Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah023 - Al-Jabbaar

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 023 kati ya 103
Al-Jabbaar — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Jabbaar: Mwenye kuunga na kurekebisha kilichovunjika, Mwenye kudhibiti viumbe vyote, Aliye juu Asiyeshindwa kufanya Atakalo.

Jina hili tukufu la Allaah (سبحانه وتعالى) limetajwa katika Qur-aan mara moja (1). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾

Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye Kusadikisha ahadi na Kuaminisha, Mwenye Kudhibiti Kushuhudia Kuchunga na Kuhifadhi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Jabari Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye Ukubwa na Uadhama, Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha. [Al-Hashr (59:23)]

Na neno hili limetajwa katika Qur-aan mara kadhaa kwa kuwahusu wanaadam, kwa maana ya ujabari wa kulaumiwa, yaani kiburi, dhulma na ukaidi; mfano Kauli ya kaumu ya Nabiy Muwsaa (عليه السلام):

قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِنَّ فِيهَا قَوْمًا جَبَّارِينَ وَإِنَّا لَن نَّدْخُلَهَا حَتَّىٰ يَخْرُجُوا مِنْهَا فَإِن يَخْرُجُوا مِنْهَا فَإِنَّا دَاخِلُونَ ﴿٢٢﴾

Wakasema: Ee Muwsaa! Hakika humo kuna watu majabari, nasi hatutoingia humo mpaka watoke humo. Watakapotoka humo, basi hakika sisi tutaingia. [Al-Maaidah (5:22)]

Na Kauli Yake kuhusu kaumu ya ‘Aad:

وَتِلْكَ عَادٌ ۖ جَحَدُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَعَصَوْا رُسُلَهُ وَاتَّبَعُوا أَمْرَ كُلِّ جَبَّارٍ عَنِيدٍ﴿٥٩﴾

Na hao ni kina ‘Aad. Wamezikanusha kwa ushupavu Aayaat (Ishara, Hoja, Dalili) za Rabb wao, na wakawaasi Rusuli Wake, na wakafuata amri ya kila jabari mkaidi. [Huwd (11:59)]

Na Anasema pia kuhusu wao:

وَإِذَا بَطَشْتُم بَطَشْتُمْ جَبَّارِينَ ﴿١٣٠﴾

Na mnapofanya uonevu, mnatumia nguvu kijabari. [Ash-Shu’araa (26:130)]

Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amesema katika tafsiyr yake ya Al-Hashr (59:23):

الْجَبَّارُ: الَّذِي قَهَرَ جَمِيعَ الْعِبَادِ، وَأَذْعَنَ لَهُ سَائِرُ الْخَلْقِ، الَّذِي يَجْبُرُ الْكَسِيرَ، وَيُغْنِي الْفَقِيرَ

“Al-Jabbaar ni Yule Aliyewadhibiti waja wote, na viumbe vyote vimemnyenyekea; Ambaye Huunga kilichovunjika, na Humtajirisha fakiri.”1

Maana Ya Al-Jabbaar:

Jina hili lina maana tatu, na zote zinaingia ndani ya Jina Al-Jabbaar:

1-Al-Jabbaar Mwenye kuunga na kurekebisha (الجَبْر). Huunga unyonge wa wanyonge katika Waja Wake, Huunga kilichovunjika, Humtajirisha fakiri, Humwepesishia mwenye dhiki. Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amesema:

فَهُوَ الَّذِي يَجْبُرُ الضَّعِيفَ وَكُلَّ قَلْبٍ مُنْكَسِرٍ لِأَجْلِهِ، فَيَجْبُرُ الْكَسِيرَ، وَيُغْنِي الْفَقِيرَ، وَيُيَسِّرُ عَلَى الْمُعْسِرِ كُلَّ عَسِيرٍ، وَيَجْبُرُ الْمُصَابَ بِتَوْفِيقِهِ لِلثَّبَاتِ وَالصَّبْرِ، وَيُعَوِّضُهُ عَلَى مُصَابِهِ أَعْظَمَ الْأَجْرِ إِذَا قَامَ بِوَاجِبِهَا، وَيَجْبُرُ جَبْرًا خَاصًّا قُلُوبَ الْخَاضِعِينَ لِعَظَمَتِهِ وَجَلَالِهِ، وَقُلُوبَ الْمُحِبِّينَ بِمَا يُفِيضُ عَلَيْهَا مِنْ أَنْوَاعِ كَرَامَاتِهِ، وَأَصْنَافِ الْمَعَارِفِ وَالْأَحْوَالِ الْإِيمَانِيَّةِ، فَقُلُوبُ الْمُنْكَسِرِينَ لِأَجْلِهِ جَبْرُهَا دَانٍ قَرِيبٌ، وَإِذَا دَعَا الدَّاعِي فَقَالَ: اللَّهُمَّ اجْبُرْنِي، فَإِنَّهُ يُرِيدُ هَذَا الْجَبْرَ الَّذِي حَقِيقَتُهُ إِصْلَاحُ الْعَبْدِ وَدَفْعُ جَمِيعِ الْمَكَارِهِ عَنْهُ

“Yeye Ndiye Anayemuunga dhaifu, na kila moyo uliovunjika kwa ajili Yake. Huunga kilichovunjika, Humtajirisha fakiri, Humwepesishia mwenye dhiki kila zito; Humuunga aliyefikwa na msiba kwa kumwafikisha kuwa imara na kusubiri, na Humlipa badala ya msiba wake ujira mkubwa kabisa ikiwa atatekeleza wajibu wake. Na Huunga kwa namna maalumu nyoyo za wanaonyenyekea Utukufu Wake na Ujalali Wake, na nyoyo za wanaompenda, kwa aina mbalimbali za karama Anazozimiminia, na aina za maarifa na hali za imaan. Basi nyoyo zilizovunjika kwa ajili Yake, kuungwa kwake ni karibu. Na muombaji anaposema: اللَّهُمَّ اجْبُرْنِي (Yaa Allaah, niunge), anakusudia jabr hii ambayo uhakika wake ni kumtengeneza mja na kumwondoshea kila anayoyachukia.”2

Na mfano wa jabr hii ni jinsi Allaah Alivyouunga moyo wa mama wa Nabiy Muwsaa (عليه السلام), na Akamtia huruma mke wa Fir’awn juu yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقَالَتِ امْرَأَتُ فِرْعَوْنَ قُرَّتُ عَيْنٍ لِّي وَلَكَ ۖ لَا تَقْتُلُوهُ عَسَىٰ أَن يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٩﴾ وَأَصْبَحَ فُؤَادُ أُمِّ مُوسَىٰ فَارِغًا ۖ إِن كَادَتْ لَتُبْدِي بِهِ لَوْلَا أَن رَّبَطْنَا عَلَىٰ قَلْبِهَا لِتَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٠﴾

Na mke wa Firawni akasema: Kiburudisho cha macho kwangu na kwako. Usimuue, asaa akatufaa au tumfanye mwana. Nao hawatambui. Na ukawa moyo wenye wahka wa mama yake Muwsaa mtupu! Alikaribia kumdhihirisha (kuwa ni mwanawe) lau kama Tusingeutia nguvu moyo wake ili awe miongoni mwa Waumini. [Al-Qaswasw (28:9-10)]

2-Al-Jabbaar Mwenye kudhibiti na kushinda (القَهْر). Anapotaka kitu, huwa kama Anavyotaka, wala hakuna yeyote wa kumzuia; kila kitu kiko chini ya Mamlaka Yake, na viumbe vya juu na vya chini vimemnyenyekea. Waja hawawezi kumdhuru wala kumnufaisha.

3-Al-Jabbaar Aliye juu (العُلُوّ). Yeye Ndiye Mkubwa Aliye juu ya kila kitu; hakuna anayemfikia wala anayeweza kumpinga.

Na katika ujabari Wake Siku ya Qiyaamah ni kwamba moto hautajaa mpaka Allaah Aweke Mguu Wake ndani yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِن مَّزِيدٍ﴿٣٠﴾

Siku Tutakapoiambia Jahannam: Je, umeshajaa? Nayo itasema: Je, kuna ziada yoyote? [Qaaf (50:30)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((تَحَاجَّتِ الْجَنَّةُ وَالنَّارُ، فَقَالَتِ النَّارُ: أُوثِرْتُ بِالْمُتَكَبِّرِينَ وَالْمُتَجَبِّرِينَ، وَقَالَتِ الْجَنَّةُ: مَا لِي لاَ يَدْخُلُنِي إِلاَّ ضُعَفَاءُ النَّاسِ وَسَقَطُهُمْ؟ قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى لِلْجَنَّةِ: أَنْتِ رَحْمَتِي أَرْحَمُ بِكِ مَنْ أَشَاءُ مِنْ عِبَادِي، وَقَالَ لِلنَّارِ: إِنَّمَا أَنْتِ عَذَابِي أُعَذِّبُ بِكِ مَنْ أَشَاءُ مِنْ عِبَادِي، وَلِكُلِّ وَاحِدَةٍ مِنْهُمَا مِلْؤُهَا، فَأَمَّا النَّارُ فَلاَ تَمْتَلِئُ حَتَّى يَضَعَ رِجْلَهُ فَتَقُولُ: قَطْ قَطْ قَطْ، فَهُنَالِكَ تَمْتَلِئُ وَيُزْوَى بَعْضُهَا إِلَى بَعْضٍ، وَلاَ يَظْلِمُ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ مِنْ خَلْقِهِ أَحَدًا ...))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Jannah na moto vilibishana. Moto ukasema: Nimechaguliwa kwa (kupokea) wenye kiburi na majabari. Na Jannah ikasema: Mbona hawaniingii isipokuwa wanyonge wa watu na wasiojulikana? Allaah (تبارك وتعالى) Akaiambia Jannah: Wewe ni Rehma Yangu, Namrehemu kwako Nimtakaye katika Waja Wangu. Na Akauambia moto: Hakika wewe ni Adhabu Yangu, Namwadhibu kwako Nimtakaye katika Waja Wangu. Na kila kimoja kitajazwa. Ama moto hautajaa mpaka (Allaah) Aweke Mguu Wake, ndipo useme: Tosha! Tosha! Tosha! Hapo ndipo utakapojaa, na sehemu zake zikusanywe pamoja; na Allaah (عزّ وجلّ) Hamdhulumu yeyote katika viumbe Vyake …” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah wanathibitisha Sifa hii ya Allaah kama ilivyokuja katika Hadiyth Swahiyh, bila kuikanusha, wala kuipotosha maana yake, wala kuifananisha na viumbe, wala kuuliza namna yake; kwani Yeye (سبحانه وتعالى) Hafanani na chochote.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Jabbaar:

1-Usijifanye Jabari Kwa Wenzako:

Kumbuka kwamba wewe ni Mja wa Al-Jabbaar, Ambaye Anatosha kuuvunja ujabari wako. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّـهِ بِغَيْرِ سُلْطَانٍ أَتَاهُمْ ۖ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ وَعِندَ الَّذِينَ آمَنُوا ۚ كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ قَلْبِ مُتَكَبِّرٍ جَبَّارٍ﴿٣٥﴾

Wale wanaobishana kuhusu Aayaat (Ishara, Hoja) za Allaah (ili wazibatilishe) bila ya dalili yoyote kuwafikia, ni chukizo kubwa mno mbele ya Allaah na mbele ya wale walioamini. Hivyo ndivyo Allaah Anavyopiga chapa juu ya kila moyo wa mwenye kutakabari, jabari. [Ghaafir (40:35)]

2-Kumbuka Hatima Ya Kila Jabari Mkaidi:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Jabbaar, kwamba kila jabari mkaidi hatima yake ni hasara, hata kama ataonekana kushinda kwa muda.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَاسْتَفْتَحُوا وَخَابَ كُلُّ جَبَّارٍ عَنِيدٍ﴿١٥﴾

Na wakaomba ushindi (kwa Allaah), na akapita patupu kila (aliyejifanya) jabari, mkaidi. [Ibraahiym (14:15)]

3-Tafakari Jinsi Al-Jabbaar Anavyoendesha Mwili Wako:

Tafakari jinsi Al-Jabbaar Anavyoyaendesha mambo ya mwili wako bila hiari yako: moyo kupiga, damu kutembea, chakula kusagika, ubongo kufanya kazi, usingizi wako na kuamka kwako. Yote hayo yako chini ya Amri Yake; basi nyenyekea Kwake kwa hiari yako katika yale Aliyokupa uwezo wa kuchagua.

4-Nyenyekea, Kwani Jannah Ni Ya Wanyonge Wanaonyenyekea:

Tambua, ee Mja wa Al-Jabbaar: Hadiyth iliyotangulia inaonyesha kwamba moto ni makazi ya wenye kiburi na majabari, na Jannah ni makazi ya wanyonge wanaonyenyekea. Basi chagua nafsi yako iwe katika wapi.

5-Unga Nyoyo Za Ndugu Zako, Na Al-Jabbaar Atakuunga:

Wasamehe makosa yao, na uwasaidie wenye kuhitaji msaada wako kwa uwezo Aliokupa Allaah, ili Al-Jabbaar Akuunge nawe utakapofikwa na shida. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنْ نَفَّسَ عَنْ مُؤْمِنٍ كُرْبَةً مِنْ كُرَبِ الدُّنْيَا نَفَّسَ اللَّهُ عَنْهُ كُرْبَةً مِنْ كُرَبِ يَوْمِ الْقِيَامَةِ، وَمَنْ يَسَّرَ عَلَى مُعْسِرٍ يَسَّرَ اللَّهُ عَلَيْهِ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ ... وَاللَّهُ فِي عَوْنِ الْعَبْدِ مَا كَانَ الْعَبْدُ فِي عَوْنِ أَخِيهِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayemwondoshea Muumini dhiki miongoni mwa dhiki za dunia, Allaah Atamwondoshea dhiki miongoni mwa dhiki za Siku ya Qiyaamah. Na atakayemfanyia wepesi mwenye uzito, Allaah Atamfanyia wepesi duniani na Aakhirah … Na Allaah Yu katika msaada wa mja maadamu mja yuko katika kumsaidia nduguye.” [Muslim]

6-Mwelekee Al-Jabbaar Moyo Wako Ukiwa Umevunjika:

Al-Jabbaar Ndiye Mwenye kuwanyanyua wanyonge na kuunga nyoyo zilizovunjika kwa ajili Yake; basi usikate tamaa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَنُرِيدُ أَن نَّمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الْأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ ﴿٥﴾

Na Tukataka Tuwafanyie fadhila wale waliokandamizwa katika ardhi, na Tuwafanye viongozi na Tuwafanye wenye kurithi. [Al-Qaswasw (28:5)]

7-Ridhika Na Qadar Ya Al-Jabbaar:

Anayojaalia Al-Jabbaar hakuna wa kuyazuia; basi ridhika na tawakali Kwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا ۚ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ﴿٥١﴾

Sema: Halitusibu (lolote) isipokuwa lile Alilotukidhia Allaah. Yeye Ni Mawlaa wetu. Basi kwa Allaah watawakali Waumini. [At-Tawbah (9:51)]

8-Iga Upole Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Ambaye Hakuwa Jabari:

Tambua, ee Mja wa Al-Jabbaar: Allaah Amemkanushia Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) ujabari juu ya watu; basi walinganie watu kwa upole bila ya kuwalazimisha kwa jeuri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ ۖ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِجَبَّارٍ ۖ فَذَكِّرْ بِالْقُرْآنِ مَن يَخَافُ وَعِيدِ﴿٤٥﴾

Sisi Tunajua zaidi yale wanayoyasema, na wala wewe si mwenye kuwalazimisha kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur-aan anayekhofu Onyo Langu. [Qaaf (50:45)]

9-Mtakase Al-Jabbaar Katika Rukuu Na Sujuud Yako:

Mtakase Al-Jabbaar katika Rukuu na Sujuud yako kwa maneno ya kumtukuza Ujabari Wake na Ufalme Wake.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema katika Rukuu yake katika Swalaah ya usiku:

عَنْ عَوْفِ بْنِ مَالِكٍ الأَشْجَعِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قُمْتُ مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) لَيْلَةً ... ثُمَّ رَكَعَ بِقَدْرِ قِيَامِهِ يَقُولُ فِي رُكُوعِهِ: ((سُبْحَانَ ذِي الْجَبَرُوتِ وَالْمَلَكُوتِ وَالْكِبْرِيَاءِ وَالْعَظَمَةِ)) ثُمَّ سَجَدَ بِقَدْرِ قِيَامِهِ، ثُمَّ قَالَ فِي سُجُودِهِ مِثْلَ ذَلِكَ

Amesimulia ‘Awf bin Maalik Al-Ashja’iyy (رضي الله عنه): Nilisimama (kuswali) pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) usiku mmoja … kisha akarukuu kwa urefu wa kisimamo chake, akisema katika Rukuu yake:

سُبْحَانَ ذِي الْجَبَرُوتِ وَالْمَلَكُوتِ وَالْكِبْرِيَاءِ وَالْعَظَمَةِ

Utakasifu ni wa Mwenye Ujabari, Ufalme, Ukubwa na Uadhama. Kisha akasujudu kwa urefu wa kisimamo chake, na akasema katika Sujuud yake mfano wa hayo. [Abuu Daawuwd, An-Nasaaiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh An-Nasaaiy (1048)]

10-Mwombe Al-Jabbaar Akuunge Katika Kila Swalaah:

Omba du’aa hii baina ya Sijda mbili katika kila Swalaah, ukimwomba Al-Jabbaar Akuunge na Akurekebishie hali zako.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema baina ya Sijda mbili:

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُولُ بَيْنَ السَّجْدَتَيْنِ: ((اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي، وَارْحَمْنِي، وَاجْبُرْنِي، وَاهْدِنِي، وَارْزُقْنِي))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema baina ya Sijda mbili:

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي، وَارْحَمْنِي، وَاجْبُرْنِي، وَاهْدِنِي، وَارْزُقْنِي

Yaa Allaah! Nighufurie, na Unirehemu, na Uniunge (Unirekebishie hali zangu), na Uniongoze, na Uniruzuku. [At-Tirmidhiy (284), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Tafsiyr As-Sa’diy, Suwrah Al-Hashr (59:23).
  • 2Imaam As-Sa’diy (رحمه الله), Tafsiyr Asmaa Allaah Al-Husnaa, Jina Al-Jabbaar; Al-Maktabah Ash-Shaamilah (kitabu 33725).