Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah039 - At-Tawwaab

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 039 kati ya 103
At-Tawwaab — Majina Mazuri ya Allaah

At-Tawwaab: Mwingi wa kupokea tawbah; Anayewawafikisha Waja Wake kutubia, kisha Anapokea tawbah yao mara baada ya mara.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara kumi na moja (11), na mara nyingi limeambatana na Jina Ar-Rahiym. Nabiy Aadam (عليه السلام) alipopokea maneno kutoka kwa Rabb wake:

فَتَلَقَّىٰ آدَمُ مِن رَّبِّهِ كَلِمَاتٍ فَتَابَ عَلَيْهِ ۚ إِنَّهُ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿٣٧﴾

Kisha Aadam akapokea maneno kutoka kwa Rabb wake, na (Rabb wake) Akapokea tawbah yake. Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Kurehemu? [Al-Baqarah (2:37)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ﴿١٠٤﴾

Je, hawajui kwamba Allaah Ndiye Anayekubali tawbah ya Waja Wake, na Anapokea swadaqa, na kwamba Allaah Ndiye Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Kurehemu? [At-Tawbah (9:104)]

Maana Ya At-Tawwaab:

1-Tawbah ya Allaah kwa mja iko kwa namna mbili: kwanza, Anamwafikisha mja kutubia; na pili, Anaipokea tawbah yake baada ya kutubia. Na hilo linaonekana katika kisa cha Swahaba watatu waliobaki nyuma katika vita vya Tabuwk:

وَعَلَى الثَّلَاثَةِ الَّذِينَ خُلِّفُوا حَتَّىٰ إِذَا ضَاقَتْ عَلَيْهِمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ وَضَاقَتْ عَلَيْهِمْ أَنفُسُهُمْ وَظَنُّوا أَن لَّا مَلْجَأَ مِنَ اللَّـهِ إِلَّا إِلَيْهِ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ لِيَتُوبُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ﴿١١٨﴾

Na (Akapokea tawbah) ya wale watatu waliobaki nyuma (wakajuta mno) mpaka ardhi ikadhikika kwao juu ya kuwa ni pana na zikadhikika nafsi zao, na wakatambua kwamba hakuna pa kumkimbia Allaah isipokuwa kuelekea Kwake, kisha (Allaah) Akapokea tawbah yao, ili watubie. Hakika Allaah Yeye Ndiye Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Kurehemu? [At-Tawbah (9:118)]

2-At-Tawwaab ni neno la kukithirisha; Anapokea tawbah ya Waja Wake wengi, na Anaipokea tena na tena kila wanaporudi Kwake.

3-Anafurahi kwa tawbah ya Mja Wake kuliko furaha ya mtu aliyepoteza kipando chake jangwani kisha akakipata. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((لَلَّهُ أَشَدُّ فَرَحًا بِتَوْبَةِ عَبْدِهِ حِينَ يَتُوبُ إِلَيْهِ مِنْ أَحَدِكُمْ كَانَ عَلَى رَاحِلَتِهِ بِأَرْضِ فَلاَةٍ، فَانْفَلَتَتْ مِنْهُ وَعَلَيْهَا طَعَامُهُ وَشَرَابُهُ، فَأَيِسَ مِنْهَا، فَأَتَى شَجَرَةً فَاضْطَجَعَ فِي ظِلِّهَا قَدْ أَيِسَ مِنْ رَاحِلَتِهِ، فَبَيْنَا هُوَ كَذَلِكَ إِذَا هُوَ بِهَا قَائِمَةً عِنْدَهُ، فَأَخَذَ بِخِطَامِهَا ثُمَّ قَالَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ: اللَّهُمَّ أَنْتَ عَبْدِي وَأَنَا رَبُّكَ، أَخْطَأَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ))

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Anafurahi zaidi kwa tawbah ya Mja Wake anapotubia Kwake, kuliko mmoja wenu aliyekuwa juu ya kipando chake katika ardhi ya jangwa, kikamponyoka, na juu yake kuna chakula chake na kinywaji chake, akakata tamaa nacho. Akaufikia mti akajilaza kivulini mwake, akiwa amekata tamaa na kipando chake. Alipokuwa katika hali hiyo, ghafla akakiona kimesimama mbele yake. Akaishika hatamu yake, kisha akasema kwa furaha kubwa: Yaa Allaah! Wewe ni mja wangu nami ni Rabb Wako! Akakosea kwa sababu ya furaha kubwa.” [Muslim]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, At-Tawwaab:

1-Tubieni Nyote Kwa Allaah, Kwani Tawbah Ni Njia Ya Kufaulu:

Tambua, ee Mja wa At-Tawwaab, kwamba tawbah si ya wenye madhambi makubwa peke yao; bali Allaah Amewaamrisha Waumini wote kutubia, kwani hakuna asiyekosea.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake. Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao (vikuku na kadhaalika). Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr (24:31)]

2-Tubia Tawbah Ya Kweli (Tawbatan Naswuwhaa):

Kumbuka, ee Mja wa At-Tawwaab, kwamba tawbah ya kweli ni ile inayotoka moyoni: kuacha kosa, kujuta, na kuazimia kutorudia.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّـهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ ۖ نُورُهُمْ يَسْعَىٰ بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٨﴾

Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli), asaa Rabb wenu Akakufutieni maovu yenu, na Akakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito. Siku ambayo Allaah Hatomfedhehesha Nabiy na wale walioamini pamoja naye. Nuru yao itatembea mbele yao na kuliani mwao, watasema: Rabb wetu! Tutimizie Nuru yetu, na Tughufurie, hakika Wewe juu ya kila kitu Ni Muweza. [At-Tahriym (66:8)]

3-Usiendelee Na Kosa Ukijua:

Tambua, ee Mja wa At-Tawwaab: Katika sifa za wenye taqwa ni kwamba hawaendelei na maovu yao wakiwa wanajua; bali wanaacha, wanajuta, na wanaazimia kutorudia. Rejea Aal-‘Imraan (3:135) katika 037-Al-Ghafuwr.

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٣٥﴾

Na ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah? Na hawaendelei katika waliyoyafanya na hali wanajua. [Aal-‘Imraan (3:135)]

4-Usiakhirishe Tawbah Mpaka Mauti Yakufikie:

Tahadhari, ee Mja wa At-Tawwaab, na kuakhirisha tawbah kwa kudhani kwamba muda bado upo; kwani hakuna ajuaye lini mauti yatamfikia.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللَّـهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ فَأُولَـٰئِكَ يَتُوبُ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١٧﴾ وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّىٰ إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٨﴾

Hakika tawbah inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujahili kisha wakatubia haraka, basi hao Allaah Anapokea tawbah yao. Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote. Lakini tawbah si kwa wale wanaofanya maovu mpaka mauti yanapomjia mmoja wao ndipo aseme: Hakika mimi sasa nimetubu. Na wala wale wanaokufa na hali wao ni makafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo. [An-Nisaa (4:17-18)]

5-Furahi Kurudi Kwa Allaah, Kwani Yeye Anafurahi Zaidi Kwa Tawbah Yako:

Kumbuka, ee Mja wa At-Tawwaab, kwamba Allaah Anafurahi kwa tawbah yako; basi usione haya kurudi Kwake.

Rejea Hadiyth ya Anas (رضي الله عنه) juu. Anayejua jinsi Allaah Anavyofurahi kwa tawbah yake, hukimbilia kutubia bila kuona haya kurudi Kwake.

6-Muombe Allaah Akuwafikishe Kutubia, Kwani Hata Tawbah Ni Tawfiyq Yake:

Tambua kwamba hata uwezo wa kutubia ni tawfiyq kutoka kwa At-Tawwaab; basi mwombe Akuwafikishe.

Rejea At-Tawbah (9:118) juu: “…kisha (Allaah) Akapokea tawbah yao, ili watubie.” Basi mwombe Allaah Akuwafikishe kutubia.

7-Jifunze Kwa Nabiy Aadam (عليه السلام):

Tambua, ee Mja wa At-Tawwaab: Aadam (عليه السلام) alipokosea, alikiri kosa lake na akaomba maghfirah (rejea Al-Baqarah (2:37) juu); tofauti na Ibliys aliyetakabari na kuendelea na kosa lake.

8-Maliza Kazi Zako Kwa Tasbiyh Na Istighfaar:

Kumbuka, ee Mja wa At-Tawwaab, kwamba hata baada ya kukamilisha amali njema, mja anahitaji istighfaar kwa upungufu uliotokea ndani yake.

Allaah Alimwamrisha Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) mwishoni mwa ujumbe wake:

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا ﴿٣﴾

Basi hapo sabbih na mhimidi Rabb wako (kwa wingi zaidi) na muombe maghfirah. Hakika Yeye daima Ni Mwingi mno wa Kupokea tawbah. [An-Naswr (110:3)]

9-Ambatanisha Tawbah Yako Na Swadaqah Na Amali Njema:

Kumbuka kuambatanisha tawbah yako na swadaqah na amali njema, kwani At-Tawwaab Ameviunganisha pamoja.

Rejea At-Tawbah (9:104) juu; Allaah Ameunganisha kupokea tawbah na kupokea swadaqah.

10-Mwombe At-Tawwaab Kama Alivyoomba Nabiy Ibraahiym Na Ismaa’iyl (عليهما السلام):

Omba du’aa, ee ndugu Muislamu, Allaah Akupokelee tawbah yako kwa Jina Lake At-Tawwaab.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿١٢٨﴾

Rabb wetu, Tujaalie tuwe wenye kujisalimisha Kwako pamoja na kizazi chetu wawe ummah wenye kujisalimisha Kwako, na Tuonyeshe taratibu za ibaada zetu na Pokea tawbah zetu, hakika Wewe Ni Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Kurehemu. [Al-Baqarah (2:128)]

Na Allaah Mjuzi zaidi