Ar-Razzaaq: Mwingi Wa Kuruzuku
Ni Jina linaloelezea wingi wa Rizqi Zake kwa viumbe Vyake. Yeye Allaah (عزّ وجلّ) Anawaruzuku viumbe kabla ya wao kumuomba, na Anawaruzuku hata pale wanapomuasi.
Jina Hili Ar-Razzaaq limetajwa katika Qur-aan mara moja tu, lakini neno rizq na yanayotokana nalo yametajwa zaidi ya mara mia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ ﴿٥٨﴾
Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa Kuruzuku, Mwenye Nguvu Madhubuti. [Adh-Dhaariyaat (51:58)]
Allaah Ndiye Ar-Raaziq, Ar-Razzaaq kwa Waja Wake wote. Amedhamini rizqi ya kila aliyemo ulimwenguni, kila nafsi na kila wakati. Hakuwapa Waumini pekee na kuwanyima makafiri, wala Hakumpa anayemuunga na kumnusuru pekee akamnyima aliye adui Yake, bali Rizqi Zake zinamuenea dhaifu asiye na uwezo na tajiri mwenye nguvu.1 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا ۚ كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٦﴾
Na hakuna kiumbe chochote kitembeacho katika ardhi isipokuwa rizki yake iko kwa Allaah, na (Allaah) Anajua mahali pake pa kustakiri na pa kuhifadhiwa kwake. Yote yamo katika Kitabu kinachobainisha. [Huwd (11:6)]
Hakuna mwenye kuruzukiwa popote alipo, juu au chini, isipokuwa atapata Rizqi ya Allaah (سبحانه وتعالى) na ataenezwa na Ukarimu Wake. Yeye (سبحانه وتعالى) Humkunjulia rizqi Amtakaye na Humkadiria Amtakaye, na Anawapa Waja Wake wote ardhini Rizqi Zake.
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ar-Razzaaq:
1-Mpwekeshe Allaah Ar-Razzaaq:
Tambua kwamba Neema zote zinatoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba Yeye Pekee Ndiye Mwenye Kuruzuku; basi Yeye Pekee Ndiye Anayestahiki kuabudiwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ ﴿٣﴾
Enyi watu! Kumbukeni Neema za Allaah kwenu. Je, kuna muumbaji yeyote badala ya Allaah Anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi vipi mnaghilibiwa? [Faatwir (35:3)]
2-Ar-Razzaaq Hupanua Na Hubana Rizki Kwa Hikmah Yake:
Tambua, ee Mja wa Ar-Razzaaq: Kupanuliwa au kubanwa rizki si dalili ya kupendwa au kuchukiwa na Allaah, bali ni mtihani na Hikmah Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ بَسَطَ اللَّـهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ وَلَـٰكِن يُنَزِّلُ بِقَدَرٍ مَّا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ بِعِبَادِهِ خَبِيرٌ بَصِيرٌ﴿٢٧﴾
Na lau kama Allaah Angelikunjua rizki kwa Waja Wake, basi wangeruka mipaka katika ardhi. Lakini Anateremsha kwa kadiri ya Akitakacho. Hakika Yeye kwa Waja Wake Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:27)]
3-Kumbuka Kwamba Rizqi Ya Jannah Ni Bora Zaidi:
Kumbuka Neema nyingi mno za Allaah (عزّ وجلّ) zisizohesabika na Rizqi Zake nyingi duniani, bali kumbuka kwamba hata katika Jannah Atakuruzuku kwa mazuri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا هَـٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٥﴾
Na wabashirie wale walioamini na wakatenda mema, kwamba watapata Jannaat (bustani) zipitazo chini yake mito, kila watakaporuzukiwa humo katika matunda kuwa ni rizki husema: Haya ndiyo yale tuliyoruzukiwa kabla. Na wataletewa hali ya kuwa yanashabihiana, na watapata humo wake waliotakaswa, nao humo watadumu. [Al-Baqarah (2:25)]
4-Unachokitoa Katika Njia Ya Allaah Ar-Razzaaq Atakulipa Badala Yake:
Swadaqah haipunguzi rizki, bali Ar-Razzaaq Hurudisha badala yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ ۚ وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٣٩﴾
Sema: Hakika Rabb wangu Anamkunjulia rizki Amtakaye kati ya Waja Wake na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Na kitu chochote mtoacho, basi Yeye Atakilipa, Naye Ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Saba-a (34:39)]
5-Malaika Wanamwombea Anayetoa Kila Siku:
Kumbuka kwamba kila unapotoa katika Njia ya Ar-Razzaaq, Malaika wanakuombea badala.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَا مِنْ يَوْمٍ يُصْبِحُ الْعِبَادُ فِيهِ إِلاَّ مَلَكَانِ يَنْزِلاَنِ، فَيَقُولُ أَحَدُهُمَا: اللَّهُمَّ أَعْطِ مُنْفِقًا خَلَفًا، وَيَقُولُ الآخَرُ: اللَّهُمَّ أَعْطِ مُمْسِكًا تَلَفًا))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna siku yoyote wanayoamka waja isipokuwa Malaika wawili huteremka; mmoja wao husema: Yaa Allaah! Mpe anayetoa badala (ya alichotoa). Na mwingine husema: Yaa Allaah! Mpe anayezuia (mali yake) maangamizi.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
6-Usiyakodolee Macho Waliyopewa Wengine, Rizki Ya Rabb Wako Ni Bora:
Tambua, ee Mja wa Ar-Razzaaq: Muumini haangalii kwa tamaa starehe za dunia walizopewa wengine, kwani rizki ya Aakhirah ni bora na ya kudumu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّنْهُمْ زَهْرَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا لِنَفْتِنَهُمْ فِيهِ ۚ وَرِزْقُ رَبِّكَ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٣١﴾
Na wala usikodoe kabisa macho yako kwa yale ya starehe Tuliyowaneemesha baadhi ya makundi (ya kikafiri) miongoni mwao. Hayo ni mapambo ya uhai wa dunia tu, ili Tuwajaribu kwayo. Na rizki ya Rabb wako ni bora zaidi na ni yenye kudumu zaidi. [Twaahaa (20:131)]
7-Tahadhari! Usitumie Rizqi Yako Katika Haraam Wala Kwa Israaf:
Tambua, ee Mja wa Ar-Razzaaq: Usitumie rizqi yako katika yaliyoharamishwa, kama vile ulevi, kamari na mengineyo, wala katika yaliyokemewa, kama vile kutumia kwa israaf na tabdhiyr (ubadhirifu).2
عَنِ الْمُغِيرَةِ بْنِ شُعْبَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((إِنَّ اللَّهَ كَرِهَ لَكُمْ ثَلاَثًا: قِيلَ وَقَالَ، وَإِضَاعَةَ الْمَالِ، وَكَثْرَةَ السُّؤَالِ))
Amesimulia Al-Mughiyrah bin Shu’bah (رضي الله عنه): Nimemsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Hakika Allaah Amekuchukizieni mambo matatu: porojo za kusema ‘imesemwa’ na ‘amesema’, na kupoteza mali, na kukithirisha kuomba.” [Al-Bukhaariy]
8-Kumbuka Kila Baada Ya Swalaah Kwamba Hakuna Wa Kuzuia Alichokitoa Allaah:
Tambua, ee Mja wa Ar-Razzaaq: Du’aa ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ambayo tunaisoma kila siku katika nyiradi za baada ya Swalaah, inathibitisha kwamba hakuna atakayeweza kukuzuilia rizqi ya Allaah:
لا إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، اللَّهُمَّ لا مَانِعَ لِمَا أَعْطَيْتَ، وَلا مُعْطِيَ لِمَا مَنَعْتَ، وَلا يَنْفَعُ ذَا الْجَدِّ مِنْكَ الْجَدُّ
Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, Peke Yake, Hana mshirika; ni Wake Ufalme, na ni Zake Himdi, Naye Ni Muweza wa kila kitu. Yaa Allaah, hakuna mwenye kukizuia Ulichokitoa, wala mwenye kutoa Ulichokizuia, na wala utajiri wa mwenye utajiri haumnufaishi mbele Yako. [Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu’bah (رضي الله عنه) - Al-Bukhaariy na Muslim]
9-Omba Du’aa Ya Kutoshelezwa Kwa Halaal:
Muombe Allaah Ar-Razzaaq Akutosheleze kwa rizqi ya halaal kwa Du’aa ifuatayo:
اللَّهُمَّ اكْفِنِي بِحَلالِكَ عَنْ حَرَامِكَ، وَأَغْنِنِي بِفَضْلِكَ عَمَّنْ سِوَاكَ
Yaa Allaah, Nitosheleze kwa Vyako vya halaal dhidi ya Vyako ambavyo ni haraam, na Nitajirishe kwa Fadhila Zako kutokana na asiyekuwa Wewe. [At-Tirmidhiy, taz. Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy (2822)]
10-Omba Du’aa Nyinginezo Za Kujaaliwa Rizqi Na Baraka:
Tambua, ee Mja wa Ar-Razzaaq: Du’aa ifuatayo ni katika nyiradi za asubuhi:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ عِلْمًا نَافِعًا، وَرِزْقًا طَيِّبًا، وَعَمَلاً مُتَقَبَّلاً
Yaa Allaah, hakika mimi nakuomba ilimu yenye kunufaisha, na rizqi njema, na amali zenye kutakabaliwa. [Hadiyth ya Ummu Salamah (رضي الله عنها) - Ibn Maajah (925), taz. Swahiyh Ibn Maajah (1/152)]
Na katika kikao baina ya Sajdah mbili:
اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي، وَارْحَمْنِي، وَاجْبُرْنِي، وَاهْدِنِي، وَارْزُقْنِي
Yaa Allaah! Nighufurie, na Unirehemu, na Uniunge (Unirekebishie hali zangu), na Uniongoze, na Uniruzuku. [At-Tirmidhiy (284), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
Na Du’aa nyinginezo:
اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي، وَوَسِّعْ لِي فِي دَارِي، وَبَارِكْ لِي فِيمَا رَزَقْتَنِي
Yaa Allaah, Nighufurie dhambi zangu, na Nipanulie katika nyumba yangu, na Nibarikie katika Uliyoniruzuku. [At-Tirmidhiy, Ahmad - Swahiyh Al-Jaami’ (1265) - Zaad Al-Ma’aad (2/354)]
اللَّهُمَّ اجْعَلْ أَوْسَعَ رِزْقِكَ عَلَيَّ عِنْدَ كِبَرِ سِنِّي وَانْقِطَاعِ عُمُرِي
Yaa Allaah, Jaalia ukunjufu wa Rizqi Yako kwangu wakati wa uzee wangu, na kukatika umri wangu. [Al-Haakim, Swahiyh Al-Jaami’ (1/396), As-Silsilah Asw-Swahiyhah (1539)]
اللَّهُمَّ لَكَ الْحَمْدُ كُلُّهُ، اللَّهُمَّ لاَ قَابِضَ لِمَا بَسَطْتَ، وَلاَ بَاسِطَ لِمَا قَبَضْتَ، وَلاَ هَادِيَ لِمَا أَضْلَلْتَ، وَلاَ مُضِلَّ لِمَنْ هَدَيْتَ، وَلاَ مُعْطِيَ لِمَا مَنَعْتَ، وَلاَ مَانِعَ لِمَا أَعْطَيْتَ، وَلاَ مُقَرِّبَ لِمَا بَاعَدْتَ، وَلاَ مُبَاعِدَ لِمَا قَرَّبْتَ، اللَّهُمَّ ابْسُطْ عَلَيْنَا مِنْ بَرَكَاتِكَ وَرَحْمَتِكَ وَفَضْلِكَ وَرِزْقِكَ
Yaa Allaah, Himdi ni Zako zote. Yaa Allaah, hakuna mwenye kuzuia Ulivyovikunjua, wala mwenye kukunjua Ulivyovizuia, wala mwenye kumhidi Uliyempotoa, wala mwenye kumpotoa Uliyemhidi, wala mwenye kutoa Ulichokizuia, wala mwenye kuzuia Ulichokitoa, wala mwenye kukurubisha Ulichokiweka mbali, wala mwenye kuweka mbali Ulichokikurubisha. Yaa Allaah, Tukunjulie katika Baraka Zako, na Rehma Yako, na Fadhila Zako, na Rizqi Yako. [Ahmad, na Al-Bukhaariy katika Al-Adab Al-Mufrad (699), na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh katika Swahiyh Al-Adab Al-Mufrad (538)]
Na Allaah Mjuzi zaidi