Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah037 - Al-Ghafuwr

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 037 kati ya 103
Al-Ghafuwr — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Ghafuwr: Mwingi wa kughufuria; Anayesitiri madhambi ya Waja Wake na kuwaepusha na Adhabu Yake.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara tisini na moja (91), na mara nyingi limeambatana na Jina Ar-Rahiym, kama katika Kauli Yake:

نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٤٩﴾ وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ﴿٥٠﴾

Wajulishe Waja Wangu, kwamba: Hakika Mimi Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. Na kwamba Adhabu Yangu, ndiyo adhabu iumizayo. [Al-Hijr (15:49-50)]

Na Anasema pia, Akiwaita Waja Wake waliopindukia mipaka kwa madhambi:

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi Waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na Rehma ya Allaah, hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Az-Zumar (39:53)]

Maana Ya Al-Ghafuwr:

1-Neno ghafara lina maana ya kusitiri na kufunika. Al-Ghafuwr ni Yule Anayezisitiri dhambi za Waja Wake duniani, na Anawaepusha na Adhabu Yake Aakhirah.

2-Maghfirah Yake ni pana, inayokusanya madhambi yote kwa anayetubia, hata yakiwa makubwa. Rejea Az-Zumar (39:53) juu.

3-Anamghufuria anayemwomba maghfirah kwa ukweli baada ya kutenda ovu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَن يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّـهَ يَجِدِ اللَّـهَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿١١٠﴾

Na atakayetenda ovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akamwomba Allaah maghfirah, basi atamkuta Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [An-Nisaa (4:110)]

4-Katika Hadiyth Al-Qudsiy, Allaah (تبارك وتعالى) Amesema:

عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِيمَا رَوَى عَنِ اللَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى أَنَّهُ قَالَ: ((... يَا عِبَادِي، إِنَّكُمْ تُخْطِئُونَ بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ، وَأَنَا أَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا، فَاسْتَغْفِرُونِي أَغْفِرْ لَكُمْ ...))

Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesimulia kutoka kwa Allaah (تبارك وتعالى) kwamba Amesema: “… Enyi Waja Wangu! Hakika nyinyi mnakosea usiku na mchana, Nami Naghufuria madhambi yote; basi niombeni maghfirah, Nitakughufurieni …” [Muslim]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Ghafuwr:

1-Usikate Tamaa Na Maghfirah Ya Allaah:

Tambua, ee Mja wa Al-Ghafuwr: Hata madhambi yakiwa mengi vipi, mlango wa maghfirah uko wazi kwa anayetubia (rejea Az-Zumar (39:53) juu).

2-Ukitenda Kosa, Mkumbuke Allaah Na Uombe Maghfirah Mara Moja:

Kumbuka kwamba Muumini akikosea hakai na kosa lake, bali humkumbuka Al-Ghafuwr mara moja na kuomba maghfirah.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٣٥﴾ أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُم مَّغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿١٣٦﴾

Na ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah? Na hawaendelei katika waliyoyafanya na hali wanajua. Hao jazaa yao ni maghfirah kutoka kwa Rabb wao na Jannaat zipitazo chini yake mito, wadumu humo. Ni uzuri ulioje ujira wa watendaji (wema). [Aal-‘Imraan (3:135-136)]

3-Tambua Kwamba Allaah Anapenda Waja Wanaorejea Kwake Baada Ya Kukosea:

Tambua kwamba kukosea ni sehemu ya maumbile ya mwanaadam, lakini lililo muhimu ni kurejea kwa Al-Ghafuwr kila unapokosea.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَوْ لَمْ تُذْنِبُوا لَذَهَبَ اللَّهُ بِكُمْ، وَلَجَاءَ بِقَوْمٍ يُذْنِبُونَ فَيَسْتَغْفِرُونَ اللَّهَ فَيَغْفِرُ لَهُمْ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mkononi Mwake, lau msingetenda dhambi, Allaah Angekuondosheni, na Angeleta watu wanaotenda dhambi kisha wakamwomba Allaah maghfirah, Naye Akawaghufuria.” [Muslim]

4-Tawbah Ya Kweli Hubadilisha Maovu Kuwa Mema:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Ghafuwr, kwamba tawbah ya kweli haifuti madhambi tu, bali huyabadilisha kuwa mema.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda amali njema. Basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema. Na Allaah daima Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Al-Furqaan (25:70)]

5-Kuwa Kati Ya Matumaini Na Khofu:

Tambua kwamba Al-Ghafuwr Ameunganisha habari ya Maghfirah Yake na habari ya Adhabu Yake (rejea Al-Hijr (15:49-50) juu); basi usitegemee maghfirah ukaendelea na maasi, wala usikate tamaa na Rehma Yake.

6-Wasamehe Na Uwaghufurie Wanaokukosea:

Tambua kwamba anayewasamehe watu, Al-Ghafuwr Humghufuria; basi samehe upate maghfirah.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ مِنْ أَزْوَاجِكُمْ وَأَوْلَادِكُمْ عَدُوًّا لَّكُمْ فَاحْذَرُوهُمْ ۚ وَإِن تَعْفُوا وَتَصْفَحُوا وَتَغْفِرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٤﴾

Enyi walioamini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu ni maadui kwenu, basi tahadharini nao. Na mkisamehe na mkapuuza na mkayafutilia mbali, basi hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [At-Taghaabun (64:14)]

7-Kithirisha Istighfaar Kama Alivyokuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

Tafakari, ee Mja wa Al-Ghafuwr: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliyeghufuriwa madhambi yake yote alikuwa akiomba maghfirah zaidi ya mara sabini kwa siku; basi sisi tunastahiki zaidi.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((وَاللَّهِ إِنِّي لأَسْتَغْفِرُ اللَّهَ وَأَتُوبُ إِلَيْهِ فِي الْيَوْمِ أَكْثَرَ مِنْ سَبْعِينَ مَرَّةً))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Wa-Allaahi, hakika mimi namwomba Allaah maghfirah na natubia Kwake kwa siku zaidi ya mara sabini.” [Al-Bukhaariy]

8-Wasitiri Watu Kama Anavyokusitiri Al-Ghafuwr:

Tambua kwamba maghfirah ni kusitiri; basi usizitangaze aibu za ndugu zako, kwani Al-Ghafuwr Hukusitiri wewe mara nyingi. Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu wanaopenda maovu yaenee:

إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾

Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini, watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui. [An-Nuwr (24:19)]

9-Ongeza Mema, Kwani Mema Yanaondosha Maovu:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Ghafuwr, kuyafuatisha maovu yako kwa mema, kwani mema yanafuta maovu.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ﴿١١٤﴾

Na simamisha Swalaah katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku, hakika mema yanaondosha maovu. Haya ni ukumbusho kwa wanaokumbuka. [Huwd (11:114)]

10-Mwombe Al-Ghafuwr Kwa Du’aa Aliyomfundisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Abuu Bakr (رضي الله عنه):

Omba du’aa hii, ee Mja wa Al-Ghafuwr, katika Swalaah yako kabla ya salaam, ukikiri dhulma yako juu ya nafsi yako.

عَنْ أَبِي بَكْرٍ الصِّدِّيقِ (رضي الله عنه) أَنَّهُ قَالَ لِرَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): عَلِّمْنِي دُعَاءً أَدْعُو بِهِ فِي صَلاَتِي. قَالَ: ((قُلِ: اللَّهُمَّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي ظُلْمًا كَثِيرًا، وَلاَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلاَّ أَنْتَ، فَاغْفِرْ لِي مَغْفِرَةً مِنْ عِنْدِكَ، وَارْحَمْنِي، إِنَّكَ أَنْتَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ))

Amesimulia Abuu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه) kwamba alimwambia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Nifundishe du’aa niombe kwayo katika Swalaah yangu. Akasema: “Sema:

اللَّهُمَّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي ظُلْمًا كَثِيرًا، وَلاَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلاَّ أَنْتَ، فَاغْفِرْ لِي مَغْفِرَةً مِنْ عِنْدِكَ، وَارْحَمْنِي، إِنَّكَ أَنْتَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

Yaa Allaah! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu dhulma nyingi, na hakuna anayeghufuria madhambi isipokuwa Wewe; basi Nighufurie maghfirah kutoka Kwako, na Unirehemu; hakika Wewe Ndiye Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi