Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah025 - Al-Khaaliq

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 025 kati ya 103
Al-Khaaliq — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Khaaliq: Muumbaji

Jina hili tukufu, Al-Khaaliq, limetajwa katika Qur-aan kwa alif na laam mara moja tu: Al-Hashr (59:24); na limekuja pia katika Kauli Yake kwamba Yeye Ni “Muumbaji wa kila kitu” mara nne: Al-An’aam (6:102), Ar-Ra’d (13:16), Az-Zumar (39:62) na Ghaafir (40:62).

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٢٤﴾

Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji, Mwanzishi wa viumbe bila kasoro, Muundaji sura na umbile, Ana Majina Mazuri kabisa. Kinamsabihi Pekee kila kilichoko katika mbingu na ardhi, Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Hashr (59:24)]

Al-Khaaliq maana yake ni kukipata kitu kisichokuwa na mfano wake hapo kabla. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ ثُمَّ جَعَلَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَأَنزَلَ لَكُم مِّنَ الْأَنْعَامِ ثَمَانِيَةَ أَزْوَاجٍ ۚ يَخْلُقُكُمْ فِي بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ خَلْقًا مِّن بَعْدِ خَلْقٍ فِي ظُلُمَاتٍ ثَلَاثٍ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ ﴿٦﴾

Amekuumbeni kutokana na nafsi moja, kisha Akamfanya kutokana nayo mkewe, na Akakuteremshieni katika wanyama wa mifugo jozi nane. Anakuumbeni matumboni mwa mama zenu umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyo Ndiye Allaah Rabb wenu Mwenye Ufalme, hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi vipi mnageuzwa? [Az-Zumar (39:6)]

Yaani: Amekuumbeni tone, kisha kipande cha nyama, kisha mfupa, kama Anavyosema pia:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾

Kwa yakini Tumemuumba binaadam kutokana na mchujo safi wa udongo. [Al-Muuminuwn (23:12)]

ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ ﴿١٣﴾

Kisha Tukamfanya kuwa tone la manii katika kalio makini. [Al-Muuminuwn (23:13)]

ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ ۚ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ ﴿١٤﴾

Kisha Tukaumba tone la manii kuwa pande la damu linaloning’inia, Tukaumba pande la damu hilo linaloning’inia kuwa kinofu cha nyama, Tukaumba kinofu hicho cha nyama kuwa mifupa, Tukavisha mifupa hiyo nyama, kisha Tukamuanzisha kiumbe kingine. Basi Amebarikika Allaah Mbora wa wenye kuumba. [Al-Muuminuwn (23:14)]

Na maana ya pili ni kukikadiria kitu na kukinyoosha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَوْثَانًا وَتَخْلُقُونَ إِفْكًا ۚ إِنَّ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَا يَمْلِكُونَ لَكُمْ رِزْقًا فَابْتَغُوا عِندَ اللَّـهِ الرِّزْقَ وَاعْبُدُوهُ وَاشْكُرُوا لَهُ ۖ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿١٧﴾

Hakika mnaabudu badala ya Allaah masanamu, na mnaunda uzushi. Hakika wale mnaowaabudu badala ya Allaah hawakumilikieni rizki, basi tafuteni rizki kwa Allaah, na mwabuduni Yeye na mshukuruni, Kwake mtarejeshwa. [Al-‘Ankabuwt (29:17)]

Yaani mnakadiria na kutayarisha, nayo ni uongo, kama ilivyo Kauli Yake Ta’aalaa:

مَا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي الْمِلَّةِ الْآخِرَةِ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا اخْتِلَاقٌ ﴿٧﴾

Hatukusikia haya katika mila ya mwisho, haya si chochote isipokuwa ni jambo lililozushwa tu. [Swaad (38:7)]

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amesema:

ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ﴿٦٢﴾

Huyo Ndiye Allaah Rabb wenu, Muumba wa kila kitu, hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi vipi mnaghilibiwa? [Ghaafir (40:62)]

Al-Khaaliq Anathibitisha Mwenyewe (عزّ وجلّ) Tawhiyd ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola), kwamba Yeye Ndiye Muumbaji, basi je, wale Atheists (Wanaokanusha kuweko kwa Allaah, Al-Khaaliq) wanalo la kujibu Allaah (سبحانه وتعالى) Anaposema?

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ ﴿٣٥﴾

Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji? [Atw-Twuwr (52:35)]

أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ ﴿٣٦﴾

Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini. [Atw-Twuwr (52:36)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Khaaliq:

1-Tafakari Uumbaji Wa Al-Khaaliq Usio Na Kasoro:

Tafakari, ee Mja wa Al-Khaaliq, Uumbaji wa Allaah na jinsi uumbaji Wake ulivyokuwa hauna kasoro. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا ۖ مَّا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَـٰنِ مِن تَفَاوُتٍ ۖ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ﴿٣﴾

Ambaye Ameumba mbingu saba matabaka. Hutaona katika Uumbaji wa Ar-Rahmaan tofauti yoyote. Basi rejesha jicho. Je, unaona mpasuko wowote ule? [Al-Mulk (67:3)]

ثُمَّ ارْجِعِ الْبَصَرَ كَرَّتَيْنِ يَنقَلِبْ إِلَيْكَ الْبَصَرُ خَاسِئًا وَهُوَ حَسِيرٌ﴿٤﴾

Kisha rejesha jicho tena na tena, litakupindukia jicho likiwa limehizika, nalo limenyong’onyea. [Al-Mulk (67:4)]

2-Hakuna Muumbaji Isipokuwa Allaah:

Tambua, ee Mja wa Al-Khaaliq: Hakuna muumbaji mwingine anayeruzuku kutoka mbinguni na ardhini; basi Yeye Pekee Ndiye Anayestahiki kuabudiwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ ﴿٣﴾

Enyi watu! Kumbukeni Neema za Allaah kwenu. Je, kuna muumbaji yeyote badala ya Allaah Anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi vipi mnaghilibiwa? [Faatwir (35:3)]

3-Tumia Akili Yako: Hukuumbwa Bila Muumba, Wala Hukujiumba Mwenyewe:

Hoja hii ya Qur-aan inavunja kila shaka juu ya kuwepo kwa Al-Khaaliq. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ ﴿٣٥﴾ أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ ﴿٣٦﴾

Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji? Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini. [Atw-Twuwr (52:35-36)]

4-Kuwa Miongoni Mwa Wenye Kushukuru Na Kuzingatia:

Tambua, ee Mja wa Al-Khaaliq: Kuwa miongoni mwa wenye kumshukuru na kumwabudu Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kutafakari Uumbaji Wake. Hii ni aina ya ‘ibaadah iliyo nzito kwa thawabu mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) na ambayo ni dalili ya kuamini Tawhiyd ya Rubuwbiyyah, na kwamba Allaah (عزّ وجلّ) Hakuumba Alivyoviumba kuwa ni bure bila ya lengo! Ametaja Allaah (سبحانه وتعالى) hayo katika Suwrah na Aayah kadhaa, miongoni mwazo ni Aayah za mwisho katika Suwrah Aal-‘Imraan ambazo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliamka usiku mmoja akaswali tahajjud kisha akalia mpaka ndevu zake zikarowa, kisha akasujudu na kulia mpaka akaifanya ardhi irowe, kisha akalala kwa upande wa kulia mpaka akaja Bilaal, akamuuliza: “Yaa Rasula-Allaah! Jambo gani linakuliza na hali Allaah (سبحانه وتعالى) Amekwishakufutia madhambi yako yaliyotangulia na yanayokuja?” Akasema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Je, nisiwe mja anayeshukuru? Nimeteremshiwa Aayah… Ole wake, yule anayezisoma lakini hazitafakari…))

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana, bila shaka ni Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa wenye akili. [Aal-‘Imraan (3:190)]

الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾

Ambao wanamdhukuru Allaah wakiwa wima, au wamekaa au wamejinyoosha, na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu Ni Wako! Basi Tukinge na adhabu ya moto. [Aal-‘Imraan (3:191)]

5-Weka Imaan Thabiti Kwamba Allaah Ndiye Muumbaji Wa Kila Kitu:

Tambua na uweke Imaan thabiti moyoni kuhusu Tawhiyd ya Al-Khaaliq na kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Hafanani na kiumbe chochote na wala Yeye Hakuumbwa. Basi tahadhari na shaytwaan asikutie wasiwasi kuhusu hilo, imetahadharishwa katika Hadiyth:

عن أبي هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((يَأْتِي الشَّيْطَانُ أَحَدَكُمْ فَيَقُولُ: مَنْ خَلَقَ كَذَا، مَنْ خَلَقَ كَذَا، حَتَّى يَقُولَ: مَنْ خَلَقَ رَبَّكَ، فَإِذَا بَلَغَهُ فَلْيَسْتَعِذْ بِاللَّهِ، وَلْيَنْتَهِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Shaytwaan humjia mmoja wenu aseme: “Nani ameumba kadhaa, nani ameumba kadhaa, mpaka mwisho husema: Nani amemuumba Rabb wako? Basi itakapofika hivyo, ajikinge kwa Allaah na aachilie mbali [mawazo hayo].”)) [Al-Bukhaariy]

6-Mshukuru Al-Khaaliq Kwa Kukuumba Ukiwa Mkamilifu:

Tambua, ee Mja wa Al-Khaaliq: Mshukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kukuumba ukiwa umekamilika viungo na uvitolee swadaqah kwa kuswali rakaa mbili za Adh-Dhwuhaa.

عن أبي ذَرٍّ رضي الله ُ عنه، عن النـَبي ِّ صلـَّى الله عليه وسلم قال: ((يـُصـْبـِحُ عـَلى كـُلِّ سـُلامى مـِنْ أحـَدِكـُمْ صـَدَقةُ: فـَكُل تـَسْبـِيحـَةِ صـَدَقةٌ، وَ كُل تـَحمِيدة صـَدَقةٌ ، وكُلُ تـَهْـليْلةٌ صـَدَقـَةٌ، وكُلُّ تـَكْبِيْرةِ صـَدقةٌ، وأمرٌ بالمـَعرُوف صـَدقةٌ، ونـَهىٌ عـَنِ المـُنْكرِ صـَدقةٌ ويـُجْزئ مـِنْ ذلكَ رَكـْعتـَانِ يـَركَعُهُما مـنَ الضـُّحى)) رواه مسلم

Kutoka kwa Abuu Dharr (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Kila kiungo katika mwili wenu hupambaukiwa kikihitaji kutolewa swadaqah, kwa hiyo kila tasbiyh - سُبْحَانَ اللَّهِ ni swadaqah, na kila tahmiyd - الْحَمْدُ لِلَّهِ ni swadaqah, na kila tahliyl - لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ ni swadaqah, na kila takbiyr - اللَّهُ أَكْبَرُ ni swadaqah, na kuamrisha mema ni swadaqah na kukataza maovu ni swadaqah na itamtosheleza (mtu) kwa rakaa mbili za Dhwuhaa)) [Muslim]

7-Msabbih Al-Khaaliq Kila Mara:

Tambua, ee Mja wa Al-Khaaliq: Msabbih Allaah (سبحانه وتعالى) kila mara kwani ni haki Yake kumsabbih kwa kuwa Ndiye Aliyetuumba. Anasema:

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى ﴿١﴾ الَّذِي خَلَقَ فَسَوَّىٰ ﴿٢﴾

Sabbih Jina la Rabb wako Mwenye ‘Uluwa Aliyetukuka kabisa kuliko vyote. Ambaye Ameumba (kila kitu) kisha Akasawazisha. [Al-A’laa (87:1-2)]

8-Usijifanye Muumbaji Kwa Kuchora Viumbe Vyenye Roho:

Tambua, ee Mja wa Al-Khaaliq: Usijifanye wewe muumbaji, nayo ni kuchora viumbe, au kutundika picha za viumbe, kwa sababu ukifanya hivyo utakuwa miongoni mwa watu waovu kabisa Siku ya Qiyaamah na adhabu zake ni kali mno!

عَنْ عَائِشَةَ (رَضِيَ اللهُ عَنْهَا) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم) قَال: ((أَشَدُّ النَّاسِ عَذَابًا يَوْمَ القِيَامَةِ الَّذِينَ يُضَاهِئُونَ بِخَلْقِ اللَّهِ))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Watakaokuwa na adhabu kali Siku ya Qiyaamah ni wanaomuiga Allaah katika uumbaji Wake)) [Al-Bukhaariy] [Muslim]

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) : سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((كُلُّ مُصَوِّرٍ فِي النَّارِ يُجْعَلُ لَهُ بِكُلِّ صُورَةٍ صَوَّرَهَا نَفْسٌ يُعَذَّبُ بِهَا فِي جَهَنَّمَ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Kila mchoraji picha atakuwa motoni. Kila picha aliyoichora, itatiwa roho nayo itamuadhibu katika Jahannam)) [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Kumbuka Du’aa Zinazotaja Uumbaji:

Tambua, ee Mja wa Al-Khaaliq: Tafakari kuwa tunaomba du’aa zinazotaja uumbaji katika nyiradi za kulala na asubuhi na jioni. Tunapolala tunatakiwa tuombe:

اللّهُـمَّ إِنَّـكَ خَلَـقْتَ نَفْسـي وَأَنْـتَ تَوَفّـاهـا لَكَ ممَـاتـها وَمَحْـياها، إِنْ أَحْيَيْـتَها فاحْفَظْـها، وَإِنْ أَمَتَّـها فَاغْفِـرْ لَـها. اللّهُـمَّ إِنَّـي أَسْـأَلُـكَ العـافِـيَة

Yaa Allaah hakika Wewe Umeiumba nafsi yangu Nawe Utaifisha. Ni Kwako uhai wa nafsi yangu na ufaji wake, Ukiipa uhai basi Ihifadhi, na Ukiifisha basi Ighufurie. Yaa Allaah hakika mimi nakuomba afya njema [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنهما) - Muslim (4/2083) [2712], na Ahmad kwa tamshi lake (2/79)]

10-Jikinge Na Shari Ya Alivyoviumba:

Tafakari, ee Mja wa Al-Khaaliq, kuwa baadhi ya viumbe Alivyoviumba Allaah (عزّ وجلّ) ni viumbe vyenye shari na hivyo tunaomba kujikinga navyo tunaposoma:

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ﴿١﴾ مِن شَرِّ مَا خَلَقَ ﴿٢﴾

Sema: Najikinga na Rabb wa mapambazuko. Kutokana na shari ya Alivyoviumba. [Al-Falaq (113:1-2)]

Na pia du’aa katika nyiradi za asubuhi na jioni:

أَعُوْذُ بِكَلِماتِ اللَّهِ التَّامَّتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ

Najikinga kwa Maneno ya Allaah yaliyotimia kutokana na shari ya Alivyoviumba [Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) - Ahmad (2/290), An-Nasaaiy katika ‘Amal Al-Yawm wal-Laylah [590], Ibn As-Sunniy [68]. Angalia: Swahiyh At-Tirmidhiy (3/187), Swahiyh Ibn Maajah (2/266), Tuhfat Al-Akhyaar (Uk. 45) na Taz katika Swahiyh Al-Jaami’ [6427]] Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Atakayesema mara tatu jioni hatodhuriwa na mdudu wa sumu usiku huo))

Na Allaah Mjuzi zaidi