Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah053 - Al-Kariym

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 053 kati ya 103
Al-Kariym — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Kariym: Mkarimu

Al-Kariym Ni Mwingi wa kheri na kutoa; Anatoa Anachotaka kumpa Amtakaye, kwa namna Atakayo, kwa kuombwa na bila ya kuombwa. Anasamehe dhambi na kusitiri kasoro. Kheri Yake ni nyepesi na kilichoko Kwake ni karibu kukipata; hakuna pazia baina Yake na mja, Naye Yuko karibu na anayemwitikia. Yeye Ni Al-Kariym Al-‘Aziyz, Mwenye cheo kikubwa, Aliyetakasika na kila upungufu. Na al-karam kilugha ni wepesi wa nafsi kuitikia na kutoa, nacho ni kinyume cha ubakhili na unyonge wa tabia.

Jina hili la Allaah Al-Kariym limetajwa katika Qur-aan mara tatu tu. Allaah (سبحانه وتعالى) Amesema:

وَمَن شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّي غَنِيٌّ كَرِيمٌ

Na yeyote yule anayeshukuru, basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na yeyote yule asiyekuwa na shukurani, basi hakika Rabb wangu ni Mkwasi, Mkarimu. [An-Naml (27:40)]

Na neno kariym ni kinachokusanya kheri zote, utukufu na fadhila. Na imekuja Hadiyth kwamba Al-Kariym bin Al-Kariym bin Al-Kariym bin Al-Kariym ni Yuwsuf bin Ya‘quwb bin Is-haaq bin Ibraahiym (عليهم السلام) [Al-Bukhaariy], kwa sababu amekusanya utukufu wa Unabii, ilimu na uzuri. Na kitu kizuri husifiwa kuwa ni kariym, kama mimea mizuri, Anaposema (سبحانه وتعالى):

أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَى الْأَرْضِ كَمْ أَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ ﴿٧﴾

Je, hawaioni ardhi? Mimea mingapi Tumeiotesha humo ya kila aina nzuri? [Ash-Shu’araa (26:7)]

Na huja kwa maana ya mtukufu, kama Anavyosema (سبحانه وتعالى):

فَلَمَّا سَمِعَتْ بِمَكْرِهِنَّ أَرْسَلَتْ إِلَيْهِنَّ وَأَعْتَدَتْ لَهُنَّ مُتَّكَأً وَآتَتْ كُلَّ وَاحِدَةٍ مِّنْهُنَّ سِكِّينًا وَقَالَتِ اخْرُجْ عَلَيْهِنَّ ۖ فَلَمَّا رَأَيْنَهُ أَكْبَرْنَهُ وَقَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ وَقُلْنَ حَاشَ لِلَّـهِ مَا هَـٰذَا بَشَرًا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا مَلَكٌ كَرِيمٌ ﴿٣١﴾

(Mke wa ‘aziyz) aliposikia hila zao (za kumchafulia jina zaidi), aliwaalika na akawaandalia hafla (na matakia), na akampa kila mmoja wao kisu. Kisha akasema: Tokeza mbele yao. Basi walipomuona (Yuwsuf) walimpa haiba na utukuzo, wakajikatakata mikono yao, na wakasema: Haasha li-LLaah! (Ametakasika Allaah Mkamilifu wa Kuumba). Huyu si mtu! Hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu. [Yuwsuf (12:31)]

Na wakati mwingine kwa maana ya aliye bora na mwenye hadhi zaidi, kama katika Al-Hujuraat (Rejea chini: Faida namba 2, Al-Hujuraat (49:13)), na kama Anavyosema (سبحانه وتعالى):

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا ﴿٧٠﴾

Na kwa yakini Tumewakirimu wana wa Aadam, na Tukawabeba katika ardhi kavu na baharini, na Tukawaruzuku katika vizuri na Tukawafadhilisha juu ya wengi miongoni mwa Tuliowaumba kwa ufadhilisho mkubwa. [Al-Israa (17:70)]

Na Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Mkarimu zaidi, Hakuna anayefanana Naye katika ukarimu, kwa sababu Yeye (سبحانه وتعالى):

1-Ni Mkarimu kushinda wote, Hana mfano Wake.

2-Ni Mwenye kheri nyingi, Mwenye kunufaisha, na kunufaisha Kwake hakukatiki.

3-Ndiye Mwenye kusamehe makosa ya Waja Wake, na kuyabadilisha maovu yao kuwa mema kwa anayetubu, akaamini na akatenda mema, kama Anavyosema (سبحانه وتعالى):

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda amali njema. Basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema. Na Allaah daima Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Al-Furqaan (25:70)]

4-Ni Mwenye kudumu katika kheri, haikatiki wala haiishi; Huanza kwa Neema kabla ya kustahiki, Hutoa kabla ya kuombwa, Huanza kutoa mema bila kuhitaji malipo, na Hutoa bila kujali ni kiasi gani Ametoa wala Amempa nani.

5-Katika Ukarimu Wake (سبحانه وتعالى) ni kwamba Huendelea kumpa hata anayezikufuru Neema Zake; kwani Allaah Ni Mkarimu kwa Dhati Yake, hata kama hakuna yeyote atakayemwabudu, na Utukufu Wake hauhitajii yeyote. Ni Mkwasi, Hahitaji shukurani ya Waja wala ibaada yao, na Mkarimu Anayewaenea kwa kheri Yake duniani; mwenye kushukuru na mwenye kukufuru, kisha Atawahesabu na kuwalipa Aakhirah.

6-Katika ukamilifu wa Ukarimu Wake ni kwamba Amemkirimu mwana-Aadam kwa namna zote za ukarimu, katika Neema zilizo dhahiri na zilizojificha zisizo na hesabu, na Akampa fadhila na mazuri ambayo Hakuwapa viumbe wengi wengineo. Na miongoni mwa Ukarimu Wake ni kwamba Amemfunza mwana-Aadam asiyoyajua, Akamtukuza kwa ilimu ambayo kwayo Aadam (عليه السلام) alibainika kuwa bora kuliko Malaika.

7-Katika Ukarimu Wake ni kuzidisha thawabu za mema; tokea mara moja, hadi mara kumi, hadi mara mia saba na zaidi, na ovu Hulihesabu kama lilivyo. Na katika Ukarimu Wake pia ni kuwaandikia watoto ambao hawajabaleghe thawabu za mema na ibaada zao.

8-Na Allaah Ameiita Qur-aan kuwa ni Kariym, kwa kuwa ndani yake mna tabia njema kabisa, na kwa sababu humtukuza anayeihifadhi na anayeisoma. Na Ameipa Jannah Sifa hii, kuwa ni mahali pa kuingia patukufu, rizqi tukufu na ujira mtukufu. Anasema (سبحانه وتعالى):

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا ﴿٣١﴾

Mkijiepusha na madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu. [An-Nisaa (4:31)]

Na Anasema (سبحانه وتعالى):

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٧٤﴾

Na wale walioamini na wakahajiri na wakafanya Jihaad katika Njia ya Allaah, na wale waliotoa makazi na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata maghfirah na rizki karimu. [Al-Anfaal (8:74)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

تَحِيَّتُهُمْ يَوْمَ يَلْقَوْنَهُ سَلَامٌ ۚ وَأَعَدَّ لَهُمْ أَجْرًا كَرِيمًا ﴿٤٤﴾

Maamkizi yao Siku watakayokutana Naye ni “Salaam.” Na Amewaandalia ujira wa ukarimu. [Al-Ahzaab (33:44)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

مَّن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ وَلَهُ أَجْرٌ كَرِيمٌ ﴿١١﴾

Nani ambaye atamkopesha Allaah karadha nzuri kisha (Allaah) Amuongezee maradufu na apate ujira mtukufu? [Al-Hadiyd (57:11)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Kariym:

1-Usighurike Na Ukarimu Wa Al-Kariym:

Katika swali la Allaah (عزّ وجلّ) baada ya kutaja matukio ya kusimama Qiyaamah na kutoweka dunia, baadhi ya wajinga hudhani kwamba neno “Al-Kariym” ni kumwelekeza mtu kwenye jibu, mpaka husema: Ukarimu Wake ndio uliomghuri! Lakini makusudio ya swali hili ni tahadharisho; kwamba haifai Al-Kariym kulipwa kwa matendo mabaya na maovu. Basi jifunze kuhusu Allaah, Majina Yake na Sifa Zake na maana zake kwako, wala usighurike na dunia wala shaytwaan. Tambua kwamba Al-Kariym Hatomwangusha kamwe anayetumia maisha yake kumtii, hata kama watu watasema kufuata Dini si jambo la kisasa. Na usidhani kamwe kwamba wale waliopewa mengi katika dunia hii huku wakimkanusha watakuwa na fungu lolote Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ ﴿٦﴾ الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ ﴿٧﴾ فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ ﴿٨﴾

Ee binaadam! Nini kilichokughuri hata umkufuru Rabb wako Mkarimu? Ambaye Amekuumba, Akakusawazisha (umbo, sura, viungo), na Akakulinganisha sawa. Katika sura Aliyotaka Akakutengeneza. [Al-Infitwaar (82:6-8)]

2-Al-Kariym Ni Mkwasi, Hahitaji Shukurani Ya Mja:

Tambua, ee Mja wa Al-Kariym: Mwenye kushukuru ananufaisha nafsi yake, na mwenye kukufuru hamdhuru Allaah; kwani Rabb ni Mkwasi, Mkarimu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالَ الَّذِي عِندَهُ عِلْمٌ مِّنَ الْكِتَابِ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ ۚ فَلَمَّا رَآهُ مُسْتَقِرًّا عِندَهُ قَالَ هَـٰذَا مِن فَضْلِ رَبِّي لِيَبْلُوَنِي أَأَشْكُرُ أَمْ أَكْفُرُ ۖ وَمَن شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّي غَنِيٌّ كَرِيمٌ ﴿٤٠﴾

Akasema yule ambaye ana ilimu kutoka katika Kitabu: Mimi nitakuletea kabla halijapepesa jicho lako. Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, (Sulaymaan) alisema: Hii ni katika Fadhila za Rabb wangu, Anijaribu; je, nitashukuru, au nitakufuru. Na yeyote yule anayeshukuru, basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na yeyote yule asiyekuwa na shukurani, basi hakika Rabb wangu ni Mkwasi, Mkarimu. [An-Naml (27:40)]

3-Al-Kariym Anapenda Ukarimu Na Tabia Njema Za Juu:

Tambua kwamba Al-Kariym Anapenda ukarimu na tabia za juu; basi jipambe nazo.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ كَرِيمٌ يُحِبُّ الْكَرَمَ، وَيُحِبُّ مَعَالِيَ الأَخْلاَقِ، وَيَكْرَهُ سَفْسَافَهَا))

Amesimulia Sahl bin Sa’d (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ni Mkarimu, Anapenda ukarimu, na Anapenda tabia za juu, na Anachukia tabia duni.” [Atw-Twabaraaniy, Al-Haakim, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Al-Jaami’ (1801)]

4-Kuwa Mkarimu Upate Kukurubia Al-Kariym:

Tambua kwamba Majina ya Al-Kariym na Sifa Zake ni ya aina mbili: yale ambayo ni Yake Pekee (kama Al-Khaaliq, Muumbaji), na yale ambayo tunaweza na tunapaswa kujitahidi kuwa na sifa zake, na miongoni mwayo ni ukarimu. Basi kuwa mkarimu kwa mali yako, wakati wako na hata kwa maneno yako; na wakirimu wageni wako na majirani zako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ فَلْيَقُلْ خَيْرًا أَوْ لِيَصْمُتْ، وَمَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ فَلْيُكْرِمْ جَارَهُ، وَمَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ فَلْيُكْرِمْ ضَيْفَهُ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho, na aseme kheri au anyamaze. Na anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho, na amkirimu jirani yake. Na anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho, na amkirimu mgeni wake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Usiogope Ufakiri Unapotoa, Kwani Al-Kariym Anakuahidi Fadhila:

Tambua kwamba shaytwaan humtisha mtoaji kwa ufakiri, lakini Al-Kariym Anaahidi maghfirah na fadhila. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُم بِالْفَحْشَاءِ ۖ وَاللَّـهُ يَعِدُكُم مَّغْفِرَةً مِّنْهُ وَفَضْلًا ۗ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٦٨﴾

Shaytwaan anakutishieni ufukara na anakuamrisheni machafu, (ubakhili), na Allaah Anakuahidini Maghfirah kutoka Kwake na Fadhila. Na Allaah Ni Mwenye Wasaa, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah (2:268)]

6-Shikamana Na Qur-aan Al-Kariym Na Uwafundishe Wengine:

Kitabu cha Allaah, Qur-aan, ni Kariym kwa kuwa kimejaa manufaa na mwongozo, mazuri na baraka, na hakina kosa lolote wala mgongano. Ifungue Qur-aan Al-Kariym angalau kila siku; hata ukisoma Aayah moja kwa siku, ifahamu na uiache ibadilishe tabia yako, akili yako na moyo wako, na utaona itakavyokufanya kuwa mkarimu zaidi, Akipenda Allaah! Na kwa kuwa Al-Kariym Ametukirimu kama wana-Aadam na hasa kama Waislamu, itumie akili Aliyokupa kuunufaisha Ummah; washirikishe wengine Aayaat za Qur-aan, mfundishe mwingine hata Hadiyth moja, na eneza ujumbe wa Uislamu kwa kuonyesha tabia nzuri na tukufu kwa wasiokuwa Waislamu. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عُثْمَانَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((خَيْرُكُمْ مَنْ تَعَلَّمَ الْقُرْآنَ وَعَلَّمَهُ))

Amesimulia ‘Uthmaan (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mbora wenu ni yule aliyejifunza Qur-aan na akaifundisha.” [Al-Bukhaariy]

7-Wakirimu Wazazi Wako:

Tambua kwamba kwa kuuheshimu na kuutukuza haki ya wazazi wawili, Al-Kariym Amewaamrisha Waja Wake adabu za kuzungumza nao; kwamba wasiwaambie hata “ah!” wala wasiwakaripie, bali wawaambie kauli tukufu, yaani kauli laini, nzuri na njema kwa adabu, heshima na kuwatukuza. Anasema (سبحانه وتعالى):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾

Na Rabb wako Ameamuru kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee, na waambie maneno ya heshima. [Al-Israa (17:23)]

Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((رَغِمَ أَنْفُ، ثُمَّ رَغِمَ أَنْفُ، ثُمَّ رَغِمَ أَنْفُ)). قِيلَ: مَنْ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: ((مَنْ أَدْرَكَ أَبَوَيْهِ عِنْدَ الْكِبَرِ أَحَدَهُمَا أَوْ كِلَيْهِمَا فَلَمْ يَدْخُلِ الْجَنَّةَ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Pua yake na ibwage mchangani, kisha pua yake na ibwage mchangani, kisha pua yake na ibwage mchangani.” Ikasemwa: Nani yaa Rasula-Allaah? Akasema: “Aliyewadiriki wazazi wake katika uzee wao, mmoja wao au wote wawili, kisha asiingie Jannah.” [Muslim]

8-Usisahau Moto Unapostarehe Na Neema Za Al-Kariym:

Unapostarehe na Neema zote Alizokupa Al-Kariym, usisahau moto wa Jahannam. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لاَ تَزَالُ جَهَنَّمُ تَقُولُ: هَلْ مِنْ مَزِيدٍ، حَتَّى يَضَعَ فِيهَا رَبُّ الْعَالَمِينَ قَدَمَهُ، فَيَنْزَوِي بَعْضُهَا إِلَى بَعْضٍ، ثُمَّ تَقُولُ: قَدْ قَدْ، بِعِزَّتِكَ وَكَرَمِكَ، وَلاَ تَزَالُ الْجَنَّةُ تَفْضُلُ حَتَّى يُنْشِئَ اللَّهُ لَهَا خَلْقًا فَيُسْكِنَهُمْ فَضْلَ الْجَنَّةِ))

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Jahannam itaendelea kusema: Je, kuna ziyada? Mpaka Rabb wa walimwengu Aweke Kiguu Chake humo, basi baadhi yake itakusanyika kwa baadhi nyingine, kisha iseme: Inatosha! Inatosha! Kwa Utukufu Wako na Ukarimu Wako! Na Jannah itaendelea kuwa na nafasi ya ziada mpaka Allaah Awaumbie viumbe wengine Awaweke katika nafasi hiyo ya ziada ya Jannah.” [Al-Bukhaariy]

9-Waombee Maiti Wa Kiislamu Kwa Al-Kariym:

Tambua, ee Mja wa Al-Kariym: Na kwa ajili hiyo, miongoni mwa Du’aa za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kumswalia maiti ni kumuombea Allaah Amkirimu makazi yake, yaani Ampe fungu zuri katika Jannah:

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ وَارْحَمْهُ وَعَافِهِ وَاعْفُ عَنْهُ، وَأَكْرِمْ نُزُلَهُ، وَوَسِّعْ مُدْخَلَهُ

Yaa Allaah, Mghufurie, na Mrehemu, na Mpe afya, na Msamehe, na Ukirimu makazi yake, na Upanue kaburi lake. [Muslim]

10-Muombe Al-Kariym Kwa Yakini Ya Kujibiwa:

Allaah Ni Mkarimu, Anaona hayaa kumrudisha Mja Wake mikono mitupu anapomuomba. Basi mnyanyulie mikono yako kwa unyenyekevu, na mwombe kwa yakini kwamba Al-Kariym Hatakurudisha bure:

عَنْ سَلْمَانَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ رَبَّكُمْ تَبَارَكَ وَتَعَالَى حَيِيٌّ كَرِيمٌ، يَسْتَحْيِي مِنْ عَبْدِهِ إِذَا رَفَعَ يَدَيْهِ إِلَيْهِ أَنْ يَرُدَّهُمَا صِفْرًا))

Amesimulia Salmaan (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Rabb wenu (تبارك وتعالى) Ni Mwenye Hayaa, Mkarimu; Anaona hayaa kwa mja Wake anaponyanyua mikono yake Kwake, kuirudisha tupu.” [Abuu Daawuwd (1488), At-Tirmidhiy, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd]

Na Allaah Mjuzi zaidi

Na Allaah Mjuzi zaidi