Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah040 - Ar-Rauwf

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 040 kati ya 103
Ar-Rauwf — Majina Mazuri ya Allaah

Ar-Rauwf: Mwenye huruma mno; Ambaye Huruma Yake kwa Waja Wake ni kubwa, laini na ya kuwaepusha na kila madhara.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara kumi, na mara nyingi limeambatana na Jina Ar-Rahiym. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِّتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ وَيَكُونَ الرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا ۗ وَمَا جَعَلْنَا الْقِبْلَةَ الَّتِي كُنتَ عَلَيْهَا إِلَّا لِنَعْلَمَ مَن يَتَّبِعُ الرَّسُولَ مِمَّن يَنقَلِبُ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ ۚ وَإِن كَانَتْ لَكَبِيرَةً إِلَّا عَلَى الَّذِينَ هَدَى اللَّـهُ ۗ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٤٣﴾

Na ndivyo hivyo Tumekufanyeni ummah bora na adilifu ili muwe mashahidi juu ya watu na awe Rasuli shahidi juu yenu. Na Hatukukifanya Qiblah ambacho ulikuwa ukikielekea (Baytul-Maqdis) isipokuwa Tupate kupambanua nani anayemfuata Rasuli kikweli, na nani atakayegeuka arudi nyuma. Na hakika ilikuwa ni jambo gumu isipokuwa kwa wale ambao Allaah Amewaongoza. Na Allaah Hakuwa Mwenye Kupoteza imaan yenu. Hakika Allaah Ni Mwenye Huruma mno kwa watu na Mwenye Kurehemu. [Al-Baqarah (2:143)]

Na Anasema pia:

هُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ عَلَىٰ عَبْدِهِ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ لِّيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ بِكُمْ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٩﴾

Yeye Ndiye Anayemteremshia Mja Wake Aayaat bayana ili Akutoeni katika viza na kukuingizeni kwenye nuru. Na hakika Allaah kwenu Ni Mwenye Huruma mno, Mwenye Kurehemu. [Al-Hadiyd (57:9)]

Maana Ya Ar-Rauwf:

1-Ar-Rauwf ni Mwenye huruma iliyo kubwa zaidi; huruma ya kuwaepusha waja na madhara na kuwawepesishia mambo yao.

2-Katika Huruma Yake ni kwamba Hakupoteza imaan ya Waumini waliokufa kabla ya kubadilishwa kwa Qiblah, bali Aliikubali Swalaah yao (rejea Al-Baqarah (2:143) juu).

3-Na katika Huruma Yake ni kuwaonya Waja Wake na Adhabu Yake kabla haijawafikia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَوْمَ تَجِدُ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ مِنْ خَيْرٍ مُّحْضَرًا وَمَا عَمِلَتْ مِن سُوءٍ تَوَدُّ لَوْ أَنَّ بَيْنَهَا وَبَيْنَهُ أَمَدًا بَعِيدًا ۗ وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّـهُ نَفْسَهُ ۗ وَاللَّـهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ ﴿٣٠﴾

Siku itakayokuta kila nafsi yale iliyoyatenda katika kheri yamehudhurishwa, na yale iliyoyatenda katika maovu, itatamani nafsi lau kama ingelikuwa baina yake na baina ya (maovu) hayo masafa ya mbali. Na Allaah Anakutahadharisheni na Nafsi Yake. Na Allaah Ni Mwenye Huruma mno kwa waja. [Aal-‘Imraan (3:30)]

4-Na Ameumba wanyama wa kubeba mizigo kwa Huruma Yake kwa waja. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَتَحْمِلُ أَثْقَالَكُمْ إِلَىٰ بَلَدٍ لَّمْ تَكُونُوا بَالِغِيهِ إِلَّا بِشِقِّ الْأَنفُسِ ۚ إِنَّ رَبَّكُم ْ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿٧﴾

Na wanabeba mizigo yenu kupeleka nchi msizoweza kuzifikia isipokuwa kwa mashaka mazito ya kuwalemeeni. Hakika Rabb wenu bila shaka Ni Mwenye Huruma mno, Mwenye Kurehemu. [An-Nahl (16:7)]

5-Na Anazuia mbingu zisianguke juu ya ardhi kwa Huruma Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ وَالْفُلْكَ تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِأَمْرِهِ وَيُمْسِكُ السَّمَاءَ أَن تَقَعَ عَلَى الْأَرْضِ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٦٥﴾

Je, huoni kwamba Allaah Amevitiisha kwa ajili yenu vile vilivyomo katika ardhi na merikebu zipitazo baharini kwa Amri Yake. Na Anazuia mbingu zisianguke juu ya ardhi isipokuwa kwa Idhini Yake. Hakika Allaah kwa watu ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu. [Al-Hajj (22:65)]

6-Na Amemsifu Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa sifa ya huruma kwa Waumini, kwa kiwango kinacholaikiana na kiumbe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٢٨﴾

Kwa yakini amekujieni Rasuli anayetokana na nyinyi wenyewe, yanamtia mashaka (na huzuni) yanayokutaabisheni, anakujalini, kwa Waumini ni mwenye huruma mno, mwenye rehma. [At-Tawbah (9:128)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ar-Rauwf:

1-Tambua Huruma Ya Ar-Rauwf Katika Wepesi Wa Sharia Yake:

Kumbuka kwamba katika Huruma ya Ar-Rauwf ni kukuwekea sharia nyepesi zisizokutaabisha; basi zipokee kwa furaha na shukurani.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٨٥﴾

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na baatwil). Kwa hiyo atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi (inampasa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu ili mkamilishe idadi na ili mumtukuze Allaah kwa kuwa Amekuongozeni, na ili mpate kushukuru. [Al-Baqarah (2:185)]

2-Mtegemee Ar-Rauwf, Kwani Hakupotezei Amali Yako:

Tambua, ee Mja wa Ar-Rauwf, kwamba hakuna amali njema inayopotea mbele ya Allaah; basi endelea kutenda mema hata kama watu hawaoni.

Rejea Al-Baqarah (2:143) juu: “Na haikuwa Allaah Kupoteza imaan yenu.” Amali njema haipotei mbele ya Ar-Rauwf.

3-Zingatia Maonyo Yake, Kwani Ni Kwa Huruma Yake:

Tahadhari na kupuuza maonyo ya Ar-Rauwf; kwani Anakuonya kwa sababu ya Huruma Yake kwako, kabla adhabu haijakufikia.

Rejea Aal-‘Imraan (3:30) juu: Allaah Anakutahadharisheni na Nafsi Yake, na Allaah Ni Mwenye huruma mno kwa waja.

4-Kuwa Mpole Katika Mambo Yako Yote:

Kumbuka kwamba upole ni sifa inayopendwa na Ar-Rauwf; basi kuwa mpole kwa familia yako, majirani zako, wafanyakazi wako na wote unaotangamana nao.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((يَا عَائِشَةُ، إِنَّ اللَّهَ رَفِيقٌ يُحِبُّ الرِّفْقَ فِي الأَمْرِ كُلِّهِ))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Yaa ‘Aaishah! Hakika Allaah Ni Mpole, Anapenda upole katika jambo lote.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Wahurumie Viumbe Ili Uhurumiwe:

Tambua kwamba kadiri unavyowahurumia viumbe, ndivyo unavyostahiki Rehma ya Ar-Rauwf; basi wahurumie wadogo, wanyonge, mayatima na hata wanyama.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الرَّاحِمُونَ يَرْحَمُهُمُ الرَّحْمَنُ، ارْحَمُوا مَنْ فِي الأَرْضِ يَرْحَمْكُمْ مَنْ فِي السَّمَاءِ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Wenye kurehemu, Ar-Rahmaan Huwarehemu. Warehemuni walioko ardhini, Atakurehemuni Aliye juu mbinguni.” [Abuu Daawuwd (4941), At-Tirmidhiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]

6-Iga Huruma Ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Kwa Waumini:

Kumbuka, ee Mja wa Ar-Rauwf, kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ndiye kiigizo chako katika huruma; basi jitahidi kumwiga.

Rejea At-Tawbah (9:128) juu. Muumini huwahurumia ndugu zake, huwaonea uchungu kwa yanayowataabisha, na huwatakia kheri.

7-Shukuru Neema Za Ar-Rauwf Katika Viumbe Alivyokutiishia:

Tafakari, ee ndugu Muislamu, Neema za Ar-Rauwf zinazokuzunguka kila siku, na umshukuru kwazo.

Rejea An-Nahl (16:7) juu; kila chombo cha usafiri na kila kinachokubebea mizigo ni neema ya Huruma Yake.

8-Jitolee Nafsi Yako Kwa Ajili Ya Ridhaa Ya Allaah:

Tambua kwamba Huruma ya Ar-Rauwf inawafikia kwa namna maalumu wale wanaojitolea kwa ajili ya Ridhaa Yake.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْرِي نَفْسَهُ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ ﴿٢٠٧﴾

Na miongoni mwa watu yupo anayeiuza nafsi yake kutafuta Radhi za Allaah. Na Allaah Ni Mwenye Huruma mno kwa waja. [Al-Baqarah (2:207)]

9-Isome Qur-aan, Kwani Ni Nuru Iliyoteremshwa Kwa Huruma Yake:

Kumbuka kwamba Qur-aan ni miongoni mwa neema kubwa kabisa za Huruma ya Ar-Rauwf kwako; basi isome, uizingatie na uifanyie kazi.

Rejea Al-Hadiyd (57:9) juu; Allaah Ameteremsha Aayaat bayana ili Akutoeni gizani kuwapeleka kwenye nuru.

10-Mwombe Ar-Rauwf Akutakase Moyo Wako Na Chuki Kwa Waumini:

Omba du’aa Ar-Rauwf Akutakase moyo wako, kama walivyoomba Waumini waliokuja baada ya Swahaba.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٠﴾

Na wale waliokuja baada yao wanasema: Rabb wetu! Tughufurie pamoja na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imaan, na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Rabb wetu! Hakika Wewe Ni Mwenye Huruma mno, Mwenye Kurehemu. [Al-Hashr (59:10)]

Na Allaah Mjuzi zaidi