Al-Baswiyr: Mwenye kuona yote; Ambaye Kuona Kwake kumezunguka kila kinachoonekana, kidogo na kikubwa, cha dhahiri na cha siri.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara arobaini na mbili (42), na mara nyingi limeambatana na Jina As-Samiy’. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾
Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku Mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumebariki pembezoni mwake, ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (Ishara) Zetu (kubwa mno). Hakika Yeye (Allaah) Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Al-Israa (17:1)]
Na Anasema pia:
وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ هُوَ الْحَقُّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِعِبَادِهِ لَخَبِيرٌ بَصِيرٌ ﴿٣١﴾
Na yale ambayo Tumekufunulia Wahy ya Kitabu, ndio haki yenye kusadikisha yale yaliyoko kabla yake. Hakika Allaah kwa Waja Wake bila shaka Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri, Mwenye Kuona yote. [Faatwir (35:31)]
Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amesema:
الْبَصِيرُ: الَّذِي يُبْصِرُ كُلَّ شَيْءٍ وَإِنْ دَقَّ وَصَغُرَ، فَيُبْصِرُ دَبِيبَ النَّمْلَةِ السَّوْدَاءِ فِي اللَّيْلَةِ الظَّلْمَاءِ عَلَى الصَّخْرَةِ الصَّمَّاءِ، وَيُبْصِرُ مَا تَحْتَ الْأَرَضِينَ السَّبْعِ كَمَا يُبْصِرُ مَا فَوْقَ السَّمَوَاتِ السَّبْعِ، وَأَيْضًا سَمِيعٌ بَصِيرٌ بِمَنْ يَسْتَحِقُّ الْجَزَاءَ بِحَسَبِ حِكْمَتِهِ
“Al-Baswiyr ni Yule Anayeona kila kitu hata kikiwa chembamba na kidogo mno; Anaona mwendo wa chungu mweusi katika usiku wa giza juu ya jabali gumu; na Anaona yaliyo chini ya ardhi saba kama Anavyoona yaliyo juu ya mbingu saba. Na pia (Yeye) Ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona kwa kumjua anayestahiki malipo kwa mujibu wa Hikmah Yake.”1
Maana Ya Al-Baswiyr:
1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ana Sifa ya Kuona ya kweli, inayolingana na Utukufu Wake; hatuifananishi na kuona kwa viumbe, wala hatuikanushi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ۖ يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾
Mwanzilishi wa mbingu na ardhi. Amekujaalieni kutokana na nafsi zenu mume na mke, na katika wanyama wa mifugo dume na jike. Anakusambazeni humo. Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:11)]
2-Kuona Kwake kumezunguka viumbe vyote, hata ndege angani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَى الطَّيْرِ فَوْقَهُمْ صَافَّاتٍ وَيَقْبِضْنَ ۚ مَا يُمْسِكُهُنَّ إِلَّا الرَّحْمَـٰنُ ۚ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ بَصِيرٌ﴿١٩﴾
Je, hawawaoni ndege juu yao, wakiwa wanakunjua na kukunja (mbawa)! Hakuna anayewashikilia isipokuwa Ar-Rahmaan. Hakika Yeye Ni Mwenye Kuona kila kitu. [Al-Mulk (67:19)]
3-Anaona kila tendo la Waja Wake popote walipo, Naye Yuko juu ya ‘Arsh, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu. Rejea Al-Hadiyd (57:4): “…Na Allaah Ni Mwenye Kuona yote myatendayo.”
هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٤﴾
Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arsh. Anajua yale yanayoingia ardhini, na yale yatokayo humo, na yale yanayoteremka kutoka mbinguni, na yale yanayopanda humo. Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah Ni Mwenye Kuona yote myatendayo. [Al-Hadiyd (57:4)]
4-Anaona viumbe vyote, lakini macho ya viumbe hayamzunguki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٠٣﴾
Macho hayamzunguki bali Yeye Anayazunguka macho yote, Naye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-An’aam (6:103)]
5-Ni Mwenye kuwaona Waja Wake kwa ujuzi wa hali zao; Anajua anayestahiki kupewa na anayestahiki kunyimwa, na Anawapa kwa mujibu wa Hikmah Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ بَسَطَ اللَّـهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ وَلَـٰكِن يُنَزِّلُ بِقَدَرٍ مَّا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ بِعِبَادِهِ خَبِيرٌ بَصِيرٌ﴿٢٧﴾
Na lau kama Allaah Angelikunjua rizki kwa Waja Wake, basi wangeruka mipaka katika ardhi. Lakini Anateremsha kwa kadiri ya Akitakacho. Hakika Yeye kwa Waja Wake Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:27)]
Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwaambia Swahaba walipopaza sauti zao katika dhikr:
عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: كُنَّا مَعَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِي سَفَرٍ، فَكُنَّا إِذَا عَلَوْنَا كَبَّرْنَا، فَقَالَ: ((أَيُّهَا النَّاسُ ارْبَعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ، فَإِنَّكُمْ لاَ تَدْعُونَ أَصَمَّ وَلاَ غَائِبًا، وَلَكِنْ تَدْعُونَ سَمِيعًا بَصِيرًا))
Amesimulia Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Tulikuwa pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) safarini, na tulikuwa tunapopanda mahali pa juu tunapiga Takbiyr (kwa sauti kubwa). Akasema: “Enyi watu! Zihurumieni nafsi zenu (msipaze sauti kupita kiasi); kwani hakika hamumwombi kiziwi wala asiyekuwepo, bali mnamwomba Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Baswiyr:
1-Mwabudu Allaah Kana Kwamba Unamwona, Kwani Yeye Anakuona:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Baswiyr, kwamba daraja ya juu kabisa ya ‘ibaadah ni ihsaan; nayo ni kumwabudu Allaah kwa hisia kwamba Yeye Anakuona daima.
عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) فِي حَدِيثِ جِبْرِيلَ، قَالَ: فَأَخْبِرْنِي عَنِ الإِحْسَانِ. قَالَ: ((أَنْ تَعْبُدَ اللَّهَ كَأَنَّكَ تَرَاهُ، فَإِنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فَإِنَّهُ يَرَاكَ))
Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) katika Hadiyth ya Jibriyl (عليه السلام): Akasema: Nijulishe kuhusu ihsaan. Akasema: “Ni umwabudu Allaah kana kwamba unamwona; na ikiwa wewe humwoni, basi hakika Yeye Anakuona.” [Muslim]
2-Kumbuka Kwamba Al-Baswiyr Anakuona Unaposimama Kuswali Na Unapokuwa Pamoja Na Wanaosujudu:
Tambua kwamba Al-Baswiyr Anakuona katika kila hali ya ‘ibaadah yako; basi ipambe na uifanye kwa ukamilifu.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ ﴿٢١٧﴾ الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ ﴿٢١٨﴾ وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ ﴿٢١٩﴾ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٢٢٠﴾
Na tawakali kwa Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu. Ambaye Anakuona wakati unaposimama. Na mageuko yako katika wenye kusujudu. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Ash-Shu’araa (26:217-220)]
3-Je, Hajui Kwamba Allaah Anaona?
Tambua, ee Mja wa Al-Baswiyr: Kila unapokusudia maasi, jiulize swali hili. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَلَمْ يَعْلَم بِأَنَّ اللَّـهَ يَرَىٰ ﴿١٤﴾
Je, hajui kwamba hakika Allaah Anaona? [Al-‘Alaq (96:14)]
4-Inamisha Macho Yako Na Yaliyoharamishwa:
Tahadhari na kuyaachia macho yako yaangalie yaliyoharamishwa, kwani Al-Baswiyr Anaona kila mtazamo.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٣٠﴾
Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao. Hivyo ni utakaso zaidi kwao. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale wayatendayo. [An-Nuwr (24:30)]
5-Macho Yako Yataulizwa, Basi Yatumie Katika Twaa’ah:
Kumbuka, ee Mja wa Al-Baswiyr, kwamba macho yako ni amana, na utaulizwa juu yake Siku ya Qiyaamah.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾
Na wala usifuate usiyo na ilimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitaulizwa. [Al-Israa (17:36)]
6-Tumia Macho Yako Kutafakari Viumbe Vya Al-Baswiyr:
Tafakari viumbe vya Al-Baswiyr vinavyokuzunguka, kwani kila kimoja ni dalili ya Ukubwa Wake.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَفَلَمْ يَنظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ﴿٦﴾
Je, hawatazami mbingu juu yao, vipi Tumezijenga na Tumezipamba, na wala hazina mipasuko yoyote! [Qaaf (50:6)]
7-Usiwe Kipofu Wa Moyo:
Tambua, ee Mja wa Al-Baswiyr: Upofu wa kweli si wa macho, bali ni wa moyo usiozingatia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَتَكُونَ لَهُمْ قُلُوبٌ يَعْقِلُونَ بِهَا أَوْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا ۖ فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾
Je, basi hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo za kuzingatia au masikio ya kusikilizia? Kwani hakika hayapofuki macho, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani. [Al-Hajj (22:46)]
8-Vuta Subira, Kwani Uko Machoni Mwa Rabb Wako:
Muumini anayejua kwamba Al-Baswiyr Anaona dhiki yake na maudhi anayofanyiwa, hupata faraja na utulivu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا ۖ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ حِينَ تَقُومُ ﴿٤٨﴾
Na vuta subira kwa hukumu ya Rabb wako, kwani hakika wewe uko chini ya Macho Yetu. Na Sabbih pamoja na kumhimidi Rabb wako, wakati unapoinuka (usiku). [Atw-Twuur (52:48)]
9-Usipaze Sauti Kupita Kiasi Katika Du’aa Na Dhikr:
Tahadhari, ee Mja wa Al-Baswiyr, na kupaza sauti kupita kiasi katika du’aa na dhikr, kwani unamwomba Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.
Rejea Hadiyth ya Abuu Muwsaa (رضي الله عنه) juu: “hamumwombi kiziwi wala asiyekuwepo, bali mnamwomba Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.”
10-Mwombe Allaah Akupe Afya Ya Macho Yako:
Omba du’aa ili Al-Baswiyr Akudumishie afya ya macho yako na viungo vyako vyote.
عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ أَبِي بَكْرَةَ أَنَّهُ قَالَ لأَبِيهِ: يَا أَبَتِ إِنِّي أَسْمَعُكَ تَدْعُو كُلَّ غَدَاةٍ: ((اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي بَدَنِي، اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي سَمْعِي، اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي بَصَرِي، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ)) تُعِيدُهَا ثَلاَثًا حِينَ تُصْبِحُ وَثَلاَثًا حِينَ تُمْسِي، فَقَالَ: إِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَدْعُو بِهِنَّ، فَأَنَا أُحِبُّ أَنْ أَسْتَنَّ بِسُنَّتِهِ
Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Abiy Bakrah kwamba alimwambia baba yake: Yaa baba yangu! Hakika mimi nakusikia ukiomba kila asubuhi:
اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي بَدَنِي، اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي سَمْعِي، اللَّهُمَّ عَافِنِي فِي بَصَرِي، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ
Yaa Allaah! Nipe afya katika mwili wangu. Yaa Allaah! Nipe afya katika kusikia kwangu. Yaa Allaah! Nipe afya katika kuona kwangu. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe. Unaikariri mara tatu unapoamka asubuhi na mara tatu unapoingia jioni. Akasema: Hakika mimi nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiomba kwa maneno hayo, nami napenda kufuata Sunnah yake. [Abuu Daawuwd (5090); Imaam Al-Albaaniy amesema isnaad yake ni Hasan katika Swahiyh Abiy Daawuwd (5090), na ameipa daraja ya Dhwa’iyf katika Dhwa’iyf Al-Jaami’ (1210)]
Na Allaah Mjuzi zaidi
- 1Imaam As-Sa’diy (رحمه الله), Tafsiyr Asmaa Allaah Al-Husnaa; imenukuliwa na Kalemtayeb katika maelezo ya Jina Al-Baswiyr.