Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah038 - Al-Ghaffaar

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 038 kati ya 103
Al-Ghaffaar — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Ghaffaar: Mwingi mno wa kughufuria; Anayeghufuria madhambi ya Waja Wake mara baada ya mara, kila wanaporudi Kwake.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara tano, na mara nyingi limeambatana na Jina Al-‘Aziyz. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا الْعَزِيزُ الْغَفَّارُ ﴿٦٦﴾

Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kughufuria. [Swaad (38:66)]

Na Anasema pia:

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ ۖ يُكَوِّرُ اللَّيْلَ عَلَى النَّهَارِ وَيُكَوِّرُ النَّهَارَ عَلَى اللَّيْلِ ۖ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۗ أَلَا هُوَ الْعَزِيزُ الْغَفَّارُ ﴿٥﴾

Ameumba mbingu na ardhi kwa haki. Anaufunika usiku juu ya mchana, na Anafunika mchana juu ya usiku. Na Ametiisha jua na mwezi; kila kimoja kinakwenda mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Tanabahi! Yeye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kughufuria. [Az-Zumar (39:5)]

Maana Ya Al-Ghaffaar:

1-Al-Ghaffaar ni neno la kukithirisha; linaonyesha wingi wa maghfirah na kurudiwa kwake. Allaah Anaghufuria madhambi mengi, na Anaghufuria tena na tena kila mja anaporudi Kwake.

2-Maghfirah Yake ina masharti: tawbah, imaan, amali njema, na kuendelea katika uongofu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ ﴿٨٢﴾

Na hakika Mimi bila shaka Ni Mwingi mno wa Kughufuria kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema, tena akathibiti katika njia ya sawa. [Twaahaa (20:82)]

3-Na katika Hadiyth Al-Qudsiy inaonyeshwa jinsi Allaah Anavyomghufuria mja kila anaporudi baada ya kukosea:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِيمَا يَحْكِي عَنْ رَبِّهِ عَزَّ وَجَلَّ قَالَ: ((أَذْنَبَ عَبْدٌ ذَنْبًا فَقَالَ: اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي. فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَذْنَبَ عَبْدِي ذَنْبًا، فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ. ثُمَّ عَادَ فَأَذْنَبَ ... اعْمَلْ مَا شِئْتَ فَقَدْ غَفَرْتُ لَكَ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesimulia kutoka kwa Rabb wake (عزّ وجلّ): “Mja alitenda dhambi, akasema: Yaa Allaah! Nighufurie dhambi yangu. (Allaah) (تبارك وتعالى) Akasema: Mja Wangu ametenda dhambi, akajua kwamba ana Rabb Anayeghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa dhambi. Kisha akarudi akatenda dhambi … (mpaka Allaah Akasema): Fanya utakavyo (maadamu unatubia kila unapokosea), kwani Nimekughufuria.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

Maana ya “Fanya utakavyo” ni kwamba maadamu mja anatubia kwa ukweli kila anapotenda dhambi, Allaah Humghufuria; si ruhusa ya kuendelea na maasi.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Ghaffaar:

1-Omba Maghfirah, Kwani Istighfaar Huleta Mvua, Mali Na Watoto:

Tambua, ee Mja wa Al-Ghaffaar: Nabiy Nuwh (عليه السلام) aliwaambia kaumu yake:

فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا﴿١٠﴾ يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا﴿١١﴾ وَيُمْدِدْكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَل لَّكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَل لَّكُمْ أَنْهَارًا﴿١٢﴾

Nikasema: Ombeni maghfirah kwa Rabb wenu, hakika Yeye Ni Mwingi mno wa Kughufuria. Atakutumieni mvua tele ya kuendelea. Na Atakuongezeeni mali na wana, na Atakupeni mabustani na Atakupeni mito. [Nuwh (71:10-12)]

2-Usichoke Kurudi Kwa Al-Ghaffaar, Hata Ukikosea Mara Nyingi:

Tahadhari, ee Mja wa Al-Ghaffaar, na hila ya shaytwaan anayekuambia kwamba umerudia kosa mara nyingi mno kiasi kwamba hutaghufuriwa.

Rejea Hadiyth Al-Qudsiy juu. Shaytwaan hupenda mja akate tamaa baada ya kurudia kosa; lakini Al-Ghaffaar Humghufuria kila anaporudi kwa ukweli.

3-Tambua Kwamba Mkono Wa Allaah Umekunjuliwa Usiku Na Mchana Kupokea Tawbah:

Tambua, ee Mja wa Al-Ghaffaar, kwamba mlango wa tawbah uko wazi saa zote, usiku na mchana.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي مُوسَى (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ يَبْسُطُ يَدَهُ بِاللَّيْلِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ، وَيَبْسُطُ يَدَهُ بِالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيْلِ، حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا))

Amesimulia Abuu Muwsaa (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah (عزّ وجلّ) Hukunjua Mkono Wake usiku ili atubie aliyekosea mchana, na Hukunjua Mkono Wake mchana ili atubie aliyekosea usiku, mpaka jua lichomoze kutoka magharibi yake.” [Muslim]

4-Tubia Kabla Mlango Wa Tawbah Haujafungwa:

Tahadhari, ee Mja wa Al-Ghaffaar, na kuakhirisha tawbah, kwani mlango wake utafungwa siku moja.

Rejea Hadiyth ya Abuu Muwsaa (رضي الله عنه) juu; mlango wa tawbah uko wazi mpaka jua lichomoze kutoka magharibi, au mpaka roho ifike kooni. Basi usiakhirishe tawbah.

5-Walinganie Watu Kwa Al-‘Aziyz Al-Ghaffaar:

Tambua, ee Mja wa Al-Ghaffaar: Muumini wa ahli wa Fir’awn aliwalingania kaumu yake kwa Majina haya mawili:

تَدْعُونَنِي لِأَكْفُرَ بِاللَّـهِ وَأُشْرِكَ بِهِ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ وَأَنَا أَدْعُوكُمْ إِلَى الْعَزِيزِ الْغَفَّارِ﴿٤٢﴾

Mnaniita ili nimkufuru Allaah na nimshirikishe na yale nisiyokuwa na ilimu nayo, na hali mimi nakuiteni kwa Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kughufuria?! [Ghaafir (40:42)]

6-Omba Maghfirah Baada Ya Kila Swalaah:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Ghaffaar, kuomba maghfirah baada ya kila Swalaah kwa upungufu uliotokea ndani yake.

Rejea du’aa ya Thawbaan (رضي الله عنه) katika 019-As-Salaam: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anapomaliza Swalaah yake huomba maghfirah mara tatu. Swalaah ni ‘ibaadah kubwa, na mja humwomba Allaah maghfirah kwa upungufu uliotokea ndani yake.

7-Kithirisha Tawbah Kila Siku:

Tafakari, ee Mja wa Al-Ghaffaar, ikiwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akitubia mara mia kwa siku, je, sisi tunahitaji kiasi gani?

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنِ الأَغَرِّ الْمُزَنِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ تُوبُوا إِلَى اللَّهِ، فَإِنِّي أَتُوبُ فِي الْيَوْمِ إِلَيْهِ مِائَةَ مَرَّةٍ))

Amesimulia Al-Agharr Al-Muzaniyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Enyi watu! Tubieni kwa Allaah, kwani hakika mimi natubia Kwake kwa siku mara mia moja.” [Muslim]

8-Omba Maghfirah Kama Alivyoomba Nabiy Aadam (عليه السلام) Na Mkewe:

Omba, ee Mja wa Al-Ghaffaar, du’aa ya Nabiy Aadam (عليه السلام) na mkewe, ukikiri kosa lako bila kulitetea.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾

Wakasema: Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na Usipotughufuria na Ukaturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Al-A’raaf (7:23)]

9-Waombee Wazazi Wako Na Waumini Maghfirah:

Tambua, ee Mja wa Al-Ghaffaar: Nabiy Nuwh (عليه السلام) aliomba:

رَّبِّ اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِمَن دَخَلَ بَيْتِيَ مُؤْمِنًا وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَلَا تَزِدِ الظَّالِمِينَ إِلَّا تَبَارًا﴿٢٨﴾

Rabb wangu! Nighufurie mimi, na wazazi wangu wawili, na kila aliyeingia nyumbani mwangu akiwa Muumini na Waumini wa kiume na Waumini wa kike, na wala Usiwazidishie madhalimu isipokuwa kuteketea kabisa. [Nuwh (71:28)]

10-Soma Sayyid Al-Istighfaar Asubuhi Na Jioni:

Dumisha, ee Mja wa Al-Ghaffaar, Sayyid Al-Istighfaar asubuhi na jioni, kwani ndiyo istighfaar bora kabisa.

Rejea Sayyid Al-Istighfaar katika 027-Al-Baariu: “Yaa Allaah! Wewe Ndiye Rabb wangu … basi Nighufurie, kwani hakuna anayeghufuria madhambi isipokuwa Wewe.” Atakayeisema kwa yakini, akafa siku hiyo au usiku huo, atakuwa miongoni mwa watu wa Jannah [Al-Bukhaariy].

Na Allaah Mjuzi zaidi