Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah036 - Al-'Afuww

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 036 kati ya 103
Al-'Afuww — Majina Mazuri ya Allaah

Al-‘Afuww: Mwingi wa kusamehe; Anayefuta madhambi ya Waja Wake na kuyaondoa athari zake, wala Hawachukulii kwayo.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara tano, mara nyingi pamoja na Jina Al-Ghafuwr, na mara moja pamoja na Jina Al-Qadiyr. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِن تُبْدُوا خَيْرًا أَوْ تُخْفُوهُ أَوْ تَعْفُوا عَن سُوءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَفُوًّا قَدِيرًا ﴿١٤٩﴾

Mkidhihirisha kheri au mkiificha au mkisamehe uovu, basi hakika Allaah daima Ni Mwingi wa Kusamehe, Muweza wa yote. [An-Nisaa (4:149)]

Na Anasema pia:

ذَٰلِكَ وَمَنْ عَاقَبَ بِمِثْلِ مَا عُوقِبَ بِهِ ثُمَّ بُغِيَ عَلَيْهِ لَيَنصُرَنَّهُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَعَفُوٌّ غَفُورٌ ﴿٦٠﴾

Ndivyo hivyo, na yeyote anayejilipizia mfano wa ubaya aliofanyiwa, kisha akaja kufanyiwa baghi (kudhulumiwa) tena, bila shaka Allaah Atamnusuru. Hakika Allaah bila shaka Ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kughufuria. [Al-Hajj (22:60)]

Maana Ya Al-‘Afuww:

1-Al-‘Afuww ni Yule Anayefuta madhambi na kuyaondoa kabisa, kiasi kwamba mja hachukuliwi kwayo. Allaah Anapokea tawbah ya Waja Wake na Anasamehe maovu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ وَيَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ﴿٢٥﴾

Naye Ndiye Ambaye Anapokea tawbah kutoka kwa Waja Wake, na Anasamehe maovu, na Anayajua mnayoyafanya. [Ash-Shuwraa (42:25)]

2-Anasamehe mengi katika makosa ya Waja Wake bila hata ya kuwaadhibu kwayo duniani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ﴿٣٠﴾

Na msiba wowote unaokusibuni, basi ni kwa sababu ya yale iliyochuma mikono yenu, na Anasamehe mengi. [Ash-Shuwraa (42:30)]

3-Na katika ‘afw Yake ni kuwasamehe wanyonge walioshindwa kufanya Aliyoyaamrisha kwa sababu ya udhaifu wao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا ﴿٩٨﴾ فَأُولَـٰئِكَ عَسَى اللَّـهُ أَن يَعْفُوَ عَنْهُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَفُوًّا غَفُورًا ﴿٩٩﴾

Isipokuwa wale waliokandamizwa kati ya wanaume na wanawake na watoto ambao hawakuweza kupata hila yoyote wala hawawezi kuongoza njia. Basi hao bila shaka Allaah Atawasamehe. Na Allaah daima Ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kughufuria. [An-Nisaa (4:98-99)]

4-‘Afw Yake inatanguliwa na Uwezo Wake; Anasamehe hali ya kuwa Anaweza kuadhibu, na huo ndio ukamilifu wa ‘afw (rejea An-Nisaa (4:149) juu: “…basi hakika Allaah daima Ni Mwingi wa Kusamehe, Muweza wa yote”).

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-‘Afuww:

1-Usikate Tamaa Na ‘Afw Ya Allaah Hata Madhambi Yakiwa Mengi:

Tambua, ee Mja wa Al-‘Afuww, kwamba ‘afw ya Allaah ni kubwa kuliko madhambi yako; basi usikate tamaa na Rehma Yake.

Rejea Ash-Shuwraa (42:25) juu. Allaah Anapokea tawbah ya kweli, na Anayafuta madhambi kana kwamba hayakuwahi kuwepo.

2-Samehe Watu, Ili Allaah Akusamehe:

Tambua, ee Mja wa Al-‘Afuww: Aayah hii iliteremka kuhusu Abuu Bakr (رضي الله عنه) alipoapa kutomsaidia jamaa yake aliyeshiriki katika kumsingizia ‘Aaishah (رضي الله عنها):

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾

Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika Njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [An-Nuwr (24:22)]

3-Kusamehe Ni Sifa Ya Wenye Taqwa:

Kumbuka, ee Mja wa Al-‘Afuww, kwamba kusamehe waliokukosea ni miongoni mwa sifa za wenye taqwa wanaoandaliwa Jannah.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ﴿١٣٣﴾ الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣٤﴾

Na kimbilieni maghfirah kutoka kwa Rabb wenu, na Jannah upana wake ni wa mbingu na ardhi imeandaliwa kwa wenye taqwa. Ambao wanatoa (kwa ajili ya Allaah) katika hali ya wasaa na katika hali ya shida, na wanazuia ghadhabu, na wenye kusamehe watu. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. [Aal-‘Imraan (3:133-134)]

4-Kusamehe Kunakaribia Zaidi Taqwa:

Tambua, ee Mja wa Al-‘Afuww, kwamba kusamehe, hata katika mambo ya haki zako za mali, ni karibu zaidi na taqwa.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إِلَّا أَن يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَ الَّذِي بِيَدِهِ عُقْدَةُ النِّكَاحِ ۚ وَأَن تَعْفُوا أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۚ وَلَا تَنسَوُا الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٢٣٧﴾

Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha, isipokuwa wakisamehe au asamehe yule ambaye fungamano la ndoa liko mikononi mwake. Na kusamehe kuko karibu zaidi na taqwa. Na wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kuona myatendayo. [Al-Baqarah (2:237)]

5-Kusamehe Hakukudhalilishi, Bali Kunakuzidishia ‘Izzah:

Tahadhari, ee Mja wa Al-‘Afuww, na kudhani kwamba kusamehe ni udhaifu; bali ni utukufu unaozidishwa na Allaah.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَا نَقَصَتْ صَدَقَةٌ مِنْ مَالٍ، وَمَا زَادَ اللَّهُ عَبْدًا بِعَفْوٍ إِلاَّ عِزًّا، وَمَا تَوَاضَعَ أَحَدٌ لِلَّهِ إِلاَّ رَفَعَهُ اللَّهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Swadaqah haipunguzi mali; na Allaah Hamzidishii mja kwa kusamehe isipokuwa ‘izzah; na hakuna aliyenyenyekea kwa ajili ya Allaah isipokuwa Allaah Humnyanyua.” [Muslim]

6-Tambua Kwamba Misiba Mingi Ni Kwa Sababu Ya Madhambi, Na Allaah Anasamehe Mengi:

Kumbuka kwamba Al-‘Afuww Anasamehe mengi katika makosa yako bila kukuadhibu; basi mshukuru na ujirekebishe.

Rejea Ash-Shuwraa (42:30) juu. Basi misiba ikufanye urejee kwa Allaah kwa tawbah, na umshukuru kwa yale Aliyokusamehe bila kukuadhibu.

7-Samehe Ukiwa Na Uwezo Wa Kulipiza:

Tambua kwamba kusamehe kwa kweli ni kusamehe pale unapoweza kulipiza kisasi, kama Al-‘Afuww Anavyosamehe hali ya kuwa Yeye Ni Muweza (rejea An-Nisaa (4:149) juu). Na malipo ya anayesamehe na kusuluhisha yako kwa Allaah:

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا ۖ فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ﴿٤٠﴾

Na jazaa ya uovu ni uovu mfano wake. Lakini atakayesamehe na akajenga mahusiano mema na aliyemkosea, basi ujira wake uko kwa Allaah. Hakika Yeye Hapendi madhalimu. [Ash-Shuwraa (42:40)]

8-Ita Mwenye Kukukosea Kwa Kumsamehe Na Kupuuza:

Tambua kwamba Al-‘Afuww Alimwamrisha Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم):

خُذِ الْعَفْوَ وَأْمُرْ بِالْعُرْفِ وَأَعْرِضْ عَنِ الْجَاهِلِينَ ﴿١٩٩﴾

Shikamana na usamehevu, na amrisha mema na jiepushe na majahili. [Al-A’raaf (7:199)]

9-Mwombe Allaah ‘Afw Na ‘Aafiyah Asubuhi Na Jioni:

Omba du’aa, ee Mja wa Al-‘Afuww, kila asubuhi na jioni, Allaah Akupe ‘afw na ‘aafiyah katika Dini yako na dunia yako.

Rejea du’aa ya asubuhi na jioni katika 019-As-Salaam: “Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba msamaha na afya katika Dini yangu, dunia yangu, ahli zangu na mali yangu.”

10-Mwombe Al-‘Afuww Akusamehe Hasa Katika Laylatul-Qadr:

Tambua, ee Mja wa Al-‘Afuww: Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) alimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aseme nini akijua kuwa ni Laylatul-Qadr:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَرَأَيْتَ إِنْ عَلِمْتُ أَيُّ لَيْلَةٍ لَيْلَةُ الْقَدْرِ، مَا أَقُولُ فِيهَا؟ قَالَ: ((قُولِي: اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Nilisema: Yaa Rasula-Allaah! Unaonaje nikijua ni usiku upi ni Laylatul-Qadr, niseme nini ndani yake? Akasema: “Sema:

اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي

Yaa Allaah! Hakika Wewe Ni Mwingi wa Kusamehe, Unapenda kusamehe, basi Nisamehe.” [At-Tirmidhiy (3513) na amesema: Hasan Swahiyh, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

Na Allaah Mjuzi zaidi