Al-Hafiydhw: Mwenye Kuhifadhi
Yeye Ndiye Aliyehifadhi Alichokiumba, na Akawahifadhi Awliyaa Wake (vipenzi Wake) wasitumbukie katika madhambi na maangamizi, na Amewadhibitia waja amali zao na Atawalipa kwazo kwa Fadhila Zake na Uadilifu Wake. Na al-hifdh (kuhifadhi) kilugha lina maana ya kukusanya na kutunza, na huenda likawa na maana ya amana.
Jina Hili Al-Hafiydhw limetajwa waziwazi katika Qur-aan mara tatu tu, likimhusu Allaah (سبحانه وتعالى). Aayah hizo ni:
إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَفِيظٌ ﴿٥٧﴾
Hakika Rabb wangu Ni Mwenye Kuhifadhi kila kitu. [Huwd (11:57)]
وَرَبُّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَفِيظٌ ﴿٢١﴾
Na Rabb wako Ni Mwenye Kuhifadhi kila kitu. [Saba-a (34:21)]
وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ اللَّـهُ حَفِيظٌ عَلَيْهِمْ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِوَكِيلٍ ﴿٦﴾
Na wale waliojichukulia badala Yake marafiki wandani na walinzi, Allaah Anayahifadhi matendo yao, nawe si mdhamini wao. [Ash-Shuwraa (42:6)]
Ama sura nyinginezo zinazotokana na neno hilo hilo zinazoonyesha Hifadhi Yake (تعالى), kama vile حَافِظًا, لَحَافِظُونَ na خَيْرٌ حَافِظًا, zimekuja katika sehemu nyinginezo mbalimbali za Qur-aan.
Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mbora wa wenye kuhifadhi, Ambaye hakipotei chochote Anachokihifadhi. Na miongoni mwa Hifadhi Yake ni:
1-Anazihifadhi mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake, zibakie muda utakaobakia; hazianguki wala hazitoweki. Na wala haimuemei kuzihifadhi, bali Anazihifadhi bila ya mashaka wala taabu, kwa Ukamilifu wa Uwezo Wake na Nguvu Zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا ۚ وَلَئِن زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِّن بَعْدِهِ ۚ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤١﴾
Hakika Allaah Anazuia mbingu na ardhi zisitoweke. Na zikitoweka, hakuna yeyote wa kuzishikilia baada Yake. Hakika Yeye daima Ni Mvumilivu, Mwingi wa Kughufuria. [Faatwir (35:41)]
2-Na Ameihifadhi Al-Ka’bah, nayo ni miongoni mwa Aayaat (Ishara) Zake kubwa; nyumba ya mawe iliyo katika bonde lisilo na mimea, Allaah Ameihifadhi isitoweke ili ibakie kuwa ni shahidi wa Uwezo Wake na Hifadhi Yake.
3-Na Amedhamini kukihifadhi Kitabu Chake kitukufu kisipotoshwe wala kubadilishwa katika zama zote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾
Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka Ndio Wenye Kuihifadhi. [Al-Hijr (15:9)]
Na hivi leo baada ya karne kumi na nne, na baada ya fitnah nzito na bid’ah zilizozushwa, wote wameshindwa kuigusa Ahadi ya Allaah Al-Hafiydhw ya kuihifadhi Qur-aan; hawakuweza kubadilisha hata herufi moja ndani yake.
4-Naye Ndiye Anayezihifadhi amali za Waja Wake; za kheri na za shari, za siri na za dhahiri, ndogo na kubwa. Amezidhibiti kauli zao na Anazijua nia zao, wala hakifichiki Kwake chochote hata kikiwa ni chembe ardhini au mbinguni, na Atawalipa kwazo Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَا يَعْزُبُ عَنْهُ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَلَا أَصْغَرُ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرُ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٣﴾
Hakuna kinachofichika Kwake hata chenye uzito wa chembe (kama atomu) mbinguni wala ardhini, wala kidogo zaidi kuliko hicho, wala kikubwa zaidi isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha. [Saba-a (34:3)]
5-Na Anawahifadhia waja amali zao hata kupitia viungo vyao; masikio yao, macho yao na ngozi zao, ili viwashuhudie Siku ya Miadi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٠﴾ وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّـهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢١﴾
Mpaka watakapoufikia, yatashuhudia dhidi yao masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. Na wataziambia ngozi zao: Mbona mnashuhudia dhidi yetu? Zitasema: Ametutamkisha Allaah Ambaye Ametamkisha kila kitu, Naye Ndiye Aliyekuumbeni mara ya kwanza, na Kwake mtarejeshwa. [Fusw-Swilat (41:20-21)]
6-Allaah Pekee Ndiye Al-Hafiydhw juu ya viumbe Vyake, wala Hamshirikishi katika hilo yeyote, hata Rusuli Wake; kama alivyosema pia Nabiy Shu’ayb (عليه السلام) kwa kaumu yake kwamba yeye si mwenye kuwahifadhi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) Akimwambia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم):
فَإِنْ أَعْرَضُوا فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا ۖ إِنْ عَلَيْكَ إِلَّا الْبَلَاغُ ۗ
Wakikengeuka, basi Hatukukutuma uwe mwenye kuwahifadhi. Si juu yako isipokuwa ubalighisho (wa Risala). [Ash-Shuwraa (42:48)]
7-Allaah Pekee Ndiye Anayemhifadhi binaadam na shari, maafa na maangamizi, na Anamkinga na mahali pa mauti mabaya. Na Amewawekea waja Malaika wanaowahifadhi kwa Amri Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِن كُلُّ نَفْسٍ لَّمَّا عَلَيْهَا حَافِظٌ ﴿٤﴾
Hakuna nafsi yoyote isipokuwa inayo (Malaika) mhifadhi juu yake. [Atw-Twaariq (86:4)]
8-Na Hifadhi ya Allaah kwa Waja Wake ni ya aina mbili:
Ya kwanza: Hifadhi ya jumla: Nayo ni kuwahifadhi waja wote kwa kuwawepesishia mahitaji yao, na kuwaongoza katika maslahi yao, na kuwapa hidaya ya jumla. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴿٥٠﴾
(Muwsaa) akasema: Rabb wetu ni Yule Aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha Akakiongoza. [Twaahaa (20:50)]
Ya pili: Hifadhi maalumu: Nayo ni kwa Awliyaa Wake waliohifadhi Wasia Wake, na wakamuogopa hali ya kuwa hawamuoni. Huwahifadhia imaan yao isipungue wala isiharibike, na Huwalinda na makosa. Nayo ni ya aina mbili:
a-Kuwahifadhia dunia yao: Huwahifadhia nafsi zao, watoto wao, wake zao na mali zao, na Huwawekea Malaika wanaowahifadhi kwa Amri Yake, kama ilivyotangulia.
b-Kuwahifadhia Dini yao na imaan yao: Huwahifadhi katika uhai wao na shubuhaat (utata) zenye kupoteza, na matamanio ya haramu, na kila kinachodhuru imaan yao au kuondosha yakini yao; Huwaokoa nayo na Huwatoa salama. Na Huwahifadhi na maadui zao miongoni mwa majini na watu; Huwanusuru dhidi yao na Huwalinda na vitimbi vyao. Na wanapokufa, Huwafisha wakiwa na imaan. Na kwa kadiri ya imaan ya mja, ndivyo Ar-Rahmaan Anavyomhifadhi.1
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Hafiydhw:
1-Tambua Kwamba Al-Hafiydhw Anahifadhi Kila Amali Yako:
Allaah Al-Hafiydhw Anajua kila unalolifanya kwa Ujuzi Wake, na Amewawekea waja Malaika wanaojua na kuandika yale wanayoyafanya. Hata amali ndogo kabisa, kama kuhudhuria darsa ya Dini, kukaa kwa adabu na kuandika mafunzo, Al-Hafiydhw Ataihifadhi na Ataithamini. Ukitambua hilo, utakuwa Mja wa Allaah (عزّ وجلّ) kwa kweli, wala si mja wa watu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ ﴿١٠﴾ كِرَامًا كَاتِبِينَ ﴿١١﴾ يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ ﴿١٢﴾
Na hakika juu yenu bila shaka kuna wenye kuhifadhi (na kuchunga). Watukufu wanaoandika (amali). Wanajua yale myafanyayo. [Al-Infitwaar (82:10-12)]
2-Muhifadhi Allaah Naye Atakuhifadhi:
Tambua, ee Mja wa Al-Hafiydhw: Anayemhifadhi Allaah duniani, Allaah Atamhifadhi na Adhabu Yake Aakhirah. Yaani: Hifadhi Amri Zake kwa kuzitekeleza, na Makatazo Yake kwa kuyaepuka, na Mipaka Yake kwa kutokuivuka, Naye Atakuhifadhi katika nafsi yako, Dini yako, mali yako, watoto wako, na katika kila Alichokupa kwa Fadhila Zake. Na Allaah Amewasifu wanaohifadhi Mipaka Yake na Amewabashiria kufuzu kukubwa.
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: كُنْتُ خَلْفَ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَوْمًا فَقَالَ: ((يَا غُلاَمُ إِنِّي أُعَلِّمُكَ كَلِمَاتٍ: احْفَظِ اللَّهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظِ اللَّهَ تَجِدْهُ تُجَاهَكَ))
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Siku moja nilikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), akaniambia: “Yaa kijana! Hakika mimi nitakufundisha maneno: Mhifadhi Allaah Naye Atakuhifadhi. Mhifadhi Allaah utamkuta yupo mbele yako.” [At-Tirmidhiy (2516), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
Abu Atw-Twayyib Atw-Twabariy, mmoja wa ‘Ulamaa wa zamani, alikuwa amefikia umri wa takriban miaka mia moja, na alikuwa bado ana nguvu za mwili kama za kijana. Siku moja, baada ya safari ya kuchosha, aliruka kutoka katika jahazi hadi nchi kavu, watu wakastaajabu. Akasema: “Viungo hivi tuliviepusha na maasi ya Allaah tulipokuwa vijana, basi Allaah Akatuhifadhia katika uzee wetu.”2
3-Mche Al-Hafiydhw:
Yeye pia Ni Al-Hafiydhw unapotenda maovu. Kumbuka kwamba hata kosa lako unaloliona ni dogo, Anaona, Analihifadhi na Atakulipa kwalo isipokuwa ukitubu. Mfano katika Swalaah unahitaji khushuw’ (unyenyekevu), nayo ni kuhudhurisha moyo pamoja na kufahamu (unayoyasoma). Huenda katika rukuu moja tu ukamkumbuka Allaah, na muda uliobakia moyo wako ukawa umeshughulika au umeghafilika. Allaah Ni Al-Hafiydhw, Anajua kwamba ulimkumbuka katika rukuu hiyo tu, basi Atakuhifadhia kumbukumbu hiyo na Atakulipa kwa mujibu wake. Na kwa kadiri amali yako ilivyo njema au ovu, Al-Hafiydhw Atakulipa thawabu au Atakuadhibu. Kwa hiyo Jina hili linakupa raja-a (matumaini) na khawf (khofu) kwa pamoja. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ﴿٧﴾ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ ﴿٨﴾
Basi yule atakayetenda kheri uzito wa chembe (kama atomu) ataiona. Na yule atakayetenda shari uzito wa chembe (kama atomu) ataiona. [Az-Zalzalah (99:7-8)]
4-Kumbuka Ahadi Ya Allaah Kwa Kila Mwenye Kuhifadhi:
Allaah Amewaahidi Waja Wake wanaohifadhi Mipaka Yake ahadi watakayoiona Aakhirah kwa macho yao, ikiwa mbele yao. Kisha baada ya kuiona, Atawaambia: Iingieni (Jannah) kwa salama; hiyo ndio siku yenye kudumu, na watapata humo wayatakayo, na Kwake kuna ziada. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ غَيْرَ بَعِيدٍ ﴿٣١﴾ هَـٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِكُلِّ أَوَّابٍ حَفِيظٍ ﴿٣٢﴾
Na italetwa karibu Jannah kwa wenye taqwa isiwe mbali. (Itasemwa): Haya ndiyo yale mliyoahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Allaah kwa yote, mwenye kuhifadhi vyema (Amri za Allaah). [Qaaf (50:31-32)]
5-Mshukuru Al-Hafiydhw:
Al-Hafiydhw Anauhifadhi mwili wako kwa namna ya ajabu; tafakari tu lau damu ingetiririka ovyo katika ubongo wako! Mshukuru Al-Hafiydhw kwa jinsi Anavyokuhifadhi na kukulinda kwa njia ambazo hata huzitambui. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ ﴿٦﴾ الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ ﴿٧﴾ فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ ﴿٨﴾
Ee binaadam! Nini kilichokughuri hata umkufuru Rabb wako Mkarimu? Ambaye Amekuumba, Akakusawazisha (umbo, sura, viungo), na Akakulinganisha sawa. Katika sura Aliyotaka Akakutengeneza. [Al-Infitwaar (82:6-8)]
6-Tafakari Mazingira Yako Uzidishe Kumuadhimisha Al-Hafiydhw:
Tazama pembezoni mwako ustaajabu jinsi Al-Hafiydhw Anavyoweza kuhifadhi hata viumbe vikubwa kabisa. Yeye Ndiye Aliyeihifadhi mbingu isituangukie. Na sisi, kwa Idhini Yake, tunabuni njia za kuhifadhi hata chakula katika majokofu na kwa chumvi ili tukitumie kwa muda mrefu zaidi, kama tunavyohifadhi pesa benki. Allaah Ni Al-Hafiydhw, Naye Ndiye Anayewaongoza wanaadam kwenye njia za kuhifadhi chakula, afya na mali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَزَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِمَصَابِيحَ وَحِفْظًا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ﴿١٢﴾
Na Tukaipamba mbingu ya dunia kwa taa na hifadhi. Hayo ni Takdiri ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote. [Fusw-Swilat (41:12)]
7-Harakisha Kutubia Kwa Al-Hafiydhw:
Jina hili linapaswa kukutikisa zaidi hata kuliko Jina Al-‘Aliym, kwa sababu Al-Hafiydhw halimaanishi tu kwamba Anajua kila kitu, bali pia Anakumbuka hata mambo madogo kabisa. Unahitaji Maghfirah ya Al-Hafiydhw; kwa hiyo mojawapo ya athari muhimu za Jina hili ni kukufanya usichelewe kutubia, bali uharakishe kutubu.
عَنْ أَبِي مُوسَى (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ يَبْسُطُ يَدَهُ بِاللَّيْلِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ، وَيَبْسُطُ يَدَهُ بِالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيْلِ، حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا))
Amesimulia Abu Muwsaa (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah (عزّ وجلّ) Hukunjua Mkono Wake usiku ili atubie aliyekosea mchana, na Hukunjua Mkono Wake mchana ili atubie aliyekosea usiku, mpaka jua lichomoze kutoka magharibi yake.” [Muslim]
8-Tahadhari! Usafishe Moyo Wako Na Ulinde Ulimi Wako:
Kwa mfano, unamsema vibaya mtu kwa sababu tu humpendi. Al-Hafiydhw Hatasahau ulilolifanya; ujuzi huo umehifadhiwa Kwake. Na huenda baada ya muda ukawekwa katika hali hiyo hiyo; ukawa huna hatia lakini mtu akakutuhumu kwa dhulma au akakusema kwa yasiyo ya kweli. Hilo linapotokea, ni fursa kwako kukumbuka na kutubia kwa uliyomfanyia mwenzako. Al-Hafiydhw Anakupa mtihani huo ili Akulee, kwa kuwa ujuzi huo umehifadhiwa Kwake ilhali wewe huenda umeusahau au uliuona ni jambo dogo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ ﴿١٨﴾
Hatamki kauli yoyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf (50:18)]
9-Hifadhi Swalaah Zako:
Tambua kwamba swalaah ni katika faradhi kubwa kabisa alizoamrishwa mja, na haikuja katika Qur-aan Amri ya Al-Hafiydhw kwa tamko la حَافِظُوا (hifadhini) isipokuwa katika Aayah ya kuhifadhi Swalaah. Na siri yake ni kwamba Swalaah ni kiungo baina ya mja na Rabb wake, na kwa kadiri ya uhusiano wa mja na Rabb wake, ndivyo anavyofunguliwa kheri na kufungiwa shari. Swalaah ina athari ya ajabu katika afya ya mwili na moyo, na katika kumhifadhi mwenye kuiswali. Na miongoni mwa sifa za Waumini, Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٣٤﴾ أُولَـٰئِكَ فِي جَنَّاتٍ مُّكْرَمُونَ ﴿٣٥﴾
Na ambao Swalaah zao wao wanazihifadhi. Hao watakuwa kwenye Jannah wakikirimiwa. [Al-Ma’aarij (70:34-35)]
10-Hifadhi Viapo Vyako:
Imekuja amri ya pili kutoka kwa Allaah (تعالى) kwa Waja Wake ya kuhifadhi viapo, kwa kutokufanya wepesi katika kuapa. Na kuhifadhi viapo ni dalili ya imaan ya mja. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ۚ
Na hifadhini viapo vyenu. [Al-Maaidah (5:89)]
11-Hifadhi Tupu Yako:
Na katika amri ya tatu ya kuhifadhi, Allaah (تعالى) Amewaamrisha Waja Wake kuhifadhi miili yao wasitumbukie katika zinaa. Na Amewasifu wenye kufanya hivyo kuwa ni wenye kufaulu mwanzoni mwa Suwrah Al-Muuminuwn, na Amewataja katika sifa za watu wa Jannah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٢٩﴾
Na ambao wanahifadhi tupu zao. [Al-Ma’aarij (70:29)]
12-Jifunze Na Uhifadhi Qur-aan:
Fanya bidii uwe miongoni mwa wanaokihifadhi Kitabu Chake, Qur-aan, kwa kukihifadhi moyoni. Na unapokihifadhi Kitabu Chake, muombe Al-Hafiydhw Akuhifadhie na Akidumishe katika akili yako.
عَنْ عُثْمَانَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((خَيْرُكُمْ مَنْ تَعَلَّمَ الْقُرْآنَ وَعَلَّمَهُ))
Amesimulia ‘Uthmaan (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mbora wenu ni yule aliyejifunza Qur-aan na akaifundisha.” [Al-Bukhaariy]
13-Hifadhi Wema Wa Watu Na Uwakumbuke:
Tambua, ee Mja wa Al-Hafiydhw: Mojawapo ya sifa za Waumini ni kuwajali na kuwakumbuka wengine. Huenda ulikutana na mtu mara moja ukamuazima kalamu yako, kisha akakumbuka hilo baada ya miaka mingi; ungefurahi sana. Na mfano bora kabisa wa sifa hii ya kukumbuka wema ni Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye hakupata kumsahau Khadiyjah (رضي الله عنها).
عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: مَا غِرْتُ عَلَى أَحَدٍ مِنْ نِسَاءِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) مَا غِرْتُ عَلَى خَدِيجَةَ، وَمَا رَأَيْتُهَا، وَلَكِنْ كَانَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم) يُكْثِرُ ذِكْرَهَا، وَرُبَّمَا ذَبَحَ الشَّاةَ ثُمَّ يُقَطِّعُهَا أَعْضَاءً، ثُمَّ يَبْعَثُهَا فِي صَدَائِقِ خَدِيجَةَ
Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Sijapata kumuonea wivu yeyote miongoni mwa wake za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kama nilivyomuonea wivu Khadiyjah, ingawa sikupata kumuona; lakini Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akimtaja mara nyingi. Na huenda akachinja mbuzi, kisha akamkata vipande vipande, kisha akavipeleka kwa marafiki wa Khadiyjah. [Al-Bukhaariy]
14-Omba Hifadhi Ya Allaah Kwa Kusoma Aayatul-Kursiy:
Miongoni mwa njia za kupata Hifadhi ya Al-Hafiydhw ni kusoma Aayatul-Kursiy unapokwenda kulala.
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: وَكَّلَنِي رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) بِحِفْظِ زَكَاةِ رَمَضَانَ، فَأَتَانِي آتٍ فَجَعَلَ يَحْثُو مِنَ الطَّعَامِ، فَأَخَذْتُهُ فَقُلْتُ: لأَرْفَعَنَّكَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم). فَذَكَرَ الْحَدِيثَ فَقَالَ: إِذَا أَوَيْتَ إِلَى فِرَاشِكَ فَاقْرَأْ آيَةَ الْكُرْسِيِّ، لَنْ يَزَالَ عَلَيْكَ مِنَ اللَّهِ حَافِظٌ، وَلاَ يَقْرَبُكَ شَيْطَانٌ حَتَّى تُصْبِحَ. فَقَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((صَدَقَكَ وَهُوَ كَذُوبٌ، ذَاكَ شَيْطَانٌ))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniwakilisha kuhifadhi Zakaah ya Ramadhwaan (Zakaatul-Fitwr). Akaja mtu akaanza kuteka chakula (cha Zakaah) kwa mikono miwili. Nikamkamata na kumwambia: Nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). (Kisha akahadithia yote), na (huyo mwizi) akasema: Utakapoingia kitandani kulala, soma Aayatul-Kursiy, kwani mhifadhi kutoka kwa Allaah atakuhifadhi, na shaytwaan hatokukaribia mpaka asubuhi. Hapo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Amekwambia ukweli japokuwa yeye ni muongo; huyo ni shaytwaan.” [Al-Bukhaariy]
15-Muombe Al-Hafiydhw Akuhifadhi:
Omba du’aa, ee ndugu Muislamu, Al-Hafiydhw Akuhifadhi pande zote.
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amewafundisha Ummah wake kuomba Hifadhi ya Allaah kwa Du’aa hii asubuhi na jioni:
اللَّهُمَّ احْفَظْنِي مِنْ بَيْنِ يَدَيَّ وَمِنْ خَلْفِي وَعَنْ يَمِينِي وَعَنْ شِمَالِي وَمِنْ فَوْقِي، وَأَعُوذُ بِعَظَمَتِكَ أَنْ أُغْتَالَ مِنْ تَحْتِي
Yaa Allaah, Nihifadhi mbele yangu, na nyuma yangu, na kuliani kwangu, na kushotoni kwangu, na juu yangu, na najikinga kwa Utukufu Wako nisiangamizwe kutoka chini yangu. [Sehemu ya Hadiyth ya Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) - Abuu Daawuwd (5074), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]
Na Allaah Mjuzi zaidi