Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah018 - Al-Qudduws

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 018 kati ya 103
Al-Qudduws — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Qudduws: Mtakatifu, Aliyetakasika na kila aina ya upungufu, kasoro na aibu; Mwenye kustahiki kutukuzwa na kutakaswa, Mwingi wa baraka.

Jina hili linatokana na neno قَدَّسَ ambalo lina maana mbili. Maana ya kwanza ni kutoharika, kuwa safi, na kutakasika na kila najisi, aibu na upungufu. Imekuja katika Qur-aan pale Malaika waliposema:

وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي جَاعِلٌ فِي الْأَرْضِ خَلِيفَةً ۖ قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ وَنَحْنُ نُسَبِّحُ بِحَمْدِكَ وَنُقَدِّسُ لَكَ ۖ قَالَ إِنِّي أَعْلَمُ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٣٠﴾

Na pindi Rabb wako Alipowaambia Malaika: Hakika Mimi Nitaweka katika ardhi khalifa. Wakasema: Utaweka humo atakayefanya ufisadi humo na kumwaga damu, na hali sisi tunakusabihi kwa Himdi Zako na tunakutukuza kwa Utakatifu Wako? (Allaah) Akasema: Hakika Mimi Nayajua zaidi msiyoyajua. [Al-Baqarah (2:30)]

Na ndio maana Msikiti wa Al-Aqswaa ukaitwa Baytul-Maqdis (Nyumba iliyotakasika), na ardhi ya Palestina ikaitwa Al-Ardhw Al-Muqaddasah (ardhi iliyotakasika). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا قَوْمِ ادْخُلُوا الْأَرْضَ الْمُقَدَّسَةَ الَّتِي كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ وَلَا تَرْتَدُّوا عَلَىٰ أَدْبَارِكُمْ فَتَنقَلِبُوا خَاسِرِينَ ﴿٢١﴾

Enyi kaumu yangu! Ingieni ardhi iliyotakaswa ambayo Amekuandikieni Allaah, na wala msirudi kugeuka nyuma mkakimbia (kupigana), hapo mtageuka kuwa wenye kukhasirika. [Al-Maaidah (5:21)]

Na Jibriyl (عليه السلام) ameitwa Ruwhul-Qudus (Roho Mtakatifu), kwa sababu ametakasika na kila aibu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ نَزَّلَهُ رُوحُ الْقُدُسِ مِن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ لِيُثَبِّتَ الَّذِينَ آمَنُوا وَهُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ﴿١٠٢﴾

Sema: Ameiteremsha Ruwh Al-Qudus (Jibriyl) kutoka kwa Rabb wako kwa haki ili iwathibitishe wale walioamini, na ni mwongozo na bishara kwa Waislamu. [An-Nahl (16:102)]

Maana ya pili ni baraka; na kutokana nayo ni neno Muqaddasah (iliyobarikiwa). Allaah (سبحانه وتعالى) Ametaja ardhi iliyobarikiwa katika Kauli Yake:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾

Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku Mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumebariki pembezoni mwake, ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (Ishara) Zetu (kubwa mno). Hakika Yeye (Allaah) Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Al-Israa (17:1)]

Jina Lake hili tukufu, Al-Qudduws, limetajwa katika Qur-aan mara mbili (2), na mara zote mbili limekuja pamoja na Jina Lake Al-Malik. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾

Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye Kusadikisha ahadi na Kuaminisha, Mwenye Kudhibiti Kushuhudia Kuchunga na Kuhifadhi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Jabari Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye Ukubwa na Uadhama, Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha. [Al-Hashr (59:23)]

Na Anasema pia:

يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ﴿١﴾

Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi, Mfalme, Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Jumu’ah (62:1)]

Maana Ya Al-Qudduws:

Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema:

فَالْقُدُّوسُ الْمُنَزَّهُ مِنْ كُلِّ شَرٍّ وَنَقْصٍ وَعَيْبٍ، كَمَا قَالَ أَهْلُ التَّفْسِيرِ: هُوَ الطَّاهِرُ مِنْ كُلِّ عَيْبٍ، الْمُنَزَّهُ عَمَّا لَا يَلِيقُ بِهِ، وَهَذَا قَوْلُ أَهْلِ اللُّغَةِ، وَأَصْلُ الْكَلِمَةِ مِنَ الطَّهَارَةِ وَالنَّزَاهَةِ، وَمِنْهُ بَيْتُ الْمَقْدِسِ لِأَنَّهُ مَكَانٌ يُتَطَهَّرُ فِيهِ مِنَ الذُّنُوبِ ... وَمِنْهُ سُمِّيَتِ الْجَنَّةُ حَظِيرَةَ الْقُدْسِ لِطَهَارَتِهَا مِنْ آفَاتِ الدُّنْيَا، وَمِنْهُ سُمِّيَ جِبْرِيلُ رُوحَ الْقُدُسِ لِأَنَّهُ طَاهِرٌ مِنْ كُلِّ عَيْبٍ

“Al-Qudduws ni Aliyetakasika na kila shari, upungufu na aibu; kama walivyosema wafasiri (wa Qur-aan): Yeye Ndiye Aliye safi na kila aibu, Aliyetakasika na kila lisilomstahiki. Na hii ndiyo kauli ya wataalamu wa lugha; na asili ya neno hili ni utohara na utakaso. Na kutokana nalo ni Baytul-Maqdis, kwa sababu ni mahali pa kujitakasa na madhambi … Na kutokana nalo Jannah imeitwa Hadhwiyratul-Quds (Uwanja mtakatifu) kwa kutakasika kwake na maafa ya dunia, na Jibriyl ameitwa Ruwhul-Qudus kwa sababu ametakasika na kila aibu.”1

Na Imaam Ibn Kathiyr (رحمه الله) amesema:

أَيِ الْمُنَزَّهُ عَنِ النَّقَائِصِ، الْمَوْصُوفُ بِصِفَاتِ الْكَمَالِ

“Yaani Aliyetakasika na kila upungufu, Mwenye kusifika kwa Sifa za ukamilifu.”2

Kwa hiyo Al-Qudduws ni Aliyetakasika na kila kinachopingana na ukamilifu Wake: katika Dhati Yake, katika Majina Yake na Sifa Zake, katika matendo Yake, na katika uendeshaji Wake wa ulimwengu. Majina Yake yote ni mazuri yasiyo na shari ndani yake, Sifa Zake zote ni za juu zisizo na upungufu, na matendo Yake yote ni hikmah yasiyo na kasoro.

Na Al-Qudduws pia ni Mwenye baraka; Neema Zake zimekithiri na kuenea kila mahali, na Baraka Zake ziko ardhini na mbinguni wakati wote. Jina Lake limebarikiwa, Sifa Zake zimebarikiwa, na matendo Yake yamebarikiwa.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Qudduws:

Kuamini Jina hili kwa vitendo kunamfanya Muumini amwadhimishe na kumtukuza Rabb wake; na kunamlazimu ajitakase na uchafu wa shirk, dhulma na maovu yote, na alazimiane na utohara wa ndani na nje katika kila hali. Na yafuatayo ni miongoni mwa njia za kujitakasa na kujipatia baraka:

1-Mtakase Allaah Katika Sifa Zake Bila Kuzikanusha Wala Kuzifananisha:

Tambua, ee Mja wa Al-Qudduws: Kumtakasa Allaah ni kuzithibitisha Sifa Zake kama zilivyokuja, na kumtakasa na kufanana na viumbe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ۖ يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾

Mwanzilishi wa mbingu na ardhi. Amekujaalieni kutokana na nafsi zenu mume na mke, na katika wanyama wa mifugo dume na jike. Anakusambazeni humo. Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:11)]

2-Mtakase Allaah Kwa Tawhiyd Na Kumtakasa Na Mke Na Mwana:

Tambua, ee Mja wa Al-Qudduws: Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Muabudiwa wa haki Pekee, Hana mshirika wala mke wala mwana. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقَالُوا اتَّخَذَ اللَّـهُ وَلَدًا ۗ سُبْحَانَهُ ۖ بَل لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ كُلٌّ لَّهُ قَانِتُونَ ﴿١١٦﴾

Na wakasema: Allaah Amejichukulia mwana. Utakasifu Ni Wake! Bali ni Vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, vyote vinamtii. [Al-Baqarah (2:116)]

Hata majini walimtakasa Allaah (سبحانه وتعالى) waliposema:

وَأَنَّهُ تَعَالَىٰ جَدُّ رَبِّنَا مَا اتَّخَذَ صَاحِبَةً وَلَا وَلَدًا﴿٣﴾

Na kwamba hakika umetukuka kabisa Ujalali wa Rabb wetu, Hakujifanyia mke wala mwana. [Al-Jinn (72:3)]

Na shirki ndiyo dhambi kubwa kabisa, kama alivyobainisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipoulizwa:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: سَأَلْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): أَيُّ الذَّنْبِ أَعْظَمُ عِنْدَ اللَّهِ؟ قَالَ: ((أَنْ تَجْعَلَ لِلَّهِ نِدًّا وَهُوَ خَلَقَكَ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Ni dhambi ipi kubwa kabisa mbele ya Allaah? Akasema: “Ni kumfanyia Allaah mlinganishi na hali Yeye Ndiye Aliyekuumba.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Basi soma vitabu vya Tawhiyd na jifunze aina zake, ili ujue yale ya kumshirikisha Allaah upate kujiepusha nayo.

3-Jitakase Kwa Kujifunza ‘Aqiydah Sahihi:

Tambua, ee Mja wa Al-Qudduws: ‘Aqiydah sahihi itakuepusha kuingia katika makundi potofu, na itakubakisha katika utakaso wa Dini ambao ndio mwenendo wa Manabii wote na wema waliotangulia (Salaf). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ ﴿٥﴾

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kuwa ni wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki, na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah. Na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara. [Al-Bayyinah (98:5)]

4-Takasa Moyo Wako Kwa Qur-aan:

Tambua, ee Mja wa Al-Qudduws: Qur-aan inaponya maradhi ya moyo yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah, kama shirki, kufru, unafiki, hasadi na ubakhili. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٥٧﴾

Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rehma kwa Waumini. [Yuwnus (10:57)]

Basi takasa moyo wako uwe na ikhlaasw katika amali zako, kwa sababu hakuna kitakachokufaa Siku ya Qiyaamah isipokuwa kumfikia Allaah (سبحانه وتعالى) kwa moyo uliosalimika. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾ إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

Siku hayatofaa mali wala watoto. Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa (26:88-89)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلَى أَجْسَادِكُمْ وَلاَ إِلَى صُوَرِكُمْ، وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Haangalii miili yenu wala sura zenu, lakini Anaangalia nyoyo zenu.” [Muslim]

Na Qur-aan nzima ni baraka; isome kwa wingi ujipatie baraka tele. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٢٩﴾

Kitabu Tumekiteremsha kwako chenye Baraka, ili wapate kuzingatia kwa makini Aayaat zake, na ili wapate kukumbuka wenye akili. [Swaad (38:29)]

5-Jitakase Kwa Twahara Na Tawbah, Kwani Allaah Anawapenda Wenye Kujitakasa:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Qudduws, kwamba Allaah Anawapenda wanaojitakasa; basi jitakase kwa twahara ya mwili na tawbah ya moyo.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾

Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: Hiyo ni dhara, hivyo basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike. Watakapotwaharika basi waendeeni kupitia pale Alipokuamrisheni Allaah. Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha. [Al-Baqarah (2:222)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي مَالِكٍ الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الطُّهُورُ شَطْرُ الإِيمَانِ))

Amesimulia Abuu Maalik Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Twahara ni nusu ya imaan.” [Muslim]

6-Jitakase Kwa Kusimamisha Swalaah Tano:

Tambua, ee Mja wa Al-Qudduws: Swalaah inamwepusha mja na machafu na maovu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۗ وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ ﴿٤٥﴾

Soma uliyofunuliwa Wahy katika Kitabu na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. Na bila shaka kumdhukuru Allaah ndilo kubwa zaidi. Na Allaah Anajua yale mnayoyatenda. [Al-‘Ankabuwt (29:45)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّهُ سَمِعَ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((أَرَأَيْتُمْ لَوْ أَنَّ نَهَرًا بِبَابِ أَحَدِكُمْ يَغْتَسِلُ فِيهِ كُلَّ يَوْمٍ خَمْسًا، مَا تَقُولُ ذَلِكَ يُبْقِي مِنْ دَرَنِهِ؟)) قَالُوا: لاَ يُبْقِي مِنْ دَرَنِهِ شَيْئًا. قَالَ: ((فَذَلِكَ مِثْلُ الصَّلَوَاتِ الْخَمْسِ، يَمْحُو اللَّهُ بِهِ الْخَطَايَا))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba alimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Mnaonaje lau kungekuwa na mto mlangoni mwa mmoja wenu, akaoga humo kila siku mara tano, je, mnasemaje, hilo litabakisha uchafu wake wowote?” Wakasema: Halitabakisha uchafu wake wowote. Akasema: “Basi huo ndio mfano wa Swalaah tano; Allaah Anafuta kwazo makosa.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

7-Jitakase Kwa Zakaah Na Swadaqah:

Tambua, ee Mja wa Al-Qudduws: Zakaah maana yake ni kutakasa; na kutoa mali kwa ajili ya Allaah ni njia ya kujitakasa na kujipatia baraka katika mali, kwani Allaah Ameahidi kuizidisha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ ۖ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿١٠٣﴾

Chukua katika mali zao swadaqa, uwatwaharishe na uwatakase kwazo, na waombee duaa (na maghfirah). Hakika duaa yako ni utulivu kwao. Allaah Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote. [At-Tawbah (9:103)]

8-Jitakase Na Dhulma Ambayo Allaah Ameiharamisha:

Tambua, ee Mja wa Al-Qudduws: Katika Hadiyth Al-Qudsiy, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِيمَا رَوَى عَنِ اللَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى أَنَّهُ قَالَ: ((يَا عِبَادِي، إِنِّي حَرَّمْتُ الظُّلْمَ عَلَى نَفْسِي، وَجَعَلْتُهُ بَيْنَكُمْ مُحَرَّمًا، فَلاَ تَظَالَمُوا))

Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesimulia kutoka kwa Allaah (تبارك وتعالى) kwamba Amesema: “Enyi Waja Wangu! Hakika Mimi Nimeiharamishia Nafsi Yangu dhulma, na Nimeijaalia kuwa ni haramu baina yenu, basi msidhulumiane.” [Muslim]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿٤٠﴾

Hakika Allaah Hadhulumu hata uzito au chembe (kama atomu). Na ikiwa ni amali njema Huizidisha na Hutoa kutoka Kwake ujira mkuu kabisa. [An-Nisaa (4:40)]

9-Mtukuze Al-Qudduws Katika Rukuu Na Sujuud Yako:

Mtukuze Al-Qudduws katika Rukuu na Sujuud yako kwa maneno haya.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametufundisha adhkaar za kumtukuza Al-Qudduws:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُولُ فِي رُكُوعِهِ وَسُجُودِهِ: ((سُبُّوحٌ قُدُّوسٌ رَبُّ الْمَلاَئِكَةِ وَالرُّوحِ))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema katika Rukuu yake na Sujuud yake:

سُبُّوحٌ قُدُّوسٌ رَبُّ الْمَلاَئِكَةِ وَالرُّوحِ

Mwingi wa kutakaswa, Mtakatifu, Rabb wa Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl). [Muslim]

10-Mtakase Al-Malik Al-Qudduws Baada Ya Swalaah Ya Witri:

Tambua, ee Mja wa Al-Qudduws: Na miongoni mwa adhkaar za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) baada ya kutoa salaam ya Witri:

عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ أَبْزَى (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يُوتِرُ بِـ﴿سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى﴾ وَ﴿قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ﴾ وَ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾، وَكَانَ يَقُولُ إِذَا سَلَّمَ: ((سُبْحَانَ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ)) ثَلاَثًا، وَيَرْفَعُ صَوْتَهُ بِالثَّالِثَةِ

Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Abzaa (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiswali Witri kwa (kusoma) ﴿سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى﴾, na ﴿قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ﴾ na ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾; na alikuwa anapotoa salaam husema:

سُبْحَانَ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ

Utakasifu ni wa Mfalme, Mtakatifu; mara tatu, na huinua sauti yake katika ya tatu. [An-Nasaaiy (1731), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh An-Nasaaiy]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله), kama ilivyokusanywa katika Tafsiyr Ibn Al-Qayyim, Aal-‘Imraan (3:26); na imenukuliwa na Kalemtayeb katika maelezo ya Jina Al-Qudduws.
  • 2Tafsiyr Ibn Kathiyr, Suwrah Al-Hashr (59:23); imenukuliwa na Kalemtayeb.