Al-‘Aliym: Mjuzi wa yote; Ambaye Ujuzi Wake umekizunguka kila kitu, cha dhahiri na cha siri, kilichopita, kilichopo na kitakachokuja.
Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan zaidi ya mara mia na hamsini (150), na mara nyingi limeambatana na Majina Al-Hakiym, As-Samiy’ na Al-Khabiyr. Malaika walisema:
قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٣٢﴾
Wakasema: Utakasifu ni Wako! Hatuna ilimu isipokuwa Uliyotufunza, hakika Wewe Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Baqarah (2:32)]
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ وَمِنَ الْأَرْضِ مِثْلَهُنَّ يَتَنَزَّلُ الْأَمْرُ بَيْنَهُنَّ لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا﴿١٢﴾
Allaah Ni Yule Aliyeumba mbingu saba na katika ardhi mfano wa hizo, inateremka amri baina yao ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu Ni Muweza, na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa Ujuzi (Wake). [Atw-Twalaaq (65:12)]
Maana Ya Al-‘Aliym:
1-Ujuzi wa Allaah (سبحانه وتعالى) umekizunguka kila kitu; hakuna jani linaloanguka isipokuwa Analijua. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٥٩﴾
Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghaibu, hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Anajua yale yote yaliyomo barani na baharini. Na halianguki jani lolote ila Hulijua, wala punje katika viza vya ardhi, wala kinyevu na kikavu isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha wazi. [Al-An’aam (6:59)]
2-Hakifichikani Kwake kitu, hata kikiwa kidogo kama chembe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَأْتِينَا السَّاعَةُ ۖ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتَأْتِيَنَّكُمْ عَالِمِ الْغَيْبِ ۖ لَا يَعْزُبُ عَنْهُ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَلَا أَصْغَرُ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرُ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٣﴾
Na wale waliokufuru wakasema: Saa haitotufikia! Sema: Sivyo hivyo! Naapa kwa Rabb wangu! Bila shaka itakufikieni, Mjuzi wa ghaibu. Hakuna kinachofichika Kwake hata chenye uzito wa chembe (kama atomu) mbinguni wala ardhini, wala kidogo zaidi kuliko hicho, wala kikubwa zaidi isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha. [Saba-a (34:3)]
Na Anasema pia:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَخْفَىٰ عَلَيْهِ شَيْءٌ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ ﴿٥﴾
Hakika Allaah Hakifichiki Kwake chochote katika ardhi wala katika mbingu. [Aal-‘Imraan (3:5)]
3-Anajua siri na yaliyofichikana zaidi ya siri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِن تَجْهَرْ بِالْقَوْلِ فَإِنَّهُ يَعْلَمُ السِّرَّ وَأَخْفَى ﴿٧﴾
Na ukinena kwa jahara, basi hakika Yeye Anajua siri na yanayofichika zaidi ya siri. [Twaahaa (20:7)]
4-Anajua yaliyomo ndani ya vifua, kwa sababu Yeye Ndiye Aliyeviumba. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَسِرُّوا قَوْلَكُمْ أَوِ اجْهَرُوا بِهِ ۖ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴿١٣﴾ أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ﴿١٤﴾
Na fanyeni siri kauli zenu, au zidhihirisheni, hakika Yeye Ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. Kwani Hajui Yule Aliyeumba! Na hali Yeye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri! [Al-Mulk (67:13-14)]
5-Ujuzi wa ghaibu ni Wake Peke Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾
Hakika Allaah Ana ujuzi wa Saa (Qiyaamah), na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika matumbo ya uzazi. Na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Khabari za dhahiri na siri. [Luqmaan (31:34)]
Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنِ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَفَاتِحُ الْغَيْبِ خَمْسٌ لاَ يَعْلَمُهَا إِلاَّ اللَّهُ: لاَ يَعْلَمُ مَا فِي غَدٍ إِلاَّ اللَّهُ، وَلاَ يَعْلَمُ مَا تَغِيضُ الأَرْحَامُ إِلاَّ اللَّهُ، وَلاَ يَعْلَمُ مَتَى يَأْتِي الْمَطَرُ أَحَدٌ إِلاَّ اللَّهُ، وَلاَ تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ، وَلاَ يَعْلَمُ مَتَى تَقُومُ السَّاعَةُ إِلاَّ اللَّهُ))
Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Funguo za ghaibu ni tano, hakuna azijuaye isipokuwa Allaah: Hakuna ajuaye yatakayotokea kesho isipokuwa Allaah; na hakuna ajuaye matumbo ya uzazi yanavyopunguza isipokuwa Allaah; na hakuna ajuaye lini mvua itakuja isipokuwa Allaah; na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani; na hakuna ajuaye lini Saa (Qiyaamah) itasimama isipokuwa Allaah.” [Al-Bukhaariy]
6-Viumbe hawaizunguki ilimu Yake isipokuwa kwa kiasi Anachokitaka; rejea Aayatul-Kursiy: “…wala hawaizunguki chochote katika ilimu Yake isipokuwa kwa Alitakalo.” [Al-Baqarah (2:255)]
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-‘Aliym:
1-Mche Al-‘Aliym Katika Siri Yako Na Dhahiri Yako:
Tambua, ee Mja wa Al-‘Aliym: Allaah Yuko pamoja nawe kwa Ujuzi Wake, Naye Yuko juu ya ‘Arsh, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُسِرُّونَ وَمَا تُعْلِنُونَ ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴿٤﴾
Anajua yale yaliyomo mbinguni na ardhini, na Anayajua yale mnayofanya siri na mnayoyatangaza. Na Allaah Ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. [At-Taghaabun (64:4)]
2-Nyenyekea Kwa Ilimu Yako, Kwani Uliyopewa Ni Kidogo:
Tahadhari na kujiona kwa ilimu uliyonayo, kwani ilimu ya viumbe wote ni kidogo mno ukilinganisha na Ujuzi wa Al-‘Aliym.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾
Na wanakuuliza kuhusu Ruwh (roho). Sema: Roho ni katika Jambo la Rabb wangu. Na hamkupewa ujuzi isipokuwa kidogo tu. [Al-Israa (17:85)]
3-Tafuta Ilimu Yenye Manufaa, Kwani Ni Njia Ya Kwenda Jannah:
Tambua, ee Mja wa Al-‘Aliym, kwamba kutafuta ilimu ya Dini ni miongoni mwa njia fupi kabisa za kufikia Jannah.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... وَمَنْ سَلَكَ طَرِيقًا يَلْتَمِسُ فِيهِ عِلْمًا سَهَّلَ اللَّهُ لَهُ بِهِ طَرِيقًا إِلَى الْجَنَّةِ ...))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “… Na atakayeshika njia akitafuta ilimu ndani yake, Allaah Atamsahilishia kwayo njia ya kwenda Jannah …” [Muslim]
4-Ilimu Ya Kweli Huzaa Khofu Ya Allaah:
Kumbuka kwamba kipimo cha ilimu ya kweli ni khofu ya Al-‘Aliym inayozaliwa moyoni mwa mwenye nayo.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمِنَ النَّاسِ وَالدَّوَابِّ وَالْأَنْعَامِ مُخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ كَذَٰلِكَ ۗ إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ ﴿٢٨﴾
Na katika watu, na viumbe wanaotembea, na wanyama wa mifugo, rangi zao vile vile zinatofautiana. Hakika wanaomkhofu Allaah katika Waja Wake ni ‘Ulamaa. Hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kughufuria. [Faatwir (35:28)]
5-Usiseme Juu Ya Allaah Bila Ilimu:
Tambua, ee Mja wa Al-‘Aliym: Kusema juu ya Allaah bila ilimu ni miongoni mwa mambo makubwa Aliyoyaharamisha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٣٣﴾
Sema: Hakika Rabb wangu Ameharamisha machafu ya wazi na ya siri, na dhambi, na baghi (ukandamizaji) bila ya haki, na kumshirikisha Allaah kwa ambayo Hakuyateremshia mamlaka, na kusema juu ya Allaah yale ambayo hamyajui. [Al-A’raaf (7:33)]
6-Usiwaendee Makuhani Na Wapiga Ramli Kutafuta Ghaibu:
Ghaibu ni ya Al-‘Aliym Pekee; anayewaendea wanaodai kuijua amejihatarisha. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ بَعْضِ أَزْوَاجِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ أَتَى عَرَّافًا فَسَأَلَهُ عَنْ شَيْءٍ لَمْ تُقْبَلْ لَهُ صَلاَةٌ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً))
Amesimulia mmoja wa wake wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayemwendea mpiga ramli akamuuliza kitu, haitakubaliwa Swalaah yake kwa usiku arubaini.” [Muslim]
7-Ridhika Na Qadar, Kwani Al-‘Aliym Anajua Kilicho Bora Kwako:
Tambua kwamba Al-‘Aliym Anajua kilicho bora kwako kuliko unavyojijua mwenyewe; basi ridhika na Anachokuchagulia.
Rejea Al-Baqarah (2:216): “…Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui.” Basi mwachie Allaah uchaguzi baada ya kuchukua sababu.
كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾
Mmeandikiwa sharia kupigana vita nako kunachukiza mno kwenu. Lakini asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni la kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah (2:216)]
8-Tulia Moyo, Kwani Al-‘Aliym Anajua Hali Yako Kabla Hujaeleza:
Tambua, ee Mja wa Al-‘Aliym: Anayejua kwamba Rabb wake Anajua dhiki yake, maradhi yake na haja zake, hupata utulivu na hamlalamikii mwingine isipokuwa Yeye.
9-Ifanyie Kazi Ilimu Yako:
Tambua kwamba ilimu isiyofanyiwa kazi ni hoja dhidi ya mwenye nayo; na Al-‘Aliym Amewakemea wanaosema wasiyoyatenda. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ﴿٢﴾ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ﴿٣﴾
Enyi walioamini! Kwa nini mnasema yale msiyoyafanya? Ni chukizo kubwa mno mbele ya Allaah kwamba mnasema yale msiyoyafanya. [Asw-Swaff (61:2-3)]
10-Mwombe Al-‘Aliym Akuzidishie Ilimu:
Tambua, ee Mja wa Al-‘Aliym: Allaah Alimwamrisha Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuomba kuzidishiwa ilimu:
فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۗ وَلَا تَعْجَلْ بِالْقُرْآنِ مِن قَبْلِ أَن يُقْضَىٰ إِلَيْكَ وَحْيُهُ ۖ وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا ﴿١١٤﴾
Basi Ametukuka Allaah kwa ‘Uluwa, Mfalme wa haki. Na wala usiiharakize Qur-aan kabla haikumalizwa kufunuliwa Wahy kwako. Na sema: Rabb wangu! Nizidishie ilimu. [Twaahaa (20:114)]
Na Allaah Mjuzi zaidi