Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah055 - Al-Latwiyf

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 055 kati ya 103
Al-Latwiyf — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Latwiyf: Mwenye Kudabiri Mambo Kwa Ulatifu, Mjuzi Wa Yaliyofichika

Yeye Ni Mjuzi wa mambo ya ndani, Kwake halijifichi lenye kujificha, na Anawafikishia Waja Wake kheri na manufaa kwa njia zilizofichika. Al-Latwiyf Ni Mpole kwa Mja Wake na kwa ajili ya Mja Wake, Anayeendesha mambo yao kwa namna yenye manufaa zaidi bila ya wao kuhisi. Naye Ni Latwiyf kwa Mja Wake kwa upole, huruma na rehma, na Ni Latwiyf juu ya Mja Wake kwa kuwa Anajua kikamilifu hali yake, amali zake, yaliyomo moyoni mwake, fikra zake na matamanio yake.

Jina Hili la Allaah, Al-Latwiyf, limetajwa katika Qur-aan mara saba. Miongoni mwa Aayah hizo ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٤﴾

Kwani Hajui Yule Aliyeumba! Na hali Yeye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri! [Al-Mulk (67:14)]

Na mzizi wa neno latwiyf ni ل ط ف, nao una maana nne: kuwa mpole, mwenye huruma, laini na mwenye kutoa kwa upole; kuwa mwembamba, mdogo na laini; kuwa na ujuzi wa undani wa mambo yote; na kumtendea mtu kwa kuzingatia hali zake. Na latwafa (kwa fat-hah) ina maana ya upole na wema, na latwufa (kwa dhwammah) ina maana ya kuwa kidogo na chembamba. Kwa hiyo al-lutwf ni kumfanyia mtu wema kwa upole mpaka asihisi, na ni kitu kilicho kidogo mno kiasi cha kutoonekana wala kuhisika.

Na Allaah (تبارك وتعالى) Ndiye Al-Latwiyf na hakuna zaidi Yake, kwa maana zifuatazo:

1-Ilimu Yake imeenea kwa yaliyojificha na yaliyo dhahiri; Anajua yaliyomo ndani ya nyoyo za watu, na yaliyomo ndani ya ardhi, na yaliyofichwa ndani ya mbegu,1 Hakifichiki Kwake kitu hata kikiwa kidogo, chembamba na duni vipi. Hata kama rizqi ya mtu ingekuwa na uzito wa punje ya hardali ndani ya jabali, au mbinguni au ardhini, Allaah Angeileta kwake. Rejea chini: Faida namba 1, Luqmaan (31:16).

2-Naye Ni Yule Aliyetakasika kwa Ulatifu Wake kutokana na kudirikiwa namna Alivyo; macho hayamdiriki, Naye Anayadiriki macho yote. Anasema (سبحانه وتعالى):

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٠٣﴾

Macho hayamzunguki bali Yeye Anayazunguka macho yote, Naye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-An‘aam (6:103)]

3-Naye (تعالى) Hupeleka mambo katika malengo yake kwa njia nzuri ya wema na upole, na Huwafikishia Waja Wake manufaa wakiwa wanajua na wasipojua.

4-Naye Ni Mwema kwa Waja Wake Waumini; Anawafikishia maslahi na manufaa yao kwa njia ya upole, wakihisi au wakighafilika, na Amewawepesishia njia ya kufikia Radhi Zake na Ukarimu Wake, na Anawahifadhi na kila sababu na njia itakayowafikisha katika Machukivu Yake.2 Na hili linahitaji ilimu ya lengo lililokusudiwa na ujuzi wa undani wa jambo lenyewe.

5-Miongoni mwa Upole Wake kwa Waja Wake ni kwamba Amewapa zaidi ya wanachohitaji, na Amewakalifisha chini ya uwezo wao, na Amewawepesishia njia ya kufikia furaha kwa muda mfupi.3

Tofauti Kati Ya “Latwafa Bihi” Na “Latwafa Lahu”:

Allaah Kumfanyia mja upole (latwafa bihi) ni katika mambo ya ndani; pale Allaah Anapomwepesishia Mja Wake njia ya kheri na Akamsaidia juu yake. Na Allaah Kumfanyia mja upole kwa ajili yake (latwafa lahu) ni katika mambo ya nje; pale Allaah Anapompangia sababu za nje zisizo chini ya uwezo wa mja, na ndani yake mna maslahi yake. Na ndio maana Nabiy Yuwsuf (عليه السلام), baada ya kupitia hali mbalimbali za mitihani, alitambua kwamba hayo yalikuwa ni Upole wa Allaah kwake, akakiri neema hii kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَرَفَعَ أَبَوَيْهِ عَلَى الْعَرْشِ وَخَرُّوا لَهُ سُجَّدًا ۖ وَقَالَ يَا أَبَتِ هَـٰذَا تَأْوِيلُ رُؤْيَايَ مِن قَبْلُ قَدْ جَعَلَهَا رَبِّي حَقًّا ۖ وَقَدْ أَحْسَنَ بِي إِذْ أَخْرَجَنِي مِنَ السِّجْنِ وَجَاءَ بِكُم مِّنَ الْبَدْوِ مِن بَعْدِ أَن نَّزَغَ الشَّيْطَانُ بَيْنِي وَبَيْنَ إِخْوَتِي ۚ إِنَّ رَبِّي لَطِيفٌ لِّمَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿١٠٠﴾

Akawapandisha wazazi wake wawili juu ya kiti cha ufalme, wakaporomoka wote kumsujudia. Na akasema: Ee baba yangu kipenzi! Hii ni tafsiri ya njozi yangu hapo kabla, Rabb wangu Ameijaalia kweli. Na hakika Amenifanyia ihsaan Aliponitoa kutoka jela, na Akakuleteni kutoka jangwani baada ya shaytwaan kuchochea baina yangu na baina ya kaka zangu. Hakika Rabb wangu Ni Latwiyf kwa Atakayo. Hakika Yeye Ndiye Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote. [Yuwsuf (12:100)]

Basi mja anaposema: “Yaa Latwiyf, nifanyie upole na unifanyie upole kwa ajili yangu, nakuomba Upole Wako”, maana yake ni: Nitengenezee hali zangu za dhahiri na za siri.

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Latwiyf:

1-Al-Latwiyf Anayafikia Macho Wala Macho Hayamfikii:

Katika maana ya Al-Latwiyf ni Ujuzi Wake wa undani wa vitu vilivyofichikana kabisa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٠٣﴾

Macho hayamzunguki bali Yeye Anayazunguka macho yote, Naye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-An’aam (6:103)]

2-Tambua Kwamba Al-Latwiyf Anajua Kila Kitu, Basi Ihesabu Nafsi Yako:

Mja anapojua undani wa Ilimu ya Allaah na jinsi Alivyoenea kwa kila kitu, huihesabu nafsi yake juu ya kauli zake na matendo yake. Al-Latwiyf Anajua kila unachokifanya, kila undani, kila fikra, kila matamanio na kila niyyah; basi kabla ya kufanya jambo lolote, jiulize: Je, kwa kweli ninalifanya hili kwa ajili ya Allaah au kwa ajili ya kitu kingine? Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ ﴿١٦﴾

Ee mwanangu! Hakika likiweko (zuri au ovu) lolote lenye uzito wa punje ya hardali, likawa katika jabali au mbinguni au ardhini, Allaah Atalileta tu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Luqmaan (31:16)]

3-Tambua Upole Wa Al-Latwiyf Katika Mitihani Yako:

Miongoni mwa Upole wa Allaah kwa mja ni kwamba Humsaidia katika mitihani ili imaan yake izidi na ujira wake uwe mkubwa; basi Ametakasika Al-Latwiyf katika mitihani Yake, afya Anayoitoa, kutoa Kwake na kuzuia Kwake. Na katika Upole Wake ni kwamba Hujaalia maasi Anayomtahini nayo mja wake kuwa ni sababu ya Rehma Yake; Humfungulia mlango wa tawbah na kunyenyekea mbele ya Rabb wake, na kuiona nafsi yake duni, na kuondoka kujiona na kiburi moyoni mwake, jambo ambalo ni bora kwake kuliko ibaada nyingi. Na huenda Al-Latwiyf Akakupitisha katika mambo unayoyachukia, basi subiri; na Anapokupa unayoyapenda, shukuru. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ صُهَيْبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((عَجَبًا لأَمْرِ الْمُؤْمِنِ، إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ، وَلَيْسَ ذَاكَ لأَحَدٍ إِلاَّ لِلْمُؤْمِنِ، إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ، وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ))

Amesimulia Swuhayb (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ajabu ya jambo la Muumini! Hakika jambo lake lote ni kheri, na hilo halipati yeyote isipokuwa Muumini. Akipatwa na furaha hushukuru, ikawa ni kheri kwake; na akipatwa na dhara husubiri, ikawa ni kheri kwake.” [Muslim]

4-Al-Latwiyf Ni Mpole Kwa Waja Wake, Huwaruzuku Awatakao:

Tambua, ee Mja wa Al-Latwiyf: Upole Wake unawaenea Waja Wake wote, Waumini na makafiri, katika rizki zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

اللَّـهُ لَطِيفٌ بِعِبَادِهِ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ ﴿١٩﴾

Allaah Ni Latifu kwa Waja Wake, Anamruzuku Amtakaye, Naye Ndiye Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika. [Ash-Shuwraa (42:19)]

5-Usishughulishwe Na Rizqi Ukaacha Faradhi:

Katika Upole Wake mkubwa ni kwamba Hakuwahusisha Waumini peke yao na rizqi. Na lau utafuatilia athari ya Upole Wake katika kuwepesisha tonge moja analolila mja bila ya taklifa yoyote, utakuta kwamba Allaah Amewatiisha viumbe wasiohesabika, wakashirikiana kulitengeneza: mkulima, mvunaji, msagaji, mkandaji, mwokaji na wengineo. Kwa hiyo Upole wa Allaah kwako unataka kwamba hima ya rizqi yako na maslahi yako isikushughulishe mpaka ukaacha kutekeleza faradhi na kufuata njia ya wale waliorudi kwa Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

اللَّـهُ لَطِيفٌ بِعِبَادِهِ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ ﴿١٩﴾

Allaah Ni Latwiyf kwa Waja Wake, Anamruzuku Amtakaye, Naye Ndiye Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika. [Ash-Shuwraa (42:19)]

6-Tafakari Upole Wa Al-Latwiyf Katika Kuihuisha Ardhi Kwa Mvua:

Tambua, ee Mja wa Al-Latwiyf: Mvua huteremka kwa upole, na ardhi hugeuka kijani bila watu kutambua jinsi inavyotokea. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَتُصْبِحُ الْأَرْضُ مُخْضَرَّةً ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ ﴿٦٣﴾

Je, huoni kwamba Allaah Ameteremsha kutoka mbinguni maji kisha ardhi ikawa chanikiwiti. Hakika Allaah bila shaka ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-Hajj (22:63)]

7-Tafakari Upole Wa Al-Latwiyf Katika Maisha Yako Na Umshukuru:

Allaah Ameutiisha ulimwengu mzima kwa ajili ya mwana-Aadam kwa malengo mawili: kwanza, ili tumjue Rabb wetu kwa Hikmah Yake, Uwezo Wake na Sifa Zake; na pili, kututukuza kwa kutuumbia ulimwengu huu mkubwa. Ukinywa bilauri ya maji kwa ajili ya kukata kiu tu bila ya kutafakari, basi umetimiza lengo dogo la kuumbwa kwake. Tazama Upole Wake: matunda Huyaivisha wakati wa joto nasi tumeghafilika; meno ya watoto hung’oka taratibu na kubadilishwa bila ya maumivu; hewa nyepesi tunayoivuta bila uzito; misimu inayobadilika; na mtu anayekuja njiani mwako na neno linalokunyanyua wakati ulipolihitaji. Na je, umewahi kupenda jambo lisilomridhisha Allaah, kisha taratibu ukaliacha mpaka usijue kwa nini ulilipenda? Hizo ni Njia za Al-Latwiyf. Basi mpende na umshukuru, na kithirisha kusema الْحَمْدُ لِلَّهِ hata kwa mambo usiyoyaona lakini yanakunufaisha, na سُبْحَانَ اللَّهِ kila unapopata nafasi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لَيَرْضَى عَنِ الْعَبْدِ أَنْ يَأْكُلَ الأَكْلَةَ فَيَحْمَدَهُ عَلَيْهَا، أَوْ يَشْرَبَ الشَّرْبَةَ فَيَحْمَدَهُ عَلَيْهَا))

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Humridhia mja anapokula chakula akamhimidi kwacho, au anapokunywa kinywaji akamhimidi kwacho.” [Muslim]

8-Tarajia Thawabu Hata Kwa Manufaa Usiyoyajua:

Tambua, ee Mja wa Al-Latwiyf: Miongoni mwa Upole wa Allaah ni kwamba Hujaalia kitu katika mali ya mja kiwe na manufaa na kheri kwa wengine, kisha Humlipa thawabu bila ya yeye kutarajia; kama mwenye mmea ukaliwa na mtu au mnyama, Allaah Humpa ujira mwenyewe bila ya yeye kujua, hasa akiwa na niyyah njema. Na vivyo hivyo kitabu mtu alichojifunza kwacho, au Mus-haf uliosomwa, na Allaah Ni Mwenye Fadhila kubwa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَغْرِسُ غَرْسًا، أَوْ يَزْرَعُ زَرْعًا، فَيَأْكُلُ مِنْهُ طَيْرٌ أَوْ إِنْسَانٌ أَوْ بَهِيمَةٌ، إِلاَّ كَانَ لَهُ بِهِ صَدَقَةٌ))

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna Muislamu yeyote anayepanda mti au kulima mmea, kisha akala kutoka humo ndege au mtu au mnyama, isipokuwa inakuwa kwake ni swadaqah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Kuwa Mpole Kwa Waja Wa Allaah:

Kuhisi Upole wa Allaah katika kila jambo la ulimwengu humpa mja fungu lake la sifa hii, kwa kuwa mpole kwa Waja wa Allaah; katika kuwalingania kwa Allaah na kuwaongoza kwenye furaha ya Aakhirah kwa maneno laini kabisa bila ya ukali, ushabiki wala ugomvi. Kwani Allaah Ni Latwiyf, Anawapenda wapole miongoni mwa Waja Wake na Huwachukia wakali wenye nyoyo ngumu. Na kama njia ya kumshukuru Al-Latwiyf kwa Upole Wake, jitahidi kuwa chanzo cha upole na wema kwa wengine; waangalie masikini, mayatima, wajane na wote wenye haja wanaokuzunguka, na uwafanyie jambo litakalowepesishia maisha yao. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ الرِّفْقَ لاَ يَكُونُ فِي شَيْءٍ إِلاَّ زَانَهُ، وَلاَ يُنْزَعُ مِنْ شَيْءٍ إِلاَّ شَانَهُ))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika upole haupatikani katika kitu isipokuwa hukipamba, na wala hauondolewi katika kitu isipokuwa hukitia aibu.” [Muslim]

10-Muombe Al-Latwiyf Akufanyie Upole:

Muombe Al-Latwiyf Akufanyie upole na Akusaidie kuwa mpole kwa wengine, na waombee wapendwa wako Baraka Zake. Na unapomuomba Akutengenezee hali zako za dhahiri na za siri, kumbuka kwamba Du’aa yenyewe ni ibaada. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ (رضي الله عنهما) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((الدُّعَاءُ هُوَ الْعِبَادَةُ))

Amesimulia An-Nu‘maan bin Bashiyr (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Du’aa ndio ibaada.” [Abuu Daawuwd (1479), At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Ibn Maajah (3101)]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Al-Haqq Al-Waadhwih Al-Mubiyn (60), na Tawdhwiyh Al-Kaafiyah Ash-Shaafiyah (123).
  • 2Sha-an Ad-Du‘aa (62), Tafsiyr As-Sa‘diy (5/488), na Tawdhwiyh Al-Kaafiyah Ash-Shaafiyah (123).
  • 3Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa (254).