Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah026 - Al-Khallaaq

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 026 kati ya 103
Al-Khallaaq — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Khallaaq: Mwingi Wa Kuumba Atakavyo

Al-Khallaaq ni sura ya mkazo (mubaalaghah) ya Al-Khaaliq; yaani Mwingi wa kuumba, Anayeumba mara kwa mara Atakavyo na Anavyotaka.

Jina hili tukufu, Al-Khallaaq, limetajwa katika Qur-aan mara mbili (2): Al-Hijr (15:86) na Yaasiyn (36:81).

Tofauti kati ya Al-Khaaliq na Al-Khallaaq:

Al-Khaaliq ni Ambaye Anakipata kitu ambacho hakikuwepo.

Al-Khallaaq ni Ambaye Anaumba kwa wingi zaidi, na Uumbaji Wake ni wa aina mbalimbali. Anaumba Atakavyo, Apendavyo.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ﴿٨٦﴾

Hakika Rabb wako Ndiye Mwingi wa kuumba Atakavyo, Mjuzi wa yote. [Al-Hijr (15:86)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿١٧﴾

Anaumba Atakacho. Na Allaah juu ya kila kitu ni Muweza. [Al-Maaidah (5:17)]

Basi Uumbaji Wake haukatiki wala hauishi; Huumba Atakavyo, wakati Atakao, kwa namna Atakayo, na Ni Mjuzi wa vyote Anavyoviumba.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Khallaaq:

1-Al-Khallaaq Anaendelea Kuumba Daima Yale Tusiyoyajua:

Jina Al-Khallaaq linaonyesha wingi wa Uumbaji Wake na kuendelea kwake; kila siku kuna viumbe vipya. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَةً ۚ وَيَخْلُقُ مَا لَا تَعْلَمُونَ﴿٨﴾

Na farasi na baghala na punda ili muwapande na wawe mapambo. Na Anaumba msivyovijua. [An-Nahl (16:8)]

2-Anayeumba Ndiye Anayestahiki Kuabudiwa, Si Asiyeumba:

Kila kinachoabudiwa badala ya Allaah hakiumbi chochote, basi vipi kiwe sawa na Al-Khallaaq? Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَفَمَن يَخْلُقُ كَمَن لَّا يَخْلُقُ ۗ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ﴿١٧﴾

Je, (Allaah) Anayeumba ni sawa na asiyeumba? Je, basi hamkumbuki? [An-Nahl (16:17)]

3-Al-Khallaaq Ameumba Kila Kitu Kwa Ukamilifu Na Uzuri:

Tambua, ee Mja wa Al-Khallaaq: Hakuna kasoro katika Uumbaji Wake; kila kitu kimeumbwa kwa umbo lililo bora kwa kazi yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِي أَحْسَنَ كُلَّ شَيْءٍ خَلَقَهُ ۖ وَبَدَأَ خَلْقَ الْإِنسَانِ مِن طِينٍ ﴿٧﴾

Ambaye Amefanya uzuri kila kitu Alichokiumba, na Akaanzisha uumbaji wa binaadam kutokana na udongo. [As-Sajdah (32:7)]

4-Tafakari Wingi Na Aina Za Uumbaji Wa Al-Khallaaq:

Tafakari Uumbaji wa Al-Khallaaq Anayeumba Atakavyo; tafakari kwanza viumbe wasioonekana kwetu kama Malaika na majini. Kisha tafakari uumbaji wa wana Aadam jinsi tunavyotofautiana umbo, rangi na wingi wetu ulimwenguni. Kisha tafakari viumbe vingapi vipya vipya vinagundulika? Tafakari aina za wanyama wa nchi kavu unapoishi na mbali walioko katika majangwa na misitu ya ulimwengu mzima! Mfano mzuri mwengine wa kutafakari ni pale mpiga mbizi baharini (diver) anapokutana huko na aina mbalimbali za samaki wa kila rangi, na aina nyengine ni za ajabu kabisa. Pia angalia mabilioni yaliyoumbwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kwa aina mbalimbali na sura za kila aina katika wanyama, vidudu, ndege, samaki, miti, na viumbe vinginevyo tusivyoviona au kuvijua, lakini Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Anavijua vilivyo kwani Anasema:

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ﴿١٤﴾

Kwani Hajui Yule Aliyeumba! Na hali Yeye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri! [Al-Mulk (67:14)]

5-Tafakari Uumbaji Wa Nafsi Yako:

Dalili za Al-Khallaaq ziko hata ndani ya nafsi yako: moyo, akili, macho na viungo vyote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَفِي أَنفُسِكُمْ ۚ أَفَلَا تُبْصِرُونَ﴿٢١﴾

Na katika nafsi zenu, je hamuoni? [Adh-Dhaariyaat (51:21)]

6-Tafakari Uumbaji Wa Mbingu Na Ardhi Kama Wanavyofanya Wenye Akili:

Tafakari, ee Mja wa Al-Khallaaq, uumbaji wa mbingu na ardhi kama alivyokuwa akifanya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipoamka usiku.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma Aayah hizi alipoamka usiku. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana, bila shaka ni Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa wenye akili. Ambao wanamdhukuru Allaah wakiwa wima, au wamekaa au wamejinyoosha, na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu Ni Wako! Basi Tukinge na adhabu ya moto. [Aal-‘Imraan (3:190-191)]

7-Jua Kwamba Al-Khallaaq Ni Muweza Wa Kukurudisha Baada Ya Mauti:

Tambua, ee Mja wa Al-Khallaaq: Anayeumba mara ya kwanza bila ya mfano uliotangulia, Ni Muweza zaidi wa kurudisha uumbaji mara ya pili. Basi jiandae kwa Siku ya kufufuliwa. Allaah (تعالى) Amesema katika Hadiyth Al-Qudsiy:

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِيمَا يَرْوِيهِ عَنْ رَبِّهِ (عزّ وجلّ) قَالَ: ((كَذَّبَنِي ابْنُ آدَمَ وَلَمْ يَكُنْ لَهُ ذَلِكَ، وَشَتَمَنِي وَلَمْ يَكُنْ لَهُ ذَلِكَ. فَأَمَّا تَكْذِيبُهُ إِيَّايَ فَقَوْلُهُ: لَنْ يُعِيدَنِي كَمَا بَدَأَنِي، وَلَيْسَ أَوَّلُ الْخَلْقِ بِأَهْوَنَ عَلَيَّ مِنْ إِعَادَتِهِ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesimulia kutoka kwa Rabb wake (عزّ وجلّ): “Mwana wa Aadam amenikadhibisha, na hakupaswa kufanya hivyo; na amenitukana, na hakupaswa kufanya hivyo. Ama kunikadhibisha kwake ni kauli yake: Hatonirudisha kama Alivyonianzisha; na si uumbaji wa mwanzo ulio mwepesi zaidi Kwangu kuliko kuurudisha.” [Al-Bukhaariy]

8-Usijaribu Kuiga Uumbaji Wa Al-Khallaaq:

Tambua kwamba kuumba ni haki ya Al-Khallaaq Pekee, na kukusudia kuiga Uumbaji Wake kwa kuchora viumbe wenye roho kumekatazwa vikali. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَشَدُّ النَّاسِ عَذَابًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ الَّذِينَ يُضَاهُونَ بِخَلْقِ اللَّهِ))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu watakaopata adhabu kali zaidi Siku ya Qiyaamah ni wale wanaoshabihisha (wanaoiga) Uumbaji wa Allaah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Usibadilishe Maumbile Aliyokuumbia Al-Khallaaq:

Tambua kwamba kubadilisha umbo Aliloliumba Al-Khallaaq kwa ajili ya urembo tu ni kupinga Uumbaji Wake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: ((لَعَنَ اللَّهُ الْوَاشِمَاتِ وَالْمُسْتَوْشِمَاتِ، وَالْمُتَنَمِّصَاتِ، وَالْمُتَفَلِّجَاتِ لِلْحُسْنِ، الْمُغَيِّرَاتِ خَلْقَ اللَّهِ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): “Allaah Amewalaani wanaochora chanjo (tattoo) na wanaochorwa, wanaonyoa nyusi, na wanaotenganisha meno kwa ajili ya urembo, wanaobadilisha Uumbaji wa Allaah.” Na akasema: Kwa nini nisimlaani ambaye Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amemlaani? [Al-Bukhaariy] [Muslim]

10-Mshukuru Al-Khallaaq Kwa Umbo Lako, Na Muombe Akupambie Tabia Yako:

Omba du’aa, ee ndugu Muislamu, ukimshukuru Al-Khallaaq kwa umbo lako na ukimwomba Akupambie tabia yako.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiomba:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((اللَّهُمَّ أَحْسَنْتَ خَلْقِي فَأَحْسِنْ خُلُقِي))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema:

اللَّهُمَّ أَحْسَنْتَ خَلْقِي فَأَحْسِنْ خُلُقِي

Yaa Allaah! Umeliboresha umbo langu, basi Niboreshee tabia yangu. [Ahmad (3823), na Shaykh Shu’ayb Al-Arna-uwtw amesema isnaad yake ni Hasan; na imepokewa pia kutoka kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Irwaa Al-Ghaliyl (1/115)]

Na Allaah Mjuzi zaidi