Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah044 - Ar-Raaziq

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 044 kati ya 103
Ar-Raaziq — Majina Mazuri ya Allaah

Ar-Raaziq: Mtoaji Rizqi

Yeye Ndiye Anayewapa rizqi viumbe wote, na Amezipanga rizqi zao kabla ya kuwaumba, na Amedhamini kuzikamilisha hata kama ni baada ya muda.

Jina Hili Ar-Raaziq limekuja katika Qur-aan kwa sura ya wingi (خَيْرُ الرَّازِقِينَ) mara tano: Al-Maaidah (5:114), Al-Hajj (22:58), Al-Muuminuwn (23:72), Saba-a (34:39) na Al-Jumu’ah (62:11). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ اللَّـهُمَّ رَبَّنَا أَنزِلْ عَلَيْنَا مَائِدَةً مِّنَ السَّمَاءِ تَكُونُ لَنَا عِيدًا لِّأَوَّلِنَا وَآخِرِنَا وَآيَةً مِّنكَ ۖ وَارْزُقْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿١١٤﴾

Akasema ‘Iysaa mwana wa Maryam: Ee Allaah, Rabb wetu! Tuteremshie meza ya chakula kutoka mbinguni ili iwe kwetu ni sikukuu kwa wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na iwe Aayah (Ishara, Hoja, Dalili) itokayo Kwako, basi Turuzuku, kwani Wewe Ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Al-Maaidah (5:114)]

Na Anasema (سبحانه وتعالى):

وَالَّذِينَ هَاجَرُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ثُمَّ قُتِلُوا أَوْ مَاتُوا لَيَرْزُقَنَّهُمُ اللَّـهُ رِزْقًا حَسَنًا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ لَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٥٨﴾

Na wale waliohajiri katika Njia ya Allaah, kisha wakauawa, au wakafa, bila shaka Allaah Atawaruzuku rizki nzuri. Na hakika Allaah bila shaka Yeye Ndiye Mbora wa wenye kuruzuku. [Al-Hajj (22:58)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

أَمْ تَسْأَلُهُمْ خَرْجًا فَخَرَاجُ رَبِّكَ خَيْرٌ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٧٢﴾

Au unawaomba ujira? Basi ujira wa Rabb wako ni bora zaidi. Naye Ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Al-Muuminuwn (23:72)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ ۚ وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٣٩﴾

Sema: Hakika Rabb wangu Anamkunjulia rizki Amtakaye kati ya Waja Wake na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Na kitu chochote mtoacho, basi Yeye Atakilipa, Naye Ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Saba-a (34:39)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

وَإِذَا رَأَوْا تِجَارَةً أَوْ لَهْوًا انفَضُّوا إِلَيْهَا وَتَرَكُوكَ قَائِمًا ۚ قُلْ مَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ مِّنَ اللَّـهْوِ وَمِنَ التِّجَارَةِ ۚ وَاللَّـهُ خَيْرُ الرَّازِقِينَ﴿١١﴾

Na wanapoona tijara au pumbao wanaikimbilia na wanakuacha umesimama. Sema: Yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi kuliko pumbao na tijara, na Allaah Ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Al-Jumu’ah (62:11)]

Na rizqi Anayowapa Waja Wake ni ya aina mbili:

i-Rizqi yenye sababu: Kama vile Alivyojaalia kilimo, biashara, viwanda na mfano wa hayo katika njia nyingi za kupata rizqi kwa watu wote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَجَعَلْنَا لَكُمْ فِيهَا مَعَايِشَ وَمَن لَّسْتُمْ لَهُ بِرَازِقِينَ ﴿٢٠﴾

Na Tukakuwekeeni humo njia na mbinu za maisha, na ya hao ambao nyinyi si wenye kuwaruzuku. [Al-Hijr (15:20)]

Yaani: Ni sababu ambazo kwazo nyinyi mnapata rizqi.

ii-Rizqi isiyo na sababu kutoka kwa mja: Allaah (سبحانه وتعالى) Humpa mja rizqi bila ya jitihada yake; Humpa kutoka mbinguni moja kwa moja, au kupitia mikono ya mtu mwengine bila ya yeye kuitafuta. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٢٢﴾

Ambaye Amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa, na Akateremsha kutoka mbinguni maji, Akawatolea kwayo matunda kuwa ni rizki zenu. Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua. [Al-Baqarah (2:22)]

Na katika ukamilifu wa Rizqi Yake (سبحانه وتعالى), Hutoa kwa sababu na bila ya sababu, Akiombwa au bila ya kuombwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَاللَّـهُ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٢١٢﴾

Na Allaah Humruzuku Amtakaye bila ya hesabu. [Al-Baqarah (2:212)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ar-Raaziq:

1-Ar-Razzaaq Hahitaji Rizki Kutoka Kwa Waja Wake:

Tambua, ee Mja wa Ar-Raaziq: Allaah Hakuwaumba waja ili Wamruzuku, bali Yeye Ndiye Mwenye kuwaruzuku wao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ ﴿٥٧﴾ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ ﴿٥٨﴾

Sitaki kutoka kwao rizki yoyote, na wala Sitaki wanilishe. Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa Kuruzuku, Mwenye Nguvu Madhubuti. [Adh-Dhaariyaat (51:57-58)]

2-Tambua Kwamba Hakuna Atakayekunufaisha Isipokuwa Kwa Alichokuandikia Allaah:

Tambua kwamba viumbe wote wakijumuika kukunufaisha au kukudhuru, hawatoweza isipokuwa kwa yale Aliyokuandikia Ar-Raaziq. Basi muombe Yeye Pekee, na utake msaada Kwake Pekee.

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: كُنْتُ خَلْفَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) يَوْمًا فَقَالَ: ((يَا غُلامُ، إِنِّي أُعَلِّمُكَ كَلِمَاتٍ: احْفَظِ اللَّهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظِ اللَّهَ تَجِدْهُ تُجَاهَكَ، إِذَا سَأَلْتَ فَاسْأَلِ اللَّهَ، وَإِذَا اسْتَعَنْتَ فَاسْتَعِنْ بِاللَّهِ، وَاعْلَمْ أَنَّ الأُمَّةَ لَوِ اجْتَمَعَتْ عَلَى أَنْ يَنْفَعُوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ لَكَ، وَإِنِ اجْتَمَعُوا عَلَى أَنْ يَضُرُّوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَضُرُّوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ عَلَيْكَ، رُفِعَتِ الأَقْلاَمُ وَجَفَّتِ الصُّحُفُ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Siku moja nilikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) (juu ya mnyama), akaniambia: “Yaa kijana! Mimi nitakufundisha maneno: Mhifadhi Allaah Naye Atakuhifadhi. Mhifadhi Allaah utamkuta yupo mbele yako. Unapoomba, muombe Allaah. Unapotaka msaada, mtake Allaah. Na fahamu kwamba lau ummah (wote) utajikusanya ili wakunufaishe kwa jambo, hawatoweza kukunufaisha isipokuwa kwa jambo Alilokuandikia Allaah; na wakijumuika ili wakudhuru kwa jambo, hawatoweza kukudhuru isipokuwa kwa jambo Alilokuandikia Allaah. Kalamu zimeshanyanyuliwa na karatasi zimeshakauka.” [At-Tirmidhiy (2516), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

3-Ridhika Na Rizqi Aliyokuruzuku Allaah:

Ridhika na rizqi Aliyokuruzuku Allaah, na kumbuka kwamba hakuna atakayeweza kukuzuilia wala kukuzidishia isipokuwa Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢﴾

Rehma yoyote Anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna wa kuizuia, na Anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake, Naye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Faatwir (35:2)]

4-Tafakari Rizqi Yako Ya Kila Siku:

Tazama chakula chako na jinsi Allaah Ar-Razzaaq Alivyokuandalia rizqi hiyo, kuanzia mvua inayoteremka mpaka nafaka na matunda unayoyala, kisha Mshukuru. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ ﴿٢٤﴾ أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا ﴿٢٥﴾ ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا ﴿٢٦﴾ فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا ﴿٢٧﴾ وَعِنَبًا وَقَضْبًا ﴿٢٨﴾ وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا ﴿٢٩﴾ وَحَدَائِقَ غُلْبًا ﴿٣٠﴾ وَفَاكِهَةً وَأَبًّا ﴿٣١﴾ مَّتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ ﴿٣٢﴾

Basi atazame binaadam chakula chake. Kwamba Sisi Tumemimina maji kwa uneemefu. Kisha Tukaipasua ardhi ikafunguka (kwa mimea). Tukaotesha humo nafaka. Na mizabibu na mimea ya mboga (ikatwayo ikamea tena). Na mizaituni na mitende. Na mabustani yaliyositawi na kusongamana. Na matunda na majani ya malisho ya wanyama. Yakiwa ni manufaa kwenu na kwa wanyama wenu wa mifugo. [‘Abasa (80:24-32)]

5-Istighfaar Ni Miongoni Mwa Sababu Kubwa Za Rizki:

Tambua, ee Mja wa Ar-Raaziq: Nabiy Nuwh (عليه السلام) aliwaahidi kaumu yake kwamba kuomba maghfirah kunaleta mvua, mali na watoto. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا﴿١٠﴾ يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا﴿١١﴾ وَيُمْدِدْكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَل لَّكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَل لَّكُمْ أَنْهَارًا﴿١٢﴾

Nikasema: Ombeni maghfirah kwa Rabb wenu, hakika Yeye Ni Mwingi mno wa Kughufuria. Atakutumieni mvua tele ya kuendelea. Na Atakuongezeeni mali na wana, na Atakupeni mabustani na Atakupeni mito. [Nuwh (71:10-12)]

6-Tawakali Kwa Ar-Raaziq Kama Ndege Wanavyotawakali:

Tambua kwamba tawakkul ya kweli ni kuchukua sababu huku moyo ukimtegemea Ar-Raaziq Pekee.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((لَوْ أَنَّكُمْ كُنْتُمْ تَوَكَّلُونَ عَلَى اللَّهِ حَقَّ تَوَكُّلِهِ لَرُزِقْتُمْ كَمَا تُرْزَقُ الطَّيْرُ، تَغْدُو خِمَاصًا وَتَرُوحُ بِطَانًا))

Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Lau mngekuwa mnatawakali kwa Allaah kwa kweli, mngeruzukiwa kama wanavyoruzukiwa ndege; wanatoka asubuhi wakiwa na njaa, na wanarudi jioni wakiwa wameshiba.” [At-Tirmidhiy (2344) na amesema: Hasan Swahiyh, Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

7-Tafuta Rizqi Ya Halaal Na Usiwe Na Papara:

Zingatia, usitafute rizqi kwa njia ya haraam, bali tafuta njia ya halaal, kwani baadhi ya watu wanamuasi Ar-Raaziq katika hilo! Na tambua kwamba rizqi yako haitakupita.

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وآله وسلم): ((لا تَسْتَبْطِئُوا الرِّزْقَ، فَإِنَّهُ لَمْ يَكُنْ عَبْدٌ لِيَمُوتَ حَتَّى يَبْلُغَهُ آخِرُ رِزْقٍ هُوَ لَهُ، فَاتَّقُوا اللَّهَ، وَأَجْمِلُوا فِي الطَّلَبِ، أَخْذِ الْحَلالِ، وَتَرْكِ الْحَرَامِ))

Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Usiwe na papara kwa ajili ya rizqi, kwani hakuna mja atakayekufa hadi apate rizqi yake ya mwisho. Basi mcheni Allaah, na muwe na kiasi katika kutafuta, mkichukua yaliyo halaal na mkiacha yaliyo haraam.” [Ibn Maajah, Ibn Hibbaan, Atw-Twabaraaniy na ameisahihisha Imaam Al-Albaaniy: Swahiyh Al-Jaami’ (7323)]

8-Unga Ukoo Upanuliwe Rizqi Yako:

Kumbuka, ee Mja wa Ar-Raaziq, kwamba kuunga ukoo ni miongoni mwa sababu za kupanuliwa rizki na kubarikiwa umri.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((مَنْ سَرَّهُ أَنْ يُبْسَطَ لَهُ فِي رِزْقِهِ، أَوْ يُنْسَأَ لَهُ فِي أَثَرِهِ، فَلْيَصِلْ رَحِمَهُ))

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Anayependa kupanuliwa rizki yake, au kurefushiwa umri wake, basi aunge ukoo wake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Usiache Swalaah Kwa Ajili Ya Kutafuta Rizqi:

Usikimbilie kutafuta rizqi ukaacha Swalaah, kwani Allaah Ndiye Mbora wa wenye kuruzuku. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٩﴾ فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّـهِ وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿١٠﴾ وَإِذَا رَأَوْا تِجَارَةً أَوْ لَهْوًا انفَضُّوا إِلَيْهَا وَتَرَكُوكَ قَائِمًا ۚ قُلْ مَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ مِّنَ اللَّـهْوِ وَمِنَ التِّجَارَةِ ۚ وَاللَّـهُ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿١١﴾

Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya Swalaah siku ya Ijumaa, basi kimbilieni kwenda kumdhukuru Allaah na acheni kuuza na kununua. Hivyo ni kheri kwenu zaidi mkiwa mnajua. Na inapomalizika Swalaah, basi tawanyikeni katika ardhi, na tafuteni Fadhila za Allaah, na mdhukuruni Allaah kwa wingi ili mpate kufaulu. Na wanapoona tijara au pumbao wanaikimbilia na wanakuacha umesimama. Sema: Yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi kuliko pumbao na tijara, na Allaah Ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Al-Jumu’ah (62:9-11)]

10-Mwombe Ar-Raaziq Rizki Njema Kila Asubuhi:

Omba du’aa hii kila asubuhi baada ya Swalaah ya Alfajiri, ukimwomba Ar-Raaziq rizki njema.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiomba baada ya kuswali Alfajiri:

عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُولُ إِذَا صَلَّى الصُّبْحَ حِينَ يُسَلِّمُ: ((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ عِلْمًا نَافِعًا، وَرِزْقًا طَيِّبًا، وَعَمَلاً مُتَقَبَّلاً))

Amesimulia Umm Salamah (رضي الله عنها) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema anapomaliza kuswali Alfajiri kwa kutoa salaam:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ عِلْمًا نَافِعًا، وَرِزْقًا طَيِّبًا، وَعَمَلاً مُتَقَبَّلاً

Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba ilimu yenye manufaa, rizki njema, na amali inayokubaliwa. [Ibn Maajah (925), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Ibn Maajah (762)]

Na Allaah Mjuzi zaidi