Al-Muhaymin: Mwenye kushuhudia, kuchunga, kudhibiti na kuhifadhi; Mjuzi wa yaliyofichikana, Mwenye kuendesha mambo ya viumbe Vyake.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾
Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye Kusadikisha ahadi na Kuaminisha, Mwenye Kudhibiti Kushuhudia Kuchunga na Kuhifadhi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Jabari Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye Ukubwa na Uadhama, Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha. [Al-Hashr (59:23)]
Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amelifasiri Jina hili kuwa ni: “Ash-Shahiyd” (Mwenye kushuhudia), na mara nyingine: “Al-Amiyn” (Mwaminifu).1 Na Imaam Al-Bayhaqiy (رحمه الله) amesema:
الْمُهَيْمِنُ: هُوَ الشَّهِيدُ عَلَى خَلْقِهِ بِمَا يَكُونُ مِنْهُمْ مِنْ قَوْلٍ أَوْ عَمَلٍ
“Al-Muhaymin ni Mwenye kushuhudia juu ya viumbe Vyake kwa kila kinachotoka kwao, kauli au kitendo.”2 Na Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amesema:
الْمُهَيْمِنُ: الْمُطَّلِعُ عَلَى خَفَايَا الْأُمُورِ وَخَبَايَا الصُّدُورِ، الَّذِي أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا
“Al-Muhaymin ni Mwenye kujua mambo yaliyofichikana na siri za vifua, Ambaye Amekizunguka kila kitu kwa ilimu.”3
Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Ameisifu Qur-aan kwa sifa hii kuwa ni muhaymin; yaani ni Kitabu kinachodhibiti na kushuhudia juu ya vitabu vyote vilivyotangulia vya mbinguni, na kinahifadhi Dini na upotofu uliopachikwa ndani ya vitabu hivyo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ الْكِتَابِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ ۖ فَاحْكُم بَيْنَهُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ عَمَّا جَاءَكَ مِنَ الْحَقِّ ۚ لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَجَعَلَكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَكُمْ فِي مَا آتَاكُمْ ۖ فَاسْتَبِقُوا الْخَيْرَاتِ ۚ إِلَى اللَّـهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ ﴿٤٨﴾
Na Tumekuteremshia Kitabu kwa haki kinachosadikisha Vitabu vilivyokuwa kabla yake. Kinayadhibiti, kinayalinda na kuyashuhudia yaliyomo humo. Basi hukumu baina yao kwa yale Aliyoyateremsha Allaah, na wala usifuate hawaa zao ukaacha haki iliyokujia. Kila ummah katika nyinyi Tumeupangia sharia na manhaj. Na kama Allaah Angetaka, basi Angelikufanyeni ummah mmoja, lakini (Hakufanya) ili Akujaribuni katika yale Aliyokupeni. Basi shindaneni mambo ya kheri. Kwa Allaah Pekee ndio marejeo yenu nyote, kisha Atakujulisheni yale mliyokuwa mkikhitilafiana. [Al-Maaidah (5:48)]
Maana Ya Al-Muhaymin:
1-Allaah (عزّ وجلّ) Ndiye Mwenye kushuhudia matendo ya Waja Wake, Mwenye kuwachunga katika kauli zao na matendo yao; hakipotei Kwake chochote katika amali zao, na Anaangalia mambo yao ya ndani na yaliyomo ndani ya nyoyo zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ ۚ وَمَا يَعْزُبُ عَن رَّبِّكَ مِن مِّثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَلَا أَصْغَرَ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرَ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٦١﴾
Na hushughuliki katika jambo lolote, wala husomi humo katika Qur-aan, wala hamtendi amali yoyote isipokuwa Tunakuwa Mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo. Na hakifichiki kwa Rabb wako hata cha uzito wa chembe (kama atomu) katika ardhi, wala mbinguni, wala kidogo kuliko hicho, wala kikubwa zaidi ya hicho, isipokuwa kimo katika Kitabu bainifu. [Yuwnus (10:61)]
2-Yeye Ndiye Anayewachunga Waja Wake, Anawahifadhi na kuwalinda. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۗ وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ ۚ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَالٍ ﴿١١﴾
Ana Malaika wanaofuatana kwa zamu mbele yake na nyuma yake wanamhifadhi kwa Amri ya Allaah. Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao. Na Allaah Akiwakusudia watu adhabu, basi hakuna wa kuirudisha. Nao hawana mlinzi yeyote ghairi Yake. [Ar-Ra’d (13:11)]
3-Yeye Ndiye Mwenye kutengeneza hali zao na mambo yao, na kuyaendesha kwa Uwezo Wake, Naye Yuko juu ya ‘Arsh Yake adhimu, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu. Anajua kilicho na maslahi kwa mja na kinachomharibia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۗ وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْيَتَامَىٰ ۖ قُلْ إِصْلَاحٌ لَّهُمْ خَيْرٌ ۖ وَإِن تُخَالِطُوهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ الْمُفْسِدَ مِنَ الْمُصْلِحِ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَأَعْنَتَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٢٢٠﴾
Katika dunia na Aakhirah. Na wanakuuliza kuhusu mayatima. Sema: Kuwatengenezea (ya kuwafaa) ni kheri zaidi. Na mkichanganya mambo yenu na yao basi hao ni ndugu zenu. Na Allaah Anamjua fisadi na mtengenezaji. Na lau Angetaka Allaah Angelikutieni katika shida. Hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Baqarah (2:220)]
4-Yeye Ndiye Mjuzi wa siri zilizofichikana ndani ya vifua, Atakayezidhihirisha Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَوْمَ تُبْلَى السَّرَائِرُ ﴿٩﴾
Siku siri zitakapopekuliwa (na kufichuka). [At-Twaariq (86:9)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muhaymin:
1-Tahadhari! Al-Muhaymin Anakuchunga Na Anashuhudia Kila Kitu:
Tahadhari, ee ndugu Muislamu! Kila unalolifanya linashuhudiwa na Al-Muhaymin, hata kama wewe umelisahau.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا ۚ أَحْصَاهُ اللَّـهُ وَنَسُوهُ ۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٦﴾
Siku Atakayowafufua Allaah wote, Awajulishe yale waliyoyatenda. Allaah Ameyatia hesabuni barabara nao wameyasahau. Na Allaah Ni Shahidi juu ya kila kitu. [Al-Mujaadalah (58:6)]
Na Hakughafiliki na matendo ya madhalimu, bali Anawaakhirisha tu:
وَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّـهَ غَافِلًا عَمَّا يَعْمَلُ الظَّالِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍ تَشْخَصُ فِيهِ الْأَبْصَارُ ﴿٤٢﴾
Na wala usidhanie kabisa kwamba Allaah Ameghafilika na yale wanayoyatenda madhalimu. Hakika Anawaakhirisha kwa ajili ya Siku ambayo macho yatakodoka. [Ibraahiym (14:42)]
2-Chunga Macho Yako Na Siri Za Moyo Wako:
Al-Muhaymin Anajua hata mtazamo wa jicho wa khiyana; basi inamisha macho yako na haramu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَعْلَمُ خَائِنَةَ الْأَعْيُنِ وَمَا تُخْفِي الصُّدُورُ﴿١٩﴾
(Allaah) Anajua khiyana za macho na yale yanayoficha vifua. [Ghaafir (40:19)]
Na Anasema pia:
قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٣٠﴾
Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao. Hivyo ni utakaso zaidi kwao. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale wayatendayo. [An-Nuwr (24:30)]
3-Kuwa Mchungaji Mwaminifu Kwa Wale Uliopewa Kuwachunga:
Tambua, ee Mja wa Al-Muhaymin: Muumini anapaswa kuhisi kwamba Allaah Anamshuhudia katika usimamizi wake binafsi, katika familia yake, katika kazi yake na katika kila jukumu. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((أَلاَ كُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، فَالإِمَامُ الَّذِي عَلَى النَّاسِ رَاعٍ وَهُوَ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، وَالرَّجُلُ رَاعٍ عَلَى أَهْلِ بَيْتِهِ وَهُوَ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، وَالْمَرْأَةُ رَاعِيَةٌ عَلَى أَهْلِ بَيْتِ زَوْجِهَا وَوَلَدِهِ وَهِيَ مَسْئُولَةٌ عَنْهُمْ، وَعَبْدُ الرَّجُلِ رَاعٍ عَلَى مَالِ سَيِّدِهِ وَهُوَ مَسْئُولٌ عَنْهُ، أَلاَ فَكُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ))
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Tanabahi! Kila mmoja wenu ni mchungaji, na kila mmoja wenu ataulizwa juu ya aliowachunga. Kiongozi wa watu ni mchungaji naye ataulizwa juu ya aliowachunga; na mwanamume ni mchungaji wa ahli wa nyumba yake naye ataulizwa juu yao; na mwanamke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe na watoto wake naye ataulizwa juu yao; na mtumishi wa mtu ni mchungaji wa mali ya bwana wake naye ataulizwa juu yake. Tanabahi! Basi kila mmoja wenu ni mchungaji, na kila mmoja wenu ataulizwa juu ya aliowachunga.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
4-Isome Qur-aan Na Uifanyie Kazi, Kwani Ni Muhaymin Na Itakushuhudia:
Tambua, ee Mja wa Al-Muhaymin: Qur-aan itakuja kushuhudia ima kwa ajili yako kwa kuisoma na kuifanyia kazi, au dhidi yako kwa kuiacha. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي مَالِكٍ الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... وَالْقُرْآنُ حُجَّةٌ لَكَ أَوْ عَلَيْكَ ...))
Amesimulia Abuu Maalik Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “… Na Qur-aan ni hoja kwa ajili yako au dhidi yako …” [Muslim]
Kwa hiyo inakupasa uhalalishe yale Aliyoyahalalisha Allaah, uharamishe yale Aliyoyaharamisha, na ubakie ndani ya Mipaka ya Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).
5-Hukumu Kwa Qur-aan Katika Kila Unachokisimamia:
Tambua, ee Mja wa Al-Muhaymin: Kwa kuwa Qur-aan ni muhaymin juu ya vitabu vyote, mwenye mamlaka ya aina yoyote anapaswa kuhukumu kwa shariy’ah zake baina ya walio chini yake, na kupatanisha magomvi yao kwa hiyo. Baada ya Allaah kuisifu Qur-aan kuwa ni muhaymin (Rejea Al-Maaidah (5:48) juu), Aliamrisha:
وَأَنِ احْكُم بَيْنَهُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ وَاحْذَرْهُمْ أَن يَفْتِنُوكَ عَن بَعْضِ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ إِلَيْكَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَاعْلَمْ أَنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُصِيبَهُم بِبَعْضِ ذُنُوبِهِمْ ۗ وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ لَفَاسِقُونَ ﴿٤٩﴾
Na wahukumu baina yao kwa yale Aliyoyateremsha Allaah, na wala usifuate hawaa zao, na tahadhari nao wasije kukufitini ukaacha baadhi ya yale Aliyokuteremshia Allaah. Na wakikengeuka, basi jua kuwa hakika Allaah Anataka kuwaadhibu kwa baadhi ya madhambi yao. Na hakika wengi katika watu ni mafasiki. [Al-Maaidah (5:49)]
6-Chunga Moyo Wako, Kwani Ndio Unaotawala Viungo Vingine:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Muhaymin, kwamba usimamizi wa kwanza unaotakiwa kwako ni kuusimamia moyo wako, kwani ukitengenea viungo vyote hutengenea.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((إِنَّ الْحَلاَلَ بَيِّنٌ، وَإِنَّ الْحَرَامَ بَيِّنٌ، وَبَيْنَهُمَا مُشْتَبِهَاتٌ لاَ يَعْلَمُهُنَّ كَثِيرٌ مِنَ النَّاسِ، فَمَنِ اتَّقَى الشُّبُهَاتِ اسْتَبْرَأَ لِدِينِهِ وَعِرْضِهِ، وَمَنْ وَقَعَ فِي الشُّبُهَاتِ وَقَعَ فِي الْحَرَامِ ... أَلاَ وَإِنَّ فِي الْجَسَدِ مُضْغَةً إِذَا صَلَحَتْ صَلَحَ الْجَسَدُ كُلُّهُ، وَإِذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ كُلُّهُ، أَلاَ وَهِيَ الْقَلْبُ))
Amesimulia An-Nu’maan bin Bashiyr (رضي الله عنهما): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Hakika halaal iko wazi, na haraam iko wazi, na baina ya hayo mawili kuna mambo yenye shaka ambayo watu wengi hawayajui. Basi atakayejiepusha na yenye shaka, ameisalimisha Dini yake na heshima yake; na atakayetumbukia katika yenye shaka, atatumbukia katika haraam … Tanabahi! Hakika mwilini kuna pande la nyama; likitengenea, mwili wote hutengenea, na likiharibika, mwili wote huharibika. Tanabahi! Nalo ni moyo.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
7-Ridhika Na Qadhwaa Na Qadar Ya Allaah:
Kwa kuwa Al-Muhaymin Anajua kilicho na maslahi kwako na kinachokuharibia (Rejea Al-Baqarah (2:220) juu), basi ridhika na Alichokuchagulia hata kama nafsi yako haikipendi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾
Mmeandikiwa sharia kupigana vita nako kunachukiza mno kwenu. Lakini asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni la kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah (2:216)]
8-Chunga Uhusiano Wako Na Allaah, Kwani Yeye Ni Mchunguzi Juu Yako:
Tambua, ee Mja wa Al-Muhaymin, kwamba Allaah Ni Mchunguzi juu yako katika kila uhusiano wako na watu; basi mche katika haki zao.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا ﴿١﴾
Enyi watu! Mcheni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Aadam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawwaa) na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana (haki zenu kwa kuunga) undugu. Hakika Allaah daima Ni Mwenye Kuwachungeni. [An-Nisaa (4:1)]
9-Ithamini Qur-aan Kuliko Vitabu Vingine Vyote:
Tambua, ee Mja wa Al-Muhaymin: Kwa kuwa Qur-aan ndiyo muhaymin juu ya vitabu vilivyotangulia, Muislamu hahitaji kutafuta uongofu katika vitabu vilivyobadilishwa; bali Qur-aan na Sunnah zinamtosha. Imaan hii inazaa kuiadhimisha Qur-aan, kuipenda, na kufurahi nayo kwa furaha kubwa kabisa, na kumshukuru Allaah kwa uongofu wake.
10-Mwombe Al-Muhaymin Akusimamie Na Akutengenezee Mambo Yako Yote:
Tambua, ee Mja wa Al-Muhaymin: Unapofikwa na shida, khofu ya maadui, au mambo yako yanapokwenda kombo, mwombe Allaah Akusimamie, Akuhifadhi na Akutengenezee mambo yako. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimfundisha binti yake Faatwimah (رضي الله عنها) du’aa hii:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) لِفَاطِمَةَ (رضي الله عنها): ((مَا يَمْنَعُكِ أَنْ تَسْمَعِي مَا أُوصِيكِ بِهِ؟ أَنْ تَقُولِي إِذَا أَصْبَحْتِ وَإِذَا أَمْسَيْتِ: يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ بِرَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ، أَصْلِحْ لِي شَأْنِي كُلَّهُ، وَلاَ تَكِلْنِي إِلَى نَفْسِي طَرْفَةَ عَيْنٍ))
Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia Faatwimah (رضي الله عنها): “Nini kinakuzuia kusikiliza ninayokuusia? Useme unapoamka asubuhi na unapoingia jioni:
يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ بِرَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ، أَصْلِحْ لِي شَأْنِي كُلَّهُ، وَلاَ تَكِلْنِي إِلَى نَفْسِي طَرْفَةَ عَيْنٍ
Yaa Uliye Hai daima, yaa Msimamizi wa kila kitu, kwa Rehma Yako naomba uokozi; Nitengenezee mambo yangu yote, wala Usiniachie nafsi yangu hata kwa muda wa kupepesa jicho.” [An-Nasaaiy katika As-Sunan Al-Kubraa, Al-Haakim, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh At-Targhiyb (661)]
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Imepokelewa na Imaam Atw-Twabariy katika tafsiyr yake, na isnaad yake ni Hasan kama ilivyo katika At-Tafsiyr Asw-Swahiyh (4/470); imenukuliwa na islamiccreed.net.
- 2Imaam Al-Bayhaqiy (رحمه الله), Al-I’tiqaad; imenukuliwa na islamiccreed.net.
- 3Tafsiyr As-Sa’diy, maelezo ya Majina ya Allaah; imenukuliwa pia na Kalemtayeb.