Al-‘Aziyz: Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika; Mwenye ‘izzah (utukufu na nguvu) zote, Asiyefikiwa wala Asiyedhurika.
Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-‘Aziyz; Mwenye maana zote za utukufu, nguvu na ufalme. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا يَحْزُنكَ قَوْلُهُمْ ۘ إِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا ۚ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴿٦٥﴾
Na wala maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika taadhima zote ni za Allaah Pekee. Yeye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Yuwnus (10:65)]
Na Anasema pia:
فَلِلَّـهِ الْحَمْدُ رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَرَبِّ الْأَرْضِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٣٦﴾ وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٣٧﴾
Basi AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi, Rabb wa walimwengu. Na Ukubwa, Uadhama, Ujalali ni Wake Pekee mbinguni na ardhini. Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Jaathiyah (45:36-37)]
Jina hili limetajwa katika Qur-aan zaidi ya mara tisini (90). Limeambatana na Jina Al-Hakiym zaidi ya mara ishirini, na Jina Ar-Rahiym zaidi ya mara kumi; katika Suwrah Ash-Shu’araa pekee limeambatana na Ar-Rahiym mara tisa, kama katika Kauli Yake:
وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٩﴾
Na hakika Rabb wako bila shaka Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu. [Ash-Shu’araa (26:9)]
Na hilo linaonyesha kwamba ‘izzah Yake imeambatana na hikmah na Rehma; si nguvu ya dhulma wala ya jeuri.
Maana Ya Al-‘Aziyz:
Imaam Al-Qurtwubiy (رحمه الله) amesema katika tafsiyr ya Kauli ya Allaah: “Hakika Wewe Ndiye Al-‘Aziyz, Al-Hakiym” (2:129):
وَالْعَزِيزُ مَعْنَاهُ الْمَنِيعُ الَّذِي لَا يُنَالُ وَلَا يُغَالَبُ
“Na Al-‘Aziyz maana yake ni: Asiyeweza kufikiwa (kwa madhara), Asiyeshindika wala Asiyeshindanwa.” Na akanukuu kutoka kwa Ibn Kaysaan kwamba maana yake ni: Ambaye hakuna kinachomshinda; na kutoka kwa Al-Kisaaiy kwamba ni: Mwenye kushinda.1
Na Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amekusanya maana tatu za ‘izzah ya Allaah katika Qaswiydah yake An-Nuwniyyah, akasema:
وَهُوَ الْعَزِيزُ فَلَنْ يُرَامَ جَنَابُهُ ... أَنَّى يُرَامُ جَنَابُ ذِي السُّلْطَانِ
وَهُوَ الْعَزِيزُ الْقَاهِرُ الْغَلَّابُ لَمْ ... يَغْلِبْهُ شَيْءٌ هَذِهِ صِفَتَانِ
وَهُوَ الْعَزِيزُ بِقُوَّةٍ هِيَ وَصْفُهُ ... فَالْعِزُّ حِينَئِذٍ ثَلَاثُ مَعَانِ
وَهِيَ الَّتِي كَمُلَتْ لَهُ سُبْحَانَهُ ... مِنْ كُلِّ وَجْهٍ عَادِمِ النُّقْصَانِ
“Naye Ni Al-‘Aziyz, Ambaye Utukufu Wake hautafikiwa (kwa madhara); vipi utafikiwa utukufu wa Mwenye mamlaka yote? Naye Ni Al-‘Aziyz, Mwenye kudhibiti, Mwenye kushinda, hakuna kitu kinachomshinda; na hizi ni Sifa mbili. Naye Ni Al-‘Aziyz kwa nguvu ambayo ni Sifa Yake; basi ‘izzah hapo ina maana tatu. Nazo ndizo zilizokamilika Kwake (سبحانه) kwa kila namna, zisizo na upungufu.”2
Kwa hiyo ‘izzah ya Allaah ina maana tatu: ‘izzah ya kutofikiwa na madhara (Hawezi kudhuriwa wala Hamhitaji yeyote), ‘izzah ya kushinda na kudhibiti, na ‘izzah ya nguvu kamili.
1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Al-‘Aziyz Mwenye nguvu na uwezo wote; kwa nguvu Zake yamedhalilika yaliyokuwa magumu, na yamelainika yaliyo mazito.
2-Ni Al-‘Aziyz Asiye na mfano wala wa kulinganishwa Naye katika ukamilifu Wake kwa kila upande.
3-Ni Al-‘Aziyz, Mwenye nguvu katika kulipiza kisasi kwa maadui Zake; Akilipiza kisasi hakuna yeyote wa kumzuia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا نَقَمُوا مِنْهُمْ إِلَّا أَن يُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿٨﴾
Na hawakuwachukia isipokuwa kwa vile wamemwamini Allaah Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Al-Buruwj (85:8)]
4-Ni Al-‘Aziyz Ambaye Humpa ‘izzah na mamlaka Amtakaye, na Humdhalilisha Amtakaye katika Waja Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلِ اللَّـهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَن تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَن تَشَاءُ ۖ بِيَدِكَ الْخَيْرُ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢٦﴾
Sema: Ee Allaah Mfalme Uliyemiliki ufalme wote, Unampa ufalme Umtakaye, na Unamuondoshea ufalme Umtakaye, na Unamtukuza Umtakaye, na Unamdhalilisha Umtakaye, kheri imo Mkononi Mwako. Hakika Wewe Ni Muweza wa kila kitu. [Aal-‘Imraan (3:26)]
5-Ni Al-‘Aziyz Ambaye Rusuli Wake hawadhalilishwi na watu, na Waumini wanapata nguvu na ‘izzah kutoka Kwake, bali makafiri ndio wenye kudhalilika. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَقُولُونَ لَئِن رَّجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الْأَعَزُّ مِنْهَا الْأَذَلَّ ۚ وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَعْلَمُونَ﴿٨﴾
Wanasema: Tutakaporudi Madiynah, mwenye hadhi zaidi lazima atamfukuza humo aliye dhalili. Na ilhali utukufu ni wa Allaah na wa Rasuli Wake na wa Waumini, lakini wanafiki hawajui. [Al-Munaafiquwn (63:8)]
6-Ni Al-‘Aziyz Mwenye shani ya juu, Mwenye utukufu wa Dhati Yake, Mwenye upekee katika ukamilifu Wake na Sifa Zake zote; na miongoni mwa ukamilifu wa ‘izzah Yake ni kutakasika Kwake na kila upungufu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
سُبْحَانَ رَبِّكَ رَبِّ الْعِزَّةِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿١٨٠﴾
Utakasifu ni wa Rabb wako; Rabb wa Enzi ya Nguvu Asiyeshindika kutokana na yale wanayoyavumisha. [Asw-Swaaffaat (37:180)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-‘Aziyz:
1-Anayetaka ‘Izzah, Basi ‘Izzah Yote Iko Kwa Allaah:
Mwombe, ee Mja wa Al-‘Aziyz, Yeye Pekee ‘izzah, kwa kumtii na kufanya amali njema. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَن كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا ۚ إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ ۚ وَالَّذِينَ يَمْكُرُونَ السَّيِّئَاتِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَمَكْرُ أُولَـٰئِكَ هُوَ يَبُورُ ﴿١٠﴾
Yeyote Anayetaka utukufu, basi utukufu wote uko kwa Allaah. Kwake Pekee linapanda Neno zuri na amali njema Huitukuza. Na wale wanaopanga njama za maovu watapata adhabu shadidi. Na njama za hao ni zenye kuangamia. [Faatwir (35:10)]
2-Tafuta Nguvu Na Nusra Kwa Al-‘Aziyz Dhidi Ya Maadui:
Ukitaka nguvu na ushindi dhidi ya maadui na wanaojifanya majabari, basi mwelekee Al-‘Aziyz; kwani Kwake hakuna linalomshinda, Analolitaka linakuwa, na Asilolitaka haliwi. Mnyenyekee na umwombe Yeye unapoishiwa nguvu na mbinu.
3-Upe Uislamu Wako ‘Izzah, Wala Usitafute ‘Izzah Kwa Maadui Wa Allaah:
Tambua kwamba utukufu si kuwa na mali, nguvu wala mamlaka; bali ni kumtii Al-‘Aziyz. Wala usiwe miongoni mwa wale Aliosema kuwahusu Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِينَ يَتَّخِذُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ ۚ أَيَبْتَغُونَ عِندَهُمُ الْعِزَّةَ فَإِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا ﴿١٣٩﴾
Wale wanaofanya makafiri kuwa ni marafiki wandani na walinzi badala ya Waumini. Je, wanatafuta utukufu kutoka kwao? Basi hakika utukufu wote ni wa Allaah Pekee. [An-Nisaa (4:139)]
Na ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) amesema:
إِنَّا كُنَّا أَذَلَّ قَوْمٍ فَأَعَزَّنَا اللَّهُ بِالْإِسْلَامِ، فَمَهْمَا نَطْلُبُ الْعِزَّةَ بِغَيْرِ مَا أَعَزَّنَا اللَّهُ بِهِ أَذَلَّنَا اللَّهُ
“Hakika sisi tulikuwa watu dhalili kabisa, Allaah Akatupa ‘izzah kwa Uislamu; basi kila tutakapotafuta ‘izzah kwa kitu kingine zaidi ya kile Alichotupa nacho Allaah ‘izzah, Allaah Atatudhalilisha.”3
Na ndio maana Uislamu utabaki kushinda dini zote kama Alivyoahidi Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ﴿٣٣﴾
Yeye Ndiye Aliyemtuma Rasuli Wake kwa mwongozo na Dini ya haki ili Aishindishe juu ya dini zote, japo watakirihika washirikina. [At-Tawbah (9:33)]
4-Wape ‘Izzah Ndugu Zako Waumini Wala Usiwachafue Heshima Zao:
Tahadhari na kuwadharau ndugu zako Waislamu au kuchafua heshima zao, kwani heshima ya Muislamu ni tukufu mbele ya Al-‘Aziyz.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... بِحَسْبِ امْرِئٍ مِنَ الشَّرِّ أَنْ يَحْقِرَ أَخَاهُ الْمُسْلِمَ، كُلُّ الْمُسْلِمِ عَلَى الْمُسْلِمِ حَرَامٌ: دَمُهُ وَمَالُهُ وَعِرْضُهُ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “… Inamtosha mtu kuwa na shari kumdharau nduguye Muislamu. Kila Muislamu juu ya Muislamu mwenziwe ni haramu: damu yake, mali yake na heshima yake.” [Muslim]
Na pia:
عَنْ أَبِي الدَّرْدَاءِ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ رَدَّ عَنْ عِرْضِ أَخِيهِ رَدَّ اللَّهُ عَنْ وَجْهِهِ النَّارَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ))
Amesimulia Abuu Ad-Dardaa (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayetetea heshima ya nduguye, Allaah Atauepusha uso wake na moto Siku ya Qiyaamah.” [At-Tirmidhiy (1931) na amesema: Hasan, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
5-Wenye Mamlaka Wakumbuke Kwamba ‘Izzah Yao Haiwezi Kushinda ‘Izzah Ya Al-‘Aziyz:
Wenye mamlaka watafakari kwamba mamlaka na hadhi zao haziwezi kushinda za Al-‘Aziyz; kwa hiyo wasiende kinyume na Amri za Allaah (سبحانه وتعالى), wala wasivuke mipaka kwa kuwadhulumu watu kwa sababu ya mamlaka yao. Rejea Aal-‘Imraan (3:26) juu.
6-Shikamana Na Qur-aan, Kitabu ‘Aziyz:
Kumbuka kwamba ‘izzah ya kweli ya Ummah huu iko katika kushikamana na Kitabu cha Al-‘Aziyz.
Rejea Qur-aan, uisome na uzingatie maana zake ukitaka kufaulu duniani na Aakhirah. Humo Jina Al-‘Aziyz limetajwa mara nyingi, na Qur-aan yenyewe imesifiwa kuwa ni Kitabu ‘aziyz. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالذِّكْرِ لَمَّا جَاءَهُمْ ۖ وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ﴿٤١﴾ لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ﴿٤٢﴾
Hakika wale waliokanusha Ukumbusho ulipowajia (wataangamia). Na hakika Hiki ni Kitabu chenye utukufu na udhibiti. Hakitokifikia baatwil mbele yake wala nyuma yake. Ni Uteremsho kutoka kwa Mwenye Hikmah wa yote, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Fusw-Swilat (41:41-42)]
7-Samehe Na Nyenyekea, Kwani Hizo Ni Njia Za Kupata ‘Izzah:
Tambua, ee Mja wa Al-‘Aziyz, kwamba njia ya kupata ‘izzah ni kusamehe na kunyenyekea, si kulipiza kisasi na kujikweza.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَا نَقَصَتْ صَدَقَةٌ مِنْ مَالٍ، وَمَا زَادَ اللَّهُ عَبْدًا بِعَفْوٍ إِلاَّ عِزًّا، وَمَا تَوَاضَعَ أَحَدٌ لِلَّهِ إِلاَّ رَفَعَهُ اللَّهُ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Swadaqah haipunguzi mali; na Allaah Hamzidishii mja kwa kusamehe isipokuwa ‘izzah (utukufu); na hakuna aliyenyenyekea kwa ajili ya Allaah isipokuwa Allaah Humnyanyua.” [Muslim]
8-Jikinge Kwa ‘Izzah Ya Allaah Na Upotofu:
Muombe, ee Mja wa Al-‘Aziyz, Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Jina hili, nyenyekea Kwake na tawakali Kwake katika kila jambo na kila shida. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiomba:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُولُ: ((اللَّهُمَّ لَكَ أَسْلَمْتُ، وَبِكَ آمَنْتُ، وَعَلَيْكَ تَوَكَّلْتُ، وَإِلَيْكَ أَنَبْتُ، وَبِكَ خَاصَمْتُ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِعِزَّتِكَ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ أَنْ تُضِلَّنِي، أَنْتَ الْحَيُّ الَّذِي لاَ يَمُوتُ، وَالْجِنُّ وَالإِنْسُ يَمُوتُونَ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema:
اللَّهُمَّ لَكَ أَسْلَمْتُ، وَبِكَ آمَنْتُ، وَعَلَيْكَ تَوَكَّلْتُ، وَإِلَيْكَ أَنَبْتُ، وَبِكَ خَاصَمْتُ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِعِزَّتِكَ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ أَنْ تُضِلَّنِي، أَنْتَ الْحَيُّ الَّذِي لاَ يَمُوتُ، وَالْجِنُّ وَالإِنْسُ يَمُوتُونَ
“Yaa Allaah! Kwako nimejisalimisha, na Kwako nimeamini, na Kwako nimetawakali, na Kwako nimerejea kutubia, na kwa (hoja Zako) nimeshindana (na maadui). Yaa Allaah! Hakika mimi najikinga kwa Utukufu wa Enzi Yako, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Usinipoteze. Wewe Ndiye Uliye Hai Usiyekufa, na majini na wanaadam wanakufa.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
9-Jikinge Kwa ‘Izzah Ya Allaah Unapopata Maumivu Mwilini:
Omba du’aa hii unapohisi maumivu yoyote mwilini, ukijikinga kwa ‘Izzah ya Al-‘Aziyz na Uwezo Wake.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimfundisha Swahaba aliyekuwa akiumwa:
عَنْ عُثْمَانَ بْنِ أَبِي الْعَاصِ الثَّقَفِيِّ (رضي الله عنه) أَنَّهُ شَكَا إِلَى رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) وَجَعًا يَجِدُهُ فِي جَسَدِهِ مُنْذُ أَسْلَمَ، فَقَالَ لَهُ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((ضَعْ يَدَكَ عَلَى الَّذِي تَأَلَّمَ مِنْ جَسَدِكَ وَقُلْ: بِاسْمِ اللَّهِ، ثَلاَثًا، وَقُلْ سَبْعَ مَرَّاتٍ: أَعُوذُ بِاللَّهِ وَقُدْرَتِهِ مِنْ شَرِّ مَا أَجِدُ وَأُحَاذِرُ))
Amesimulia ‘Uthmaan bin Abil-‘Aasw Ath-Thaqafiyy (رضي الله عنه) kwamba alimlalamikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) maumivu aliyokuwa akiyahisi mwilini mwake tangu aliposilimu. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia: “Weka mkono wako juu ya sehemu ya mwili wako inayouma, kisha sema mara tatu:
بِاسْمِ اللَّهِ
Kwa Jina la Allaah. Na sema mara saba:
أَعُوذُ بِاللَّهِ وَقُدْرَتِهِ مِنْ شَرِّ مَا أَجِدُ وَأُحَاذِرُ
Najikinga kwa Allaah na kwa Uwezo Wake kutokana na shari ya ninachokihisi na ninachokiogopa.” [Muslim]
Na katika riwaayah nyingine:
أَعُوذُ بِعِزَّةِ اللَّهِ وَقُدْرَتِهِ مِنْ شَرِّ مَا أَجِدُ
“Najikinga kwa ‘Izzah ya Allaah na kwa Uwezo Wake kutokana na shari ya ninachokihisi.” [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha]
10-Mtakase Al-‘Aziyz Mwishoni Mwa Vikao Vyako Na Mwishoni Mwa Swalaah:
Tambua, ee Mja wa Al-‘Aziyz: Suwrah Asw-Swaaffaat inamalizika kwa kumtakasa Rabb Mwenye ‘izzah; basi mtakase na yale yasiyomstahiki, na mswalie Rasuli Wake, na umhimidi. Rejea Asw-Swaaffaat (37:180) juu, na Aayah mbili zinazofuatia:
وَسَلَامٌ عَلَى الْمُرْسَلِينَ ﴿١٨١﴾ وَالْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٨٢﴾
Na Salaamun! (Amani) iwe juu ya Rusuli. Na AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Rabb wa walimwengu. [Asw-Swaaffaat (37:181-182)]
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Tafsiyr Al-Qurtwubiy (Al-Jaami’ Li-Ahkaam Al-Qur-aan), Suwrah Al-Baqarah (2:129).
- 2Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله), Al-Kaafiyah Ash-Shaafiyah (An-Nuwniyyah), fasli ya aina ya pili ya Ath-Thubuwt; Shamela (kitabu 11375, uk. 205).
- 3Al-Haakim, Al-Mustadrak (1/236-237), Kitaab Al-Iymaan; amesema: “Hadiyth hii ni Swahiyh kwa sharti ya Ash-Shaykhayn (Al-Bukhaariy na Muslim).” (Islamweb, maktaba ya Al-Mustadrak).