauingiza usiku katika mchana, na Anauingiza mchana katika usiku, na Ametiisha jua na mwezi; kila kimoja kinakwenda mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Huyo Ndiye Allaah Rabb wenu, Ufalme ni Wake Pekee. Na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende. [Faatwir (35:13)]
3-Siku Ya Qiyaamah Hakuna Nafsi Itakayoimiliki Nafsi Nyingine Kitu:
Tambua, ee Mja wa Al-Maalik: Siku hiyo umiliki wote wa kidhahiri wa viumbe utakatika, na Amri itabaki kwa Allaah Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ ﴿١٩﴾
Siku ambayo nafsi haitokuwa na uwezo wowote juu ya nafsi nyingine, na amri Siku hiyo ni ya Allaah Pekee. [Al-Infitwaar (82:19)]
4-Kumbuka Siku Al-Maalik Atakapoikunja Ardhi Na Mbingu:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Maalik, Siku ambayo wafalme wote wa dunia watatoweka, na atabakia Mfalme wa haki Peke Yake.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((يَقْبِضُ اللَّهُ الأَرْضَ، وَيَطْوِي السَّمَوَاتِ بِيَمِينِهِ، ثُمَّ يَقُولُ: أَنَا الْمَلِكُ، أَيْنَ مُلُوكُ الأَرْضِ؟))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Allaah Ataishika ardhi, na Atazikunja mbingu kwa Mkono Wake wa kulia, kisha Atasema: Mimi Ndiye Mfalme! Wako wapi wafalme wa ardhi?” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
5-Tafakari Kauli Yako Katika Kila Swalaah: مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ:
Tafakari, ee Mja wa Al-Maalik, Aayah katika Suwratul-Faatihah unayoisoma katika kila Swalaah yako:
مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٤﴾
Mfalme wa Siku ya Malipo. [Al-Faatihah (1:4)]
Kwamba umesimama mbele ya Al-Maalik na Mfalme wa wafalme duniani na kwamba utasimamishwa mbele Yake tena Siku ya Qiyaamah kulipwa mema uliyoyatenda na kuhesabiwa maovu uliyoyatenda wala hakuna cha kufichikia siku hiyo!
يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ﴿١٦﴾
Siku watakayotokeza wao, hakitofichika kitu chochote chao kwa Allaah. Ufalme ni wa nani leo? (Allaah Mwenyewe Atajijibu): Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Asiyepingika. [Ghaafir (40:16)]
الْيَوْمَ تُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۚ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ﴿١٧﴾
Leo kila nafsi italipwa kwa yale iliyoyachuma, hakuna dhulma leo! Hakika Allaah Ni Mwepesi wa Kuhesabu. [Ghaafir (40:17)]
وَأَنذِرْهُمْ يَوْمَ الْآزِفَةِ إِذِ الْقُلُوبُ لَدَى الْحَنَاجِرِ كَاظِمِينَ ۚ مَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ حَمِيمٍ وَلَا شَفِيعٍ يُطَاعُ﴿١٨﴾
Na waonye Siku inayokurubia sana pale nyoyo zitakapofika kooni nao wamejaa huzuni na majuto. Madhalimu hawatokuwa na rafiki wa dhati, wala mwombezi anayetiiwa. [Ghaafir (40:18)]
Tafakari pia Aayah katika Suwratul-Infitwaar (Rejea juu: Al-Infitwaar (82:19)).
6-Tambua Kwamba Mali Uliyonayo Ni Amana Ya Al-Maalik, Basi Itoe Katika Njia Yake:
Tambua, ee Mja wa Al-Maalik: Wewe si mmiliki halisi wa mali yako, bali ni mwakilishi uliyepewa kuisimamia kwa muda. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
آمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَأَنفِقُوا مِمَّا جَعَلَكُم مُّسْتَخْلَفِينَ فِيهِ ۖ فَالَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَأَنفَقُوا لَهُمْ أَجْرٌ كَبِيرٌ ﴿٧﴾
Muaminini Allaah na Rasuli Wake, na toeni kutokana na yale Aliyokufanyieni kuwa warithi kwayo. Basi wale walioamini miongoni mwenu, na wakatoa, watapata ujira mkubwa. [Al-Hadiyd (57:7)]
7-Mali Yako Halisi Ni Ile Uliyoitoa Swadaqah:
Tambua, ee Mja wa Al-Maalik, kwamba mali yako halisi ni ile uliyoitanguliza kwa Allaah, si ile uliyoiacha nyuma.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ مُطَرِّفٍ عَنْ أَبِيهِ (رضي الله عنه) قَالَ: أَتَيْتُ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) وَهُوَ يَقْرَأُ: ﴿أَلْهَاكُمُ التَّكَاثُرُ﴾ قَالَ: ((يَقُولُ ابْنُ آدَمَ: مَالِي مَالِي، قَالَ: وَهَلْ لَكَ يَا ابْنَ آدَمَ مِنْ مَالِكَ إِلاَّ مَا أَكَلْتَ فَأَفْنَيْتَ، أَوْ لَبِسْتَ فَأَبْلَيْتَ، أَوْ تَصَدَّقْتَ فَأَمْضَيْتَ))
Amesimulia Mutwarrif kutoka kwa baba yake (رضي الله عنه): Nilimwendea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akiwa anasoma: “Alhaakumut-Takaathur”, akasema: “Mwanaadam anasema: Mali yangu! Mali yangu! Na je, ee mwanaadam, una nini katika mali yako isipokuwa ulichokula ukakimaliza, au ulichovaa ukakichakaza, au ulichotoa swadaqah ukakitanguliza?” [Muslim]
8-Usijivune Kwa Mali Kana Kwamba Umeimiliki Kwa Ujuzi Wako:
Tambua, ee Mja wa Al-Maalik: Qaaruwn alijiona kuwa mmiliki wa hazina zake kwa ujuzi wake, na mwisho wake ukawa kuangamizwa pamoja na mali yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قَالَ إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَىٰ عِلْمٍ عِندِي ۚ أَوَلَمْ يَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَهْلَكَ مِن قَبْلِهِ مِنَ الْقُرُونِ مَنْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُ قُوَّةً وَأَكْثَرُ جَمْعًا ۚ وَلَا يُسْأَلُ عَن ذُنُوبِهِمُ الْمُجْرِمُونَ ﴿٧٨﴾
(Qaaruwn) akasema: Hakika nimepewa haya kwa sababu ya ilimu yangu. Je, hajui kwamba Allaah Ameangamiza kabla yake karne ambazo zilikuwa ni zenye nguvu zaidi kuliko yeye na zenye mkusanyiko (wa mali) mwingi zaidi? Na wala hawatoulizwa kuhusu dhambi zao wahalifu. [Al-Qaswasw (28:78)]
9-Tamani Ufalme Wa Kudumu Katika Jannah:
Tafakari neema za Jannah Anazotuahidi Allaah (عزّ وجلّ) huko. Kwa hiyo, tenda mema na jiepushe na maovu na lenga uingie Jannah. Pale utakapoingia Jannah ukafunguliwa milango yake na Malaika wakakupokea kwa Salaamun ‘alaykum! Ukaanza kuona Anayoyamiliki Al-Maalik, huko:
وَإِذَا رَأَيْتَ ثَمَّ رَأَيْتَ نَعِيمًا وَمُلْكًا كَبِيرًا﴿٢٠﴾
Na utakapoona huko, utaona neema na ufalme adhimu. [Al-Insaan (76:20)]
10-Mwombe Al-Maalik Kwa Unyenyekevu Wa Mja Kwa Mmiliki Wake:
Tambua, ee Mja wa Al-Maalik: Katika du’aa ya kufungulia Swalaah, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema:
عَنْ عَلِيِّ بْنِ أَبِي طَالِبٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ كَانَ إِذَا قَامَ إِلَى الصَّلاَةِ قَالَ: ... ((اللَّهُمَّ أَنْتَ الْمَلِكُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ، أَنْتَ رَبِّي وَأَنَا عَبْدُكَ، ظَلَمْتُ نَفْسِي، وَاعْتَرَفْتُ بِذَنْبِي، فَاغْفِرْ لِي ذُنُوبِي جَمِيعًا، إِنَّهُ لاَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلاَّ أَنْتَ))
Amesimulia ‘Aliy bin Abiy Twaalib (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anaposimama kuswali husema: …
اللَّهُمَّ أَنْتَ الْمَلِكُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ، أَنْتَ رَبِّي وَأَنَا عَبْدُكَ، ظَلَمْتُ نَفْسِي، وَاعْتَرَفْتُ بِذَنْبِي، فَاغْفِرْ لِي ذُنُوبِي جَمِيعًا، إِنَّهُ لاَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلاَّ أَنْتَ
Yaa Allaah! Wewe Ndiye Mfalme, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe. Wewe Ndiye Rabb wangu, nami ni Mja Wako. Nimeidhulumu nafsi yangu, na nimekiri dhambi yangu, basi Nighufurie madhambi yangu yote, kwani hakuna anayeghufuria madhambi isipokuwa Wewe. [Muslim]
Na Allaah Mjuzi zaidi