As-Salaam: Aliyesalimika na kila aibu, kasoro na upungufu; Mwenye kuwasalimisha Waja Wake, na Chanzo cha kila amani na usalama.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾
Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye Kusadikisha ahadi na Kuaminisha, Mwenye Kudhibiti Kushuhudia Kuchunga na Kuhifadhi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Jabari Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye Ukubwa na Uadhama, Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha. [Al-Hashr (59:23)]
Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Mwenye haki ya Jina hili tukufu Peke Yake, Jina lenye maana zote za ukamilifu; kwani Yeye Ni As-Salaam katika kila hali na kwa kila namna. Yeye Ndiye Aliyesalimika na kila ovu, shari, aibu, kasoro na upungufu: Ni As-Salaam katika Dhati Yake, katika Majina Yake na Sifa Zake, na katika matendo Yake Aliyesalimika na dhulma. Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema:
فَهُوَ سَلَامٌ سُبْحَانَهُ فِي ذَاتِهِ عَنْ كُلِّ عَيْبٍ وَنَقْصٍ يَتَخَيَّلُهُ وَهْمٌ، وَسَلَامٌ فِي صِفَاتِهِ مِنْ كُلِّ عَيْبٍ وَنَقْصٍ، وَسَلَامٌ فِي أَفْعَالِهِ مِنْ كُلِّ عَيْبٍ وَنَقْصٍ وَشَرٍّ وَظُلْمٍ، وَفِعْلٍ وَاقِعٍ عَلَى غَيْرِ الْحِكْمَةِ، بَلْ هُوَ السَّلَامُ الْحَقُّ مِنْ كُلِّ وَجْهٍ
“Yeye (سبحانه) Ni As-Salaam katika Dhati Yake, Amesalimika na kila aibu na upungufu unaoweza kuwaziwa; na Ni As-Salaam katika Sifa Zake, Amesalimika na kila aibu na upungufu; na Ni As-Salaam katika matendo Yake, Amesalimika na kila aibu, upungufu, shari, dhulma, na kitendo kisicho cha hikmah. Bali Yeye Ndiye As-Salaam wa haki kwa kila namna.”1
As-Salaam Huwasalimisha Waja Wake:
1-Yeye (تبارك وتعالى) Ndiye Aliyewasalimisha Waja Wake na kila adhabu wasiyoistahiki, na Amewasalimisha na kila dhulma duniani na Aakhirah.
2-Amewasalimisha Manabii Wake, Akawasifu na kuwatakasa na aibu na maovu, na Akawasalimisha vipenzi Vyake Aliowachagua. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ وَسَلَامٌ عَلَىٰ عِبَادِهِ الَّذِينَ اصْطَفَىٰ ۗ آللَّـهُ خَيْرٌ أَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٥٩﴾
Sema: AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) na amani iwe juu ya Waja Wake Aliowakhitari. Je, Allaah Ni bora au wale wanaowashirikisha (Naye)? [An-Naml (27:59)]
Na Akamsalimisha Nabiy Nuwh (عليه السلام):
سَلَامٌ عَلَىٰ نُوحٍ فِي الْعَالَمِينَ ﴿٧٩﴾
Salaamun! (Amani) iwe juu ya Nuwh ulimwenguni. [Asw-Swaaffaat (37:79)]
Na Nabiy Ibraahiym (عليه السلام):
سَلَامٌ عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ ﴿١٠٩﴾
Salaamun! (Amani) iwe juu ya Ibraahiym. [Asw-Swaaffaat (37:109)]
Na Nabiy Muwsaa na Haaruwn (عليهما السلام):
سَلَامٌ عَلَىٰ مُوسَىٰ وَهَارُونَ ﴿١٢٠﴾
Salaamun! (Amani) iwe juu ya Muwsaa na Haaruwn. [Asw-Swaaffaat (37:120)]
Na Nabiy Ilyaas (عليه السلام):
سَلَامٌ عَلَىٰ إِلْ يَاسِينَ ﴿١٣٠﴾
Salaamun! (Amani) iwe juu ya Ilyaasiyn. [Asw-Swaaffaat (37:130)]
Na Akawasalimisha Rusuli Wake wote:
وَسَلَامٌ عَلَى الْمُرْسَلِينَ ﴿١٨١﴾
Na Salaamun! (Amani) iwe juu ya Rusuli. [Asw-Swaaffaat (37:181)]
3-Na Aakhirah Atawasalimisha Waja Wake watakapoingia Jannah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ ﴿٥٥﴾ هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ ﴿٥٦﴾ لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُم مَّا يَدَّعُونَ ﴿٥٧﴾ سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾
Hakika watu wa Jannah leo wamo katika kushughulika wakifurahi. Wao na wake zao, wakiwa katika vivuli, juu ya makochi ya fakhari wakiegemea. Watapata humo kila aina ya matunda, na watapata wanavyoomba. Salaamun! Kauli kutoka kwa Rabb Mwenye Kurehemu. [Yaasiyn (36:55-58)]
Na Anasema pia:
تَحِيَّتُهُمْ يَوْمَ يَلْقَوْنَهُ سَلَامٌ ۚ وَأَعَدَّ لَهُمْ أَجْرًا كَرِيمًا ﴿٤٤﴾
Maamkizi yao Siku watakayokutana Naye ni “Salaam.” Na Amewaandalia ujira wa ukarimu. [Al-Ahzaab (33:44)]
Ni salama itokayo kwa Allaah (سبحانه وتعالى), inayotosheleza kuliko salama nyingine yoyote na maamkizi mengine yoyote. Basi ni vipi kuhusu maamkizi ya Mfalme wa wafalme, Rabb wa walimwengu, kwa vipenzi Vyake?
4-Yeye Ndiye chanzo cha amani na usalama; kila amani hutoka Kwake, basi usitafute amani na usalama isipokuwa Kwake (تبارك وتعالى). Huwasalimisha Awatakao katika Waja Wake kwa mujibu wa Hikmah Yake na Uadilifu Wake duniani. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((مَثَلُ الْمُجَاهِدِ فِي سَبِيلِ اللَّهِ - وَاللَّهُ أَعْلَمُ بِمَنْ يُجَاهِدُ فِي سَبِيلِهِ - كَمَثَلِ الصَّائِمِ الْقَائِمِ، وَتَوَكَّلَ اللَّهُ لِلْمُجَاهِدِ فِي سَبِيلِهِ بِأَنْ يَتَوَفَّاهُ أَنْ يُدْخِلَهُ الْجَنَّةَ، أَوْ يَرْجِعَهُ سَالِمًا مَعَ أَجْرٍ أَوْ غَنِيمَةٍ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Mfano wa Mujaahid katika Njia ya Allaah, na Allaah Anamjua zaidi anayepigana katika Njia Yake, ni kama mfano wa mwenye kufunga Swawm na kusimama (usiku kuswali). Na Allaah Amemdhamini Mujaahid katika Njia Yake kwamba Akimfisha Atamwingiza Jannah, au Atamrudisha salama pamoja na ujira au ngawira.” [Al-Bukhaariy]
5-Na Siku ya Qiyaamah, wakati watu watakapovuka Asw-Swiraatw, du’aa ya Rusuli itakuwa ni kumwomba As-Salaam salama. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) فِي حَدِيثِ الرُّؤْيَةِ الطَّوِيلِ، قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... فَأَكُونُ أَوَّلَ مَنْ يُجِيزُ، وَدُعَاءُ الرُّسُلِ يَوْمَئِذٍ: اللَّهُمَّ سَلِّمْ سَلِّمْ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) katika Hadiyth ndefu ya kumwona Allaah: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “… nami nitakuwa wa kwanza kuvuka (Asw-Swiraatw), na du’aa ya Rusuli siku hiyo itakuwa:
اللَّهُمَّ سَلِّمْ سَلِّمْ
Yaa Allaah, salimisha! Salimisha!” [Al-Bukhaariy]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, As-Salaam:
1-Mwombe As-Salaam Salama Ya Dini Yako Na Moyo Uliosalimika:
Tambua, ee Mja wa As-Salaam: Salama ya Aakhirah ni salama katika Dini: kuomba kusalimika na ukafiri, shirki, unafiki, bid’ah na maasi, na kumfikia Rabb wako kwa imaan yenye nguvu na moyo uliosalimika. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾ إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾
Siku hayatofaa mali wala watoto. Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa (26:88-89)]
2-Mwombe As-Salaam Afya Na Salama Duniani:
Tambua, ee Mja wa As-Salaam: Salama ya duniani ni kama kuomba afya kutokana na maradhi, maafa na kila unalolichukia. Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisisitiza kuomba afya, na akabainisha kwamba hakuna kitu bora baada ya yakini (imaan) kuliko afya:
عَنْ أَبِي بَكْرٍ الصِّدِّيقِ (رضي الله عنه) أَنَّهُ قَامَ عَلَى الْمِنْبَرِ ثُمَّ بَكَى فَقَالَ: قَامَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) عَامَ الأَوَّلِ عَلَى الْمِنْبَرِ ثُمَّ بَكَى فَقَالَ: ((سَلُوا اللَّهَ الْعَفْوَ وَالْعَافِيَةَ، فَإِنَّ أَحَدًا لَمْ يُعْطَ بَعْدَ الْيَقِينِ خَيْرًا مِنَ الْعَافِيَةِ))
Amesimulia Abuu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه) kwamba alisimama juu ya minbari kisha akalia, akasema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisimama mwaka uliopita juu ya minbari kisha akalia, akasema: “Mwombeni Allaah msamaha na afya; kwani hakika hakuna aliyepewa kitu bora baada ya yakini kuliko afya.” [At-Tirmidhiy (3558), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan Swahiyh katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
3-Kuwa Na Moyo Uliosalimika Na Chuki Kwa Waumini Wenzako:
Mwenye kumjua As-Salaam hutakasa moyo wake na chuki na husuda dhidi ya ndugu zake, na huwaombea kama walivyowaombea Waumini waliokuja baada ya Swahaba:
وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٠﴾
Na wale waliokuja baada yao wanasema: Rabb wetu! Tughufurie pamoja na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imaan, na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Rabb wetu! Hakika Wewe Ni Mwenye Huruma mno, Mwenye Kurehemu. [Al-Hashr (59:10)]
4-Salimisha Ulimi Wako Na Mkono Wako Na Kuwaudhi Watu:
Kumbuka, ee Mja wa As-Salaam, kwamba alama ya Muislamu wa kweli ni kwamba watu wanasalimika na shari ya ulimi wake na mkono wake.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو (رضي الله عنهما) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((الْمُسْلِمُ مَنْ سَلِمَ الْمُسْلِمُونَ مِنْ لِسَانِهِ وَيَدِهِ، وَالْمُهَاجِرُ مَنْ هَجَرَ مَا نَهَى اللَّهُ عَنْهُ))
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنهما) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Muislamu ni yule ambaye Waislamu wamesalimika na ulimi wake na mkono wake; na Muhaajir ni yule aliyehama yale Aliyoyakataza Allaah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
5-Eneza Salaam, Kwani Ni Jina La Allaah Aliloliweka Ardhini:
Unapomwamkia mtu kwa kusema: “As-Salaamu ‘alaykum” (Amani iwe juu yenu), maana yake ni: Mko katika amani, na hamtapata ovu lolote kutoka kwangu. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((السَّلاَمُ اسْمٌ مِنْ أَسْمَاءِ اللَّهِ تَعَالَى، وَضَعَهُ فِي الأَرْضِ، فَأَفْشُوا السَّلاَمَ بَيْنَكُمْ))
Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “As-Salaam ni Jina miongoni mwa Majina ya Allaah (تعالى), Ameliweka ardhini; basi enezeni salaam baina yenu.” [Al-Bazzaar, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Al-Jaami’ (3697)]
6-Eneza Salaam Upate Kuingia Daarus-Salaam Kwa Salama:
Tambua, ee Mja wa As-Salaam: Hii ilikuwa miongoni mwa mafundisho ya kwanza kabisa ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipofika Madiynah:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ سَلاَمٍ (رضي الله عنه) قَالَ: ... فَكَانَ أَوَّلُ شَيْءٍ تَكَلَّمَ بِهِ أَنْ قَالَ: ((أَيُّهَا النَّاسُ، أَفْشُوا السَّلاَمَ، وَأَطْعِمُوا الطَّعَامَ، وَصَلُّوا وَالنَّاسُ نِيَامٌ، تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ بِسَلاَمٍ))
Amesimulia ‘Abdullaah bin Salaam (رضي الله عنه): … Na jambo la kwanza alilolizungumza (Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم) ni kusema: “Enyi watu! Enezeni salaam, lisheni chakula, na swalini usiku watu wakiwa wamelala; mtaingia Jannah kwa salama.” [At-Tirmidhiy (2485), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
Na Jannah yenyewe imeitwa Daarus-Salaam (Nyumba ya Amani). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاللَّـهُ يَدْعُو إِلَىٰ دَارِ السَّلَامِ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴿٢٥﴾
Na Allaah Anaitia katika Daar As-Salaam (Nyumba ya amani) na Anamwongoza Amtakaye kuelekea njia iliyonyooka. [Yuwnus (10:25)]
7-Itikia Salaam Kwa Iliyo Bora Zaidi:
Tambua, ee Mja wa As-Salaam, kwamba kuitikia salaam ni wajibu, na kuiitikia kwa iliyo bora zaidi ni fadhila.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذَا حُيِّيتُم بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّوا بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَسِيبًا ﴿٨٦﴾
Na mtakapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo au yarudisheni hayo hayo. Hakika Allaah daima Ni Mwenye Kuhesabu kila kitu. [An-Nisaa (4:86)]
8-Kithirisha Kumswalia Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) Na Kumwombea Salama:
Kumbuka kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa wingi, kwani As-Salaam na Malaika Wake Wanamswalia.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾
Hakika Allaah na Malaika Wake Wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini! Mswalieni na msalimieni kwa maamkizi ya amani. [Al-Ahzaab (33:56)]
9-Mwombe Allaah Kwa Jina Lake As-Salaam Unapofikwa Na Shida:
Allaah Ameamrisha Aombwe kwa Majina Yake Mazuri. Basi unapofikwa na maradhi, maafa au dhiki, mwombe kwa Jina Lake As-Salaam Akusalimishe nayo na Akuponye. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٨٠﴾
Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaopotoa na kuharibu Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’raaf (7:180)]
10-Usiache Du’aa Ya Baada Ya Kila Swalaah Inayomtaja As-Salaam:
Omba du’aa hii baada ya kila Swalaah ya faradhi, ukikiri kwamba salama yote inatoka kwa As-Salaam.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ ثَوْبَانَ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) إِذَا انْصَرَفَ مِنْ صَلاَتِهِ اسْتَغْفَرَ ثَلاَثًا، وَقَالَ: ((اللَّهُمَّ أَنْتَ السَّلاَمُ، وَمِنْكَ السَّلاَمُ، تَبَارَكْتَ ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرَامِ))
Amesimulia Thawbaan (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapomaliza Swalaah yake huomba maghfirah mara tatu, na husema:
أَسْتَغْفِرُ اللَّهَ، أَسْتَغْفِرُ اللَّهَ، أَسْتَغْفِرُ اللَّهَ، اللَّهُمَّ أَنْتَ السَّلاَمُ، وَمِنْكَ السَّلاَمُ، تَبَارَكْتَ ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرَامِ
Namuomba Allaah maghfirah (mara tatu). Yaa Allaah! Wewe Ndiye As-Salaam, na Kwako ndiko kutokako salama; Umebarikika, yaa Mwenye Ujalali na Ukarimu. [Muslim]
11-Dumisha Du’aa Ya Asubuhi Na Jioni Ya Kuomba Salama:
Omba, ee Mja wa As-Salaam, du’aa hii kila asubuhi na jioni, kama alivyokuwa akifanya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) bila kuiacha.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwa akiacha du’aa hii asubuhi na jioni:
عَنِ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَالَ: لَمْ يَكُنْ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَدَعُ هَؤُلاَءِ الدَّعَوَاتِ حِينَ يُمْسِي وَحِينَ يُصْبِحُ: ((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَفْوَ وَالْعَافِيَةَ فِي دِينِي وَدُنْيَايَ وَأَهْلِي وَمَالِي، اللَّهُمَّ اسْتُرْ عَوْرَاتِي، وَآمِنْ رَوْعَاتِي، اللَّهُمَّ احْفَظْنِي مِنْ بَيْنِ يَدَيَّ، وَمِنْ خَلْفِي، وَعَنْ يَمِينِي، وَعَنْ شِمَالِي، وَمِنْ فَوْقِي، وَأَعُوذُ بِعَظَمَتِكَ أَنْ أُغْتَالَ مِنْ تَحْتِي))
Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwa akiziacha du’aa hizi anapoingia jioni na anapoamka asubuhi:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَفْوَ وَالْعَافِيَةَ فِي دِينِي وَدُنْيَايَ وَأَهْلِي وَمَالِي، اللَّهُمَّ اسْتُرْ عَوْرَاتِي، وَآمِنْ رَوْعَاتِي، اللَّهُمَّ احْفَظْنِي مِنْ بَيْنِ يَدَيَّ، وَمِنْ خَلْفِي، وَعَنْ يَمِينِي، وَعَنْ شِمَالِي، وَمِنْ فَوْقِي، وَأَعُوذُ بِعَظَمَتِكَ أَنْ أُغْتَالَ مِنْ تَحْتِي
Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba afya duniani na Aakhirah. Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba msamaha na afya katika Dini yangu, dunia yangu, ahli zangu na mali yangu. Yaa Allaah! Nisitiri aibu zangu, na Unitulize khofu zangu. Yaa Allaah! Nihifadhi mbele yangu, nyuma yangu, kuliani kwangu, kushotoni kwangu, na juu yangu; na najikinga kwa Utukufu Wako nisiangamizwe kwa ghafla kutoka chini yangu. [Abuu Daawuwd (5074), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله), Badaai’ Al-Fawaaid, fasli ya maana ya As-Salaam; kama ilivyokusanywa katika Tafsiyr Ibn Al-Qayyim (tafsir.app), Al-Hashr (59:23).