Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah046 - Al-Fattaah

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 046 kati ya 103
Al-Fattaah — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Fattaah: Mwingi Wa Kufungua, Mwenye Kuhukumu

Yeye Ndiye Anayefungua Atakacho katika hazina za Ufalme Wake, Rehma Zake na rizqi Zake, kwa namna inayolingana na Hikmah Yake na Ujuzi Wake.

Jina Hili Al-Fattaah limetajwa katika Qur-aan mara mbili: mara moja kwa sura ya umoja, katika Kauli Yake (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ الْفَتَّاحُ الْعَلِيمُ ﴿٢٦﴾

Naye Ndiye Hakimu, Mjuzi wa yote. [Saba-a (34:26)]

Na mara moja kwa sura ya wingi, katika Kauli Yake:

وَأَنتَ خَيْرُ الْفَاتِحِينَ ﴿٨٩﴾

Nawe Ndiye Mbora wa Kuhukumu kuliko wote. [Al-A’raaf (7:89)]

Ufunguaji uko aina mbili:

Ya kwanza: Ufunguaji wa kihisia (unaohisika kwa viungo): Kama vile kufungua mlango na mfano wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَمَّا فَتَحُوا مَتَاعَهُمْ وَجَدُوا بِضَاعَتَهُمْ رُدَّتْ إِلَيْهِمْ ۖ

Walipofungua mizigo yao, walikuta bidhaa zao zimerudishwa kwao. [Yuwsuf (12:65)]

Ya pili: Ufunguaji wa kimaana unaofahamika kwa utambuzi: Kama vile kufungua (kuondosha) matatizo, kuondosha ufukara, kumsahilishia mwenye shida, na kufungua ilimu zilizofungika. Na Al-Fattaah linakuja pia kwa maana ya Al-Qadhwaa (kuhukumu),1 na hukumu ya kupambanua mambo,2 na linakuja kwa maana ya kunusuru, kama katika istiftaah (kuomba nusura).3

Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Fattaah, Naye Ni Mbora wa wenye kufungua.

1-Allaah Ndiye Aliyefungua (Aliyepambanua) baina ya haki na batili; Akaibainisha haki, na Akaibatilisha (أَدْحَضَ) batili na kuiondosha.4

2-Naye (تعالى) Ndiye Al-Fattaah Anayewafungulia Awliyaa Wake (vipenzi Wake) manufaa ya dunia na Dini. Huwafungulia Waja Wake Aliowateua, kwa Upole Wake na Utunzaji Wake, vifuli vya nyoyo zao ili wapate kumjua na kumpenda, na Hufungua macho (ya nyoyo) yao wapate kuiona haki, na wapate maarifa ya Rabb wao na hakika za imaan zinazotengeneza hali zao, na wanyooke katika njia iliyonyooka.5

3-Na Yeye Ndiye Anayewafungulia Waja Wake watiifu hazina za Ukarimu Wake na Ukwasi Wake, na Anawafungulia maadui Zake kinyume cha hayo; na hilo ni kwa Fadhila Zake na Uadilifu Wake.6

4-Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mbora wa wenye kufungua, yaani: Mbora wa wenye kuhukumu. Yeye Ndiye Mwadilifu Asiyedhulumu katika Hukumu Yake abadani.7 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu Du’aa ya Nabiy Shu’ayb (عليه السلام):

رَبَّنَا افْتَحْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ قَوْمِنَا بِالْحَقِّ وَأَنتَ خَيْرُ الْفَاتِحِينَ ﴿٨٩﴾

Rabb wetu! Hukumu baina yetu na baina ya kaumu yetu kwa haki, Nawe Ndiye Mbora wa Kuhukumu kuliko wote. [Al-A’raaf (7:89)]

Na Nabiy Nuwh (عليه السلام) alimuomba Rabb wake:

قَالَ رَبِّ إِنَّ قَوْمِي كَذَّبُونِ ﴿١١٧﴾ فَافْتَحْ بَيْنِي وَبَيْنَهُمْ فَتْحًا وَنَجِّنِي وَمَن مَّعِيَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١١٨﴾

Akasema: Rabb wangu! Hakika watu wangu wamenikadhibisha. Basi Hukumu baina yangu na baina yao (kwa) Hukmu (Yako), na Uniokoe mimi na wale walio pamoja nami miongoni mwa Waumini. [Ash-Shu’araa (26:117-118)]

Allaah Akamuokoa yeye na wafuasi wake, na Akawaangamiza wakaidi. Na hii ni katika Hukumu Yake (تعالى) duniani.

Na Rusuli (عليهم السلام) walimwelekea Allaah Al-Fattaah (سبحانه وتعالى) wakimuomba Ahukumu baina yao na baina ya kaumu zao wakaidi kutokana na mabishano na ugomvi uliotokea baina yao; Allaah Akawaitikia kwa kuwaangamiza majabari. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَاسْتَفْتَحُوا وَخَابَ كُلُّ جَبَّارٍ عَنِيدٍ ﴿١٥﴾

Na wakaomba ushindi (kwa Allaah), na akapita patupu kila (aliyejifanya) jabari, mkaidi. [Ibraahiym (14:15)]

5-Naye Ndiye Allaah Ambaye Huwafungulia Waja Wake wema Waumini falme na miji (kwa kuwapa ushindi).

Naye Amejinasibishia Mwenyewe al-futuwh (ushindi) ili Awatanabahishe Waja Wake kwamba nusura na ushindi ni kutoka Kwake Pekee, na si kutoka kwa mwengine. Amesema Akimwambia Rasuli Wake wa mwisho (صلى الله عليه وآله وسلم):

إِنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُّبِينًا ﴿١﴾

Hakika Tumekupa ushindi, ushindi bayana. [Al-Fat-h (48:1)]

Na Anasema katika Suwrah nyingine:

وَأُخْرَىٰ تُحِبُّونَهَا ۖ نَصْرٌ مِّنَ اللَّـهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ ۗ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٣﴾

Na jengine mlipendalo, (nalo ni) nusura kutoka kwa Allaah na ushindi wa karibu. Na wabashirie Waumini. [Asw-Swaff (61:13)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema siku ya (vita vya) Khaybar:

عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ يَوْمَ خَيْبَرَ: ((لأُعْطِيَنَّ هَذِهِ الرَّايَةَ غَدًا رَجُلاً يَفْتَحُ اللَّهُ عَلَى يَدَيْهِ، يُحِبُّ اللَّهَ وَرَسُولَهُ، وَيُحِبُّهُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ))

Amesimulia Sahl bin Sa’d (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema siku ya (vita vya) Khaybar: “Kwa yakini kesho nitampa bendera hii mtu ambaye Allaah Atamfungulia (Atamjaalia ushindi) kupitia mikono yake; anampenda Allaah na Rasuli Wake, na Allaah na Rasuli Wake wanampenda.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

6-Naye (عزّ وجلّ), kama vile Anavyofungua hazina za Fadhila Zake na Ukarimu Wake kwa Amtakaye katika Waja Wake, vilevile Hufungua (milango ya neema) kwa istidraaj (kuwavuta taratibu kuelekea adhabu), kuwapa mtihani, na kwa Hikmah Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَلَمَّا نَسُوا مَا ذُكِّرُوا بِهِ فَتَحْنَا عَلَيْهِمْ أَبْوَابَ كُلِّ شَيْءٍ حَتَّىٰ إِذَا فَرِحُوا بِمَا أُوتُوا أَخَذْنَاهُم بَغْتَةً فَإِذَا هُم مُّبْلِسُونَ ﴿٤٤﴾

Waliposahau yale waliyokumbushwa, Tuliwafungulia milango ya (neema za) kila kitu, mpaka walipofurahia kwa yale waliyopewa, Tukawachukua ghafla (kuwaadhibu), basi tahamaki wakawa wenye kukata tamaa. [Al-An’aam (6:44)]

7-Naye Ndiye Mfunguaji Mwenye Kunusuru: Ambaye Huinusuru haki na watu wa haki, na Huwadhalilisha watu wa batili na batili yao;8 hivyo Humnusuru Muumini dhidi ya kafiri, aliyedhulumiwa dhidi ya dhalimu, na wema dhidi ya uovu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِن تَسْتَفْتِحُوا فَقَدْ جَاءَكُمُ الْفَتْحُ ۖ وَإِن تَنتَهُوا فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَإِن تَعُودُوا نَعُدْ وَلَن تُغْنِيَ عَنكُمْ فِئَتُكُمْ شَيْئًا وَلَوْ كَثُرَتْ وَأَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٩﴾

Mkitafuta hukmu (enyi makafiri), basi imeshakujieni hukmu. Na mkikoma (uhalifu) basi hivyo ni kheri kwenu. Na mkirudia (kuhujumu) Nasi Tutarudia, na wala kundi lenu halitokufaeni kitu chochote japo likikithiri. Na hakika Allaah Yu Pamoja na Waumini. [Al-Anfaal (8:19)]9

8-Naye (سبحانه وتعالى) Ndiye Al-Fattaah Al-Hakam: Anayehukumu baina ya Waja Wake kwa haki na uadilifu duniani na Aakhirah. Na Siku ya Qiyaamah Atahukumu baina ya watu katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana duniani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ يَجْمَعُ بَيْنَنَا رَبُّنَا ثُمَّ يَفْتَحُ بَيْنَنَا بِالْحَقِّ وَهُوَ الْفَتَّاحُ الْعَلِيمُ ﴿٢٦﴾

Sema: Rabb wetu Atatukusanya, kisha Atahukumu baina yetu kwa haki, Naye Ndiye Hakimu, Mjuzi wa yote. [Saba-a (34:26)]

Na Allaah (تعالى) Ameiita Siku ya Qiyaamah kuwa ni Yawm Al-Fat-h (Siku ya Hukumu). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ يَوْمَ الْفَتْحِ لَا يَنفَعُ الَّذِينَ كَفَرُوا إِيمَانُهُمْ وَلَا هُمْ يُنظَرُونَ ﴿٢٩﴾

Sema: Siku ya hukmu haitowafaa wale waliokufuru imaan zao, na wala hawatopewa muhula. [As-Sajdah (32:29)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Fattaah:

1-Amini Na Tambua Kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee Mkononi Mwake ziko funguo za hazina za mbingu na ardhi; hakuna mwengine anayezifungua wala kuzifunga isipokuwa Yeye. Yeye Ndiye Anayefungua milango ya rizqi, Rehma na kheri nyingi kwa Waja Wake, na Anawafungulia wale waliofungikiwa mambo yao; hivyo Anamtajirisha fukara, Anawafariji wenye matatizo, na Anamsahilishia mwenye haja haja yake.10 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢﴾

Rehma yoyote Anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna wa kuizuia, na Anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake, Naye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Faatwir (35:2)]

Aayah hii ina athari nzuri kwako ikiwa wewe ni Muumini wa kweli; utatambua kwamba kila kinachokutokea kiko chini ya Uendeshaji wa Allaah Al-Fattaah. Funga milango kwa ajili Yake kwa kuacha tabia mbaya, marafiki waovu, au mahali pa kutenda maasi, hata kama itakusababishia mashaka ya kimwili, Naye Atakufungulia mlango wa kheri. Usikate tamaa wala usisalimu amri. Tambua kwamba Al-Fattaah daima Anaweza kukupa njia ya kutokea. Na jua kwamba mahusiano yote katika maisha yako yanafungamana na uhusiano wako na Allaah Al-Fattaah.

2-Rehma Anayoifungua Al-Fattaah Hakuna Wa Kuizuia:

Milango ya kheri iko Mkononi mwa Al-Fattaah; Akiifungua hakuna wa kuifunga. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢﴾

Rehma yoyote Anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna wa kuizuia, na Anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake, Naye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Faatwir (35:2)]

3-Mwamini Hakimu (Allaah):

Maisha yamejaa mabishano. Baadhi ya watu huwatuhumu wengine na kudai kuwa wao ndio walio kwenye haki. Nani Ndiye Hakimu? Nani Anayejua uhakika wa watu? Ni Al-Fattaah. Ifanye Qur-aan na Sunnah kuwa ndio hakimu wa matendo yako daima. Watu wanaweza kukusema vibaya na kukutuhumu kwa uongo, lakini ikiwa uko upande wa haki, usiogope, kwa sababu Allaah Al-Fattaah Ndiye Hakimu Mwadilifu. Na pia usiwe na haraka kuwahukumu wengine; Al-Fattaah Anaweza kuufungua moyo wa yeyote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبِّي عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ ﴿١٠﴾

Na katika lolote lile mlilokhitilafiana, basi hukumu yake irejesheni kwa Allaah. Huyo Ndiye Allaah Rabb wangu, Kwake nimetawakali, na Kwake naelekea kwa mambo yangu yote. [Ash-Shuwraa (42:10)]

4-Al-Fattaah Atahukumu Baina Ya Waja Wake Kwa Haki:

Miongoni mwa maana za Al-Fattaah ni Hakimu Anayehukumu baina ya Waja Wake kwa haki na kuwatenganisha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ يَجْمَعُ بَيْنَنَا رَبُّنَا ثُمَّ يَفْتَحُ بَيْنَنَا بِالْحَقِّ وَهُوَ الْفَتَّاحُ الْعَلِيمُ ﴿٢٦﴾

Sema: Rabb wetu Atatukusanya, kisha Atahukumu baina yetu kwa haki, Naye Ndiye Hakimu, Mjuzi wa yote. [Saba-a (34:26)]

5-Kuwa Na Ikhlaasw:

Ufunguaji bora kuliko yote ni kufunguliwa moyo. Al-Fattaah Hufungua nyoyo zilizokuwa zimefungika, kama moyo wa ‘Umar bin al-Khatwtwaab (رضي الله عنه) ambao kabla (ya kusilimu kwake) ulikuwa umejaa chuki dhidi ya Waislamu. Baadhi ya watu husema: Nasoma Qur-aan lakini sielewi neno hata moja! Lakini baada ya muda huanza kuelewa; huanza kutafuta majibu, kuhifadhi, kuingiliana nayo, kuifurahikia, na kuyalingania Maneno ya Allaah. Fanya bidii na jitahidi kuwa na ikhlaasw ili Al-Fattaah Akufungulie mlango wa ilimu, mlango wa ukuruba Naye, na mlango wa kuridhika katika maisha haya. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا ﴿٢٤﴾

Je, hawaizingatii Qur-aan! Au nyoyoni (mwao) mna kufuli? [Muhammad (47:24)]

6-Imaan Na Taqwa Hufungua Baraka Za Mbingu Na Ardhi:

Tambua, ee Mja wa Al-Fattaah: Njia ya kufunguliwa milango ya baraka ni imaan na taqwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَىٰ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَيْهِم بَرَكَاتٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَلَـٰكِن كَذَّبُوا فَأَخَذْنَاهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٩٦﴾

Na lau kama watu wa miji wangeliamini na wakashikamana na taqwa, Tungeliwafungulia baraka tele kutoka mbinguni na ardhini, lakini walikadhibisha, Nasi Tukawachukua kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma. [Al-A’raaf (7:96)]

7-Jifunze Suwrah Al-Faatihah (Ufunguzi):

Jifunze kuisoma, kuihifadhi na kuielewa Suwrah Al-Faatihah; Suwrah inayofungua Kitabu cha Al-Fattaah.

Na jifunze Tafsiyr ya Suwrah hii tukufu; na unapoisoma katika Swalaah hakikisha unasita baada ya kila Aayah, na utekeleze mafunzo yake katika maisha yako ya kila siku.

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: بَيْنَمَا جِبْرِيلُ قَاعِدٌ عِنْدَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) سَمِعَ نَقِيضًا مِنْ فَوْقِهِ، فَرَفَعَ رَأْسَهُ فَقَالَ: ((هَذَا بَابٌ مِنَ السَّمَاءِ فُتِحَ الْيَوْمَ لَمْ يُفْتَحْ قَطُّ إِلاَّ الْيَوْمَ، فَنَزَلَ مِنْهُ مَلَكٌ فَقَالَ: هَذَا مَلَكٌ نَزَلَ إِلَى الأَرْضِ لَمْ يَنْزِلْ قَطُّ إِلاَّ الْيَوْمَ، فَسَلَّمَ وَقَالَ: أَبْشِرْ بِنُورَيْنِ أُوتِيتَهُمَا لَمْ يُؤْتَهُمَا نَبِيٌّ قَبْلَكَ: فَاتِحَةُ الْكِتَابِ، وَخَوَاتِيمُ سُورَةِ الْبَقَرَةِ، لَنْ تَقْرَأَ بِحَرْفٍ مِنْهُمَا إِلاَّ أُعْطِيتَهُ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Jibriyl (عليه السلام) alipokuwa amekaa pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), alisikia mlio juu yake, akainua kichwa chake, akasema: “Huu ni mlango wa mbinguni uliofunguliwa leo, haujapata kufunguliwa kamwe isipokuwa leo.” Akateremka kupitia mlango huo Malaika, (Jibriyl) akasema: “Huyu ni Malaika aliyeteremka ardhini, hajapata kuteremka kamwe isipokuwa leo.” Akasalimia na akasema: “Pokea bishara ya nuru mbili ulizopewa ambazo hajapewa Nabiy yeyote kabla yako: Faatihatul-Kitaab na Aayah za mwisho za Suwrah Al-Baqarah. Hutasoma herufi yoyote katika hizo mbili isipokuwa utapewa (ulichokiomba ndani yake).” [Muslim]

8-Wanufaishe Wengine:

Wafungulie wengine milango ya matendo yako mema, na jishughulishe katika miradi yenye manufaa kwa wengine. Ikiwa una ujuzi fulani, uendeleze na uwasaidie wengine kwa ujuzi huo, ili kwa Tawfiyq ya Al-Fattaah wote waweze kushirikiana kufungua milango ya kila lililo jema kwa jamii. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. [Al-Maaidah (5:2)]

9-Muombe Al-Fattaah:

Kila mlango unapofungwa mbele yako, mkumbuke Al-Fattaah na umuombe Akufungulie. Hili ni katika hali zote, ziwe nzito au nyepesi; hata kama simu yako, pochi yako, au kitu kingine chochote, kiwe cha thamani au si cha thamani, kimepotea. Ukifungua jengo jipya, ukitaka kuoa (au kuolewa), au ukitaka kufanya jambo lolote, muombe Al-Fattaah msaada na tawfiyq. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ ﴿٦٠﴾

Na Rabb wenu Amesema: Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu wataingia Jahannam wadhalilike. [Ghaafir (40:60)]

Na anza kila jambo linaloruhusika kwa Jina Lake kwa kusema:

بِسْمِ اللَّهِ

Kwa Jina la Allaah.

Na pia unapohisi unyonge, au unapohisi kuwa huna ufahamu wa Dini, muombe Akufungulie moyo wako na nyoyo za wapendwa wako. Mojawapo ya Du’aa za watu wema waliotutangulia ilikuwa: “Allaah Akufungulie milango ya kheri.”

10-Omba Du’aa Za Kufunguliwa Milango Ya Kheri:

Omba du’aa, ee ndugu Muislamu, Al-Fattaah Akufungulie milango ya Rehma Yake na Fadhila Zake.

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametufundisha Du’aa kadhaa za kufunguliwa milango ya kheri na kadhaalika. Miongoni mwazo ni:

عَنْ أَبِي حُمَيْدٍ أَوْ عَنْ أَبِي أُسَيْدٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِذَا دَخَلَ أَحَدُكُمُ الْمَسْجِدَ فَلْيَقُلِ: اللَّهُمَّ افْتَحْ لِي أَبْوَابَ رَحْمَتِكَ، وَإِذَا خَرَجَ فَلْيَقُلِ: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ مِنْ فَضْلِكَ))

Amesimulia Abu Humayd au Abu Usayd (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mmoja wenu anapoingia Msikitini aseme:

اللَّهُمَّ افْتَحْ لِي أَبْوَابَ رَحْمَتِكَ

Yaa Allaah, Nifungulie milango ya Rehma Zako

Na anapotoka aseme:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ مِنْ فَضْلِكَ

Yaa Allaah, hakika mimi nakuomba katika Fadhila Zako.” [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kuhusu Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Rabb wetu! Tufungulie baina yetu na baina ya kaumu yetu kwa haki.” Amesema Ibn ‘Abbaas: “Hukumu baina yetu na kaumu yetu.” At-Tafsiyr Asw-Swahiyh (2/336).
  • 2Al-Mufradaat (380).
  • 3Lisaan Al-Arab (5/3337).
  • 4Tafsiyr Asmaa-Allaah Al-Husnaa (39).
  • 5Angalia Tafsiyr As-Sa’diy (5/489) na Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam (34).
  • 6Al-Haqq Al-Waadhwih Al-Mubiyn (84).
  • 7Tafsiyr Ibn Kathiyr (3/444).
  • 8Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam (34).
  • 9Sha-nu Ad-Du’aa (56).
  • 10Sha-nu Ad-Du’aa (56) na Al-Asnaa Fiy Sharh Al-Asmaa Al-Husnaa (1/220).