Al-Hakam: Mwamuzi; Anayehukumu baina ya viumbe Vyake kwa uadilifu bila kumdhulumu yeyote, na Aliyeteremsha Kitabu Chake kiwe hakimu baina ya watu.
Jina hili limekuja katika Qur-aan katika Kauli Yake (سبحانه وتعالى):
أَفَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْتَغِي حَكَمًا وَهُوَ الَّذِي أَنزَلَ إِلَيْكُمُ الْكِتَابَ مُفَصَّلًا ۚ وَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْلَمُونَ أَنَّهُ مُنَزَّلٌ مِّن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ ۖ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ ﴿١١٤﴾
(Sema): Je, nitafute hakimu ghairi ya Allaah na hali Yeye Ndiye Aliyekuteremshieni Kitabu kilichofasiliwa waziwazi? Na wale Tuliowapa Kitabu (kabla) wanajua kwamba kimeteremshwa kutoka kwa Rabb wako kwa haki. Basi usijekuwa miongoni mwa wanaotia shaka. [Al-An’aam (6:114)]
Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameithibitisha katika Sunnah:
عَنْ هَانِئٍ (رضي الله عنه) أَنَّهُ لَمَّا وَفَدَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) مَعَ قَوْمِهِ سَمِعَهُمْ يَكْنُونَهُ بِأَبِي الْحَكَمِ، فَدَعَاهُ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) فَقَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ هُوَ الْحَكَمُ، وَإِلَيْهِ الْحُكْمُ، فَلِمَ تُكْنَى أَبَا الْحَكَمِ؟)) ...
Amesimulia Haani-u (رضي الله عنه) kwamba alipomjia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na kaumu yake, (Nabiy) aliwasikia wakimwita kwa kun-ya ya Abul-Hakam. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwita, akasema: “Hakika Allaah Ndiye Al-Hakam, na Kwake ndiko kuna hukumu; basi kwa nini unaitwa Abul-Hakam?” … [Abuu Daawuwd (4955), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha]
Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amejisifu kuwa Ndiye Mbora wa wanaohukumu. Anasema kuhusu Nabiy Shu’ayb (عليه السلام):
وَإِن كَانَ طَائِفَةٌ مِّنكُمْ آمَنُوا بِالَّذِي أُرْسِلْتُ بِهِ وَطَائِفَةٌ لَّمْ يُؤْمِنُوا فَاصْبِرُوا حَتَّىٰ يَحْكُمَ اللَّـهُ بَيْنَنَا ۚ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ ﴿٨٧﴾
Na kama liko kundi miongoni mwenu limeamini yale niliyotumwa nayo na kundi halikuamini, basi subirini mpaka Allaah Ahukumu baina yetu. Naye Ndiye Mbora wa Kuhukumu kuliko wote. [Al-A’raaf (7:87)]
Na Anasema kuhusu du’aa ya Nabiy Nuwh (عليه السلام):
وَنَادَىٰ نُوحٌ رَّبَّهُ فَقَالَ رَبِّ إِنَّ ابْنِي مِنْ أَهْلِي وَإِنَّ وَعْدَكَ الْحَقُّ وَأَنتَ أَحْكَمُ الْحَاكِمِينَ﴿٤٥﴾
Na Nuwh akamwita Rabb wake, akasema: Rabb wangu! Hakika mwanangu ni katika ahli zangu, na hakika Ahadi Yako ni ya kweli, Nawe Ni Mwadilifu zaidi wa kuhukumu kuliko mahakimu wote. [Huwd (11:45)]
Na Anasema:
أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ ﴿٨﴾
Je, kwani Allaah Si Mwadilifu zaidi kuliko mahakimu wote? [At-Tiyn (95:8)]
Maana Ya Al-Hakam:
1-Allaah (سبحانه وتعالى) Anahukumu baina ya Waja Wake kwa uadilifu kamili; Hambebeshi mtu mzigo wa mwingine, wala Hamlipi mja zaidi ya dhambi zake, na Humfikishia kila mwenye haki haki yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَّنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا ۚ وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۗ وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا ﴿١٥﴾
Anayehidika, basi anahidika kwa manufaa ya nafsi yake. Na anayepotoka, basi anapotoka kwa hasara yake. Na wala mbebaji (wa dhambi) hatobeba mzigo wa mwengine. Na Hatukuwa Wenye Kuadhibu mpaka Tupeleke Rasuli. [Al-Israa (17:15)]
2-Hukumu Zake kwa Waja Wake ni za aina mbili:
a-Hukumu ya Kiulimwengu (Kawniyy): Nayo ni hali halisi isiyoepukika, inayohusiana na Mapenzi Yake (عزّ وجلّ); Anayoyataka ndiyo yanayokuwa, na Asiyoyataka hayawi. Hukumu Yake hairudishwi, wala hakuna wa kuipinga. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَأْتِي الْأَرْضَ نَنقُصُهَا مِنْ أَطْرَافِهَا ۚ وَاللَّـهُ يَحْكُمُ لَا مُعَقِّبَ لِحُكْمِهِ ۚ وَهُوَ سَرِيعُ الْحِسَابِ﴿٤١﴾
Je, hawaoni kwamba Tunaifikia ardhi Tukaipunguza mipaka yake? Na Allaah Anahukumu na hakuna wa kupinga Hukmu Yake. Naye Ni Mwepesi wa kuhesabu. [Ar-Ra’d (13:41)]
b-Hukumu ya Kishariy’ah (Shar’iyy): Nazo ni hukumu Alizowawekea waja katika Dini Yake; ndizo hukumu bora kabisa, zenye maslahi yao na ukamilifu wake, wala Dini yao haiongoki isipokuwa kwa kuzifuata. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ ۚ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّـهِ حُكْمًا لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ ﴿٥٠﴾
Je, wanataka hukumu za kijahiliya? Na nani mbora zaidi kuliko Allaah katika kuhukumu kwa watu wenye yakini? [Al-Maaidah (5:50)]
Hukumu hii ya Kishariy’ah ndiyo ambayo mja atalipwa kwayo thawabu au adhabu Siku ya Hesabu. Na aina zote mbili za hukumu zinampitia mja: hukumu ya Kiulimwengu inampitia apende au asipende, wala hawezi kwenda kinyume nayo; ama hukumu ya Kishariy’ah, mja anaweza kuikhalifu, na hapo ndipo atakapoadhibiwa.
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Hakam:
1-Hakuna Mshirika Pamoja Na Allaah Katika Hukumu Yake:
Tambua, ee Mja wa Al-Hakam: Kama ambavyo hakuna mshirika pamoja Naye katika kuabudiwa, vilevile hakuna anayeshirikiana Naye katika Hukumu Zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلِ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا ۖ لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ ۚ مَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا يُشْرِكُ فِي حُكْمِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾
Sema: Allaah Anajua zaidi muda waliokaa. Ni Yake Pekee ghaibu za mbingu na ardhi. Kuona kulioje Kwake na Kusikia! Hawana pasi Naye mlinzi yeyote na wala Hamshirikishi katika Hukumu Zake yeyote. [Al-Kahf (18:26)]
2-Rejesha Kila Mnachokhitilafiana Kwa Hukumu Ya Allaah:
Kumbuka kwamba Muumini hana hukumu nyingine ya kurejea anapokhitilafiana na wenzake isipokuwa Hukumu ya Al-Hakam na Rasuli Wake.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبِّي عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ﴿١٠﴾
Na katika lolote lile mlilokhitilafiana, basi hukumu yake irejesheni kwa Allaah. Huyo Ndiye Allaah Rabb wangu, Kwake nimetawakali, na Kwake naelekea kwa mambo yangu yote. [Ash-Shuwraa (42:10)]
3-Ikubali Hukumu Ya Allaah Na Rasuli Wake Kwa Moyo Mkunjufu:
Tambua, ee Mja wa Al-Hakam: Muumini anapaswa kuikubali na kuiridhia Hukumu ya Allaah (سبحانه وتعالى). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾
Basi mambo si kama wanavyodai. Naapa kwa Rabb wako, hawatakuwa Waumini wa kweli mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao ukakasi katika yale uliyohukumu, na waikubali hukmu yako kwa moyo safi na maridhio. [An-Nisaa (4:65)]
Na sababu ya kuteremshwa Aayah hii ni kama ilivyothibiti:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ الزُّبَيْرِ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَجُلاً مِنَ الأَنْصَارِ خَاصَمَ الزُّبَيْرَ عِنْدَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِي شِرَاجِ الْحَرَّةِ الَّتِي يَسْقُونَ بِهَا النَّخْلَ ... فَقَالَ الزُّبَيْرُ: وَاللَّهِ إِنِّي لأَحْسِبُ هَذِهِ الآيَةَ نَزَلَتْ فِي ذَلِكَ: ﴿فَلاَ وَرَبِّكَ لاَ يُؤْمِنُونَ حَتَّى يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ﴾
Amesimulia ‘Abdullaah bin Az-Zubayr (رضي الله عنهما) kwamba mtu mmoja katika Answaar aligombana na Az-Zubayr mbele ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu mifereji ya maji ya mvua ya Al-Harrah waliyokuwa wakimwagilia kwayo mitende … Az-Zubayr akasema: Wa-Allaahi, hakika mimi nadhani Aayah hii ilishuka kuhusu jambo hilo: “Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
4-Sema Kama Wanavyosema Waumini: Tumesikia Na Tumetii:
Tambua kwamba alama ya imaan ya kweli ni kuitikia Hukumu ya Al-Hakam bila kusita wala kutafuta njia za kuikwepa.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٥١﴾
Hakika kauli ya Waumini (wa kweli) wanapoitwa kwa Allaah na Rasuli Wake ili Awahukumu baina yao ni kusema: Tumesikia na tumetii. Na hao ndio wenye kufaulu. [An-Nuwr (24:51)]
5-Ukiwa Hakimu Au Msimamizi, Hukumu Kwa Uadilifu Bila Kupendelea:
Tambua, ee Mja wa Al-Hakam: Allaah (عزّ وجلّ) Anasema:
إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٥٨﴾
Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe. Na mtakapohukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Ni uzuri ulioje wa Anayokuwaidhini kwayo Allaah! Hakika Allaah daima Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [An-Nisaa (4:58)]
6-Ukidhulumiwa, Subiri Na Mwachie Al-Hakam Hukumu:
Muombe Al-Hakam Akuhukumie dhulma uliyotendewa, kwani Yeye Ndiye Mbora wa wanaohukumu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاتَّبِعْ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ وَاصْبِرْ حَتَّىٰ يَحْكُمَ اللَّـهُ ۚ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ﴿١٠٩﴾
Na fuata yale uliyofunuliwa Wahy, na subiri mpaka Allaah Ahukumu. Naye Ni Mbora wa wanaohukumu. [Yuwnus (10:109)]
7-Usijipe Majina Na Lakabu Zinazomhusu Allaah Pekee:
Tahadhari na kujipa au kuwapa watu majina na lakabu zinazomhusu Allaah Pekee, kama “Al-Hakam” kwa maana yake kamili.
Rejea Hadiyth ya Haani-u (رضي الله عنه) juu; Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alibadilisha kun-ya yake kwa sababu Al-Hakam wa kweli ni Allaah Pekee.
8-Kumbuka Siku Ambayo Al-Hakam Atahukumu Baina Ya Waja Wake Katika Yote Waliyokhitilafiana:
Kumbuka Siku ambayo kila mzozo utamalizika mbele ya Al-Hakam, na hakuna dhulma itakayobaki bila kuhukumiwa.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلِ اللَّـهُمَّ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ أَنتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادِكَ فِي مَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ﴿٤٦﴾
Sema: Ee Allaah! Mwanzilishi wa mbingu na ardhi, Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, Wewe Utahukumu baina ya Waja Wako katika yale ambayo walikuwa wakikhitilafiana. [Az-Zumar (39:46)]
9-Mwombe Al-Hakam Akuongoze Kwenye Haki Katika Yale Watu Wanayokhitilafiana:
Omba du’aa ili Al-Hakam Akuongoze kwenye haki pale watu wanapokhitilafiana na mambo yanapochanganyika.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akifungua Swalaah yake ya usiku kwa du’aa hii:
عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: كَانَ نَبِيُّ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) إِذَا قَامَ مِنَ اللَّيْلِ افْتَتَحَ صَلاَتَهُ: ((اللَّهُمَّ رَبَّ جَبْرَائِيلَ وَمِيكَائِيلَ وَإِسْرَافِيلَ، فَاطِرَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ، أَنْتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادِكَ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ، اهْدِنِي لِمَا اخْتُلِفَ فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِكَ، إِنَّكَ تَهْدِي مَنْ تَشَاءُ إِلَى صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ))
Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Nabiy wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anaposimama usiku (kuswali) hufungua Swalaah yake kwa:
اللَّهُمَّ رَبَّ جَبْرَائِيلَ وَمِيكَائِيلَ وَإِسْرَافِيلَ، فَاطِرَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ، أَنْتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادِكَ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ، اهْدِنِي لِمَا اخْتُلِفَ فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِكَ، إِنَّكَ تَهْدِي مَنْ تَشَاءُ إِلَى صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ
Yaa Allaah! Rabb wa Jibraaiyl, Miykaaiyl na Israafiyl, Mwanzilishi wa mbingu na ardhi, Mjuzi wa ghaibu na dhahiri; Wewe Ndiye Unayehukumu baina ya Waja Wako katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana. Niongoze kwenye haki katika yale yaliyokhitilafiwa kwa Idhini Yako; hakika Wewe Unamwongoza Umtakaye kwenye njia iliyonyooka. [Muslim]
10-Unapofikwa Na Huzuni, Mwombe Allaah Ukikiri Kwamba Hukumu Yake Imepita Kwako:
Omba du’aa hii unapofikwa na hamu au huzuni, ukikiri kwamba Hukumu ya Al-Hakam ndiyo inayopita juu yako, na kwamba uamuzi Wake ni uadilifu.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَا أَصَابَ أَحَدًا قَطُّ هَمٌّ وَلاَ حَزَنٌ فَقَالَ: اللَّهُمَّ إِنِّي عَبْدُكَ، ابْنُ عَبْدِكَ، ابْنُ أَمَتِكَ، نَاصِيَتِي بِيَدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤُكَ، أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ، سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوِ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ، أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ رَبِيعَ قَلْبِي، وَنُورَ صَدْرِي، وَجِلاَءَ حُزْنِي، وَذَهَابَ هَمِّي، إِلاَّ أَذْهَبَ اللَّهُ هَمَّهُ وَحُزْنَهُ، وَأَبْدَلَهُ مَكَانَهُ فَرَجًا))
Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna yeyote aliyewahi kufikwa na hamu wala huzuni akasema:
اللَّهُمَّ إِنِّي عَبْدُكَ، ابْنُ عَبْدِكَ، ابْنُ أَمَتِكَ، نَاصِيَتِي بِيَدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤُكَ، أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ، سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوِ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ، أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ رَبِيعَ قَلْبِي، وَنُورَ صَدْرِي، وَجِلاَءَ حُزْنِي، وَذَهَابَ هَمِّي
Yaa Allaah! Hakika mimi ni Mja Wako, mwana wa Mja Wako, mwana wa kijakazi Chako; utosi wangu uko Mkononi Mwako, Hukumu Yako inapita kwangu, uadilifu ni uamuzi Wako juu yangu. Nakuomba kwa kila Jina ambalo ni Lako, Ulilojiita Nalo, au Ulioliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilomfundisha yeyote katika viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi katika ilimu ya ghaibu iliyo Kwako, Uijaalie Qur-aan kuwa ni machipuo ya moyo wangu, na nuru ya kifua changu, na kiondoshaji cha huzuni yangu, na kiondoshaji cha hamu yangu; isipokuwa Allaah Humwondoshea hamu yake na huzuni yake, na Humbadilishia mahali pake faraja.” [Ahmad, Ibn Hibbaan, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (199)]
Na Allaah Mjuzi zaidi