Al-Muumin: Mwenye kusadikisha Ahadi Zake, Mwenye kuwapa Waja Wake amani na usalama.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾
Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye Kusadikisha ahadi na Kuaminisha, Mwenye Kudhibiti Kushuhudia Kuchunga na Kuhifadhi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Jabari Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye Ukubwa na Uadhama, Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha. [Al-Hashr (59:23)]
Maana za Jina hili zimetumika katika Qur-aan kwa namna mbili. Kwanza, kusadikisha, kama katika kisa cha nduguze Nabiy Yuwsuf (عليه السلام) walipomwambia baba yao:
قَالُوا يَا أَبَانَا إِنَّا ذَهَبْنَا نَسْتَبِقُ وَتَرَكْنَا يُوسُفَ عِندَ مَتَاعِنَا فَأَكَلَهُ الذِّئْبُ ۖ وَمَا أَنتَ بِمُؤْمِنٍ لَّنَا وَلَوْ كُنَّا صَادِقِينَ﴿١٧﴾
Wakasema: Ee baba yetu! Hakika sisi tulikwenda kushindana mbio na tulimwacha Yuwsuf kwenye vitu vyetu, basi mbwa mwitu akamla. Nawe hutotuamini japo ni wakweli. [Yuwsuf (12:17)]
Na pili, amani na usalama, ambayo ni kinyume cha khofu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَلْيَعْبُدُوا رَبَّ هَـٰذَا الْبَيْتِ ﴿٣﴾ الَّذِي أَطْعَمَهُم مِّن جُوعٍ وَآمَنَهُم مِّنْ خَوْفٍ ﴿٤﴾
Basi wamuabudu Rabb wa Nyumba hii (Ka’bah). Ambaye Anawalisha kuwaokoa na njaa, na Anawapa amani kutokana na khofu. [Quraysh (106:3-4)]
Maana Ya Al-Muumin:
Jina hili tukufu lina maana nyingi za ukamilifu na utukufu:
1-Allaah (عزّ وجلّ) Amewapa watu amani kwamba Yeye Hatawadhulumu hata kidogo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ النَّاسَ شَيْئًا وَلَـٰكِنَّ النَّاسَ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ﴿٤٤﴾
Hakika Allaah Hadhulumu watu chochote, lakini watu wenyewe ni wenye kudhulumu nafsi zao. [Yuwnus (10:44)]
Na Atawapa amani ya kutodhulumiwa wanaostahiki Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَالْيَوْمَ لَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا وَلَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٥٤﴾
Basi leo nafsi yoyote haitodhulumiwa kitu chochote, na wala hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda. [Yaasiyn (36:54)]
2-Yeye (عزّ وجلّ) Anasadikisha Ahadi Zake kwa Waja Wake, kila Anachowabashiria katika mambo ya ghaibu kwa njia ya Wahy; ahadi za mazuri na maonyo, duniani na Aakhirah. Anawasadikishia Waumini ahadi ya thawabu:
جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًاۖ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُۚ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ ﴿٨﴾
Jazaa yao iko kwa Rabb wao. Nayo ni Jannaat za kudumu milele zipitazo chini yake mito, wadumu humo abadi. Allaah Ataridhika nao, nao wataridhika Naye. Hayo ni kwa yule anayemkhofu Rabb wake. [Al-Bayyinah (98:8)]
Na Anawasadikishia makafiri na wanafiki onyo la adhabu:
وَعَدَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْكُفَّارَ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ هِيَ حَسْبُهُمْ ۚ وَلَعَنَهُمُ اللَّـهُ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّقِيمٌ﴿٦٨﴾
Allaah Amewaahidi wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri moto wa Jahannam, wadumu humo, inawatosheleza hiyo (adhabu)! Na Allaah Amewalaani, na watapata adhabu ya kudumu. [At-Tawbah (9:68)]
3-Yeye (عزّ وجلّ) Anawapa amani wale waliomwamini na kumpwekesha, kwamba hawatapata Adhabu Yake kwa kuwa wamejiepusha na dhulma ya kumshirikisha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٨٢﴾
Wale walioamini na hawakuchanganya imaan zao na dhulma, hao ndio watakaopata amani nao ndio waliohidika. [Al-An’aam (6:82)]
4-Wanaopewa amani zaidi na Allaah (سبحانه وتعالى) ni waja wema; Huwapa amani katika nyoyo zao duniani na Siku ya Mwisho:
Duniani: Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا ۚ وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٥٥﴾
Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba bila shaka Atawafanya warithi katika ardhi kama Alivyowafanya warithi wale waliokuwa kabla yao, na bila shaka Atawamakinishia Dini yao Aliyowaridhia, na bila shaka Atawabadilishia amani badala ya khofu yao, wawe wananiabudu Mimi wasinishirikishe na chochote. Na yeyote atakayekufuru baada ya hapo, basi hao ndio mafasiki. [An-Nuwr (24:55)]
Na katika jihaad na mitihani huteremsha sababu za amani, kama usingizi wa utulivu:
إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ﴿١١﴾
Pindi Alipokufunikeni kwa usingizi kuwa ni amani kutoka Kwake, na Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, ili Akutwaharisheni kwayo, na Akuondosheeni wasiwasi na rai ovu za shaytwaan, na ili Atie nguvu nyoyo zenu, na Aisimamishe kwayo imara miguu. [Al-Anfaal (8:11)]
Na utulivu katika nyoyo za Waumini:
هُوَ الَّذِي أَنزَلَ السَّكِينَةَ فِي قُلُوبِ الْمُؤْمِنِينَ لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ ۗ وَلِلَّـهِ جُنُودُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا﴿٤﴾
Yeye Ndiye Aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili wazidi imaan pamoja na imaan zao. Na ni ya Allaah Pekee majeshi ya mbinguni na ardhini. Na Allaah daima Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Fat-h (48:4)]
Na Akawapa Rusuli Wake ushindi dhidi ya maadui Zake, Akawasadikishia ahadi:
ثُمَّ صَدَقْنَاهُمُ الْوَعْدَ فَأَنجَيْنَاهُمْ وَمَن نَّشَاءُ وَأَهْلَكْنَا الْمُسْرِفِينَ ﴿٩﴾
Kisha Tukawasadikishia ahadi, Tukawaokoa wao na wale Tuliowataka, na Tukaangamiza wapindukiaji mipaka. [Al-Anbiyaa (21:9)]
Na Anasema pia (Pamoja na Malaika kwa Nusra Yake na Msaada Wake):
إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ فَاضْرِبُوا فَوْقَ الْأَعْنَاقِ وَاضْرِبُوا مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ﴿١٢﴾
Pindi Rabb wako Alipowatia ilhamu Malaika (kuwaambia): Hakika Mimi Niko pamoja nanyi, basi wathibitisheni wale walioamini. Nitatia kizaazaa katika nyoyo za waliokufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kila kiungo (au ncha za vidole). [Al-Anfaal (8:12)]
Wakati wa mauti: Allaah (سبحانه وتعالى) Anawapa Waumini amani pale Malaika wanapoteremka kutoa roho zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾ نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ﴿٣١﴾ نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ﴿٣٢﴾
Hakika wale waliosema: Rabb wetu ni Allaah, kisha wakathibiti imara, Malaika huwateremkia (kuwaambia): Msikhofu, wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa. Sisi ni rafiki zenu walinzi katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoyahitajia. Ni mapokezi ya takrima kutoka kwa Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Fusw-Swilat (41:30-32)]
Katika Al-Barzakh (maisha baina ya kufariki mpaka kufufuliwa): Allaah Anawapa amani Waja Wake wanaolinda mipaka ya Waislamu katika Njia Yake kwa kuwahifadhi na fitna ya kaburi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ فَضَالَةَ بْنِ عُبَيْدٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ قَالَ: ((كُلُّ مَيِّتٍ يُخْتَمُ عَلَى عَمَلِهِ، إِلاَّ الَّذِي مَاتَ مُرَابِطًا فِي سَبِيلِ اللَّهِ، فَإِنَّهُ يُنْمَى لَهُ عَمَلُهُ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ، وَيَأْمَنُ مِنْ فِتْنَةِ الْقَبْرِ))
Amesimulia Fadhwaalah bin ‘Ubayd (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kila maiti amali zake hufungwa, isipokuwa aliyekufa akiwa analinda mipaka katika Njia ya Allaah; hakika huyo amali zake huzidishwa mpaka Siku ya Qiyaamah, na atapata amani kutokana na fitna ya kaburi.” [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy (1621) na amesema: Hasan Swahiyh, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
Aakhirah: Allaah (سبحانه وتعالى) Anawapa Waumini amani katika mfazaiko mkubwa wa Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ ﴿١٠١﴾ لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا ۖ وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَالِدُونَ ﴿١٠٢﴾ لَا يَحْزُنُهُمُ الْفَزَعُ الْأَكْبَرُ وَتَتَلَقَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ هَـٰذَا يَوْمُكُمُ الَّذِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿١٠٣﴾
Hakika wale ambao imewatangulia Al-Husnaa (furaha, Rehma) kutoka Kwetu, hao watabaidishwa nao (moto). Hawatosikia mvumo wake. Nao watadumu katika ambayo zimetamani nafsi zao. Hautowahuzunisha mfazaiko mkubwa kabisa, na Malaika watawapokea (wakiwaambia): Hii ni ile Siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa. [Al-Anbiyaa (21:101-103)]
Na Anawapa amani kutokana na adhabu ya moto:
إِنَّ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي آيَاتِنَا لَا يَخْفَوْنَ عَلَيْنَا ۗ أَفَمَن يُلْقَىٰ فِي النَّارِ خَيْرٌ أَم مَّن يَأْتِي آمِنًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ ۖ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٤٠﴾
Hakika wale wanaozipotosha Aayaat Zetu hawawezi kujificha Tusiwaone. Je, basi yule atakayetupwa katika moto ni bora au yule atakayekuja akiwa katika amani Siku ya Qiyaamah? Tendeni mpendavyo, hakika Yeye Ni Mwenye Kuona yote myatendayo. [Fusw-Swilat (41:40)]
Jannah: Anawasadikishia Ahadi Yake na Anawapa amani katika maisha ya furaha ya milele:
وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي صَدَقَنَا وَعْدَهُ وَأَوْرَثَنَا الْأَرْضَ نَتَبَوَّأُ مِنَ الْجَنَّةِ حَيْثُ نَشَاءُ ۖ فَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ﴿٧٤﴾
Watasema: AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Ambaye Ametuhakikishia kweli Ahadi Yake, na Ameturithisha ardhi tunakaa popote katika Jannah tutakapo. Basi uzuri ulioje ujira wa watendao! [Az-Zumar (39:74)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muumin:
1-Amini Ahadi Za Allaah Bila Shaka, Na Mkimbilie Al-Muumin Wakati Wa Khofu:
Muumini anapaswa kuzingatia maana ya Al-Muumin na kutenda kwa mujibu wake; asiwe na shaka yoyote katika Ahadi za Allaah (تعالى), na ajue kwamba Yeye Ndiye Mwenye kumpa amani kutokana na kila khofu. Basi marejeo yake yote katika hali ya khofu na upungufu yawe kwa Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾
Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa Dhikru-Allaah. Tanabahi! Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia! [Ar-Ra’d (13:28)]
2-Waaminishe Watu Juu Ya Nafsi Zao Na Mali Zao:
Tambua, ee Mja wa Al-Muumin: Muumini anapaswa kuwapa Waumini wenzake amani kutokana na shari za kila aina. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ فَضَالَةَ بْنِ عُبَيْدٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((أَلاَ أُخْبِرُكُمْ بِالْمُؤْمِنِ؟ مَنْ أَمِنَهُ النَّاسُ عَلَى أَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ، وَالْمُسْلِمُ مَنْ سَلِمَ النَّاسُ مِنْ لِسَانِهِ وَيَدِهِ، وَالْمُجَاهِدُ مَنْ جَاهَدَ نَفْسَهُ فِي طَاعَةِ اللَّهِ، وَالْمُهَاجِرُ مَنْ هَجَرَ الْخَطَايَا وَالذُّنُوبَ))
Amesimulia Fadhwaalah bin ‘Ubayd (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Je, nikujulisheni Muumini ni nani? Ni yule ambaye watu wanamwamini juu ya mali zao na nafsi zao. Na Muislamu ni yule ambaye watu wamesalimika na ulimi wake na mkono wake. Na Mujaahid ni yule anayepambana na nafsi yake katika kumtii Allaah. Na Muhaajir ni yule aliyehama makosa na madhambi.” [Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Ibn Maajah (3193) na As-Silsilah Asw-Swahiyhah (549)]
Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لاَ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مَنْ لاَ يَأْمَنُ جَارُهُ بَوَائِقَهُ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hataingia Jannah yule ambaye jirani yake hana amani na shari zake.” [Muslim]
3-Jiepushe Na Shari Za Ulimi Na Mkono:
Tambua, ee Mja wa Al-Muumin: Mifano ya shari za ulimi ni: ghiybah (kusengenya), namiymah (kufitinisha), kuwatusi watu, kuwakashifu, kuwakaripia, kuwadhihaki, na kushuhudia uongo.
Na mifano ya shari za mkono ni: kuwapiga watu na kuwaumiza, kuwaibia au kuwapunja mali zao, kuharibu mali zao, kupokea rushwa, kuandika maneno ya uongo, kashfa au matusi (kwa kalamu, simu au mitandao ya kijamii), na hata kuwatishia kwa silaha kwa mzaha. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لاَ يُشِيرُ أَحَدُكُمْ عَلَى أَخِيهِ بِالسِّلاَحِ، فَإِنَّهُ لاَ يَدْرِي لَعَلَّ الشَّيْطَانَ يَنْزِعُ فِي يَدِهِ فَيَقَعُ فِي حُفْرَةٍ مِنَ النَّارِ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Asimwashirie mmoja wenu nduguye kwa silaha, kwani hajui huenda shaytwaan akaiponyosha mkononi mwake, akaangukia shimo la moto.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
4-Kuwa Mkweli Katika Kauli Zako Na Amali Zako:
Tambua, ee Mja wa Al-Muumin: Muumini anapaswa kuwa mkweli daima katika kila hali, mpaka aandikwe mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa ni mkweli. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((عَلَيْكُمْ بِالصِّدْقِ، فَإِنَّ الصِّدْقَ يَهْدِي إِلَى الْبِرِّ، وَإِنَّ الْبِرَّ يَهْدِي إِلَى الْجَنَّةِ، وَمَا يَزَالُ الرَّجُلُ يَصْدُقُ وَيَتَحَرَّى الصِّدْقَ حَتَّى يُكْتَبَ عِنْدَ اللَّهِ صِدِّيقًا))
Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Lazimianeni na ukweli, kwani ukweli unaongoza kwenye wema, na wema unaongoza kwenye Jannah. Na mtu huendelea kusema kweli na kujitahidi kuwa mkweli mpaka huandikwa mbele ya Allaah kuwa ni mkweli mno.” [Muslim]
5-Tenda Mema Upate Amani Na Mfazaiko Wa Siku Ya Qiyaamah:
Tambua, ee Mja wa Al-Muumin: Muumini atende amali njema, aamini yaliyoahidiwa huko Jannah, na aogope yaliyoonywa ya adhabu na mafazaiko ya Siku hiyo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا وَهُم مِّن فَزَعٍ يَوْمَئِذٍ آمِنُونَ ﴿٨٩﴾
Atakayekuja na jema, basi atapata bora zaidi kuliko hilo, nao watakuwa katika amani na mafazaiko (kifo cha mshtuko) Siku hiyo. [An-Naml (27:89)]
6-Kuwa Mwaminifu Na Tekeleza Amana:
Tambua, ee Mja wa Al-Muumin: Aminika kwa watu; wanapokupa amana zao uzitunze, na wanapozitaka uwakabidhi. Tunza siri za watu. Na mwili wako pia ni amana, basi uutunze na uuhifadhi na maasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٥٨﴾
Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe. Na mtakapohukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Ni uzuri ulioje wa Anayokuwaidhini kwayo Allaah! Hakika Allaah daima Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [An-Nisaa (4:58)]
7-Kithirisha Kumdhukuru Allaah Upate Amani Ya Moyo:
Tambua, ee Mja wa Al-Muumin: Mdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa wingi pale imaan yako inapopungua, unapokosa utulivu na unapokuwa katika dhiki; kwani kumdhukuru Al-Muumin kunatuliza nyoyo na kunakubakisha katika amani (Rejea Ar-Ra’d (13:28) juu).
8-Mwombe Al-Muumin Akuthibitishe Katika Imaan Mpaka Kufa:
Omba du’aa ili Al-Muumin Akuthibitishe juu ya Dini Yake, kwani nyoyo ziko Mkononi Mwake Anazigeuza Atakavyo.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akikithirisha du’aa hii:
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يُكْثِرُ أَنْ يَقُولَ: ((يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِكَ))
Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akikithirisha kusema:
يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِكَ
Yaa Mgeuzaji wa nyoyo! Uthibitishe moyo wangu juu ya Dini Yako. [At-Tirmidhiy (2140), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
9-Mwombe Al-Muumin Akupe Amani Unapokuwa Na Khofu:
Tambua kwamba katika du’aa ya asubuhi na jioni ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwa akiiacha, alikuwa akimwomba Al-Muumin amani kutokana na khofu, akisema:
عَنِ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَالَ: لَمْ يَكُنْ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَدَعُ هَؤُلاَءِ الدَّعَوَاتِ حِينَ يُمْسِي وَحِينَ يُصْبِحُ: ((... اللَّهُمَّ اسْتُرْ عَوْرَاتِي، وَآمِنْ رَوْعَاتِي ...))
Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwa akiziacha du’aa hizi anapoingia jioni na anapoamka asubuhi: “…
اللَّهُمَّ اسْتُرْ عَوْرَاتِي، وَآمِنْ رَوْعَاتِي
Yaa Allaah! Nisitiri aibu zangu, na Unitulize (Unipe amani) khofu zangu …” (Du’aa kamili imo katika 019-As-Salaam). [Abuu Daawuwd (5074), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
10-Mwombe Al-Muumin Akuhifadhi Na Shari Ya Viungo Vyako:
Omba, ee Mja wa Al-Muumin, du’aa ya kujikinga na shari ya viungo vyako, kwani kila kiungo kinaweza kukutumbukiza katika maasi.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimfundisha Swahaba du’aa hii:
عَنْ شَكَلِ بْنِ حُمَيْدٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قُلْتُ: يَا نَبِيَّ اللَّهِ، عَلِّمْنِي تَعَوُّذًا أَتَعَوَّذُ بِهِ. قَالَ: ((قُلِ: اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ سَمْعِي، وَمِنْ شَرِّ بَصَرِي، وَمِنْ شَرِّ لِسَانِي، وَمِنْ شَرِّ قَلْبِي، وَمِنْ شَرِّ مَنِيِّي))
Amesimulia Shakal bin Humayd (رضي الله عنه): Nilisema: Yaa Nabiyya-Allaah! Nifundishe kinga ya kujikinga nayo. Akasema: “Sema:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ سَمْعِي، وَمِنْ شَرِّ بَصَرِي، وَمِنْ شَرِّ لِسَانِي، وَمِنْ شَرِّ قَلْبِي، وَمِنْ شَرِّ مَنِيِّي
Yaa Allaah! Hakika mimi najikinga Kwako kutokana na shari ya kusikia kwangu, na shari ya kuona kwangu, na shari ya ulimi wangu, na shari ya moyo wangu, na shari ya manii yangu.” [Abuu Daawuwd (1551), At-Tirmidhiy (3492), An-Nasaaiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
Na Allaah Mjuzi zaidi