Al-Mutakabbir: Mwenye Ukubwa na Utukufu wote, Aliyetakasika na kila aibu, dhulma na upungufu.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾
Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye Kusadikisha ahadi na Kuaminisha, Mwenye Kudhibiti Kushuhudia Kuchunga na Kuhifadhi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Jabari Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye Ukubwa na Uadhama, Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha. [Al-Hashr (59:23)]
Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amesema katika tafsiyr yake ya Aayah hii:
الْمُتَكَبِّرُ: الَّذِي لَهُ الْكِبْرِيَاءُ وَالْعَظَمَةُ، الْمُتَنَزِّهُ عَنْ جَمِيعِ الْعُيُوبِ وَالظُّلْمِ وَالْجَوْرِ
“Al-Mutakabbir ni Yule Ambaye Ana Ukubwa na Utukufu, Aliyetakasika na kila aibu, dhulma na uonevu.”1
Neno al-kibriyaa katika lugha lina maana ya ukubwa, utukufu, hadhi na mamlaka. Limekuja katika Qur-aan katika maneno ya kaumu ya Fir’awn kwa Nabiy Muwsaa na Haaruwn (عليهما السلام):
قَالُوا أَجِئْتَنَا لِتَلْفِتَنَا عَمَّا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا وَتَكُونَ لَكُمَا الْكِبْرِيَاءُ فِي الْأَرْضِ وَمَا نَحْنُ لَكُمَا بِمُؤْمِنِينَ﴿٧٨﴾
Wakasema: Je, umetujia ili utugeuze tuyaache yale tuliyowakuta nayo baba zetu, na ili muwe nyinyi wawili na ukubwa na uadhama katika nchi? Na sisi hatutawaamini nyinyi. [Yuwnus (10:78)]
Na Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mwenye Ukubwa wote wa kweli. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْكَبِيرُ الْمُتَعَالِ ﴿٩﴾
Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, Mkubwa kabisa Mwenye Uluwa. [Ar-Ra’d (13:9)]
Na Anasema pia:
وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٣٧﴾
Na Ukubwa, Uadhama, Ujalali ni Wake Pekee mbinguni na ardhini. Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Jaathiyah (45:37)]
Maana Ya Al-Mutakabbir:
1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mkubwa, Aliyetukuka katika Dhati Yake, Sifa Zake, matendo Yake na Ufalme Wake; na kila kitu kilicho chini Yake ni kidogo na dhalili mbele Yake. Ufalme Wake haumaliziki, na Yeye Ndiye Mwenye kudumu milele.
2-Yeye Ni Al-Mutakabbir Aliyetakasika na dhulma dhidi ya Waja Wake; Hamdhulumu yeyote katika Waja Wake, hata kama ni kafiri. Na Ametakasika na kila upungufu na kila aibu, na kila lisilolingana na Utukufu Wake; hakitoki Kwake isipokuwa kheri.
3-Yeye Ndiye Mwenye kuwashinda wanaojifanya majabari katika Waja Wake, na Ameahidi kuwaadhibu kwa kiburi chao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيَوْمَ يُعْرَضُ الَّذِينَ كَفَرُوا عَلَى النَّارِ أَذْهَبْتُمْ طَيِّبَاتِكُمْ فِي حَيَاتِكُمُ الدُّنْيَا وَاسْتَمْتَعْتُم بِهَا فَالْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَسْتَكْبِرُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَبِمَا كُنتُمْ تَفْسُقُونَ﴿٢٠﴾
Na siku watakaposimamishwa hadharani wale waliokufuru kwenye moto (waambiwe): Je, mshamaliza vizuri vyenu katika uhai wenu wa dunia na mshajistarehesha navyo? Basi leo mtalipwa adhabu ya udhalilifu kwa vile mlivyokuwa mkitakabari katika ardhi bila ya haki, na kwa ufasiki mliokuwa mnaufanya. [Al-Ahqaaf (46:20)]
Na Anasema pia:
وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَى اللَّـهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ﴿٦٠﴾
Na Siku ya Qiyaamah utawaona wale waliomsingizia uongo Allaah, nyuso zao zimesawajika. Je, kwani si katika Jahannam ndio makazi kwa ajili ya wanaotakabari? [Az-Zumar (39:60)]
4-Ukubwa na Utukufu wa Allaah hauna mwisho, wala viumbe hawawezi kuudiriki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا ﴿١١٠﴾
Anajua yale yaliyoko mbele yao, na yale yaliyoko nyuma yao, na wala hawawezi kufikia kuelewa chochote cha Ujuzi Wake. [Twaahaa (20:110)]
5-Yeye Ni Al-Mutakabbir katika Rubuwbiyyah Yake, Hana mshirika katika Ufalme Wake; na katika Uluwhiyyah Yake, Hakubali Aabudiwe pamoja Naye asiyekuwa Yeye. Na Amewalaumu wanaotakabari kutamka Kalimah ya Tawhiyd:
فَإِنَّهُمْ يَوْمَئِذٍ فِي الْعَذَابِ مُشْتَرِكُونَ ﴿٣٣﴾ إِنَّا كَذَٰلِكَ نَفْعَلُ بِالْمُجْرِمِينَ ﴿٣٤﴾ إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ ﴿٣٥﴾
Basi hakika wao Siku hiyo, watashirikiana katika adhabu. Hivyo ndivyo Tuwafanyavyo wahalifu. Wao walipokuwa wakiambiwa: Laa ilaaha illa Allaah (hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah), wakitakabari. [Asw-Swaaffaat (37:33-35)]
Na katika Hadiyth Al-Qudsiy, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَنَا أَغْنَى الشُّرَكَاءِ عَنِ الشِّرْكِ، مَنْ عَمِلَ عَمَلاً أَشْرَكَ فِيهِ مَعِي غَيْرِي تَرَكْتُهُ وَشِرْكَهُ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (تبارك وتعالى) Amesema: Mimi Ni Mkwasi zaidi kuliko washirika wote kutokana na kushirikishwa. Atakayefanya amali akanishirikisha ndani yake na mwingine asiyekuwa Mimi, Nitamwacha yeye na shirki yake.” [Muslim]
6-Yeye Ndiye Anayestahiki Ukubwa wote na Utukufu wote. Kiburi kwa kiumbe ni sifa mbaya, lakini kwa Allaah ni Sifa ya ukamilifu, kwa sababu ni Yeye Pekee Ambaye ni Mkubwa kwa kweli. Katika Hadiyth Al-Qudsiy:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ وَأَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنهما) قَالاَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الْعِزُّ إِزَارُهُ، وَالْكِبْرِيَاءُ رِدَاؤُهُ، فَمَنْ يُنَازِعُنِي عَذَّبْتُهُ))
Wamesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy na Abuu Hurayrah (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “(Allaah Amesema:) ‘Izzah ni Izari Yake, na Kibriyaa ni Ridaa Yake; basi atakayeshindana Nami katika hayo, Nitamwadhibu.” [Muslim]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Mutakabbir:
1-Mtukuze Allaah Kwa Takbiyr, Na Muadhimishe Kwa Kila Adhama:
Kumbuka kwamba Yeye Ndiye Al-Mutakabbir, Mwenye Ukubwa na Uadhama. Katika Swalaah ya usiku, Swahaba mmoja alifungua Swalaah kwa kumtukuza Allaah kwa maneno ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliyapendezewa:
عَنِ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَالَ: بَيْنَمَا نَحْنُ نُصَلِّي مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) إِذْ قَالَ رَجُلٌ مِنَ الْقَوْمِ: اللَّهُ أَكْبَرُ كَبِيرًا، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ كَثِيرًا، وَسُبْحَانَ اللَّهِ بُكْرَةً وَأَصِيلاً. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنِ الْقَائِلُ كَلِمَةَ كَذَا وَكَذَا؟)) قَالَ رَجُلٌ مِنَ الْقَوْمِ: أَنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ. قَالَ: ((عَجِبْتُ لَهَا، فُتِحَتْ لَهَا أَبْوَابُ السَّمَاءِ))
Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما): Tulipokuwa tukiswali pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), mtu mmoja katika watu alisema:
اللَّهُ أَكْبَرُ كَبِيرًا، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ كَثِيرًا، وَسُبْحَانَ اللَّهِ بُكْرَةً وَأَصِيلاً
Allaah Ni Mkubwa zaidi kwa ukubwa kamili, na Himdi Anastahiki Allaah kwa wingi, na Utakasifu ni wa Allaah asubuhi na jioni. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Nani aliyesema maneno kadhaa na kadhaa?” Mtu mmoja katika watu akasema: Ni mimi, Yaa Rasula-Allaah. Akasema: “Nimeyastaajabia; milango ya mbingu ilifunguliwa kwa ajili yake.” [Muslim]
2-Tahadhari Na Kiburi, Maasi Ya Kwanza Yaliyotendwa Na Ibliys:
Tambua, ee Mja wa Al-Mutakabbir: Ibliys alikataa kutii Amri ya Allaah kwa sababu ya kiburi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ ﴿٣٤﴾
Na pale Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys alikataa na akatakabari, akawa miongoni mwa makafiri. [Al-Baqarah (2:34)]
Kwa hiyo tahadhari, ee Muislamu, usipinge Amri za Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) ukawa miongoni mwa wanaotakabari.
3-Kiburi Kinazuia Uongofu Na Husababisha Moyo Kupigwa Chapa:
Tahadhari, ee Mja wa Al-Mutakabbir, na kiburi, kwani kinaweza kukuzuia kuikubali haki hata ikiwa wazi mbele yako.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّـهِ بِغَيْرِ سُلْطَانٍ أَتَاهُمْ ۖ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ وَعِندَ الَّذِينَ آمَنُوا ۚ كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ قَلْبِ مُتَكَبِّرٍ جَبَّارٍ﴿٣٥﴾
Wale wanaobishana kuhusu Aayaat (Ishara, Hoja) za Allaah (ili wazibatilishe) bila ya dalili yoyote kuwafikia, ni chukizo kubwa mno mbele ya Allaah na mbele ya wale walioamini. Hivyo ndivyo Allaah Anavyopiga chapa juu ya kila moyo wa mwenye kutakabari, jabari. [Ghaafir (40:35)]
Na Anasema pia:
سَأَصْرِفُ عَنْ آيَاتِيَ الَّذِينَ يَتَكَبَّرُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَإِن يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا بِهَا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الرُّشْدِ لَا يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ ﴿١٤٦﴾
Nitawaepusha na Aayaat (na Ishara, Dalili, Hukmu, Hoja) Zangu wale waliotakabari katika ardhi bila ya haki. Na wanapoona kila Aayah (Ishara, Dalili) hawaiamini. Na wanapoona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndio njia. Na wanapoona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndio njia. Hivyo ni kwa kuwa wao walikadhibisha Aayaat Zetu na walikuwa wenye kughafilika nazo. [Al-A’raaf (7:146)]
4-Jiepushe Na Kiburi Hata Kiwe Kidogo Vipi, Kwani Kinazuia Kuingia Jannah:
Tambua, ee Mja wa Al-Mutakabbir: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amebainisha maana ya kiburi:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لاَ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مَنْ كَانَ فِي قَلْبِهِ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ مِنْ كِبْرٍ)). قَالَ رَجُلٌ: إِنَّ الرَّجُلَ يُحِبُّ أَنْ يَكُونَ ثَوْبُهُ حَسَنًا وَنَعْلُهُ حَسَنَةً. قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ جَمِيلٌ يُحِبُّ الْجَمَالَ، الْكِبْرُ بَطَرُ الْحَقِّ وَغَمْطُ النَّاسِ))
Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hataingia Jannah ambaye moyoni mwake mna kiburi uzito wa chembe.” Mtu mmoja akasema: Hakika mtu hupenda nguo yake iwe nzuri na viatu vyake viwe vizuri. Akasema: “Hakika Allaah Ni Mzuri, Anapenda uzuri. Kiburi ni kuikataa haki na kuwadharau watu.” [Muslim]
5-Ukitaka Kunyanyuliwa, Basi Nyenyekea:
Kumbuka kwamba anayenyenyekea kwa ajili ya Al-Mutakabbir hunyanyuliwa, na anayejikweza hushushwa.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَا نَقَصَتْ صَدَقَةٌ مِنْ مَالٍ، وَمَا زَادَ اللَّهُ عَبْدًا بِعَفْوٍ إِلاَّ عِزًّا، وَمَا تَوَاضَعَ أَحَدٌ لِلَّهِ إِلاَّ رَفَعَهُ اللَّهُ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Swadaqah haipunguzi mali; na Allaah Hamzidishii mja kwa kusamehe isipokuwa ‘izzah; na hakuna aliyenyenyekea kwa ajili ya Allaah isipokuwa Allaah Humnyanyua.” [Muslim]
6-Usiwadharau Wenzako:
Tambua, ee Mja wa Al-Mutakabbir: Usiwadharau wenzako kwa namna yoyote ile, kwani huenda wakawa bora mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuliko wewe, hata kama una mali nyingi zaidi, sura nzuri zaidi, au cheo kikubwa zaidi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَىٰ أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَىٰ أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ ۖ وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ ۖ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴿١١﴾
Enyi walioamini! Wanaume wasiwafanyie dhihaka na kuwadharau wanaume wengineo asaa wakawa bora kuliko wao, wala wanawake kwa wanawake wengineo, asaa wakawa bora kuliko wao. Na wala msifedheheshane na kutukanana, na wala msiitane majina ya kejeli. Ubaya ulioje kuita jina la ufasiki baada ya imaan! Na yeyote asiyetubu, basi hao ndio madhalimu. [Al-Hujuraat (49:11)]
7-Usitembee Ardhini Kwa Majivuno:
Tambua, ee Mja wa Al-Mutakabbir: Kiburi kinadhihirika pia katika mwendo na tabia. Luqmaan alimuusia mwanawe:
وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿١٨﴾
Na wala usiwageuzie watu uso wako kwa kiburi, na wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika Allaah Hampendi kila mwenye kujivuna mwenye kujifakharisha. [Luqmaan (31:18)]
8-Tambua Kwamba Kiburi Ni Haki Ya Allaah Pekee:
Tambua kwamba kiumbe kinachojivuna kinashindana na Al-Mutakabbir katika Sifa isiyomstahiki isipokuwa Yeye; rejea Hadiyth Al-Qudsiy iliyotangulia: “Kibriyaa ni Ridaa Yake.” Basi mja atambue udhaifu wake na umasikini wake mbele ya Rabb wake.
9-Muombe Al-Mutakabbir Akulinde Na Kila Mwenye Kutakabari:
Tambua, ee Mja wa Al-Mutakabbir: Nabiy Muwsaa (عليه السلام) alijikinga kwa Rabb wake kutokana na kila mwenye kiburi:
وَقَالَ مُوسَىٰ إِنِّي عُذْتُ بِرَبِّي وَرَبِّكُم مِّن كُلِّ مُتَكَبِّرٍ لَّا يُؤْمِنُ بِيَوْمِ الْحِسَابِ﴿٢٧﴾
Na Muwsaa akasema: Hakika mimi najikinga kwa Rabb wangu na Rabb wenu, kutokana na kila mwenye kutakabari asiyeamini Siku ya Hesabu. [Ghaafir (40:27)]
10-Kumbuka Hatima Ya Wenye Kiburi Siku Ya Qiyaamah:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Mutakabbir, hatima ya wenye kiburi Siku ya Qiyaamah, na ujiepushe na njia yao.
Rejea Az-Zumar (39:60) na Al-Ahqaaf (46:20) juu; wenye kiburi watalipwa adhabu ya udhalilifu, na makazi yao ni Jahannam. Basi jiepushe na njia yao, na mnyenyekee Al-Mutakabbir.
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Tafsiyr As-Sa’diy, Suwrah Al-Hashr (59:23).