Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah028 - Al-Muswawwir

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 028 kati ya 103
Al-Muswawwir — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Muswawwir: Muundaji wa sura na maumbo; Ambaye Ameunda sura za viumbe vyote kama Atakavyo, na Akakipa kila kimoja sura yake maalumu.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٢٤﴾

Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji, Mwanzishi wa viumbe bila kasoro, Muundaji sura na umbile, Ana Majina Mazuri kabisa. Kinamsabihi Pekee kila kilichoko katika mbingu na ardhi, Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Hashr (59:24)]

Imaam Ibn Kathiyr (رحمه الله) amesema katika tafsiyr ya Aayah hii:

﴿الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ﴾ أَيِ: الَّذِي إِذَا أَرَادَ شَيْئًا قَالَ لَهُ: كُنْ، فَيَكُونُ عَلَى الصِّفَةِ الَّتِي يُرِيدُ، وَالصُّورَةِ الَّتِي يَخْتَارُ

“‘Al-Khaaliq, Al-Baariu, Al-Muswawwir’, yaani: Ambaye Anapotaka kitu, Hukiambia: Kuwa! Nacho huwa, kwa sifa Anayoitaka na sura Anayoichagua.”1 Na Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema kwamba Al-Baariu na Al-Muswawwir ni ufafanuzi wa maana ya Jina Al-Khaaliq.2

Maana Ya Al-Muswawwir:

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Muundaji wa sura na maumbo; Ameunda sura za viumbe Vyake vyote vilivyomo ulimwenguni, Akavipanga, na Akakipa kila kimoja sura maalumu na umbo lake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ ﴿٧﴾ فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ ﴿٨﴾

Ambaye Amekuumba, Akakusawazisha (umbo, sura, viungo), na Akakulinganisha sawa. Katika sura Aliyotaka Akakutengeneza. [Al-Infitwaar (82:7-8)]

2-Anamuunda kila mwanaadam katika tumbo la mama yake kwa namna Anavyotaka. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ الَّذِي يُصَوِّرُكُمْ فِي الْأَرْحَامِ كَيْفَ يَشَاءُ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٦﴾

Yeye Ndiye Anayekusawirini umbo katika matumbo ya uzazi vile Atakavyo. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Aal-‘Imraan (3:6)]

3-Ameanzisha Uumbaji Wake kwa sura mbalimbali na maumbo mengi yanayotofautiana: warefu na wafupi, wanaume na wanawake, kila mmoja na sura yake na umbo lake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَقَدْ خَلَقْنَاكُمْ ثُمَّ صَوَّرْنَاكُمْ ثُمَّ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ لَمْ يَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ ﴿١١﴾

Na kwa yakini Tumekuumbeni kisha Tukakutieni sura, kisha Tukawaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys hakuwa miongoni mwa waliosujudu. [Al-A’raaf (7:11)]

Na Anasema pia:

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ ۖ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴿٣﴾

Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, na Akakutengenezeni sura, kisha Akafanya nzuri zaidi sura zenu, na Kwake ndio mahali pa kuishia. [At-Taghaabun (64:3)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muswawwir:

1-Tafakari Upweke Wa Allaah Katika Kuunda Viumbe Vyake:

Tafakari, ee Mja wa Al-Muswawwir, jinsi Alivyounda sura za wanaadam, rangi zao na miili yao; na tafakari wanyama wa angani, baharini na nchi kavu, kila mmoja na sura yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِكُمْ وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ ۚ وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ ﴿١٠﴾ هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١١﴾

(Allaah) Ameumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona, na Akaweka katika ardhi milima iliyosimama imara ili isiyumbe nanyi, na Akaeneza humo kila viumbe vinavyotembea. Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji, Tukaotesha humo kila aina ya mimea mizuri yenye manufaa. Huu ni Uumbaji wa Allaah, basi nionyesheni nini walichokiumba wasiokuwa Yeye. Bali madhalimu wamo katika upotofu bayana. [Luqmaan (31:10-11)]

2-Tafakari Jinsi Al-Muswawwir Alivyokuunda Tumboni Hatua Kwa Hatua:

Tafakari, ee ndugu Muislamu, hatua ulizopitia tumboni mwa mama yako, na jinsi Al-Muswawwir Alivyokuunda hatua kwa hatua.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾ ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ ﴿١٣﴾ ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ ۚ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ ﴿١٤﴾

Kwa yakini Tumemuumba binaadam kutokana na mchujo safi wa udongo. Kisha Tukamfanya kuwa tone la manii katika kalio makini. Kisha Tukaumba tone la manii kuwa pande la damu linaloning’inia, Tukaumba pande la damu hilo linaloning’inia kuwa kinofu cha nyama, Tukaumba kinofu hicho cha nyama kuwa mifupa, Tukavisha mifupa hiyo nyama, kisha Tukamuanzisha kiumbe kingine. Basi Amebarikika Allaah Mbora wa wenye kuumba. [Al-Muuminuwn (23:12-14)]

3-Mshukuru Al-Muswawwir Aliyekuunda Katika Sura Nzuri Kabisa:

Tambua, ee Mja wa Al-Muswawwir: Kila kiungo Amekiweka mahali pake panapostahiki; tafakari lau ungekuwa na kiungo kimoja kisicho mahali pake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ﴿٤﴾

Kwa yakini Tumemuumba binaadam katika umbile bora kabisa. [At-Tiyn (95:4)]

4-Usimdharau Mtu Kwa Sababu Ya Sura Yake:

Sura ni kazi ya Al-Muswawwir, wala mja hana hiari katika sura yake; na kipimo cha mtu mbele ya Allaah si sura yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلَى صُوَرِكُمْ وَأَمْوَالِكُمْ، وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ وَأَعْمَالِكُمْ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Haangalii sura zenu wala mali zenu, lakini Anaangalia nyoyo zenu na amali zenu.” [Muslim]

5-Tumia Viungo Vya Mwili Wako Katika Yale Yanayomridhisha Al-Muswawwir:

Tambua, ee Mja wa Al-Muswawwir: Mwanamke aliyejaaliwa sura nzuri ajisitiri, na ajiepushe na kujionyesha kwa wanaume wasio mahram wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾

Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Al-Ahzaab (33:59)]

Na kumbuka kwamba viungo vyako vitashuhudia juu yako Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٢٠﴾ وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّـهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٢١﴾

Mpaka watakapoufikia, yatashuhudia dhidi yao masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. Na wataziambia ngozi zao: Mbona mnashuhudia dhidi yetu? Zitasema: Ametutamkisha Allaah Ambaye Ametamkisha kila kitu, Naye Ndiye Aliyekuumbeni mara ya kwanza, na Kwake mtarejeshwa. [Fusw-Swilat (41:20-21)]

Na Anasema pia:

يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾

Siku zitakaposhuhudia dhidi yao ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [An-Nuwr (24:24)]

6-Ridhika Na Sura Aliyokuundia Al-Muswawwir Wala Usiibadilishe:

Zingatia, usilalamike, wala usibadilishe umbo lako kwa ajili ya kujipamba tu; kwani kubadilisha Uumbaji wa Al-Muswawwir ni miongoni mwa mambo anayoyaamrisha shaytwaan. Allaah Anasema kuhusu shaytwaan:

وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللَّـهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا ﴿١١٩﴾

Na hakika nitawapoteza, na nitawashawishi matamanio ya kulaghai, na nitawaamrisha. Basi watakata masikio ya wanyama (wawatukuze), na nitawaamrisha watabadili Uumbaji wa Allaah. Na atakayemfanya shaytwaan kuwa rafiki mlinzi badala ya Allaah basi kwa yakini amekhasirika khasara bayana. [An-Nisaa (4:119)]

7-Ukimwona Mwenye Mtihani, Usimcheke Bali Mshukuru Allaah:

Tahadhari na kumcheka au kumdharau aliyepatwa na mtihani katika mwili wake; bali mshukuru Al-Muswawwir kwa afya Aliyokupa.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنْ رَأَى مُبْتَلًى فَقَالَ: الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي عَافَانِي مِمَّا ابْتَلاَكَ بِهِ، وَفَضَّلَنِي عَلَى كَثِيرٍ مِمَّنْ خَلَقَ تَفْضِيلاً، لَمْ يُصِبْهُ ذَلِكَ الْبَلاَءُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayemwona aliyepatwa na mtihani akasema:

الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي عَافَانِي مِمَّا ابْتَلاَكَ بِهِ، وَفَضَّلَنِي عَلَى كَثِيرٍ مِمَّنْ خَلَقَ تَفْضِيلاً

Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Ameniepusha na kile Alichokupa mtihani nacho, na Akanifadhilisha kuliko wengi miongoni mwa Aliowaumba; hatafikwa na mtihani huo.” [At-Tirmidhiy (3432), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

8-Jiepushe Na Kuiga Uundaji Wa Al-Muswawwir Kwa Kuchora Picha Za Viumbe Wenye Roho:

Tambua, ee Mja wa Al-Muswawwir: Jambo hili limeharamishwa katika nususi kadhaa, zikiwemo:

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: سَمِعْتُ مُحَمَّدًا (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((مَنْ صَوَّرَ صُورَةً فِي الدُّنْيَا كُلِّفَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَنْ يَنْفُخَ فِيهَا الرُّوحَ، وَلَيْسَ بِنَافِخٍ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nimemsikia Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Atakayechora picha (ya kiumbe mwenye roho) duniani, atalazimishwa Siku ya Qiyaamah aitie roho, na hatoweza kuitia.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Na pia:

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((كُلُّ مُصَوِّرٍ فِي النَّارِ، يَجْعَلُ لَهُ بِكُلِّ صُورَةٍ صَوَّرَهَا نَفْسًا فَتُعَذِّبُهُ فِي جَهَنَّمَ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Kila mchoraji picha (za viumbe wenye roho) atakuwa motoni; kwa kila picha aliyoichora itajaaliwa kuwa nafsi, nayo itamwadhibu katika Jahannam.” [Muslim]

9-Mwombe Al-Muswawwir Akudumishie Afya Ya Mwili Wako:

Tambua kwamba wangapi wamepoteza viungo au sura zao baada ya maafa na maradhi! Basi mwombe Al-Muswawwir afya, kama alivyokuwa akiomba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kila asubuhi na jioni:

عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ أَبِي بَكْرَةَ أَنَّهُ قَالَ لأَبِيهِ: يَا أَبَتِ إِنِّي أَسْمَعُكَ تَدْعُو كُلَّ غَدَاةٍ: ((اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي بَدَنِي، اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي سَمْعِي، اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي بَصَرِي، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ)) تُعِيدُهَا ثَلاَثًا حِينَ تُصْبِحُ وَثَلاَثًا حِينَ تُمْسِي، فَقَالَ: إِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَدْعُو بِهِنَّ، فَأَنَا أُحِبُّ أَنْ أَسْتَنَّ بِسُنَّتِهِ

Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Abiy Bakrah kwamba alimwambia baba yake: Yaa baba yangu! Hakika mimi nakusikia ukiomba kila asubuhi:

اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي بَدَنِي، اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي سَمْعِي، اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي بَصَرِي، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ

Yaa Allaah! Nipe afya katika mwili wangu. Yaa Allaah! Nipe afya katika kusikia kwangu. Yaa Allaah! Nipe afya katika kuona kwangu. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe. Unaikariri mara tatu unapoamka asubuhi na mara tatu unapoingia jioni. Akasema: Hakika mimi nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiomba kwa maneno hayo, nami napenda kufuata Sunnah yake. [Abuu Daawuwd (5090); Imaam Al-Albaaniy amesema isnaad yake ni Hasan katika Swahiyh Abiy Daawuwd (5090), na ameipa daraja ya Dhwa’iyf katika Dhwa’iyf Al-Jaami’ (1210)]

10-Mtukuze Al-Muswawwir Katika Sujuud Yako:

Mtukuze Al-Muswawwir katika Sujuud yako kwa du’aa hii, ukikiri kwamba Yeye Ndiye Aliyekuumba na Akakutia sura.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema katika Sujuud yake:

عَنْ عَلِيِّ بْنِ أَبِي طَالِبٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَنَّهُ كَانَ إِذَا سَجَدَ قَالَ: ((اللَّهُمَّ لَكَ سَجَدْتُ، وَبِكَ آمَنْتُ، وَلَكَ أَسْلَمْتُ، سَجَدَ وَجْهِي لِلَّذِي خَلَقَهُ وَصَوَّرَهُ، وَشَقَّ سَمْعَهُ وَبَصَرَهُ، تَبَارَكَ اللَّهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ))

Amesimulia ‘Aliy bin Abiy Twaalib (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anaposujudu husema:

اللَّهُمَّ لَكَ سَجَدْتُ، وَبِكَ آمَنْتُ، وَلَكَ أَسْلَمْتُ، سَجَدَ وَجْهِي لِلَّذِي خَلَقَهُ وَصَوَّرَهُ، وَشَقَّ سَمْعَهُ وَبَصَرَهُ، تَبَارَكَ اللَّهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ

Yaa Allaah! Kwako nimesujudu, na Kwako nimeamini, na Kwako nimejisalimisha. Uso wangu umemsujudia Yule Aliyeuumba na Akautia sura, na Akaupasulia kusikia kwake na kuona kwake. Amebarikika Allaah, Mbora wa waumbaji. [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Tafsiyr Ibn Kathiyr, Suwrah Al-Hashr (59:24).
  • 2Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله); imenukuliwa na Kalemtayeb katika maelezo ya Majina Al-Khaaliq, Al-Baariu na Al-Muswawwir.