Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 041 kati ya 103
Al-Barr — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Barr: Mwingi wa wema na ihsaan; Ambaye wema Wake umewaenea viumbe Vyake vyote, na Anawafanyia Waumini wema maalumu duniani na Aakhirah.

Jina hili tukufu limetajwa katika Qur-aan mara moja (1), katika maneno ya watu wa Jannah watakapokumbuka Neema ya Allaah juu yao:

وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ ﴿٢٥﴾ قَالُوا إِنَّا كُنَّا قَبْلُ فِي أَهْلِنَا مُشْفِقِينَ ﴿٢٦﴾ فَمَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَوَقَانَا عَذَابَ السَّمُومِ ﴿٢٧﴾ إِنَّا كُنَّا مِن قَبْلُ نَدْعُوهُ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ ﴿٢٨﴾

Na wataelekeana wao kwa wao wakiulizana. Watasema: Hakika sisi tulikuwa kabla tukiishi baina ya ahli zetu huku tukiogopa. Basi Allaah Akatuneemesha, na Akatuokoa na adhabu ya moto unaobabua. Hakika sisi tulikuwa kabla tunamuomba Yeye Pekee. Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa Ihsaan na Fadhila, Mwenye Kurehemu. [Atw-Twuur (52:25-28)]

Maana Ya Al-Barr:

1-Wema wa Allaah (سبحانه وتعالى) umewaenea viumbe vyote: Amewaumba, Amewaruzuku, na Amewapa neema zisizohesabika, hata kabla hawajaziomba.

2-Na Ana wema maalumu kwa Waumini: Anawaongoza, Anawasamehe, Anawakinga na adhabu, na Atawaingiza Jannah. Hivyo ndivyo walivyoshuhudia watu wa Jannah: “Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa wema, Mwenye Kurehemu.”

3-Na neno al-birr katika Qur-aan linakusanya kila aina ya kheri na utiifu; Allaah Amelieleza hivi:

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا ۖ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ ﴿١٧٧﴾

Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na Magharibi, lakini wema ni mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na akawapa mali juu ya kuipenda kwake jamaa wa karibu na mayatima na masikini na msafiri na waombao na katika kukomboa watumwa, na akasimamisha Swalaah na akatoa Zakaah, na watimizao ahadi zao wanapoahidi, na wenye subira katika dhiki za ufukara na maafa ya magonjwa na njaa na katika vita. Hao ndio waliosadikisha na hao ndio wenye taqwa. [Al-Baqarah (2:177)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Barr:

1-Tafakari Wema Wa Allaah Juu Yako Katika Kila Hali:

Kumbuka, ee ndugu Muislamu, kwamba kila kheri uliyonayo, katika mwili wako, familia yako na Dini yako, ni wema kutoka kwa Al-Barr. Tafakari kama walivyotafakari watu wa Jannah walipokumbuka hali yao duniani (rejea At-Twuwr (52:25-28) juu).

2-Tambua Kwamba Wema Wa Kweli Ni Imaan Na Amali, Si Sura Za Nje Tu:

Tambua, ee Mja wa Al-Barr, kwamba birr si kuelekeza uso Mashariki au Magharibi tu, bali ni imaan ya kweli, kutoa mali, kusimamisha Swalaah, kutekeleza ahadi, na kusubiri (rejea Al-Baqarah (2:177) juu).

3-Toa Katika Unavyovipenda Upate Wema:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Barr, kwamba kiwango cha juu cha wema hakifikiwi isipokuwa kwa kujitolea katika vitu unavyovipenda. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٩٢﴾

Hamtoweza kuufikia wema uliokunjuka mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachotoa basi hakika Allaah kwacho Ni Mjuzi. [Aal-‘Imraan (3:92)]

4-Wafanyie Wema Wazazi Wako:

Tambua, ee Mja wa Al-Barr, kwamba wema kwa wazazi ni miongoni mwa amali zinazopendwa zaidi na Allaah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: سَأَلْتُ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم): أَيُّ الْعَمَلِ أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ؟ قَالَ: ((الصَّلاَةُ عَلَى وَقْتِهَا)). قَالَ: ثُمَّ أَيٌّ؟ قَالَ: ((ثُمَّ بِرُّ الْوَالِدَيْنِ)). قَالَ: ثُمَّ أَيٌّ؟ قَالَ: ((الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Nilimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ni amali ipi inayopendwa zaidi na Allaah? Akasema: “Swalaah kwa wakati wake.” Nikasema: Kisha ipi? Akasema: “Kisha kuwafanyia wema wazazi wawili.” Nikasema: Kisha ipi? Akasema: “Jihaad katika Njia ya Allaah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Iga Manabii Katika Wema Kwa Wazazi:

Tafakari jinsi Al-Barr Alivyomsifu Nabiy Yahyaa (عليه السلام):

وَبَرًّا بِوَالِدَيْهِ وَلَمْ يَكُن جَبَّارًا عَصِيًّا ﴿١٤﴾

Na mtiifu mno kwa wazazi wake wawili, na wala hakuwa jabari wala muasi. [Maryam (19:14)]

Na Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) alisema:

وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا ﴿٣٢﴾

Na niwe mtiifu mno kwa mama yangu, na wala Hakunijaalia kuwa jabari, mwovu. [Maryam (19:32)]

6-Pamba Tabia Yako, Kwani Wema Ni Tabia Njema:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Barr, kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameeleza wema kwa neno fupi lenye maana pana:

عَنِ النَّوَّاسِ بْنِ سَمْعَانَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَأَلْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) عَنِ الْبِرِّ وَالإِثْمِ فَقَالَ: ((الْبِرُّ حُسْنُ الْخُلُقِ، وَالإِثْمُ مَا حَاكَ فِي صَدْرِكَ وَكَرِهْتَ أَنْ يَطَّلِعَ عَلَيْهِ النَّاسُ))

Amesimulia An-Nawwaas bin Sam’aan (رضي الله عنه): Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu wema na dhambi, akasema: “Wema ni tabia njema; na dhambi ni kile kinachokutatiza kifuani mwako, na ukachukia watu wakijue.” [Muslim]

7-Shirikiana Na Wenzako Katika Wema Na Taqwa:

Tambua kwamba Al-Barr Ameamrisha kushirikiana katika kheri, na Amekataza kushirikiana katika maasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُحِلُّوا شَعَائِرَ اللَّـهِ وَلَا الشَّهْرَ الْحَرَامَ وَلَا الْهَدْيَ وَلَا الْقَلَائِدَ وَلَا آمِّينَ الْبَيْتَ الْحَرَامَ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّن رَّبِّهِمْ وَرِضْوَانًا ۚ وَإِذَا حَلَلْتُمْ فَاصْطَادُوا ۚ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ أَن صَدُّوكُمْ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ أَن تَعْتَدُوا ۘ وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢﴾

Enyi walioamini! Msikhalifu utukufu wa Ishara za Allaah, wala Miezi Mitukufu wala wanyama wanaopelekwa Haram kuchinjwa, wala vigwe (vyao), wala (kukhalifu amani kwa) wanaoiendea Nyumba Tukufu (Makkah) wanatafuta Fadhila kutoka kwa Rabb wao na Radhi. Na mkishatoka kwenye ihraam basi windeni (mkitaka). Na wala isikuchocheeni chuki mliyonayo kwa watu kwa vile walikuzuieni na Al-Masjid-Al-Haraam ikakupelekeni kufanya uonevu. Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah, hakika Allaah Ni Mkali wa Kuakibu. [Al-Maaidah (5:2)]

8-Kuwa Mkweli, Kwani Ukweli Unaongoza Kwenye Wema:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Barr, kwamba njia ya wema huanzia kwenye ukweli. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ الصِّدْقَ يَهْدِي إِلَى الْبِرِّ، وَإِنَّ الْبِرَّ يَهْدِي إِلَى الْجَنَّةِ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika ukweli unaongoza kwenye wema, na wema unaongoza kwenye Jannah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Wafanyie Wema Hata Wasio Waislamu Wasiowapiga Vita Waislamu:

Tambua, ee Mja wa Al-Barr, kwamba Uislamu unafundisha wema na uadilifu kwa watu wote wasiowapiga vita Waislamu wala kuwafukuza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ﴿٨﴾

Allaah Hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale wasiokupigeni vita katika Dini, na wala hawakukutoeni kutoka majumbani mwenu. Hakika Allaah Anapenda wafanyao uadilifu. [Al-Mumtahinah (60:8)]

10-Mwombe Al-Barr Akufishe Pamoja Na Watu Wema:

Omba du’aa, ee Mja wa Al-Barr, kama walivyoomba wenye akili:

رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلْإِيمَانِ أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا ۚ رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الْأَبْرَارِ ﴿١٩٣﴾

Rabb wetu! Hakika sisi tumemsikia mwitaji anaita kwenye imaan kwamba: Mwaminini Rabb wenu. Basi tukaamini. Rabb wetu! Tughufurie madhambi yetu na Tufutie mabaya yetu na Tufishe pamoja na Waumini wema. [Aal-‘Imraan (3:193)]

Na Allaah Mjuzi zaidi