Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah034 - Al-Qariyb

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 034 kati ya 103
Al-Qariyb — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Qariyb: Aliye karibu na Waja Wake kwa Ujuzi Wake, Kusikia Kwake na Kuona Kwake, na karibu na wanaomwomba kwa kuwaitikia; pamoja na kuwa Yuko juu ya ‘Arsh Yake.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan katika Aayaat kadhaa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza Waja Wangu kuhusu Mimi, basi (waambie) hakika Mimi Niko Karibu (kwa ujuzi). Naitikia duaa ya muombaji anaponiomba. Hivyo basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah (2:186)]

Na Kauli ya Nabiy Swaalih (عليه السلام):

وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۚ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ هُوَ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُّجِيبٌ﴿٦١﴾

Na kwa Thamuwd (Tulimpeleka) ndugu yao Swaalih. Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Yeye Ndiye Aliyekuanzisheni kutokana na ardhi, na Akakufanyieni makazi humo, basi mwombeni maghfirah, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu Yuko Karibu, Mwenye Kuitikia. [Huwd (11:61)]

Na Anasema pia:

قُلْ إِن ضَلَلْتُ فَإِنَّمَا أَضِلُّ عَلَىٰ نَفْسِي ۖ وَإِنِ اهْتَدَيْتُ فَبِمَا يُوحِي إِلَيَّ رَبِّي ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ قَرِيبٌ ﴿٥٠﴾

Sema: Ikiwa nimepotoka, basi hakika nimepotoka kwa khasara ya nafsi yangu, na ikiwa nimehidika, basi ni kwa yale Aliyonifunulia Wahy Rabb wangu. Hakika Yeye Ni Mwenye Kusikia yote, Yu Karibu. [Saba-a (34:50)]

Maana Ya Al-Qariyb:

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Yuko karibu na Waja Wake wote kwa Ujuzi Wake, Kusikia Kwake, Kuona Kwake na Uwezo Wake; na Dhati Yake (سبحانه وتعالى) Iko juu ya mbingu, juu ya ‘Arsh, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu. Na hivi ndivyo Tarjama ya Alhidaaya ilivyobainisha katika Al-Baqarah (2:186): “hakika Mimi Niko Karibu (kwa ujuzi)”.

2-Na Yuko karibu kwa namna maalumu na wanaomwomba na wanaomwabudu, kwa kuwaitikia, kuwasaidia na kuwaongoza. Na mahali ambapo mja huwa karibu zaidi na Rabb wake ni katika Sujuud. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((أَقْرَبُ مَا يَكُونُ الْعَبْدُ مِنْ رَبِّهِ وَهُوَ سَاجِدٌ، فَأَكْثِرُوا الدُّعَاءَ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mja huwa karibu zaidi na Rabb wake anapokuwa amesujudu; basi kithirisheni du’aa (katika Sujuud).” [Muslim]

3-Na katika ukaribu Wake ni kwamba Anasikia hata mnong’ono, wala hahitaji mja kupaza sauti. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: كُنَّا مَعَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِي سَفَرٍ، فَجَعَلَ النَّاسُ يَجْهَرُونَ بِالتَّكْبِيرِ، فَقَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((أَيُّهَا النَّاسُ ارْبَعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ، إِنَّكُمْ لَيْسَ تَدْعُونَ أَصَمَّ وَلاَ غَائِبًا، إِنَّكُمْ تَدْعُونَ سَمِيعًا قَرِيبًا، وَهُوَ مَعَكُمْ))

Amesimulia Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Tulikuwa pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) safarini, watu wakaanza kupaza sauti kwa Takbiyr. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Enyi watu! Zihurumieni nafsi zenu; hakika hamumwombi kiziwi wala asiyekuwepo; hakika mnamwomba Mwenye kusikia yote, Aliye karibu, Naye Yu pamoja nanyi (kwa Ujuzi Wake).” [Muslim]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Qariyb:

1-Mwombe Allaah Moja Kwa Moja Bila Mwombezi Wa Kiumbe:

Tambua, ee Mja wa Al-Qariyb: Kwa kuwa Allaah Yuko karibu na Anaitikia, Muumini humwomba Yeye moja kwa moja. Ama washirikina walidai kwamba wanawaabudu wengine ili wawakurubishe kwa Allaah:

أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ ۚ وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ ﴿٣﴾

Tanabahi! Ni ya Allaah Pekee Dini iliyotakasika. Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi (wakisema): Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha karibu kabisa kwa Allaah. Hakika Allaah Atahukumu baina yao katika yale wanayokhitilafiana nayo. Hakika Allaah Hamhidi aliye mkadhibishaji, kafiri mkubwa. [Az-Zumar (39:3)]

2-Mwombe Kwa Yakini Kwamba Atakuitikia:

Kumbuka kwamba Al-Qariyb Ameahidi kuitikia, na Ahadi Yake ni kweli; basi omba kwa yakini.

Rejea Al-Baqarah (2:186) juu: “…Naitikia duaa ya muombaji anaponiomba.” Basi omba kwa yakini, wala usikate tamaa.

3-Rudi Kwake Kwa Istighfaar Na Tawbah:

Tambua, ee Mja wa Al-Qariyb: Nabiy Swaalih (عليه السلام) aliwaamrisha kaumu yake kuomba maghfirah na kutubia, akawabainishia kwamba Rabb wao Yuko karibu na Anaitikia (rejea Huwd (11:61) juu).

4-Kithirisha Du’aa Katika Sujuud:

Tambua, ee Mja wa Al-Qariyb, kwamba Sujuud ndio hali ambayo mja huwa karibu zaidi na Rabb wake; basi itumie kwa du’aa nyingi.

Rejea Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) juu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

كَلَّا لَا تُطِعْهُ وَاسْجُدْ وَاقْتَرِب ۩﴿١٩﴾

Laa hasha! Usimtii. Na sujudu na kurubia (kwa Allaah). [Al-‘Alaq (96:19)]

5-Jikurubishe Kwa Allaah Kwa Faradhi Kisha Kwa Nawaafil:

Tambua, ee Mja wa Al-Qariyb: Katika Hadiyth Al-Qudsiy:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((يَقُولُ اللَّهُ تَعَالَى: أَنَا عِنْدَ ظَنِّ عَبْدِي بِي، وَأَنَا مَعَهُ إِذَا ذَكَرَنِي ... وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ بِشِبْرٍ تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ ذِرَاعًا، وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ ذِرَاعًا تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ بَاعًا، وَإِنْ أَتَانِي يَمْشِي أَتَيْتُهُ هَرْوَلَةً))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (تعالى) Anasema: Mimi Niko kwa dhana ya Mja Wangu juu Yangu, na Niko pamoja naye anaponidhukuru … Na akijikurubisha Kwangu shibiri, Najikurubisha kwake dhiraa; na akijikurubisha Kwangu dhiraa, Najikurubisha kwake pima; na akinijia kwa kutembea, Namjia kwa haraka.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

6-Mhusishe Al-Qariyb Na Dhana Njema:

Kumbuka kwamba Al-Qariyb Huamiliana na mja kwa kadiri ya dhana yake juu Yake; basi mdhanie kheri daima.

Rejea Hadiyth Al-Qudsiy juu: “Mimi Niko kwa dhana ya Mja Wangu juu Yangu.” Basi mdhanie Allaah kheri, na utarajie Rehma Yake na kuitikia Kwake.

7-Tumia Theluthi Ya Mwisho Ya Usiku Kwa Du’aa:

Tumia, ee Mja wa Al-Qariyb, theluthi ya mwisho ya usiku, wakati ambao Allaah Anawaita Waja Wake ili Awaitikie.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا، حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الآخِرُ، يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Rabb wetu (تبارك وتعالى) Huteremka kila usiku kwenye mbingu ya dunia inapobaki theluthi ya mwisho ya usiku, Anasema: Nani ananiomba Nimwitikie? Nani ananitaka kitu Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Ahlus-Sunnah wanauthibitisha Uteremkaji huu kama ulivyokuja, bila kuufananisha na uteremkaji wa viumbe, wala kuuliza namna yake.

8-Usipaze Sauti Kupita Kiasi, Na Mwombe Kwa Unyenyekevu Na Siri:

Tahadhari na kuomba kwa kelele na makeke; bali mwombe Al-Qariyb kwa unyenyekevu na kwa siri.

Rejea Hadiyth ya Abuu Muwsaa (رضي الله عنه) juu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٥٥﴾

Muombeni Rabb wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye Hapendi wenye kupindukia mipaka. [Al-A’raaf (7:55)]

9-Kumbuka Ukaribu Wa Malaika Wake Wakati Wa Kukata Roho:

Kumbuka saa ya kukata roho, ambapo Malaika wa Al-Qariyb watakuwa karibu nawe kuliko watu walio karibu nawe.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ ﴿٨٣﴾ وَأَنتُمْ حِينَئِذٍ تَنظُرُونَ ﴿٨٤﴾ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ ﴿٨٥﴾

Basi mbona roho ifikapo kooni. Nanyi wakati huo mnatazama. Nasi Tuko karibu naye zaidi kuliko nyinyi, lakini hamuoni. [Al-Waaqi’ah (56:83-85)]

10-Muombe Al-Qariyb Katika Dhiki Kama Alivyoomba Nabiy Yuwnus (عليه السلام):

Omba du’aa ya Nabiy Yuwnus (عليه السلام) unapofikwa na dhiki, kwani Al-Qariyb Alimwitikia na kumwokoa.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾ فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾

Na Dhan-Nuwn (Yuwnus), alipoondoka akiwa ameghadhibika, akadhani kwamba Hatutamdhikisha. Akaita vizani kwamba: Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu. Basi Tukamuitikia, na Tukamuokoa kutokana na ghamu. Na hivyo ndivyo Tuwaokoavyo Waumini. [Al-Anbiyaa (21:87-88)]

Na Allaah Mjuzi zaidi