As-Samiy’: Mwenye kusikia yote daima; Ambaye Usikivu Wake umeenea kila sauti, ya siri na ya dhahiri, na Anayesikia na kuitikia du’aa za Waja Wake.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara arobaini na tano (45), na hilo linaonyesha umuhimu wa Jina hili na Sifa hii tukufu. Mara nyingi limeambatana na Jina Al-Baswiyr au Al-‘Aliym. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ۖ يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾
Mwanzilishi wa mbingu na ardhi. Amekujaalieni kutokana na nafsi zenu mume na mke, na katika wanyama wa mifugo dume na jike. Anakusambazeni humo. Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:11)]
Na Anasema pia:
وَاللَّـهُ يَقْضِي بِالْحَقِّ ۖ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَقْضُونَ بِشَيْءٍ ۗ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿٢٠﴾
Na Allaah Anahukumu kwa haki. Na wale wanaowaomba badala Yake hawawezi kuhukumu chochote. Hakika Allaah Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Ghaafir (40:20)]
Na Anasema:
إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٥٨﴾
Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe. Na mtakapohukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Ni uzuri ulioje wa Anayokuwaidhini kwayo Allaah! Hakika Allaah daima Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [An-Nisaa (4:58)]
Maana Ya As-Samiy’:
Usikivu wa Allaah (سبحانه وتعالى) umeenea kila sauti, kwa lugha zote mbalimbali, na haja zote za watu; siri Kwake ni sawa na dhahiri, na mnong’ono ni sawa na sauti ya juu, na aliye mbali ni sawa na aliye karibu. Na Usikivu Wake uko kwa namna mbili:
Kwanza: Usikivu Wake wa sauti zote, za dhahiri na za siri, kwa ukamilifu wake; sauti hazichanganyiki Kwake hata zikizidi na kuwa za aina mbalimbali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
سَوَاءٌ مِّنكُم مَّنْ أَسَرَّ الْقَوْلَ وَمَن جَهَرَ بِهِ وَمَنْ هُوَ مُسْتَخْفٍ بِاللَّيْلِ وَسَارِبٌ بِالنَّهَارِ ﴿١٠﴾
Ni sawa (Kwake) mmoja wenu akisema maneno yake kwa siri au kwa sauti, na anayenyemelea usiku na anayetembea mchana kwa uhuru. [Ar-Ra’d (13:10)]
Pili: Kusikia kwa maana ya kuitikia du’aa za Waja Wake na kuwalipa, kama alivyosema Nabiy Ibraahiym (عليه السلام):
الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي وَهَبَ لِي عَلَى الْكِبَرِ إِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ ۚ إِنَّ رَبِّي لَسَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٩﴾
AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Amenitunukia juu ya umri mkubwa wangu Ismaa’iyl na Is-haaq. Hakika Rabb wangu bila shaka Ni Mwenye Kusikia duaa yangu. [Ibraahiym (14:39)]
Yaani: Mwenye kuitikia du’aa za Waja Wake. Na hii ndiyo maana ya kauli ya Imaam katika Swalaah:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِذَا قَالَ الإِمَامُ: سَمِعَ اللَّهُ لِمَنْ حَمِدَهُ، فَقُولُوا: اللَّهُمَّ رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ، فَإِنَّهُ مَنْ وَافَقَ قَوْلُهُ قَوْلَ الْمَلاَئِكَةِ غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Imaam anaposema:
سَمِعَ اللَّهُ لِمَنْ حَمِدَهُ
Allaah Anamsikia (Anamwitikia) anayemhimidi; basi semeni:
اللَّهُمَّ رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ
Yaa Allaah, Rabb wetu, Himdi ni Zako; kwani atakayeafikiana kauli yake na kauli ya Malaika, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Na Kusikia kwa Allaah kunakuja pia kwa makusudio mengine:
i-Kuonya na kutisha, kama Kauli Yake:
أَمْ يَحْسَبُونَ أَنَّا لَا نَسْمَعُ سِرَّهُمْ وَنَجْوَاهُم ۚ بَلَىٰ وَرُسُلُنَا لَدَيْهِمْ يَكْتُبُونَ﴿٨٠﴾
Au wanadhania kwamba Sisi Hatusikii siri zao na minong’ono yao? Bali ndio (Tunasikia!) Na Wajumbe Wetu wako kwao wanaandika. [Az-Zukhruf (43:80)]
Na Kauli Yake:
لَّقَدْ سَمِعَ اللَّـهُ قَوْلَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ فَقِيرٌ وَنَحْنُ أَغْنِيَاءُ ۘ سَنَكْتُبُ مَا قَالُوا وَقَتْلَهُمُ الْأَنبِيَاءَ بِغَيْرِ حَقٍّ وَنَقُولُ ذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴿١٨١﴾
Kwa yakini Allaah Ameisikia kauli ya wale (Mayahudi) waliosema: Hakika Allaah ni fakiri na sisi ni matajiri. Tutayaandika waliyoyasema na kuua kwao Manabii pasi na haki na Tutasema: Onjeni adhabu ya kuunguza! [Aal-‘Imraan (3:181)]
ii-Kunusuru na kuunga mkono, kama Kauli Yake kwa Nabiy Muwsaa na Haaruwn (عليهما السلام):
قَالَ لَا تَخَافَا ۖ إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ ﴿٤٦﴾
(Allaah) Akasema: Msikhofu. Hakika Mimi Niko pamoja nanyi, Nasikia na Naona. [Twaahaa (20:46)]
Yaani: Niko pamoja nanyi kwa Nusra Yangu, Msaada Wangu, Kusikia Kwangu na Kuona Kwangu; na Dhati Yake (سبحانه وتعالى) Iko juu ya ‘Arsh, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu.
iii-Kubainisha upana wa Usikivu Wake, kama Kauli Yake kuhusu mwanamke aliyekuja kumshitakia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) mumewe:
قَدْ سَمِعَ اللَّـهُ قَوْلَ الَّتِي تُجَادِلُكَ فِي زَوْجِهَا وَتَشْتَكِي إِلَى اللَّـهِ وَاللَّـهُ يَسْمَعُ تَحَاوُرَكُمَا ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ﴿١﴾
Allaah Amekwishasikia kauli ya yule mwanamke anayejadiliana nawe kuhusu mumewe, na anamshitakia Allaah, na Allaah Anayasikia majibizano yenu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Al-Mujaadalah (58:1)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, As-Samiy’:
1-Tahadhari Na Maneno Maovu, Kwani Allaah Anakusikia Popote Ulipo:
Tambua, ee Mja wa As-Samiy’, kwamba hakuna siri mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى); Anasikia hata minong’ono yako. Rejea Az-Zukhruf (43:80) juu.
2-Jiepushe Na Kusikiliza Yaliyoharamishwa:
Tambua, ee Mja wa As-Samiy’: Jiepushe na kusikiliza ghiybah (kusengenya), namiymah (kufitinisha), na yote yasiyomridhisha Allaah; kwani masikio yako yataulizwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾
Na wala usifuate usiyo na ilimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitaulizwa. [Al-Israa (17:36)]
Na yatashuhudia juu yako Siku ya Qiyaamah:
حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٢٠﴾ وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّـهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٢١﴾
Mpaka watakapoufikia, yatashuhudia dhidi yao masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. Na wataziambia ngozi zao: Mbona mnashuhudia dhidi yetu? Zitasema: Ametutamkisha Allaah Ambaye Ametamkisha kila kitu, Naye Ndiye Aliyekuumbeni mara ya kwanza, na Kwake mtarejeshwa. [Fusw-Swilat (41:20-21)]
3-Omba Du’aa Kwa Ikhlaasw, Kwa Siri Na Unyenyekevu:
Tambua, ee Mja wa As-Samiy’: Allaah Anasikia du’aa ya siri kama Anavyosikia ya dhahiri; basi mwombe kwa ikhlaasw na unyenyekevu, si kwa kujionyesha kwa watu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٥٥﴾
Muombeni Rabb wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye Hapendi wenye kupindukia mipaka. [Al-A’raaf (7:55)]
4-Mwombe Allaah Kwa Jina Lake As-Samiy’ Kama Walivyoomba Manabii:
Tambua, ee Mja wa As-Samiy’: Nabiy Ibraahiym na Ismaa’iyl (عليهما السلام) walipojenga Al-Ka’bah waliomba:
وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿١٢٧﴾
Na aliponyanyua Ibraahiym na Ismaa’iyl msingi wa Nyumba (Al-Ka’bah): Rabb wetu, Tutakabalie, hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah (2:127)]
5-Mwombe As-Samiy’ Akutakabalie Nadhiri Na Amali Zako:
Tambua, ee Mja wa As-Samiy’: Mke wa ‘Imraan, mama wa Maryam (عليها السلام), aliomba:
إِذْ قَالَتِ امْرَأَتُ عِمْرَانَ رَبِّ إِنِّي نَذَرْتُ لَكَ مَا فِي بَطْنِي مُحَرَّرًا فَتَقَبَّلْ مِنِّي ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٣٥﴾
Pale aliposema mke wa ‘Imraan: Rabb wangu! Hakika mimi nimeweka nadhiri Kwako kilichomo katika tumbo langu kuwa ni wakfu kukutumikia, basi Nitakabalie. Hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Aal-‘Imraan (3:35)]
6-Mwombe As-Samiy’ Kizazi Chema:
Tambua, ee Mja wa As-Samiy’: Nabiy Zakariyyaa (عليه السلام) aliomba:
هُنَالِكَ دَعَا زَكَرِيَّا رَبَّهُ ۖ قَالَ رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً ۖ إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٨﴾
Hapo hapo Zakariyyaa akamwomba Rabb wake, akasema: Rabb wangu! Nitunukie kutoka Kwako kizazi chema, hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia duaa yangu. [Aal-‘Imraan (3:38)]
7-Mhimidi Allaah Katika Swalaah Yako Kwa Yakini Kwamba Anakusikia:
Kumbuka, ee Mja wa As-Samiy’, kwamba kila unaposimama baada ya Rukuu, Allaah Anakusikia unapomhimidi; basi usiseme maneno hayo kwa mazoea tu.
Rejea Hadiyth ya “سَمِعَ اللَّهُ لِمَنْ حَمِدَهُ” juu; basi sema “اللَّهُمَّ رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ” kwa kuhudhurisha moyo, kwani Allaah Anamsikia anayemhimidi.
8-Jikinge Na Du’aa Isiyoitikiwa:
Omba du’aa, ee Mja wa As-Samiy’, ya kujikinga na du’aa isiyoitikiwa, na moyo usionyenyekea, na ilimu isiyonufaisha.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema:
عَنْ زَيْدِ بْنِ أَرْقَمَ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((... اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عِلْمٍ لاَ يَنْفَعُ، وَمِنْ قَلْبٍ لاَ يَخْشَعُ، وَمِنْ نَفْسٍ لاَ تَشْبَعُ، وَمِنْ دَعْوَةٍ لاَ يُسْتَجَابُ لَهَا))
Amesimulia Zayd bin Arqam (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema: “…
اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عِلْمٍ لاَ يَنْفَعُ، وَمِنْ قَلْبٍ لاَ يَخْشَعُ، وَمِنْ نَفْسٍ لاَ تَشْبَعُ، وَمِنْ دَعْوَةٍ لاَ يُسْتَجَابُ لَهَا
Yaa Allaah! Hakika mimi najikinga Kwako kutokana na ilimu isiyonufaisha, na moyo usionyenyekea, na nafsi isiyoshiba, na du’aa isiyoitikiwa.” [Muslim]
9-Jikinge Na Shari Ya Masikio Yako Na Viungo Vyako Vingine:
Omba, ee Mja wa As-Samiy’, du’aa ya kujikinga na shari ya masikio yako na viungo vyako vingine, kwani viungo hivyo vinaweza kukuingiza katika maasi.
عَنْ شَكَلِ بْنِ حُمَيْدٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قُلْتُ: يَا نَبِيَّ اللَّهِ، عَلِّمْنِي تَعَوُّذًا أَتَعَوَّذُ بِهِ. قَالَ: ((قُلِ: اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ سَمْعِي، وَمِنْ شَرِّ بَصَرِي، وَمِنْ شَرِّ لِسَانِي، وَمِنْ شَرِّ قَلْبِي، وَمِنْ شَرِّ مَنِيِّي))
Amesimulia Shakal bin Humayd (رضي الله عنه): Nilisema: Yaa Nabiyya-Allaah! Nifundishe kinga ya kujikinga nayo. Akasema: “Sema:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ سَمْعِي، وَمِنْ شَرِّ بَصَرِي، وَمِنْ شَرِّ لِسَانِي، وَمِنْ شَرِّ قَلْبِي، وَمِنْ شَرِّ مَنِيِّي
Yaa Allaah! Hakika mimi najikinga Kwako kutokana na shari ya kusikia kwangu, na shari ya kuona kwangu, na shari ya ulimi wangu, na shari ya moyo wangu, na shari ya manii yangu.” [Abuu Daawuwd (1551), At-Tirmidhiy (3492), An-Nasaaiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
10-Mdhukuru As-Samiy’ Kila Asubuhi Na Jioni Upate Hifadhi Kutokana Na Kila Shari:
Dumisha dhikr hii asubuhi na jioni, ukiamini kwamba As-Samiy’ Anakusikia na Atakuhifadhi.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبَانَ بْنِ عُثْمَانَ قَالَ: سَمِعْتُ عُثْمَانَ بْنَ عَفَّانَ (رضي الله عنه) يَقُولُ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَا مِنْ عَبْدٍ يَقُولُ فِي صَبَاحِ كُلِّ يَوْمٍ وَمَسَاءِ كُلِّ لَيْلَةٍ: بِسْمِ اللَّهِ الَّذِي لاَ يَضُرُّ مَعَ اسْمِهِ شَيْءٌ فِي الأَرْضِ وَلاَ فِي السَّمَاءِ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ، ثَلاَثَ مَرَّاتٍ، فَيَضُرَّهُ شَيْءٌ))
Amesimulia Abaan bin ‘Uthmaan: Nilimsikia ‘Uthmaan bin ‘Affaan (رضي الله عنه) akisema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna mja yeyote anayesema asubuhi ya kila siku na jioni ya kila usiku:
بِسْمِ اللَّهِ الَّذِي لاَ يَضُرُّ مَعَ اسْمِهِ شَيْءٌ فِي الأَرْضِ وَلاَ فِي السَّمَاءِ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ
Kwa Jina la Allaah Ambaye pamoja na Jina Lake hakidhuru kitu chochote ardhini wala mbinguni, Naye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote; mara tatu, kisha kitu chochote kikamdhuru.” [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy (3388) na amesema: Hasan Swahiyh Ghariyb, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan Swahiyh katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
Na Allaah Mjuzi zaidi