Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah054 - Al-Akram

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 054 kati ya 103
Al-Akram — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Akram: Mkarimu Kushinda Wote

Al-Akram Ni Aliyefikia ukomo wa ukarimu; Akram Al-Akramiyn (Mkarimu kuliko wakarimu wote), Hana wa kufanana Naye katika hilo asilani wala wa kulingana Naye. Kheri zote zinatoka Kwake; Anawalipa Waumini kwa Fadhila Zake, na Anawapa muda wapinzani na kuwahesabu kwa Uadilifu Wake.

Jina hili la Allaah Al-Akram limetajwa katika Qur-aan mara moja tu, nalo limekuja katika Suwrah ya kwanza kabisa kuteremshwa kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Allaah (سبحانه وتعالى) Amesema:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ ﴿١﴾ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ ﴿٢﴾ اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ ﴿٣﴾ الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ ﴿٤﴾ عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ ﴿٥﴾

Soma kwa Jina la Rabb wako Aliyeumba. Amemuumba binaadam kutokana na pande la damu linaloninginia. Soma. Kwani Rabb wako Ni Mkarimu kushinda wote. Ambaye Amefunza kwa kalamu. Amemfunza binaadam asiyoyajua. [Al-‘Alaq (96:1-5)]

Na katika Aayaat hizi kuna dalili ya Ukarimu Wake (سبحانه وتعالى) uliokamilika; kwani Amemuumba binaadam kutokana na kitu duni kabisa, kisha Akamkirimu kwa ilimu na kwa kalamu, na Akamfunza yale asiyokuwa akiyajua. Basi ukarimu wa ilimu ndio ukarimu ulio bora kabisa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

Na Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Akram kwa maana zifuatazo:

1-Ni Mkarimu kushinda wakarimu wote; kila ukarimu unaopatikana kwa viumbe unatoka Kwake, na Yeye Ndiye Aliyewapa hao wakarimu ukarimu wao.

2-Ukarimu Wake hauchanganyiki na upungufu wowote; Hatoi kwa kutaraji malipo, wala kwa kuhitajia, wala kwa kuogopa, bali Hutoa kwa Fadhila Zake Pekee.

3-Ukarimu Wake hauna mwisho wala haukatiki; Hutoa kwa wingi kabla ya kuombwa, na Huzidisha baada ya kuombwa, wala Hatarajii malipo kutoka kwa Waja Wake.

4-Ni Mwenye kuwakirimu Waja Wake duniani kwa Neema zisizohesabika, na kuwakirimu zaidi Aakhirah kwa yale ambayo jicho halijapata kuona.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Akram:

1-Usidanganyike Na Ukarimu Wa Al-Akram Ukaendelea Kumuasi:

Tambua, ee Mja wa Al-Akram: Ukarimu wa Allaah kwa mja hauna maana ya kumpa ruhusa ya kumuasi, bali unapaswa kumfanya aone haya na kumtii zaidi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ ﴿٦﴾ الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ ﴿٧﴾

Ee binaadam! Nini kilichokughuri hata umkufuru Rabb wako Mkarimu? Ambaye Amekuumba, Akakusawazisha (umbo, sura, viungo), na Akakulinganisha sawa. [Al-Infitwaar (82:6-7)]

2-Tambua Kwamba Ukarimu Wake Umekuenea Kabla Hujaomba:

Al-Akram Amekupa kila kitu ulichokihitaji hata kabla ya kukiomba. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَآتَاكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ ۚ وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ الْإِنسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ ﴿٣٤﴾

Na Akakupeni kila mlichomuomba. Na mkihesabu Neema za Allaah hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. Hakika binaadam ni mwingi wa dhulma, mwingi wa kukufuru. [Ibraahiym (14:34)]

3-Heshimu Utukufu Aliompa Al-Akram Mwanaadam:

Tambua kwamba Al-Akram Amemkirimu mwanaadam juu ya viumbe wengi; basi usimdhalilishe mwanaadam mwenzako wala usijidhalilishe kwa maasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا ﴿٧٠﴾

Na kwa yakini Tumewakirimu wana wa Aadam, na Tukawabeba katika ardhi kavu na baharini, na Tukawaruzuku katika vizuri na Tukawafadhilisha juu ya wengi miongoni mwa Tuliowaumba kwa ufadhilisho mkubwa. [Al-Israa (17:70)]

4-Tambua Kwamba Utukufu Wa Kweli Ni Taqwa:

Sababu kubwa kabisa ya kuwa na utukufu mbele ya Allaah ni taqwa; huo ndio utukufu wa kweli utakaobakia kwa wenye nao Aakhirah mpaka waingie Nyumba ya utukufu, nayo ni Jannah. Ama heshima na hadhi wanayostarehe nayo makafiri duniani, ni yenye kutoweka na itageuka kinyume chake Siku ya Qiyaamah. Na ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنهما) aliitazama Al-Ka‘bah siku moja akasema: Ukubwa ulioje wako na ukubwa ulioje wa utukufu wako, na Muumini ana utukufu mkubwa zaidi mbele ya Allaah kuliko wewe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿١٣﴾

Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamme na mwanamke, na Tukakufanyeni mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye na hadhi zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni mwenye taqwa zaidi kati yenu. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Khabari za dhahiri na siri. [Al-Hujuraat (49:13)]

5-Tafuta Ilimu Kutoka Kwa Al-Akram:

Ukarimu wa kwanza kabisa aliopewa mwanaadam katika Wahy ni ukarimu wa ilimu; Al-Akram Amefunza kwa kalamu na Akamfunza binaadam asiyoyajua. Rejea juu: Al-‘Alaq (96:1-5). Basi tafuta ilimu ya Dini yako, uisome, uifanyie kazi na uwafundishe wengine. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... وَمَنْ سَلَكَ طَرِيقًا يَلْتَمِسُ فِيهِ عِلْمًا، سَهَّلَ اللَّهُ لَهُ بِهِ طَرِيقًا إِلَى الْجَنَّةِ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “... Na atakayeishika njia akitafuta ndani yake ilimu, Allaah Atamsahilishia kwayo njia ya kwendea Jannah.” [Muslim]

6-Kuwa Mkarimu Kwa Wageni:

Mwenye kumjua Al-Akram hujipamba na ukarimu. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ فَلْيَقُلْ خَيْرًا أَوْ لِيَصْمُتْ، وَمَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ فَلْيُكْرِمْ جَارَهُ، وَمَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ فَلْيُكْرِمْ ضَيْفَهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho, basi aseme la kheri au anyamaze. Na anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho, basi amkirimu jirani yake. Na anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho, basi amkirimu mgeni wake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

7-Wazungumzie Wazazi Wako Kwa Maneno Ya Karama:

Tambua, ee Mja wa Al-Akram: Katika ukarimu mkubwa kabisa ni ukarimu kwa wazazi, kwa maneno na vitendo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾

Na Rabb wako Ameamuru kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee, na waambie maneno ya heshima. [Al-Israa (17:23)]

8-Tamani Karama Ya Al-Akram Katika Jannah:

Miongoni mwa picha nzuri kabisa za Ukarimu wa Al-Kariym Al-Akram ni yale Aliyowaandalia Waja Wake wema katika Jannah:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((قَالَ اللَّهُ: أَعْدَدْتُ لِعِبَادِي الصَّالِحِينَ مَا لاَ عَيْنٌ رَأَتْ، وَلاَ أُذُنٌ سَمِعَتْ، وَلاَ خَطَرَ عَلَى قَلْبِ بَشَرٍ، فَاقْرَءُوا إِنْ شِئْتُمْ: فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Amesema: Nimewaandalia Waja Wangu wema yale ambayo jicho halijapata kuona, wala sikio halijapata kusikia, wala hayajapita katika moyo wa mwana-Aadam. Someni mkipenda: Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichwa kwa ajili yao katika yanayoburudisha macho.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Rejea Kwa Al-Akram Ukiwa Umekosea:

Hata dhambi zako zikiwa nyingi kiasi gani, usikate tamaa na Ukarimu wa Al-Akram; kwani Ukarimu Wake ni mkubwa kuliko madhambi yako. Allaah (تعالى) Amesema katika Hadiyth Al-Qudsiy:

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((قَالَ اللَّهُ تَعَالَى: يَا ابْنَ آدَمَ، إِنَّكَ مَا دَعَوْتَنِي وَرَجَوْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ عَلَى مَا كَانَ فِيكَ وَلاَ أُبَالِي، يَا ابْنَ آدَمَ لَوْ بَلَغَتْ ذُنُوبُكَ عَنَانَ السَّمَاءِ ثُمَّ اسْتَغْفَرْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ، يَا ابْنَ آدَمَ إِنَّكَ لَوْ أَتَيْتَنِي بِقُرَابِ الأَرْضِ خَطَايَا ثُمَّ لَقِيتَنِي لاَ تُشْرِكُ بِي شَيْئًا لأَتَيْتُكَ بِقُرَابِهَا مَغْفِرَةً))

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Allaah (تعالى) Amesema: Ee mwana wa Aadam! Hakika wewe madamu unaniomba na unanitaraji, Nitakughufuria yale uliyo nayo wala Sijali. Ee mwana wa Aadam! Lau dhambi zako zingefika mawinguni kisha ukaniomba maghfirah, Nitakughufuria. Ee mwana wa Aadam! Hakika wewe lau ungenijia na makosa yanayokaribia kuijaza ardhi, kisha ukakutana Nami hali hunishirikishi na chochote, bila shaka Nitakujia na maghfirah inayokaribia kuijaza (ardhi).” [At-Tirmidhiy (3540), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy (na amesema ni Hasan katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (127))]

10-Muombee Maiti Ili Al-Akram Aukirimu Ukaribisho Wake:

Tambua, ee Mja wa Al-Akram: Katika du’aa za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa maiti ni:

عَنْ عَوْفِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: صَلَّى رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) عَلَى جَنَازَةٍ فَحَفِظْتُ مِنْ دُعَائِهِ وَهُوَ يَقُولُ: ((اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ وَارْحَمْهُ، وَعَافِهِ وَاعْفُ عَنْهُ، وَأَكْرِمْ نُزُلَهُ، وَوَسِّعْ مُدْخَلَهُ، وَاغْسِلْهُ بِالْمَاءِ وَالثَّلْجِ وَالْبَرَدِ، وَنَقِّهِ مِنَ الْخَطَايَا كَمَا نَقَّيْتَ الثَّوْبَ الأَبْيَضَ مِنَ الدَّنَسِ))

Amesimulia ‘Awf bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliswalia jeneza, nikahifadhi katika du’aa yake akisema:

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ وَارْحَمْهُ، وَعَافِهِ وَاعْفُ عَنْهُ، وَأَكْرِمْ نُزُلَهُ، وَوَسِّعْ مُدْخَلَهُ، وَاغْسِلْهُ بِالْمَاءِ وَالثَّلْجِ وَالْبَرَدِ، وَنَقِّهِ مِنَ الْخَطَايَا كَمَا نَقَّيْتَ الثَّوْبَ الأَبْيَضَ مِنَ الدَّنَسِ

Yaa Allaah! Mghufurie na Umrehemu, Mwafu na Umsamehe, Ukirimu ukaribisho wake, Upanue mahali pake pa kuingia, Umwoshe kwa maji, theluji na barafu, na Umtakase na makosa kama Ulivyolitakasa vazi jeupe na uchafu. [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi

Na Allaah Mjuzi zaidi