Al-Hakiym: Mwenye Hikmah wa yote; Mwenye kuweka kila kitu mahali pake, Ambaye Maneno Yake, matendo Yake na Hukumu Zake zote ni haki, uadilifu na usahihi.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara tisini na moja (91), na mara nyingi limeambatana na Majina Al-‘Aziyz, Al-‘Aliym na Al-Khabiyr. Malaika walipoulizwa juu ya ilimu, walisema:
قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٣٢﴾
Wakasema: Utakasifu ni Wako! Hatuna ilimu isipokuwa Uliyotufunza, hakika Wewe Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Baqarah (2:32)]
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ ﴿١٨﴾
Naye Ndiye Aliyedhibiti vyote chini ya Mamlaka Yake, Aliye juu ya Waja Wake. Naye Ndiye Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-An’aam (6:18)]
Maana Ya Al-Hakiym:
1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mwenye Hikmah katika Maneno Yake, matendo Yake na Hukumu Zake; Hasemi, Hafanyi, wala Hahukumu isipokuwa kwa haki, uadilifu na usahihi. Hakitoki kitu katika Hikmah Yake, wala hakiingii katika mpangilio Wake kosa lolote.
2-Ni Mwenye Hikmah ya juu kabisa katika Uumbaji Wake na katika Amri Zake. Haumbi kwa mchezo, wala Hawekei sharia bila lengo, wala Hawaachi Waja Wake bure. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ۚ ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّارِ ﴿٢٧﴾
Na wala Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake bila kusudio. Hiyo ndio dhana ya wale waliokufuru. Basi ole wao wale waliokufuru kwa moto utakaowapata. [Swaad (38:27)]
3-Haamrishi isipokuwa kilicho na maslahi, wala Hakatazi isipokuwa kilicho na madhara; na Kitabu Chake kimetengenezwa kwa hikmah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الر ۚ كِتَابٌ أُحْكِمَتْ آيَاتُهُ ثُمَّ فُصِّلَتْ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ خَبِيرٍ﴿١﴾
Alif Laam Raa. Kitabu ambacho Aayaat Zake zimetimizwa barabara, kisha zikafasiliwa waziwazi kutoka kwa Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Huwd (11:1)]
4-Na katika ukamilifu wa Hikmah Yake ni kutumwa kwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Dini ya Kiislamu na Qur-aan, ambayo haifikiwi na ubatili. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ﴿٤٢﴾
Hakitokifikia baatwil mbele yake wala nyuma yake. Ni Uteremsho kutoka kwa Mwenye Hikmah wa yote, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Fusw-Swilat (41:42)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Hakiym:
1-Zingatia Hikmah Ya Al-Hakiym Katika Uumbaji Wa Dunia:
Tafakari, ee Mja wa Al-Hakiym, jinsi Alivyoumba dunia, Akaweka kila kitu na mahitaji yote ya Waja Wake, Akainua mbingu na Akaitandaza ardhi ili viumbe viweze kuishi humo; na hayo ndiyo mazingatio ya wenye akili:
إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾
Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana, bila shaka ni Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa wenye akili. Ambao wanamdhukuru Allaah wakiwa wima, au wamekaa au wamejinyoosha, na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu Ni Wako! Basi Tukinge na adhabu ya moto. [Aal-‘Imraan (3:190-191)]
2-Zingatia Hikmah Yake Katika Uumbaji Wa Mwili Wako:
Tafakari, ee Mja wa Al-Hakiym, jinsi Alivyojaalia kila kiungo kiwe mahali panapofaa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الَّذِي أَحْسَنَ كُلَّ شَيْءٍ خَلَقَهُ ۖ وَبَدَأَ خَلْقَ الْإِنسَانِ مِن طِينٍ ﴿٧﴾ ثُمَّ جَعَلَ نَسْلَهُ مِن سُلَالَةٍ مِّن مَّاءٍ مَّهِينٍ ﴿٨﴾ ثُمَّ سَوَّاهُ وَنَفَخَ فِيهِ مِن رُّوحِهِ ۖ وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ ۚ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٩﴾
Ambaye Amefanya uzuri kila kitu Alichokiumba, na Akaanzisha uumbaji wa binaadam kutokana na udongo. Kisha Akajaalia kizazi chake kutokana na mchujo safi wa maji dhalilifu. Kisha Akamsawazisha, na Akapuliza humo roho yake (Aliyoiumba Allaah). Na Akakujaalieni kusikia na kuona na nyoyo, ni machache mno yale mnayoshukuru. [As-Sajdah (32:7-9)]
3-Mwombe Allaah Akujaalie Kuwa Mwenye Hikmah:
Tambua, ee Mja wa Al-Hakiym: Anayepewa hikmah hakika amepewa kheri nyingi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يُؤْتِي الْحِكْمَةَ مَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُؤْتَ الْحِكْمَةَ فَقَدْ أُوتِيَ خَيْرًا كَثِيرًا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٢٦٩﴾
Humpa hikmah Amtakaye. Na anayepewa hikmah basi kwa yakini huwa amepewa kheri nyingi. Lakini hawakumbuki isipokuwa wenye akili. [Al-Baqarah (2:269)]
4-Tamani Kuwa Kama Aliyepewa Hikmah Akahukumu Kwayo Na Kuifundisha:
Tambua, ee Mja wa Al-Hakiym, kwamba hikmah ni neema kubwa kiasi kwamba inastahiki kutamaniwa; na aliyepewa hikmah ana jukumu la kuitumia na kuifundisha.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((لاَ حَسَدَ إِلاَّ فِي اثْنَتَيْنِ: رَجُلٌ آتَاهُ اللَّهُ مَالاً فَسُلِّطَ عَلَى هَلَكَتِهِ فِي الْحَقِّ، وَرَجُلٌ آتَاهُ اللَّهُ الْحِكْمَةَ فَهُوَ يَقْضِي بِهَا وَيُعَلِّمُهَا))
Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna husuda (ya kutamani) isipokuwa katika mambo mawili: Mtu ambaye Allaah Amempa mali, akawezeshwa kuitumia katika haki; na mtu ambaye Allaah Amempa hikmah, naye anahukumu kwayo na kuifundisha.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
5-Tumia Hikmah Katika Kuwalingania Watu Na Kutangamana Nao:
Tumia, ee Mja wa Al-Hakiym, hikmah katika kusuluhisha baina ya watu, katika kutoa ushauri, na katika kuwalingania kwa Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ﴿١٢٥﴾
Lingania waje katika Njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa njia bora yenye kunasibiana na hali. Hakika Rabb wako, Yeye Anamjua zaidi aliyepotea Njia Yake, Naye Anawajua zaidi waliohidika. [An-Nahl (16:125)]
6-Unapofikwa Na Mitihani, Amini Kwamba Al-Hakiym Anajua Hikmah Yake:
Mitihani ni majaaliwa ya Allaah (عزّ وجلّ), na huenda ikawa ni kheri kwako; kwani Al-Hakiym Anajua kwa nini Ameijaalia ikufike. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾
Mmeandikiwa sharia kupigana vita nako kunachukiza mno kwenu. Lakini asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni la kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah (2:216)]
7-Jisalimishe Kwa Hukumu Za Al-Hakiym Hata Kama Hujaijua Hikmah Yake:
Tambua kwamba hukumu zote za Al-Hakiym ni hikmah; basi Muumini hazipingi kwa sababu tu hajaijua hikmah yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾
Na haiwi kwa Muumini mwanamume wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana khiari katika jambo lao. Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab (33:36)]
8-Jifunze Sunnah, Kwani Hiyo Ndiyo Hikmah Aliyoiteremsha Allaah:
Tambua kwamba Al-Hakiym Aliwaamrisha wake wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) wakumbuke Aayaat Zake na hikmah inayosomwa majumbani mwao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَىٰ فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ وَالْحِكْمَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ لَطِيفًا خَبِيرًا ﴿٣٤﴾
Na kumbukeni yale yanayosomwa majumbani mwenu katika Aayaat za Allaah na Hikmah (Sunnah). Hakika Allaah daima Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-Ahzaab (33:34)]
9-Ishukuru Neema Ya Kufundishwa Kitabu Na Hikmah:
Tambua kwamba hii ilikuwa du’aa ya Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) kwa ajili ya ummah huu, na Al-Hakiym Akaiitikia kwa kumtuma Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم):
رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١٢٩﴾
Rabb wetu, Wapelekee Rasuli miongoni mwao atakayewasomea Aayaat Zako na atakayewafunza Kitabu na Hikmah na atakayewatakasa. Hakika Wewe Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Baqarah (2:129)]
10-Mwombe Al-Hakiym Akupe Hikmah Na Akuunganishe Na Watu Wema:
Tambua, ee Mja wa Al-Hakiym: Hii ni du’aa ya Nabiy Ibraahiym (عليه السلام):
رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿٨٣﴾
Rabb wangu! Nitunukie hukmah, na Unikutanishe na Swalihina. [Ash-Shu’araa (26:83)]
Na Allaah Mjuzi zaidi